El Niño yaanza na kutishia hali mbaya ya hewa, wanasayansi wanasema
Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
El Niño - hali ya hewa ya asili ya Pasifiki inayoongeza joto
duniani - imeanza rasmi, wanasayansi wa Marekani wanasema.
Utawala wa Kitaifa wa Bahari na Anga wa Marekani (NOAA)
umetangaza kwamba hali ya El Niño sasa inaendelea katika Pasifiki ya kitropiki,
huku halijoto ya uso wa bahari ikiongezeka kwa kasi katika miezi ya hivi
karibuni.
Utabiri mwingi unaonyesha kuwa hii inaweza kuishia kama El
Niño inayoitwa "super", na hata kuwa miongoni mwa El Niño kali zaidi
kuwahi kurekodiwa.
Hali hii inawadia wakati tayari kuna miongo kadhaa ya
ongezeko la joto linalosababishwa na binadamu, inaweza kusababisha mwaka
mwingine wenye joto kali zaidi - uwezekano mkubwa mwaka wa 2027 - huku ikivuruga
hali ya hewa, usambazaji wa chakula na uchumi mwaka huo.
Bei ya mafuta yapanda baada ya vitisho vya Trump
Chanzo cha picha, Getty Images
Bei ya mafuta imepanda kwa takriban dola mbili baada ya Rais
wa Marekani Donald Trump kuahidi kuishambulia Iran "vikali" kwa
mashambulizi mapya, na kuchukua udhibiti wa masoko yake ya mafuta na gesi.
Bei ya mafuta ghafi iliongezeka hadi $94.16 kwa pipa ndani
ya dakika chache alasiri ya leo, kabla ya kurudi chini kidogo.
"Hivi karibuni, tutachukua Kisiwa cha Kharg, na maeneo
mengine ya miundombinu ya mafuta, na kuchukua udhibiti kamili wa Masoko yao ya
Mafuta na Gesi, kama tulivyofanya Venezuela, ambayo inafanya kazi vizuri sana
kwa Venezuela na Marekani," Trump aliandika kwenye mtandao wake wa Truth
Social.
Mapema Alhamisi, bei ya mafuta ilikuwa imeshuka kidogo
kutoka zaidi ya $95 baada ya saa 01:00 BST, hadi chini kidogo ya $92 ifikapo
saa sita mchana kwa saa za Uingereza.
Trump asema Marekani itashambulia Iran 'vibaya mno usiku wa leo'
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais Donald Trump amesema kwamba Marekani itaishambulia Iran "vikali usiku wa leo" katika chapisho jipya kwenye mtandao wa Truth Social.
Hichi ndicho alisema rais:
"Marekani itaishambulia Iran (Ambayo Jeshi lake la Wanamaji, Jeshi la Anga, Rada, Ndege za Kupambana na Mashambulizi, na aina nyingine zote za Ulinzi, pamoja na vyenye uwezo mkubwa wa kushambulia, ZIMEENDA!), HALI ITAKUWA NGUMU SANA USIKU WA LEO
"Wakati fulani siku za hivi karibuni, tutachukua Kisiwa cha Kharg, na maeneo mengine ya miundombinu ya mafuta, na kuchukua udhibiti kamili wa Masoko yao ya Mafuta na Gesi, kama tulivyofanya Venezuela, ambayo sasa inafanya kazi vizuri sana kwa Venezuela na Marekani."
Tangu mwanzo wa mzozo huo, Trump ametishia mara kwa mara kuteka Kisiwa cha Kharg, kisiwa kidogo kilichoko pwani ya Iran ambacho ni makao ya kituo kikuu cha mafuta.
Marekani yathibitisha kushambulia meli ya tatu katika Ghuba ikiwa na mabaharia wa India
Chanzo cha picha, US Centcom
Marekani imethibitisha kuwa ilifanya shambulizi kwenye meli
ya M/T Jalveer yenye bendera ya Guinea-Bissau.
Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) inasema meli hiyo
"ilikiuka kizuizi" kwa kujaribu kusafirisha mafuta ya Iran kupitia
Ghuba ya Oman.
India yaishutumu Marekani kwa kuishambulia meli ya tatu
iliyokuwa na mabaharia wake
Wakati huo huo, Wizara ya mambo ya nje ya India imeishutumu
Marekani kwa kuishambulia meli ya tatu iliyokuwa imewabeba mabaharia wa India
karibu na bandari ya Shinas ya Oman asubuhi ya leo.
Meli ya M/T Jalveer, yenye bendera ya Guinea-Bissau, ilikuwa
na mabaharia 20 wa India ndani yake, ambao wote wanaripotiwa kuwa salama,
kulingana na wizara ya meli ya India, ambayo inasema uokoaji bado unaendelea.
Katika mkutano na waandishi wa habari mjini New Dehli
asubuhi ya leo, wizara ya mambo ya nje ilisema mashambulizi matatu tofauti
kwenye meli za Settebello, Marivex na Jalveer "
yamefanywa na Jeshi la Wanamaji la Marekani".
Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) imethibitisha mashambulizi
dhidi ya meli Settebello na Marivex.
Mawaziri waliongeza kuwa meli 13 zenye bendera ya India na
zaidi ya mabaharia 18,000 wa India walikuwa wamekwama katika eneo la Ghuba,
wakiwemo 562 kwenye meli zenye bendera ya India.
Marekani yashambulia meli ya Iran katika Ghuba ya Oman - ripoti
Marekani imeshambulia meli ya mizigo ya Iran iliyokuwa
imebeba "bidhaa muhimu" katika Ghuba ya Oman asubuhi ya leo,
kulingana na gavana wa Sirik, ambaye alinukuliwa na shirika la habari la
serikali la Iran Mehr news.
Wafanyakazi watano waliokolewa baada ya kombora kushambulia
meli hiyo, ambayo inasemekana ilishambuliwa ilipokuwa ikiondoka kutoka mji wa
Khasab, Oman, kuelekea mji wa Sirik nchini Iran.
Marekani haijatoa maoni yoyote kuhusu shambulio hilo.
Mashambulizi yanafanya usitishaji mapigano na Marekani 'hauna maana yoyote' - Iran
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Wizara ya mambo ya nje ya Iran imesema mashambulizi ya hivi
karibuni ya Marekani yanaacha usitishaji mapigano kati ya nchi hizo mbili "yasiwe
na maana yoyote".
Wizara ilisema
katika taarifa yake: "Mashambulizi hayo yameifanya usitishaji mapigano uwe
hauna maana yoyote," ikisisitiza kwamba matukio ya hivi karibuni
yamedhoofisha uwezekano wa mapatano yoyote kati ya pande hizo mbili.
Taarifa hiyo
imeongeza kuwa: "Tunalaani vikali vitendo vya jinai vya utawala wa
Marekani katika mashambulizi yake makubwa dhidi ya Iran jana usiku," na kuzingatia
operesheni hizo kuwa ni ongezeko hatari na ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Inaongeza kuwa viongozi wa Marekani watawajibika kwa athari
zinazojitokeza.
Hii inakuja baada ya Kamandi Kuu ya Marekani kusema
imekamilisha wimbi la "mashambulizi ya kujilinda" yakilenga maeneo ya
kijeshi, ufuatiliaji na rada kusini mwa Iran siku ya Jumatano.
Kamandi Kuu ya
Marekani ilisema katika taarifa yake kwenye jukwaa la X kwamba "Vikosi vya
Jeshi la Wanamaji la Marekani, vilianzisha mashambulizi ya mabomu yaliyoongozwa
kwa usahihi ili kushambulia maeneo ya Iran ambayo yalikuwa tishio kwa vikosi
vya Marekani na meli za kibiashara za kimataifa zinazopita kwenye maeneo ya
bahari."
Iran pia ilifanya mashambulizi, ikilenga mali za kijeshi za
Marekani katika eneo lote la Bahrain, Kuwait na Jordan.
Mjadala unaendelea kati ya Iran na Marekani kuhusu kufungwa
kwa Mlango-Bahari wa Hormuz.
Siku ya Jumatano, vyombo vya habari vya serikali ya Iran
viliripoti kwamba njia yenye shughuli nyingi ya usafirishaji wa meli
"imefungwa kabisa kwa kila aina ya meli".
Siku ya Alhamisi asubuhi, mamlaka ya njia za maji ya Iran imesema
tena mlangobahari huo umefungwa, vyombo vya habari vya serikali vinaripoti,
kufuatia wimbi jipya la mashambulizi ya Marekani hapo jana.
Hata hivyo, usiku kucha, Kamandi Kuu ya Marekani ilikanusha
kuwa njia hiyo imefungwa, na kusema: "Meli za kibiashara zinaendelea
kusafiri ndani na nje ya Mlango-Bahari wa Hormuz usiku wa leo."
Mlango-Bahari wa Hormuz unasalia kuwa kitovu cha mazungumzo,
huku Marekani na Iran zikijaribu kudhibiti mustakabali wake.
Iran imekuwa ikifunga njia hiyo tangu vita vilipoanza na
kuwaacha maelfu ya mabaharia wakiwa wamekwama, huku Marekani ikiweka vizuizi
kwenye bandari za Iran kama njia ya kulipiza kisasi.
Iran imetengeneza Mamlaka ya Mlango-Bahari wa Ghuba ya
Uajemi, ambayo inasema itaruhusu jeshi la Iran kusimamia meli zinazopita baada
ya vita.
Lakini Marekani inasisitiza kwamba Iran haitaruhusiwa
kudhibiti mlangobahari baada ya vita - Donald Trump alidai Jumatano kwamba
jeshi la Marekani lilisaidia meli 200 za kibiashara kupita kwenye njia hiyo ya
majini kama sehemu ya "misheni ya siri".
Mabaharia watatu wa India wauawa katika shambulio la Marekani karibu na Oman
Chanzo cha picha, Reuters
Waziri wa Meli wa New Delhi, Sarbananda Sonowal, ametangaza
kwamba mabaharia watatu wa India wameuawa baada ya shambulio la Marekani kwenye
meli ya Settebello yenye bendera ya Palau, akielezea tukio hilo kuwa la "kusikitisha".
Katika chapisho kwenye mtandao wa X, amesema kwamba vifo
vyao ni "pigo kubwa".
Meli ya Settebello yenye bendera ya Palau ilishambuliwa
Jumatano baada ya jeshi la Marekani kuishutumu kwa kukiuka kizuizi cha Marekani
kwa "kujaribu kusafirisha mafuta kutoka Iran". Kulikuwa na
wafanyakazi 24 wa India ndani ya meli hiyo - 21 waliokolewa.
Kamandi Kuu ya Marekani ilisema ilifyatua risasi kwenye
chumba cha injini cha meli hiyo baada ya wafanyakazi "kushindwa mara kadhaa
kufuata" masharti ya vikosi vya Marekani.
Manoj Yadav, katibu mkuu wa Muungano wa Mabaharia nchini
India, aliliambia gazeti la The Economic Times kwamba "haamini" kuwa
Marekani haikuwa na taarifa kuhusu uraia wa watu waliokuwa ndani ya meli hizo.
Alisema kuwa kuzuia meli hizo badala yake ni "njia mbadala iliyofaa".
Hii ni meli ya pili yenye wafanyakazi wa India ambayo
imeshambuliwa wiki hii. Siku ya Jumatatu, vikosi vya Marekani viliishambulia
Marivex, ambayo pia ni meli ya mafuta yenye bendera ya Palau yenye wafanyakazi
wa India, katika Ghuba ya Oman baada ya kushindwa kufuata maagizo ya Marekani,
Centcom ilisema.
Wafanyakazi wote 24 waliokolewa na jeshi la Oman, mamlaka ya
India ilisema.
Siku ya Bajeti Afrika Mashariki: Bajeti ‘kubwa zaidi’ Kenya na Rwanda
Chanzo cha picha, AFP
Peter Mwangangi
BBC Swahili, Nairobi
Kwa upande wake, Kenya inapanga
kusoma bajeti ya $37.2 bilioni (Kes 4.84 trilioni) ambayo ni kubwa zaidi kuwahi
kuwasilishwa nchini humo. Katika mwaka wa kifedha uliopita, bajeti ya taifa
hilo ilikuwa ya dola $33 bilioni.
Sekta ambazo zinaratajiwa kunufaika
na ongezeko katika bajeti hii ni huduma za usalama wa ndani na ulinzi wa taifa,
idara ya ujasusi, pamoja na sekta za nishati, elimu, afya na maji.
Hata hivyo katika vikao vya umma na
pia mitandaoni, kumekuwa na maswali kuhusu iwapo taifa hilo kweli linahitaji
bajeti kubwa kiasi hicho.
Rwanda nayo inatarajiwa kutangaza
bajeti ya $5.4 bilioni (Rwf 7.8 bilioni), ambayo ni ongezeko la asilimia 12%
kutoka kwa bajeti ya mwaka uliopita ya $4.8 bilioni.
Bajeti hiyo inatarajiwa kuimarisha
ukuaji wa uchumi wa Rwanda, na asilimia 68% inatarajiwa kufadhiliwa na mapato
ya ndani.
Gharama ya maisha
Bajeti hizi zinawasilishwa wakati
wananchi wakiendelea kukabiliwa na changamoto za kupanda kwa gharama za maisha,
hususan bei ya mafuta kutokana na mzozo wa Mashariki ya Kati, pamoja na uhaba
wa ajira.
Hizi ni baadhi ya kauli za wananchi
tuliozungumza nao jijini Dodoma:
"Suala la mafuta ndio
linalotuumiza sana. Serikali inatupa ahadi ya kila siku kuwa bei itapunguzwa,
lakini hakuna mabadiliko," anasema mkazi mmoja.
Mwingine alisema: "Bajeti
inasomwa lakini matumizi sio mazuri. Hii inapunguza mzunguko wa fedha
mtaani."
Ongezeko la bei ya mafuta
limeshuhudiwa katika mataifa yote ya Afrika Mashariki, hali ambayo imesababisha
kupanda kwa nauli, chakula na gharama za kufanya biashara kwa jumla.
Kodi mpya
Wananchi watakuwa makini kuona ni
mapendekezo gani ya kikodi ambayo yatatolewa na serikali za kila nchi ili
kufadhili bajeti hizo, na yatakuwa na athari gani kwao.
Tanzania na Rwanda tayari zimesema
zitalenga mapato ya ndani zaidi kufadhili bajeti zao – na wengi wanasubiri
kuona ni maeneo gani ambayo yataguswa zaidi.
Nchini Kenya, bajeti huambatana na
mswada wa fedha unaoelezea jinsi bajeti hiyo itakavyofadhiliwa kupitia kodi,
mikopo na njia nyinginezo. Wananchi wamekuwa wakitoa maoni kuhusu mapendekezo
ya mwaka huu, ambapo baadhi yamezua mjadala kama vile ushuru wa simu za
mkononi, miamala ya fedha na mamlaka ya shirika la ukusanyaji ushuru KRA.
Polisi wa China wamkamata mtu mmoja baada ya video za mateso kwa mbwa kuzua hasira mtandaoni
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mamlaka nchini China zimemkamata mwanaume aliyesababisha hasira kubwa miongoni mwa umma kwa madai ya kuwatesa mbwa na kurekodi ukatili huo ili kuuza video hizo mtandaoni.
Mwanaume huyo anadaiwa kujifanya kuwa mtu mwenye shauku ya kuasili wanyama, lakini baadaye aliwafanyia ukatili paka na mbwa kadhaa aliowachukua.
Vitendo vyake vilifichuliwa baada ya rafiki wa mwanamke aliyekuwa ameweka watoto wa mbwa kwa ajili ya kuasili kusimulia matendo hayo mtandaoni.
Zaidi ya watu 100 walikusanyika nje ya nyumba ya mwanaume huyo mapema wiki hii katika mji wa Chongqing kusini-magharibi mwa China wakipinga matendo yake.
Polisi hawajafichua ni kosa gani hasa mwanaume huyo anachunguzwa nalo. Ukatili dhidi ya wanyama kwa sasa si kosa linaloadhibiwa kisheria nchini China. Hata hivyo, uelewa kuhusu ustawi na haki za wanyama umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni.
Mwanaume huyo, anayejulikana kwa jina la ukoo la Li, aliweka tangazo kwenye Douyin mapema mwezi huu akisema kuwa anataka kuasili mbwa bila malipo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya eneo hilo, alidai kwamba watoto wake wawili "waliwapenda sana watoto wa mbwa."
Siku ya Jumapili, wanaharakati wa kundi la kutetea haki za wanyama waligundua mmoja wa watoto wa mbwa waliokuwa wameasiliwa akiwa ametupwa kwenye ngazi za jengo analoishi Li. Mbwa huyo alikuwa na mguu uliovunjika, mkia uliokatwa na kichwa kilichovimba.
Video zilizosambazwa mtandaoni zinaonesha zaidi ya watu 100 wakikusanyika nje ya nyumba yake, huku baadhi yao wakibeba mabango ya kupinga vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya wanyama.
Trump asema atasitisha mashambulizi baada ya ombi la Iran
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa mashambulizi dhidi ya Iran "yataisha hivi karibuni" baada ya ombi kutoka Iran.
Kwa mujibu wa taarifa iliyoripotiwa na Fox News Trump alisema katika mahojiano kwamba aliamuru kusitishwa kwa mashambulizi mapya dhidi ya Iran baada ya kupokea "simu ya moja kwa moja kutoka Iran" na ombi kutoka kwa afisa mwandamizi wa Iran.
Hata hivyo, vyombo vya habari rasmi vinavyohusishwa kwa karibu na jeshi la mapinduzi ya Iran vimekanusha madai hayo hadharani, vikisema kuwa ni "uongo" kwamba Iran iliomba mashambulizi hayo yasitishwe.
Mwandishi wa Fox News pia alisema kuwa Trump alieleza katika mahojiano hayo kwamba mashambulizi yaliyofanyika ndani ya Iran yalihusisha makombora ya aina ya Tomahawk, yaliyolenga rada za ulinzi, vituo vya ulinzi na mifumo ya kuongozea ndege zisizo na rubani za Iran.
Mashambulizi hayo yanaripotiwa kufanyika ndani ya Iran, kilomita chache kutoka mji mkuu, Tehran.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa Iran kukataa makubaliano yaliyopendekezwa na Marekani, Trump alijibu:
"Iwapo watafanya hivyo, watashambuliwa tena kwa mabomu."
Kauli hizi zinaonesha kuendelea kwa mvutano mkubwa kati ya Marekani na Iran, huku pande zote zikitoa taarifa zinazokinzana kuhusu mawasiliano na juhudi za kusitisha mashambulizi.
Siku ya Bajeti Afrika Mashariki: Bajeti ‘ya kipekee’ Tanzania
Chanzo cha picha, BANK OF TANZANIA
Peter Mwangangi
BBC Swahili, Nairobi
Mawaziri wa fedha kutoka nchi za Afrika Mashariki wanatarajiwa kuwasilisha makadirio ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2026/2027 leo Alhamisi (Juni 11), wakiangazia mipango ya matumizi na mapato ya nchi zao, pamoja na vipaumbele vya kila taifa katika juhudi za kukuza uchumi na kuimarisha maisha ya wananchi.Wananchi watarajie nini? Haya ni mambo matano yanayojitokeza kufikia sasa.
Tanzania imeahidi kuwa hii itakuwa bajeti ya ‘kipekee’, ikiwa ya kwanza katika awamu ya pili ya rais Samia Suluhu Hassan madarakani kufuatia uchaguzi wa mwaka uliopita.Waziri wa fedha Khamis Mussa Omar amesema kuwa bajeti ya $23.8 bilioni (Tsh 62.3 trilioni) itakayosomwa bungeni Dodoma itafadhiliwa zaidi na mapato ya ndani zaidi, huku serikali ikipunguza utegemezi wa misaada ya nje."
Kwa bajeti ya mwaka unaofuata, sehemu ya matumizi ambayo itagharamiwa na mapato ya ndani itakuwa ni asilimia 70% ambayo ni kiwango cha juu zaidi ya kiwango cha mwaka wa sasa wa kifedha unaomalizika.
Nayo misaada kutoka nje haitafika hata Tsh trilioni moja kwenye bajeti hiyo ya Tsh 62.3 trilioni," alisema Waziri Khamis Mussa katika kikao na waandishi wa habari jijini Dodoma, siku moja kabla ya kuwasilishwa kwa makadirio ya bajeti bungeni.
Maeneo makuu ya kipaumbele mwaka huu nchini humo yatakuwa miradi ya maendeleo ya kimkakati kama kuendeleza mradi wa reli ya kisasa (SGR), barabara, uwekezaji katika sekta za nishati na sekta nyinginezo ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Bill Gates ajutia kukutana kwake na Jeffrey Epstein
Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanzilishi wa Microsoft Bill Gates, amesema kuwa Jeffrey Epstein alitaka kuwa na uhusiano wa karibu wa binafsi naye.
Gates alisisitiza kwamba hakuwahi kumdhuru au kumtumia vibaya mtu yeyote, huku akikabiliwa na maswali kutoka kwa kamati ya Bunge la Marekani inayochunguza uhusiano kati ya Epstein, aliyetuhumiwa kwa makosa ya kingono na watu matajiri na wenye ushawishi, akiwemo yeye mwenyewe.
Katika taarifa iliyoandaliwa mapema na kuchapishwa kwenye tovuti yake binafsi, Gates alisema hajawahi kutembelea kisiwa cha Epstein, mashamba yake, wala nyumba yake iliyoko Florida.
Aliongeza kuwa hakuwahi kuona dalili zozote kwamba Epstein alikuwa akijihusisha na shughuli za uhalifu.
Bilionea huyo ameeleza tena majuto yake kuhusu mikutano aliyokuwa nayo na Epstein, akiitaja kuwa "kosa kubwa la maamuzi". Alisisitiza kuwa mikutano yao ilihusu tu majadiliano kuhusu misaada na ufadhili wa shughuli za hisani kupitia taasisi yake ya kutoa misaada.
Trump asema ‘anapenda mfumuko wa bei’ wakati bei nchini Marekani zikiongezeka kwa kasi kubwa
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa "anapenda mfumuko wa bei" baada ya bei nchini Marekani kupanda mwezi uliopita kwa kasi kubwa zaidi katika kipindi cha miaka mitatu.
Takwimu za Bureau of Labor (BLS) zilionesha kuwa bei ziliongezeka kwa asilimia 4.2 mwezi Mei ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Hili ni ongezeko kutoka asilimia 3.8 mwezi Aprili. Kuongezeka huko kulichangiwa na kupanda kwa gharama za nishati kufuatia vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
"Ninapenda. Takwimu zilikuwa nzuri. Mnajua ninachopenda zaidi? Ninapenda mfumuko wa bei," Trump alisema akiwa Ikulu ya Marekani.
Hata hivyo, aliahidi kuwa bei hizo zinazopanda "zitashuka kwa kasi kubwa" mara tu vita na Iran vitakapomalizika. Baadaye siku hiyo, jeshi la Marekani lilifanya mashambulizi ya anga dhidi ya Iran.
Akizungumzia takwimu za mfumuko wa bei siku ya Jumatano, rais huyo alisema vikosi vya Marekani vilifanya operesheni za usiku na kuchukua "mamilioni ya mapipa" ya mafuta kutoka Iran, jambo ambalo alisema limechangia kushuka kidogo kwa bei za mafuta.
"Mgogoro huu ukimalizika... mtashuhudia bei ya mafuta ikishuka na kurudi katika kiwango ilichokuwa kabla ya vita," aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani.
Trump pia alirejelea safari yake katika jimbo la Iowa mapema mwaka 2026, akisema aliona petroli ikiuzwa kwa dola 1.85 kwa galoni moja, na kuongeza kuwa "tutarudi kwenye viwango hivyo hivi karibuni."
Hata hivyo, bei ya mafuta ghafi ya aina ya Brent crude bado inaendelea kuuzwa kwa kiwango cha juu zaidi ikilinganishwa na bei zilizokuwepo kabla ya vita kuanza.
Tetesi za soka Alhamisi:Arsenal yamuwinda Williams
Chanzo cha picha, Getty Images
Arsenal bado inaendelea kuweka juhudi katika mbio za kumsajili Nico Williams, winga wa Athletic Club na timu ya taifa ya Hispania mwenye umri wa miaka 23.
Liverpool, Manchester City na Manchester United pia zinaonyesha nia ya kumsajili.
Juventus ipo kwenye mazungumzo na Aston Villa kwa ajili ya kumsajili mlinda lango wa Argentina Emiliano Martinez (33), ambaye anaripotiwa tayari amekubaliana masharti binafsi.
Paris Saint-Germain inatarajia kujaribu kumsajili mshambuliaji wa Ufaransa Michael Olise (24) kutoka Bayern Munich msimu huu wa kiangazi.
Manchester United inamfuatilia mshambuliaji wa Senegal Iliman Ndiaye (26) wa Everton huku ikitafuta kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya kurejea kwenye UEFA Champions League msimu ujao.
Liverpool iko tayari kumuuza mshambuliaji wa Italia Federico Chiesa (28) kwa takribani pauni milioni 17, huku mchezaji huyo akipendelea kurejea katika ligi ya Italia, Serie A.
Barcelona inafahamu kuwa Chelsea na Arsenal zinamuwania winga wa Hispania Dani Olmo (28), lakini haitamruhusu kuondoka isipokuwa thamani yake ya pauni milioni 60 ilipwe.
Mshambuliaji wa Ufaransa Mathys Tel (21) anaweza kufanya uhamisho wa kushangaza kutoka Tottenham Hotspur kwenda AFC Bournemouth msimu huu wa kiangazi.
Barcelona inapanga kumuuza kiungo wa Hispania Marc Casado (22) ili kupata fedha za kufanya usajili mwingine. Bayer Leverkusen pamoja na vilabu vya Ligi Kuu ya England vinamfuatilia.
Leeds United inataka kuvunja rekodi yake ya usajili kwa kumsajili mlinzi wa Ivory Coast Ousmane Diomande kutoka Sporting CP kwa dau linaloweza kufikia pauni milioni 35 pamoja na nyongeza ya pauni milioni 8.
Crystal Palace inajiandaa kushindana na Everton katika mbio za kumsajili kiungo wa England Hayden Hackney (23) kutoka Middlesbrough kwa ofa ya pauni milioni 20.
Tehran yalenga kambi za Marekani katika nchi za Ghuba baada ya majeshi ya Marekani kuanzisha mashambulizi mapya
Chanzo cha picha, US Central Command
Iran imeshambulia kambi za kijeshi za Marekani katika eneo la Ghuba kulipiza kisasi duru ya hivi karibuni ya mashambulizi ya Marekani, yaliyokuja baada ya Donald Trump kusema kwamba ataishambulia Iran “kwa nguvu kubwa”.
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema imekamilisha siku ya pili mfululizo ya mashambulizi ya “kujilinda”, yaliyofanyika usiku mmoja baada ya Trump kusema kwamba Tehran ilikuwa imechukua “muda mrefu sana kufikia makubaliano” ya kumaliza vita.
Kwa kujibu, Iran ilisema imeshambulia vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Bahrain na Kuwait, ambayo ni malengo yale yale yaliyolengwa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyofanywa na Iran siku iliyotangulia.
Kuongezeka huku kwa mashambulizi ya kulipizana kisasi katika siku za hivi karibuni kumefanya juhudi za makubaliano ya usitishaji kuwa dhaifu kati ya nchi hizo mbili.
Baada ya shambulio la hivi karibuni la Marekani, milipuko ilisikika katika miji ya kusini mwa Iran karibu na Mlango bahari wa Hormuz, ambapo vikosi vya Marekani pia vilishambulia mifumo ya ulinzi wa anga, rada na maeneo mengine katika duru ya awali ya mashambulizi.
Katika ongezeko hili jipya la mzozo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) pia lilisema limepiga meli mbili za kubeba mafuta zilizokuwa zikivuka Mlango wa Hormuz, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Iran, ingawa hakukuwa na uthibitisho wa haraka kutoka vyanzo huru.
Hii ilikuja baada ya vyombo vya habari vya serikali ya Iran kuripoti kwamba Mlango bahari wa Hormuz ulikuwa “umefungwa kabisa kwa aina zote za meli”. Hata hivyo, CENTCOM ilisema kwamba “meli za kibiashara zinaendelea kupita kuingia na kutoka katika Mlango wa Hormuz”.
Bei za mafuta zilipanda muda mfupi baada ya kutangazwa kufungwa kwa njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa baharini na baada ya taarifa za shambulio dhidi ya meli hizo kutolewa.