Katiba mpya au Katiba ya aina gani? Kauli ya Nchimbi ilivyohamisha mjadala

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Kwa zaidi ya muongo mmoja, mjadala kuhusu Katiba mpya nchini Tanzania umekuwa ukijikita katika swali la kama mchakato ulioanza mwaka 2011 unapaswa kufufuliwa na kukamilishwa. Lakini kauli ya Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi, imeonekana kuhamisha mjadala huo kutoka kwenye swali la 'iwapo' kwenda kwenye 'namna ambayo Katiba hiyo inapaswa kupatikana na kuwa.

Katika hotuba yake wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa 15 wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) juma lililopita, Dkt. Nchimbi hakuwataka Watanzania kupambania Katiba mpya pekee. Aliitaja pia aina ya Katiba anayosema taifa linahitaji- Katiba yenye makubaliano ya wadau wote, muafaka wa kitaifa, inayoheshimu haki za wananchi na inayoweza kuliongoza taifa kwa miongo ijayo.

Kauli hiyo imekuja wakati Serikali tayari imesema mchakato wa Katiba mpya utaendelezwa kabla ya mwaka 2030, huku Ilani ya Uchaguzi ya chama tawala, CCM ya mwaka 2025 pia ikiweka ahadi ya kuendeleza mchakato huo. Kwa mtazamo huo, hoja ya kama Katiba mpya inahitajika haionekani tena kuwa ndiyo kiini cha mjadala.

Badala yake, mjadala ulioibuka baada ya kauli ya Makamu wa Rais umeanza kuzunguka maswali mengine: ikiwa viongozi wa juu wa nchi wanasema wanaunga mkono Katiba mpya, kwa nini wananchi waambiwe waipambanie? Na ikiwa mchakato utaendelea, je, utazaa Katiba ambayo itakubalika kwa makundi mbalimbali ya Watanzania?

Maswali hayo ndiyo yameifanya kauli ya Dkt. Nchimbi isiwe tamko la kisiasa pekee, bali mwanzo wa mjadala mpana kuhusu mazingira ya sasa ya kisiasa, mchakato wa kuandika Katiba na aina ya Katiba ambayo Tanzania inaweza kuipata.

Kutoka 'tunaitaka' hadi 'itapatikanaje?

Kauli ya Dkt. Nchimbi imeibua mjadala kwa sababu imekuja katika kipindi ambacho hoja ya Katiba mpya tayari imo katika ajenda ya Serikali na chama tawala. Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa mchakato huo utafufuliwa kabla ya mwaka 2030, huku Dkt. Nchimbi akisema tafiti zilizotumika wakati wa kuandaa Ilani ya CCM, pamoja na mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai na Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2025, zinaonesha kuwa wananchi wanataka Katiba mpya.

Kwa mazingira hayo, baadhi ya wachambuzi wanaona kwamba kauli ya Makamu wa Rais haijafungua mjadala kuhusu umuhimu wa Katiba mpya, bali imeuhamisha kwenda hatua nyingine. Hilo linaonekana pia katika maelezo yake aliposisitiza kuwa Katiba inayohitajika ni ile "yenye makubaliano ya wadau wote" na "muafaka katika taifa," kauli iliyoweka msisitizo kwenye maudhui na uhalali wa mchakato, badala ya uwepo wa Katiba mpya pekee.

Mwandishi mkongwe Ansbert Ngurumo anaona uzito wa kauli hiyo unatokana na nafasi ya aliyeitoa. Kwa mtazamo wake, hakuna ubaya kwa Makamu wa Rais kulizungumzia suala la Katiba mpya, na hilo linaweza kuashiria kwamba hoja ambayo hapo awali ilionekana kuwa ya upinzani au ya wanaharakati sasa inazungumzwa wazi na mmoja wa viongozi wakuu wa Serikali kwa namna ya 'kupambania'. Hata hivyo, anasema wapo pia wanaoiona kauli hiyo kama sehemu ya mkakati wa kisiasa kutokana na mazingira ambayo imetolewa.

Lakini historia ya mchakato wa Katiba mpya ndiyo inayofanya mjadala huu uwe na uzito zaidi. Mwaka 2011, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba ilikusanya maoni ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania. Rasimu iliyotokana na maoni hayo iliwasilishwa katika Bunge Maalum la Katiba, ambako tofauti za kisiasa kuhusu baadhi ya mapendekezo ziliibuka na hatimaye kura ya maoni 'ikafa kibudu'. Tangu wakati huo, swali la kama mchakato utaanza tena limekuwa likijitokeza mara kwa mara.

Huenda ndiyo maana kauli ya Dkt. Nchimbi imeonekana kubadili mwelekeo wa mjadala. Badala ya kuibua hoja mpya kuhusu hitaji la Katiba mpya, imefanya mjadala uanze kuangalia zingine pamoja na msukumo mwingine, ikiwa mazingira ya sasa yanaweza kuruhusu mchakato utakaowezesha kupatikana kwa Katiba ambayo itakubalika kwa upana wa kutosha.

"Tupambane" na nani?

Ikiwa kuna neno moja lililotawala mjadala baada ya hotuba ya Dkt. Nchimbi, basi ni "kupambana." Wakati wito wa kupatikana kwa Katiba mpya ulionekana kukubalika kwa kiasi kikubwa na wadau wengi, tafsiri ya neno hilo ndiyo iliyozua maswali mengi. Je, "kupambana" kulimaanisha kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika mchakato wa Katiba, au kulikuwa na kikwazo ambacho wananchi wanapaswa kukishinda ili Katiba hiyo ipatikane?

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila, anasema kinachohitajika sasa ni vitendo zaidi ya kauli. Kwa mtazamo wake, mjadala kuhusu Katiba mpya umedumu kwa muda mrefu, hivyo kilichobaki ni kuona hatua za utekelezaji.

Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, kwake swali ni la moja kwa moja na liko wazi zaidi. Ikiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema anataka Katiba mpya na Makamu wa Rais pia anasema hivyo, basi ni nini kinachozuia mchakato huo kuendelea? Kwa mtazamo wake, ikiwa viongozi wakuu wa Serikali na chama tawala wana msimamo unaofanana kuhusu suala hilo, hakuna sababu ya wananchi kuambiwa "wapambane" ili kupata jambo ambalo tayari viongozi wanasema wanaliunga mkono.

Maswali yanayofanana yanaibuliwa pia na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dkt. Benson Bagonza. Anahoji kwamba ikiwa hitaji la Katiba mpya ni sehemu ya msimamo wa Serikali na limejumuishwa katika Ilani ya CCM, basi wananchi wanapaswa kupambana na nani ili kuipata? Kwa mtazamo wake, kauli ya Dkt. Nchimbi imeibua maswali mapya kuhusu mchakato huo, badala ya kutoa ufafanuzi wa namna utakavyotekelezwa.

Lakini ndani ya CCM, kauli ya Nchimbi ikaleta na kubebwa na tafsiri mbalimbali. Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi ya CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Rajabu Maganya, anasema hakuna aliyesema mchakato wa Katiba mpya umesitishwa au hautafanyika. Kwa mujibu wake, utekelezaji wa ahadi hiyo tayari umo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM na mchakato wake hauwezi kukamilika ndani ya kipindi kifupi. Kwa mtazamo huo, kauli ya Dkt. Nchimbi haipaswi kutafsiriwa kama ishara kwamba kuna anayezuia Katiba mpya, bali kama msisitizo wa umuhimu wa kuendelea na mchakato uliokwisha kuahidiwa.

Tofauti hizo za mitazamo zinaonyesha kwamba mjadala hauko tena katika swali la iwapo Tanzania inahitaji Katiba mpya. Badala yake, unaonekana kuelekea kwenye maswali yanayohusu uaminifu wa mchakato, kasi ya utekelezaji na wajibu wa kila upande katika kuhakikisha ahadi hiyo inafikiwa. Hapo ndipo neno "kupambana" limepata tafsiri tofauti, kwa baadhi likiwa wito wa kuongeza shinikizo la wananchi, na kwa wengine likiwa wito wa kuendelea kushiriki katika mchakato ambao tayari umewekwa kwenye ajenda ya taifa.

Katiba mpya au Katiba ya aina gani?

Kauli ya Dkt. Nchimbi imeonekana pia kuhamisha mjadala kwenye hoja ambayo imekuwa ikijitokeza kila suala la Katiba mpya linaporejea: je, mafanikio yatakuwa ni kupatikana kwa Katiba mpya pekee, au kupatikana kwa Katiba ambayo itakubalika kwa upana wa kutosha? Tofauti hiyo si ndogo. Inaakisi mjadala uliowahi kujitokeza wakati wa mchakato wa kwanza wa Katiba mpya, ambapo pamoja na kukusanywa kwa maoni ya wananchi na kuandaliwa kwa Rasimu ya Jaji Joseph Warioba, hatua zilizofuata ziliibua tofauti kubwa kuhusu maudhui ya Katiba na namna ya kuifikia.

Ndiyo maana baadhi ya wachambuzi wanaona kuwa kauli ya Dkt. Nchimbi haipaswi kutazamwa kupitia maneno "Katiba mpya" pekee, bali kupitia maelezo aliyoyatoa kuhusu sifa za Katiba hiyo. Alizungumza kuhusu Katiba "yenye makubaliano ya wadau wote", "yenye muafaka katika taifa", inayoheshimu haki za wananchi na inayoweza kuliongoza taifa kwa miongo ijayo. Kwa mtazamo huo, uzito wa kauli yake hauko kwenye wito wa kupata Katiba mpya, bali kwenye aina ya Katiba aliyosema Watanzania wanapaswa kuipambania.

Hilo ndilo ambalo mwandishi mkongwe Ansbert Ngurumo analiona kuwa swali muhimu zaidi. Kwa mtazamo wake, hofu ya wengi si kwamba Tanzania inaweza kukosa Katiba mpya, bali kwamba inaweza kupata Katiba ambayo haitajenga maridhiano ya kitaifa. "Kuna uwezekano mkubwa tukapata Katiba mpya lakini Katiba ya hovyo," amesema.

Anaongeza kuwa ili Katiba iweze kudumu na kukubalika, ni lazima kila upande ujione umepata jambo fulani na pia umekubali kuachia jambo fulani kwa ajili ya maslahi mapana ya taifa.

"Ni lazima tuhakikishe kuna kundi linapata lakini linapoteza, lakini kundi lingine vile vile linapoteza lakini linapata, tusipokubaliana hivyo hakuna katiba mpya". Kwa maoni yake, muafaka ndiyo unaoweza kuifanya Katiba hiyo iwe ya Watanzania wote badala ya kuwa ya upande mmoja.

Lakini swali la kama mazingira ya sasa yanaweza kuzalisha muafaka huo linaendelea kujadiliwa. Wakati Serikali ikisisitiza kuwa mchakato wa Katiba mpya utaendelea kama ulivyoahidiwa, baadhi ya vyama vya upinzani vinaendelea kueleza wasiwasi kuhusu mazingira ya kisiasa, vikitaja kukamatwa kwa baadhi ya viongozi na wanachama wao pamoja na changamoto nyingine wanazodai zinaathiri uwanja wa kisiasa.

Serikali imekuwa ikisema hatua hizo zinachukuliwa kwa mujibu wa sheria na si kwa misingi ya kisiasa. Hali hiyo inaonyesha kuwa pamoja na kuwepo kwa kauli zinazounga mkono Katiba mpya, bado kuna mjadala kuhusu mazingira yanayoweza kujenga imani miongoni mwa wadau watakaoshiriki mchakato huo.

Huenda hapo ndipo mchango mkubwa wa kauli ya Dkt. Nchimbi ulipo. Badala ya kurejesha tu mjadala wa Katiba mpya, umehamisha uzito wa hoja kutoka kwenye swali la "Je, Tanzania inahitaji Katiba mpya sasa?" kwenda kwenye maswali yanayoonekana kuwa magumu kwa baadhi ya watu: Katiba hiyo itapatikanaje? Itajengwa juu ya maridhiano ya kiwango gani? itakuwa ya watanzania au ya vyama vya siasa, itajali maoni ya watanzania au ya wanasiasa wachache? Na je, mazingira ya sasa yanaweza kuwezesha kupatikana kwa Katiba ambayo, kama alivyosema Dkt. Nchimbi, "kila Mtanzania atajivunia" kwa sababu itakuwa imejengwa juu ya makubaliano ya wadau wote?