Eda ni nini? Je, Rais Samia kuendelea kuongoza akiwa eda?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Kifo cha Hafidh Ameir, mume wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, kimeibua maswali kuhusu kipindi ambacho mwanamke Mwislamu huingia baada ya kufiwa na mume wake.

Kipindi hicho kinachojulikana kama eda kina masharti gani, huchukua muda gani na kinatofautianaje na maombolezo ya kawaida?

Na je, mwanamke akiwa katika eda anaweza kuendelea na kazi na majukumu yake ya kila siku?

Swali hilo linapata uzito zaidi linapomhusu mwanamke mwenye wadhifa mkubwa wa umma, kama Rais wa nchi ambaye ni Mwislam. Je, Eda ni nini? Je, rais Samia kuendelea kuongoza akiwa eda?

BBC Swahili imeangalia Qur'an, hadithi na maelezo ya wanazuoni mbalimbali kuhusu eda, masharti yake na maisha ya mjane katika kipindi hicho.

Eda ni nini?

Eda, au iddah kwa Kiarabu, ni kipindi ambacho mwanamke anatakiwa kusubiri baada ya kuvunjika kwa ndoa au kufiwa na mume kabla ya kuingia katika ndoa nyingine. Kwa mjane ambaye si mjamzito, Qur'an katika Surah Al-Baqarah 2:234 inaweka kipindi cha miezi minne na siku 10. Katika kipindi hicho, mwanamke hawezi kuolewa tena.

Sheria hii inamhusu mjane bila kujali umri wake wala cheo chake. Lakini suala la ujauzito lina mitazamo tofauti katika vyanzo mbalimbali.

Sheikh Ahmad Kutty, Mhadhiri Mwandamizi na mwanazuoni wa Kiislamu kutoka Taasisi ya Kiislam ya Toronto, Canada, anaeleza kuwa eda ya mjane mjamzito huendelea hadi kujifungua. Kwa upande mwingine, Sayyid Ali Al-Husseini Al-Sistani, mwanazuoni mashuhuri wa Kishia kutoka Iraq, anaeleza kuwa ikiwa mtoto atazaliwa kabla ya kutimia kwa miezi minne na siku 10, mjane huendelea kusubiri hadi muda huo utimie. Wanazuoni wengine wa Afrika Mashariki wanakubaliana kwenye hili.

Eda v Kuomboleza

Kuna mtazamo wa kijamii unakanganya wakati mwingine kuhusu Eda na kuomboleza. Kiislamu hivi ni vitu viwili tofauti, vinavyoweza kushabihiana kwa namna ndogo.

Eda yenyewe ni kipindi cha kusubiri kilichowekwa na sheria ya Kiislamu baada ya kifo cha mume, wakati kuomboleza kunahusu namna ya kuonyesha huzuni na kujizuia katika mambo fulani baada ya msiba.

Sheikh Ahmad Kutty anaeleza kuwa mjane katika kipindi hiki anatakiwa kuepuka mambo ya kujifurahisha na kujipamba, kama sehemu ya maombolezo yanayoambatana na eda. Shaykh Haytham Tamim, mwanazuoni wa Kiislamu, anaeleza kuwa kwa ujumla Uislamu hauweki kipindi kirefu cha maombolezo kwa kila msiba. Kwa mwanamke aliyefiwa na mume, hata hivyo, kuna kipindi maalumu cha miezi minne na siku 10, wakati maombolezo yanaweza kukamilika katika siku tatu tu.

Hivyo, kuwa katika eda hakumaanishi kwamba mwanamke anapaswa kusimamisha maisha yake yote au kukaa katika hali ya huzuni isiyokoma. Kuna masharti maalumu yanayohusu kipindi hicho.

Masharti ama sheria 7 za eda

Sheikh Ahmad Kutty anaeleza mambo saba muhimu yanayohusiana na eda ya mjane. Miongoni mwa masharti hayo ni muda wa eda, kujiepusha na mapambo na namna mwanamke anavyoweza kuendelea na shughuli zake.

1. Eda huchukua miezi minne na siku 10

Kwa mjane ambaye si mjamzito, kipindi cha eda ni miezi minne na siku 10, hii ni kwa mujibu wa Qur'an katika Surah Al-Baqarah 2:234.

2. Ujauzito una masharti yake

Kwa mujibu wa Sheikh Ahmad Kutty, mjane mjamzito huendelea na eda hadi kujifungua.

Sayyid Al-Sistani ana mtazamo wenye tofauti katika hali ambayo mtoto anazaliwa kabla ya miezi minne na siku 10 kutimia. Anaeleza kuwa mjane huyo huendelea kusubiri hadi kipindi hicho kitimie.

3. Hawezi kuolewa wakati wa eda

Mwanamke aliye katika eda ya kufiwa na mume hawezi kuingia katika ndoa nyingine hadi kipindi hicho kiishe.

Hili ni miongoni mwa masharti yaliyo wazi katika Qur'an na katika maelezo ya wanazuoni kuhusu eda.

4. Anaepuka kujipamba

Mwanamke katika eda anatakiwa kujiepusha na mapambo yanayolenga kumremba au kumfanya avutie hasa wanaume.

Sheikh Ahmad Kutty anataja mambo kama vipodozi, manukato, vito na mavazi ya kujipamba. Sayyid Al-Sistani pia anasema mwanamke aliye katika eda ya kufiwa haruhusiwi kufanya mambo yanayohesabiwa kuwa mapambo, au kuvaa mavazi ya kujipamba.

5. Si lazima avae nguo nyeupe

Hakuna katika vyanzo hivi sheria inayomtaka mjane kuvaa nguo nyeupe kwa kipindi chote cha eda.

Kinachozingatiwa ni kujiepusha na mapambo. Hivyo, rangi ya nguo yenyewe si sharti la eda.

6. Anaweza kutoka kwa mahitaji

Eda haimaanishi kwamba mwanamke haruhusiwi kabisa kutoka nyumbani.

Sheikh Ahmad Kutty anaeleza kuwa mjane anaweza kutoka kwa mahitaji muhimu, kama kwenda kazini, kupata matibabu au kununua mahitaji ya nyumbani, na kurejea nyumbani baada ya shughuli hizo.

Sayyid Al-Sistani pia anaeleza kwamba kutoka nje ya nyumba si haramu kwa mjane aliye katika eda ya kufiwa.

7. Anaweza kuendelea na kazi na shughuli nyingine

Mwanamke anayefanya kazi au anayesoma anaweza kuendelea na shughuli hizo wakati wa eda, kwa mujibu wa maelezo ya Sheikh Ahmad Kutty, huku akizingatia masharti ya kipindi hicho.

Hata masuala ya usafi binafsi hayaachiwi. Kutty anaeleza kuwa mwanamke anaweza kujisafisha na kutumia mafuta ya kawaida, ingawa anapaswa kuepuka manukato na vitu vinavyolenga kujipamba.

Dhana 4 kuhusu eda - ukweli au si kweli?

"Mjane haruhusiwi kutoka nyumbani"

Si sahihi kusema kwamba mwanamke aliye katika eda haruhusiwi kabisa kutoka. Anaweza kutoka kwa mahitaji muhimu, ikiwemo kazi, matibabu na mahitaji ya nyumbani, kwa mujibu wa maelezo ya Sheikh Ahmad Kutty. Sayyid Al-Sistani pia anaeleza kwamba kutoka nje si haramu.

"Lazima avae nguo nyeupe"

Sharti hili halitajwi kama ni lalazima. Kinachotakiwa ni kujiepusha na mapambo, si kuvaa rangi fulani ya nguo.

"Haruhusiwi kuzungumza na wanaume"

Eda haimaanishi kwamba mwanamke anatengwa kabisa na jamii.

Sheikh Ahmad Kutty anaeleza kwamba mwanamke anaweza kuzungumza na wanaume inapohitajika, huku akizingatia mipaka na adabu za mawasiliano kati ya mwanaume na mwanamke asiye mke wake.Ikiwemo kutoshikana mikono ambapo ni sharti la kawaida kwa mwanamke Mwislam.

"Haruhusiwi kujipaka mafuta au kujisafisha"

Hapa kuna tofauti kati ya usafi na kujipamba.

Mwanamke katika eda anaweza kuendelea na usafi wake binafsi. Kinachozuiwa ni matumizi ya vitu vinavyohesabiwa kuwa mapambo au manukato, si usafi wenyewe.

Je, Rais Samia kukaa eda?

Kifo cha Hafidh Ameir Hassan kinazua swali hili; Kwa sababu ni Mwislam, na uislam una weka masharti ya eda, Je, Rais Samia atakaa eda? je, anaweza kuendelea kutekeleza majukumu yake ya urais?

"Rais Samia Suluhu anapaswa, inapowezekana, kuambatana na mtu ambaye haruhusiwi kumuoa, yaani mahrim, katika shughuli zake za kila siku na vikao, ili kupunguza vishawishi. Pia anapaswa kujiepusha na kujipamba kupita kiasi au kuvaa mavazi ya kuvutia. Hata hivyo, majukumu yake ya urais yanaendelea na dini inamruhusu kuyatekeleza akiwa katika eda, ilimradi ajiepushe na mazungumzo yanayohusu uchumba au ndoa katika kipindi hicho," amesema Sheikh Dkt. Hassan Kinywa, mwanazuoni wa Kiislam na Mwenyekiti wa Wataala wa Kiislamu barani Afrika.

Hata hivyo, maelezo ya Sheikh Kinywa na hata Sheikh Ahmad Kutty kuhusu mwanamke anayefanya kazi yanaonyesha kuwa eda yenyewe si sababu ya kusimamisha kazi ama kuacha kuendelea na kazi.

Kwa mujibu wa Kutty, mwanamke anayefanya kazi anaweza kwenda kazini wakati wa eda na kurejea nyumbani baada ya kazi. Hivyo, kuwa katika eda hakumaanishi moja kwa moja kwamba mwanamke hawezi kuwa na shughuli za kikazi.

Lakini kazi ni jambo moja, urais ni suala tofauti. Rais si mfanyakazi wa kawaida; ni wadhifa wa kikatiba unaohusisha mamlaka na majukumu maalumu ya kitaifa.

"Watanzania wanapaswa kumuelewa Rais Samia katika kipindi hiki cha miezi minne na siku kumi. Wakimuona akitembea na mtoto wake au mtu mwingine wa familia, wanapaswa kuelewa kuwa dini inamruhusu kufanya hivyo," amesema mwanazuoni Kinywa.

"Eda haimzuii Rais Samia Suluhu kutekeleza majukumu yake kama Rais, kwa sababu ni wajibu wake wa kikatiba kuongoza nchi. Hata hivyo, anaweza kupunguza safari zinazomhusisha na wanaume wengi au safari za mbali," amesema.

"Dini ya kiislamu imeeleza kuwa kwa kipindi hiki cha eda mjane hafai kutamkiwa maneno ya kumchumbia lakini unaweza kumuonyesha ishara hadi baada ya edda kukamilika.''- Sheikh Kinywa .

Kilicho wazi ni kwamba eda ni kipindi cha kidini chenye masharti yake, lakini haimaanishi moja kwa moja kwamba mjane anaacha kazi na shughuli zote za maisha.