Viongozi 5 wanaolipwa mishahara mikubwa zaidi duniani

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Tangazo la ongezeko kubwa la mshahara wa Waziri Mkuu wa Singapore, Lawrence Wong, limeibua mjadala kuhusu kiasi ambacho viongozi wa kisiasa hulipwa katika nchi mbalimbali duniani.

Kuanzia Oktoba 15, 2026, mshahara wa mwaka wa Wong utaongezeka kwa asilimia 64, kutoka dola za Singapore milioni 2.2 hadi milioni 3.6, sawa na takriban dola milioni 2.85 za Marekani. Hii inamfanya kuwa kiongozi wa kisiasa anayelipwa zaidi duniani.

Wong amesema suala la mishahara ya viongozi ni nyeti nchini Singapore, lakini serikali inatetea mfumo huo kwa kusema mishahara mikubwa husaidia kuvutia watu wenye uwezo mkubwa kuingia kwenye siasa na kupunguza vishawishi vya rushwa.

Hata hivyo, ongezeko hilo limekosolewa na baadhi ya wananchi, hasa wakati Singapore ikikabiliwa na gharama za maisha na wasiwasi kuhusu ajira. Wong amesema ataongeza mchango wake kwa jamii kwa kutoa ongezeko lote la mshahara wake kwa mashirika ya hisani kwa kipindi cha miaka mitano.

Lakini Wong si kiongozi pekee anayelipwa kiasi kikubwa. Tukitazama viongozi wengine wakubwa wa kisiasa duniani, tofauti ya mishahara yao na ile ya watu wa kawaida ni kubwa sana. Hawa ndio viongozi watano wanaoongoza katika orodha hii.

5. Donald Trump – Marekani

Rais wa Marekani, Donald Trump, hupokea mshahara wa dola 400,000 kwa mwaka. Kiasi hicho kimewekwa kisheria nchini Marekani na hakijabadilika tangu mwaka 2001. Rais pia anaweza kupata posho ya matumizi ya kikazi ya dola 50,000 kwa mwaka, lakini hiyo si sehemu ya mshahara wake wa msingi.

Kwa kutumia makadirio ya sasa ya dola moja kuwa karibu TSh2,647, mshahara wa Trump ni takriban TSh1.06 bilioni kwa mwaka ni kama TSh83mil kwa mwezi

Hiyo ni sawa na kujenga takriban madarasa 53 ya kisasa kwa mwaka ama madarasa manne kwa mwezi, kama kila darasa lingekuwa na thamani ya TSh20 milioni.

Au kwa bei ya TSh3 milioni kwa bodaboda mpya, mshahara huo ungeweza kununua takriban bodaboda 353.

Kwa bei ya TSh4,000 kwa kilo ya sukari, ni sawa na takriban kilo 265,000 za sukari.

Na kama nyumba ya kawaida ya kisasa kijijini inagharimu TSh25 milioni, kiasi hicho kingeweza kujenga takriban nyumba 42.

4. Anthony Albanese – Australia

Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese, anapokea takriban dola 622,110 za Australia kwa mwaka, kulingana na mfumo wa malipo unaowekwa na Remuneration Tribunal ya Australia. Mfumo huo wa malipo ulisasishwa mwaka 2026.

Kwa thamani inayotumika katika ulinganisho huu, ni takriban dola 622,110 za Marekani, sawa na karibu TSh1.65 bilioni kwa mwaka.

Kwa fedha hizo, mtu angeweza kujenga takriban madarasa 82 ya kisasa ya TSh20 milioni kila moja.

Au kununua takriban bodaboda 549 za TSh3 milioni.

Kwa bei ya TSh4,000 kwa kilo, ni sawa na kilo zaidi ya 411,000 za sukari.

Na kwa nyumba ya TSh25 milioni, mshahara huo ni sawa na kujenga karibu nyumba 66 za kawaida za kisasa kijijini.

3. Guy Parmelin – Uswisi

Guy Parmelin ndiye Rais wa Shirikisho la Uswisi kwa mwaka 2026. Mfumo wa uongozi wa Uswisi ni tofauti na nchi nyingi, kwa sababu urais huzunguka miongoni mwa wajumbe saba wa Federal Council.

Mshahara wake wa mwaka ni takriban dola 606,000, sawa na karibu TSh1.60 bilioni kwa makadirio ya ubadilishaji huo.

Kwa kiasi hicho, mshahara wa mwaka mmoja ungeweza kujenga takriban madarasa 80 ya TSh20 milioni.

Au kununua karibu bodaboda 535 za TSh3 milioni.

Kwa sukari ya TSh4,000 kwa kilo, ni sawa na takriban kilo 401,000 za sukari.

Na kama nyumba ya kawaida kijijini ni TSh25 milioni, ni sawa na karibu nyumba 64.

2. John Lee Ka-chiu – Hong Kong

Kiongozi wa Hong Kong, John Lee Ka-chiu, anapokea takriban dola 719,000 kwa mwaka, jambo linalomweka katika nafasi ya pili katika orodha hii. Lee amekuwa Chief Executive wa Hong Kong tangu Julai 2022.

Hii ni sawa na takriban TSh1.90 bilioni kwa mwaka.

Kwa fedha hizo, unaweza kufikiria kujenga karibu madarasa 95 ya kisasa yenye thamani ya TSh20 milioni kila moja.

Au kununua takriban bodaboda 634 za TSh3 milioni.

Kwa bei ya TSh3,000 kwa kilo ya mchele, mshahara huo ni sawa na karibu kilo 634,000 za mchele.

Na kwa nyumba ya TSh25 milioni, ni sawa na kujenga takriban nyumba 76 za kawaida za kisasa kijijini.

Lakini kama ungeamua kutumia fedha hizo kujenga nyumba ya thamani ya TSh100 milioni katika maeneo kama Salasala jijini Dar es Salaam, ungeweza kujenga karibu nyumba 19.

1. Lawrence Wong – Singapore

Na namba moja ni Waziri Mkuu wa Singapore, Lawrence Wong.

Kwa sasa Wong anapata takriban dola za Singapore milioni 2.2 kwa mwaka, sawa na karibu dola milioni 1.74 za Marekani. Lakini kuanzia 15 Oktoba 2026, mshahara wake utaongezeka kwa asilimia 64 hadi S$3.6 milioni, sawa na karibu US$2.85 milioni kwa mwaka.

Kwa kutumia kiwango cha ubadilishaji tulichotumia, hiyo ni karibu TSh7.54 bilioni kwa mwaka.

Ili kuiona kwa ukubwa unaoeleweka zaidi, kiasi hicho kingeweza kujenga takriban madarasa 377 ya kisasa ya TSh20 milioni.

Au kununua zaidi ya bodaboda 2,500 za TSh3 milioni.

Kwa bei ya TSh4,000 kwa kilo ya sukari, ni sawa na zaidi ya kilo milioni 1.88 za sukari.

Kwa mchele wa TSh3,000 kwa kilo, ni zaidi ya kilo milioni 2.5 za mchele. Mchele huu unaweza kugawa karibu kilo moja na robo kwa Wazanzibar wote, ama nusu kilo kwa watu wote katika mikoa minne ya Katavi, Njombe, Iringa na Lindi.

Na kama nyumba ya kawaida ya kisasa kijijini ni TSh25 milioni, mshahara huo ungeweza kujenga takriban nyumba 302.

Lakini kwa nyumba ya thamani ya TSh100 milioni katika maeneo kama Salasala, Dar es Salaam, ungeweza kujenga takriban nyumba 75 kwa mshahara wa mwaka mmoja.

Hivyo, ongezeko la mshahara wa Wong linamfanya kuwa mbali zaidi na viongozi wengine wakuu duniani kwa kiwango cha mshahara. Viongozi wa Afrika hawajatajwa kwneye orodha hii, huenda wasiwe na mishahara rasmi yenye kiwango hiki lakini marupurupu na magendo mengine yakawaweka juu.