Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Trump asema Marekani na Iran zinakaribia mwafaka
Rais wa Marekani Donald Trump amesema nchi yake inaendelea na mazungumzo na Iran yaliyofikia mahali pazuri, mazungumzo yaliyofanyika siku nzima hapo jana.
Muhtasari
- Tuko katika hatua za mwisho za makubaliano na Oman - Iran
- Guimaraes atua Arsenal, Chalobah, Tomiyasu wako njiani
- Israel yatekeleza mashambulizi kusini mwa Lebanon, licha ya usitishaji mapigano
- WFP : Watu millioni 49 wako katika hatari ya kukumbwa na njaa kali ifikiapo mwaka ujao
- Makubaliano na Oman hayamaanishi Mlango Bahari wa Hormuz utafunguliwa mara moja - Iran
- UN: Watu 56 wamenyongwa Iran kwa mashtaka yanayohusiana na usalama wa taifa
- Wanasayansi wafuatilia athari za roketi ya Space X kugonga mwezi
- Trump: Iran na Marekani zinaendelea na mazungumzo, tumepiga hatua nzuri
- Watu 17 wauawa katika shambulio la Urusi mjini Kyiv
- Asilimia 87 ya wafanyakazi wa Kenya waripoti msongo wa mawazo - Utafiti
- Axio: Iran, Oman na Marekani zakaribia kufikia makubaliano ya kufungua tena Mlango-bahari wa Hormuz
- Vifo vya ajabu vya tembo nchini Kenya vyaibua maswali kuhusu dawa za kuuwa wadudu
- Tazama Video ya droni ya Urusi ikimfukuza mchuuzi nchini Ukraine
- Klabu ya Uturuki Trabzonspor yaanza mazungumzo ya kumsajili Mohamed Salah
- Bei ya mafuta yashuka kufuatia matumaini ya kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz
- Meli ya India yazama baada ya kupigwa kombora karibu na maji ya Yemen
- Bloomberg: Iran inazingatia kuruhusu Ulaya kushiriki katika kuondoa mabomu ya baharini yaliotegwa katika Mlango-bahari wa Hormuz
- CBS: Marekani imetumia karibu akiba yake yote ya makombora ya masafa marefu katika vita dhidi ya Iran
Moja kwa moja
Abdalla Seif Dzungu & Beldeen Waliaula
Tuko katika hatua za mwisho za makubaliano na Oman - Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni wa Iran, Esmail Baghaei, amesema kuwa makubaliano kati ya Iran na Oman yako katika hatua ya mwisho ya kuandaliwa.
Kulingana na Baghaei, mataifa hayo mawili yatatoa taarifa ya pamoja, ambayo itajumuisha mambo muhimu yaliyokubaliwa na pande zote mbili.
Aliongezea kuwa uratibu wa njia ya usafiri wa meli kupitia Mlango Bahari wa Hormuz tayari umekubaliwa na pande zote mbili.
Baghaei alielezea kuwa mazungumzo kati ya Iran na Oman yalikuwa ya kitaalamu na yenye mtazamo wa mbele, akiongeza kuwa iwapo hakutakuwa na kuingiliwa na upande wowote, nchi hizo mbili ziko katika hatua ya mwisho ya kutoa taarifa yao ya pamoja.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa makubaliano kati ya Iran na Oman hayamaanishi kuwa Mlango Bahari wa Hormuz utakuwa salama kwa usafiri wa meli, akidai kuwa sababu zinazoifanya njia hiyo isiwe salama ni kizuizi cha kijeshi cha Marekani baharini na vitisho dhidi ya Iran.
Iran imekuwa ikidai kuwa kuingiliwa na Marekani kumechelewesha kufikiwa kwa makubaliano hayo na imesisitiza kuwa mazungumzo yake na Oman hayahusiani na Marekani.
Mapema leo, Shirika la habari la kitaifa la Iran (IRIB) lilimnukuu afisa mmoja akisema kuwa makubaliano na Oman hayamaanishi Mlango Bahari wa Hormuz utafunguliwa mara moja.
Soma pia:
Guimaraes atua Arsenal, Chalobah, Tomiyasu wako njiani
- Arsenal imefikia makubaliano na Newcastle kuhusu usajili wa nahodha Bruno Guimaraes; Guimaraes amebakiza miaka 2 kwneye mkataba wake wa sasa St James' Park; Arsenal imekubali kutoa £75m kumsajili Mbrazil huyo ambaye amesharuhusiwa kufanya vipimo vya afya. (Skysport)
- Beki wa Japan Takehiro Tomiyasu anatarajiwa kujiunga na Crystal Palace baada ya kufaulu vipimo vya afya jijini London. Anatarajiwa kusaini mkataba ndani ya saa 48 zijazo baada ya kuondoka Ajax kama mchezaji huru msimu huu wa joto. (Fabrizio Romano)
- Chelsea iko katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa Pep Chavarría kutoka Rayo Vallecano. Klabu hizo zinakamilisha maelezo ya mwisho ya ada ya uhamisho inayokadiriwa kuwa euro milioni 19 pamoja na nyongeza mbalimbali kabla ya mchezaji kusafiri. (Fabrizio Romano)
- Barcelona bado ina imani kubwa kuwa itafanikiwa kumsajili João Cancelo kabla ya dirisha la usajili kufungwa. Mazungumzo na Al Hilal kuhusu ada ya uhamisho yanaendelea, huku ikielezwa kuwa beki huyo wa Ureno anataka kujiunga na Barcelona pekee. (Fabrizio Romano)
- Arsenal imechunguza kwa kina uwezo wake wa kifedha katika jaribio la kumsajili Vinicius Jr wa Real Madrid. Kwa mujibu wa taarifa, ndani ya klabu kuna imani kwamba iwapo Vinicius ataondoka Madrid, chaguo lake la kwanza litakuwa kuhamia Arsenal. (AS)
- Trevoh Chalobah anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya leo kabla ya kujiunga na Como akitokea Chelsea. Beki huyo wa England mwenye umri wa miaka 27 anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka mitano baada ya Chelsea kukubali dau la pauni milioni 25 pamoja na nyongeza zinazoweza kufikisha pauni milioni 30. (The Athletic)
Israel yatekeleza mashambulizi kusini mwa Lebanon, licha ya usitishaji mapigano
Jeshi la Israel limesema limeanzisha mashambulizi mapya katika maeneo ya kusini mwa Lebanon kwa kile walichokitaja kuwa ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano uliofanywa na Hezbollah.
Mashambulizi haya yanajiri wakati mazungumzo kati ya Israel na serikali ya Lebanon yanaendelea mjini Rome.
Katika taarifa yake, jeshi hilo limesema:
"Katika kujibu ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano uliofanywa na kundi la kigaidi la Hezbollah, vikosi vya Jeshi la Israel vimefanya mashambulizi kusini mwa Lebanon."
Taarifa hiyo ilitolewa muda mfupi baada ya jeshi la Israel kuwaagiza wakazi wa kijiji kimoja kusini mwa Lebanon kuondoka katika eneo hilo.
Hezbollah, ambayo ni mshirika wa Iran, imekuwa ikiikosoa serikali ya Lebanon kwa kufanya mazungumzo na Israel, ikisema hatua hiyo inakiuka katiba ya Lebanon.
Kiongozi wa Hezbollah, Naim Qassem, ametoa kauli kali akisema hatakubali makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani kati ya Lebanon na Israel.
Makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Lebanon yanatajwa kuwa sehemu ya kwanza ya makubaliano ya maelewano kati ya Iran na Marekani.
Soma pia:
WFP : Watu millioni 49 wako katika hatari ya kukumbwa na njaa kali ifikiapo mwaka ujao
Hali ya hewa ya El Nino huenda ikasababisha watu takriban milioni 49 kukosa chakula ifikiapo mwaka ujao.Hii ni kulingana na ripoti iliyotolewa na shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema kuna uwezekano wa asilimia 81 wa kutokea kwa El Niño yenye nguvu kubwa, huku halijoto ya bahari ikiwa katika viwango vya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka wa 1982. Na ikiwa hali hiyo itaendelea, inaweza kuwa El Niño yenye nguvu zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka wa 1950.
El Niño ni hali ya ongezeko la joto la uso wa Bahari inayojitokeza mara kwa mara na kubadili mifumo ya hali ya hewa duniani.
Mara nyingi hali hii husababisha ukame Kusini mwa Afrika, kuchelewa kwa mvua za msimu katika baadhi ya maeneo ya Asia na mvua zisizotabirika katika maeneo mengine ya dunia.
"Mara nyingi matukio kama haya yamesababisha njaa kwa kiwango kikubwa," amesema Jean-Martin Bauer, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uchambuzi wa Usalama wa Chakula na Lishe cha WFP.
Kulingana na uchambuzi wa WFP nchi 45 zinakadiriwa kuwa katika hatari kubwa ya kuathiriwa na El Niño, na idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula inaweza kuongezeka kutoka milioni 49, na kufikia jumla ya watu milioni 274.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Amerika ya Kati na Kusini mwa Afrika zitakuwa miongoni mwa maeneo yatakayoathirika zaidi. Idadi ya watu wanaokabiliwa na ukosefu wa chakula inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 83 Amerika ya Kati na karibu asilimia 75 Kusini mwa Afrika.
Makubaliano na Oman hayamaanishi Mlango Bahari wa Hormuz utafunguliwa mara moja - Iran
Shirika la habari la kiislamu la Iran (IRIB) limesema kuwa makubaliano kati ya Iran na Omanhayamaanishi kuwa Mlango Bahari wa Hormuz utafunguliwa mara moja.
Shirika hilo linalosimamiwa na serikali ya Iran, limemnukuu afisa mmoja wa Iran aliyesema kuwa"mazungumzo kuhusu utaratibu wa usafiri wa meli kupitia Mlango Bahari wa Hormuz yanahusu Iran na Oman pekee, na hayahusiani na Marekani."
Kulingana na afisa huyo"Iwapo ukiukaji unaodaiwa kufanywa na Marekani utaendelea, Mlango Bahari wa Hormuz hautafunguliwa hata kama kutakuwa na makubaliano kati ya Iran na Oman. Kufunguliwa kwa mlango huo kunategemea Marekani kubadili mwenendo wake na kusahihisha ukiukaji wake."
Vyombo vya habari vya Iran, vikiwemo Shirika la Habari laTasnim, vimesema kuwa"sababu kuu ya kuchelewa kwa makubaliano kati ya Iran na Oman kuhusu Mlango Bahari wa Hormuz ni uingiliaji wa Marekani na vitisho vya Rais Donald Trump."
Soma pia:
UN: Watu 56 wamenyongwa Iran kwa mashtaka yanayohusiana na usalama wa taifa
Mkuu wa shirika la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa amesema takriban watu 56 wameuawa kwa kunyongwa nchini Iran kwa makosa yanayohusiana na usalama wa taifa tangu mwezi Machi.
Volker Türk amesema kuwa, kulingana taarifa rasmi za mamlaka za Iran, watu 27 kati ya 56 waliohukumiwa na kunyongwa, walishtakiwa na kesi zinazohusiana na maandamano yaliyofanyika mwezi Januari.
Katika taarifa yake, Türk amesema kuwa tangu kuanza kwa vita, idadi ya hukumu za kifo na utekelezaji wake umeongezeka nchini Iran.
Turk amewataka viongozi wa Iran kusitisha mara moja utekelezaji wa hukumu za kifo na kufuta adhabu hiyo.
Aidha mkuu wa mahakama ya Iran ameripotiwa mara kadhaa akiwataka waendesha mashtaka kuhakikisha hukumu dhidi ya waliokamatwa wakati wa maandamano ya Januari na wale waliofungwa baada ya vita vya siku 40 zinatolewa na kutekelezwa haraka na bila huruma.
Soma pia:
Wanasayansi wafuatilia athari za roketi ya Space X kugonga mwezi
Sehemu ya roketi ya Falcon 9 ya kampuni ya anga ya Marekani ya SpaceX inaaminika imegongana na mwezi.
Sehemu ya juu ya roketi hiyo ilikuwa na ukubwa unaokadiriwa kuwa sawa na jengo la ghorofa tano na uzito wa angalau kilo 4,000.
Kabla ya kugongana na mwezi,roketi hiyo ilikuwa ikizunguka angani kwa kasi ya takriban kilomita 2.43 kwa sekunde au kilomita 8690.458 kwa saa.
Roketi hiyo ilirushwa angani mwezi Januari mwaka wa 2025 katika ushirikiano wa Marekani na Japan.
Kazi yake ilikuwa kusukuma vyombo vingine viwili vya anga vilivyotakiwa kutua mwezini kwa nguvu ya kutosha ili vitoke kwenye mzunguko wa Dunia na kuanza safari ya kuelekea mwezini.
Baada ya kukamilika kwa misheni hiyo, sehemu hiyo ya roketi iliendelea kuzunguka angani. Katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, mzunguko wa mwezi na jua ulibadilisha hatua kwa hatua mwelekeo wake hadi ikaishia kuwa kwenye njia ya kugongana na Mwezi.
Hakukuwa na chombo chochote cha anga kilichokuwa kikizunguka Mwezi kilichokuwa katika nafasi ya kunasa picha za moja kwa moja za tukio hilo.
Wanasayansi watalinganisha picha za eneo hilo kabla na baada ya mgongano huo ili kubaini kama kuna kreta mpya au alama nyingine zilizotokana na athari hiyo.
Wanaanga wanasema faida kubwa ya tukio hilo haitajulikana mara moja, labda ndani ya takriban wiki moja, wakati wanasayansi watakapochambua picha na taarifa za kina kutoka eneo la mgongano.
Kulingana na wataalamu, mgongano kati ya mwezi na sehemu ya roketi ya SpaceX iliyokuwa ikizurura angani haina tishio lolote, hasa kwa dunia.
Msemaji wa NASA, Jamie Russell, alisema kuwa ingawa shirika hilo litaendelea kufuatilia eneo la mgongano kwa madhumuni ya kisayansi, "hakuna tishio lolote kwa dunia."
Wanasayansi wa NASA wanapanga kutumia taarifa zitakazokusanywa kutokana na tukio hilo kuboresha mbinu za kufuatilia na kuchunguza vitu vinavyozunguka angani.
Soma pia:
Trump: Iran na Marekani zinaendelea na mazungumzo, tumepiga hatua nzuri
Rais wa Marekani Donald Trump amesema utawala wake unafanya "mazungumzo mazuri sana" na Iran,mazungumzo yaliyofanyika siku nzima hapo jana.
"Walifanya mazungumzo ya siku nzima," Trump alisema katika kipindikimojacha Fox News.
Aliongeza kuwa, "Mlango Bahari wa Hormuz utafunguliwa hivi karibuni. Wakibadili msimamo wao tena, watakumbana na mashambulizi makali sana."
Bei ya mafuta ilishuka huku bei ya hisa zikipanda Marekani na bara Asia hii leo kutokana na matumaini kuwa makubaliano yanaweza kufikiwa hivi karibuni na Mlango bahari wa Hormuz kufunguliwa tena.
Soma pia:
Watu 17 wauawa katika shambulio la Urusi mjini Kyiv
Urusi imetekeleza mashambulizi dhidi ya Ukraine kwa kutumia makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani na kuwaua takriban watu 17.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema wangekuwa na makombora ya kuzuia mashambulizi wangeweza kuokoa maisha
Hii imetajwa kuwa shambulizi mbaya Zaidi kuwahi kushuhudia mjini Kyiv mwaka huu, huku Zaidi ya watu 44 wakijeruhiwa.
Urusi ililenga kituo cha reli, maghala na makazi ya watu katika mashambulizi hayo.
Ukraine, kwa muda mrefu imekuwa ikiwasihi washirika wake kuwapatia makombora zaidi ya kuzuia mashambulizi ya angani ya balistiki ya aina ya Patriot yanayotengenezwa Marekani.
Rais Zelensky amesema kucheleweshwa kwa upatikanaji wa mifumo ya kuzuia makombora ya balistiki kutoka kwa washirika wake kumesababisha vifo na uharibifu mkubwa.
Soma pia:
Infantino aitisha kikao cha FIFA huku ukosoaji ukiongezeka
Gianni Infantino amewaita viongozi wakuu wa shirikisho la soka duniani (FIFA) kwenye mkutano nchini Morocco siku ya Jumatano, kufuatia siku nyingine ambapo rais wa shirikisho hilo amekabiliwa na ukosoaji mkali kuhusu mpango wake uliositishwa wa kuuza kuuza hisa za mashindano ya FIFA kwa wawekezaji binafsi.
Mkuu wa maendeleo ya soka duniani wa FIFA, Arsene Wenger, Katibu Mkuu Mattias Grafstrom, na Mwana mfalme Ali, rais wa Shirikisho la Soka la Jordan, wote walionyesha wazi kupinga mpango wa Infantino unaojulikana kama 'Fifa Forward Enterprise'.
Infantino, ambaye amekuwa nchini Morocco kwa wiki iliyopita, aliitisha mkutano wa maafisa watendaji mjini Rabat katika juhudi za kutafuta suluhisho la utata huo.
Katika taarifa iliyotolewa kupitia FIFA, Wenger alisema kuwa kusitisha mpango huo kulikuwa "jambo la lazima kabisa na lisilo na shaka yoyote".
Grafstrom alielezea wiki iliyopita kama "mfululizo wa matukio ya kusikitisha na ya kulaumiwa" katika barua pepe ya ndani iliyotumwa kwa wafanyakazi wa FIFA.
Wakati huo huo, Mwana mfalme Ali aliishutumu FIFA kwa kuunda hali ambayo "inaweza kuchukuliwa kama shinikizo la kulazimisha mambo" kuhusiana na fedha za zawadi ambazo hazijalipwa na uungaji mkono kwa ajili ya kuchaguliwa tena kwa Infantino.
Tangu mwaka 2019, Wenger amekuwa akishikilia wadhifa unaohusisha uchambuzi wa takwimu za mchezo huo, mafunzo ya mtandaoni ya FIFA, na mashindano ya vijana.
Aliyekuwa kocha mkuu wa Arsenal hapo awali aliunga mkono pendekezo la Infantino la kuandaa Kombe la Dunia la wanaume kila baada ya miaka miwili
Asilimia 87 ya wafanyakazi wa Kenya waripoti msongo wa mawazo - Utafiti
Sekta ya biashara nchini Kenya inakabiliwa na mgogoro unaoongezeka wa ustawi kazini, huku utafiti mpya ukionyesha kuwa takriban wafanyakazi tisa kati ya kumi (87%) wanaripoti kupata msongo wa mawazo, na kuibua wasiwasi mpya kuhusu tija, ushiriki wa wafanyakazi na utendaji.
Matokeo hayo, yaliyotolewa na shirika la Niche Human Capital Advisory, yanajiri wakati ambapo waajiri wanakabiliwa na kuongezeka kwa uchovu, mabadiliko ya matarajio ya wafanyakazi na kuongezeka kwa ushindani wa vipaji.
Nchini humo, asilimia 80.4% ya wafanyakazi wanaripoti msongo wa mawazo wa wastani hadi uliokithiri kazini, huku 67.8% ya wafanyakazi katika Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara wakiripoti uchovu wa kihisia na uchovu, wakisisitiza ukubwa wa changamoto inayowakabili waajiri.
Wakati huo huo, 82.5% ya wafanyakazi wanaamini mashirika yanahitaji kufanya zaidi ili kusaidia kuimarisha afya ya akili.
Axio: Iran, Oman na Marekani zakaribia kufikia makubaliano ya kufungua tena Mlango-bahari wa Hormuz
Axios iliripoti, ikinukuu vyanzo viwili vya kikanda na afisa wa Marekani, kwamba Marekani, Iran, na Oman ziko karibu kufikia makubaliano ya muda ya kufungua tena Mlango-bahari wa Hormuz.
Kulingana na vyanzo vya habari vya Axios, serikali ya Marekani inatarajia kutangaza makubaliano hayo siku ya Jumatano.
Maelezo ya makubaliano hayo yanayoweza kufikiwa bado hayajatolewa na hakuna hata upande mmoja kati ya pande hizo tatu uliothibitisha rasmi ripoti hiyo; hata hivyo, siku ya Jumanne, vyombo vya habari vya Marekani vikinukuu vyanzo vyao vilijaribu kuripoti vipengele vikuu vya mazungumzo hayo na masharti yanayotakiwa na pande husika. Kama ilivyoripotiwa na Axios, vipengele vya mazungumzo hayo vilikuwa kama ifuatavyo:
- Meli zote zinazoingia Ghuba ya Uajemi zitasafiri kupitia njia ya kaskazini na kupita katika maji ya Iran.
- Meli zote zinazotoka Ghuba ya Uajemi kuelekea Bahari ya Oman zitapita kupitia njia ya kusini na katika maji ya Oman, kwa uratibu na Iran.
- Katika kipindi cha utekelezaji wa siku 60 cha makubaliano hayo ya muda, hakuna ushuru au ada yoyote itakayotozwa kwa meli zinazopita.
- Pande zinazohusika na makubaliano hayo zitajitolea kutekeleza operesheni ya kuondoa mabomu ya baharini katika njia ya katikati ya Mlango-bahari wa Hormuz ndani ya siku 30.
- Mara tu njia ya katikati itakapokuwa imesafishwa, itatumika kwa ajili ya usafiri wa meli zinazoingia na kutoka. Utaratibu wa matumizi ya njia hiyo utaamuliwa katika makubaliano ya kudumu yatakayojadiliwa kati ya Iran na Oman.
Vifo vya ajabu vya tembo nchini Kenya vyaibua maswali kuhusu dawa za kuuwa wadudu
Habari kwamba vifo vya hivi karibuni vya tembo 15 huenda vilisababishwa na dawa za kuuwa wadudu zilizopulizwa kwenye mashamba ya nyanya yanayozunguka Hifadhi ya Taifa ya Amboseli vimezua wasiwasi na maswali nchini Kenya.
Wiki iliyopita, Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini Kenya (KWS) lilisema kuwa baadhi ya tembo hao waliokufa kati ya tarehe 24 Juni na 24 Julai walionyesha dalili za "kupooza kwa sehemu ya mwili," jambo lililoashiria sumu inayotokana na kemikali ya 'cyanide' inayopatikana katika dawa hizo za kuuwa wadudu.
Hata hivyo, wanaharakati wa uhifadhi wameiambia BBC kwamba huenda hiyo isiwe ndiyo picha kamili ya hali halisi.
Wakulima tuliozungumza nao katika eneo hilo pia walionyesha kutokuwa na uhakika na madai hayo.
"Tumeishi na wanyamapori hawa kwa miongo kadhaa na hatujawahi kushuhudia jambo kama hili," Daniel Nina, anayewakilisha baadhi ya wamiliki wa ardhi katika eneo hilo, aliambia BBC.
"Ndiyo maana tunajiuliza ni kwa nini jambo hili linatokea leo."
Mashamba hayo ya nyanya yanapatikana katika eneo la Kimana, ambalo ni sehemu ya njia ya wanyama inayounganisha Hifadhi ya Taifa ya Amboseli na Hifadhi ya Taifa ya Tsavo kusini mwa Kenya.
Eneo hilo kubwa, linalojulikana kama mfumo wa ikolojia wa Amboseli, linapakana na nchi jirani ya Tanzania na ni njia inayotumiwa na zaidi ya tembo 2,000 kutafuta chakula na maji.
Mashamba hayo hustawi kutokana na maji yanayotiririka kutoka Mlima Kilimanjaro ulio karibu, na hutoa mazao yanayouzwa katika masoko ya Nairobi, mji mkuu wa Kenya, na maeneo mengine.
Daktari Mkuu wa Mifugo katika Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini Kenya, Dkt. Isaac Lekolool, alituambia kuwa waligundua chembechembe za sumu ya 'cyanide' katika sampuli zilizochukuliwa kutoka kwenye matumbo ya tembo hao.
Anasema kuwa hawajaacha uwezekano wa sumu kuwekwa makusudi, lakini kwa sasa haiwezekani kubaini nini hasa kilichosababisha vifo vya tembo hao.
"Ni vigumu kusema kwa sababu hatujawahi kushuhudia visa vya aina hii hapo awali. Ni tukio la kipekee, na lilitokea ndani ya kipindi cha takriban mwezi mmoja," alisema Lekolool.
Dhana yao ya awali ni kwamba tembo hao walikumbana na sumu hiyo kupitia dawa za kuuwa wadudu zilizopulizwa katika mashamba ya nyanya yaliyo karibu.
"Huenda ilitokea bila kukusudiwa. Labda watu walikuwa wakijaribu kudhibiti wadudu kwenye mazao yao, na hilo linaweza kuwa ndilo chanzo."
Tatizo la dawa za kuua wadudu.
Ripoti ya mwaka 2024 kutoka kwa shirika la Kenya linaloshughulikia usalama wa chakula, Route to Food, ilibaini mkulima mmoja katika eneo la Kimana akitumia dawa ya kuuwa wadudu iliyokuwa na "kiambato amilifu" ambacho ni " kemikali ya sianidi".
Wangunyu Njuguna, mwandishi wa ripoti hiyo, alisema kuwa licha ya kupigwa marufuku nchini Kenya, baadhi ya kemikali hatari za kilimo huingizwa nchini kwa njia ya magendo kupitia mpaka wa Tanzania.
"Tatizo kubwa ni kwamba hatutekelezi viwango sawa katika eneo hili," alisema Njuguna. "Hakuna anayekagua ninachoenda kununua ninapovuka mpaka, hivyo naweza kwenda kununua chochote na kupita mpakani bila mtu yeyote kunizuia."
Kemikali hatari sana zinapatikana kwa wingi katika mashamba ya Kenya na baadhi yake zimehusishwa na magonjwa hatari.
Ingawa kuna kanuni zinazopiga marufuku kemikali haramu za kilimo, utekelezaji wake ni dhaifu na hakuna umakini wa kutosha kuhusu jinsi kemikali hizo zinavyoweza kuathiri wanyama.
Tazama Video ya droni ya Urusi ikimfukuza mchuuzi nchini Ukraine
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amechapisha video kwenye mitandao ya kijamii inayoonyesha droni ikimwinda mwanamume kusini mwa Ukraine, akisema kuwa tukio hilo linaonyesha shambulio la Kirusi la aina ya "safari" (uwindaji wa burudani) dhidi ya raia.
Video hiyo inaonyesha droni ikimfuatilia mchuuzi katika barabara ya jiji katika eneo la Kherson.
Mwanamume huyo anajaribu kujiepusha na droni inayoning'inia juu yake, kabla ya droni hiyo kuanza kumkimbiza huku akikimbia kuzunguka gari jeupe la aina ya van.
Hatimaye, droni hiyo inashuka kwa kasi na kulipuka ilipomgonga.
Mwanamume huyo alinusurika akiwa na majeraha mengi ya vipande vya chuma, mtikiso wa ubongo na mshtuko wa kisaikolojia, daktari alisema.
Matumizi ya droni zinazoendeshwa kwa mbali dhidi ya raia, jambo ambalo wakati mwingine huitwa "uwindaji wa binadamu" (human safari) yamekuwa yakitumiwa mara kwa mara na Warusi kuwatia hofu wakazi wa maeneo ya mstari wa mbele wa vita nchini Ukraine.
"Lazima dunia ione hili," Zelensky aliandika kwenye Telegram. "Lazima ione kila ushahidi kwamba Urusi imepoteza akili, na kila ukweli kwamba askari wa Urusi wanafurahia kuua na kuwatesa watu."
Video hiyo ilionyesha "uhalifu wa kivita wa kikatili," alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha.
Vitendo hivyo vya uwindaji vilikuwa "mkakati wa makusudi na wa kimfumo wa Urusi," Sybiha alisema.
"Mtu huyo mwenye tabia ya kikatili na ya kufurahia mateso anayeendesha droni hii anajua kwamba anamshambulia raia."
Aliongeza kuwa shambulio hilo lilikuwa sehemu ya kampeni ya makusudi ya Urusi ya kuwatisha raia na akataka kulaaniwa kimataifa.
Klabu ya Uturuki Trabzonspor yaanza mazungumzo ya kumsajili Mohamed Salah
Klabu ya Trabzonspor ya Uturuki imetangaza kuwa imeanza mazungumzo ya kumsajili Mohamed Salah.
Mshambuliaji huyo raia wa Misri, mwenye umri wa miaka 34, aliondoka Liverpool mwishoni mwa msimu uliopita na kwa sasa yuko katika mazungumzo ya kujiunga na timu hiyo kama mchezaji huru, bila kufungwa na mkataba rasmi na klabu yoyote ya michezo.
Katika taarifa yake, Trabzonspor imesema kuwa Salah atawasili Istanbul siku ya Jumatano.
Taarifa hiyo iliongeza: "Mchezaji huyo anatarajiwa kuwasili Trabzon jioni hiyo hiyo."
Iliongeza pia: "Tarehe ya kuwasili kwa mchezaji huyo na maelezo mengine kuhusu ratiba ya mapokezi yake huko Trabzon yatatangazwa kupitia njia rasmi za mawasiliano za klabu hiyo katika kipindi cha siku hiyo."
Bei ya mafuta yashuka kufuatia matumaini ya kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz
Bei ya mafuta ilishuka hadi kiwango cha chini cha wiki tatu Jumanne huku maafisa wakuu wa Marekani wakiongeza matumaini ya makubaliano na Iran ya kufungua tena njia kuu ya maji ya Hormuz.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na Waziri wa Hazina Scott Bessent wote walitangaza kwamba mazungumzo yameendelea ili kuruhusu uwezekano wa usafirishaji kuanza tena haraka iwezekanavyo wiki hii.
Gharama ya pipa la mafuta ghafi ya Brent, kipimo cha kimataifa cha bei ya mafuta, ilishuka kwa karibu 5% hadi chini ya $80 (£60) kutokana na habari za usumbufu wa usambazaji unaoweza kupungua.
Lakini kushindwa kwa mazungumzo ya awali katika miezi ya hivi karibuni ili kupunguza mzozo kati ya Marekani na Iran kumesababisha soko la mafuta tete, huku madereva hatimaye wakiathiriwa na bei kubwa za mafuta kwenye pampu.
Siku ya Jumanne, pamoja na kushuka kwa mafuta ghafi ya Brent, bei za kati za Marekani Magharibi mwa Texas zilishuka kwa zaidi ya 5%, hadi $76 kwa pipa.
Mikataba yote miwili ilishuka hadi viwango vyao vya chini kabisa tangu Julai 13.
Rubio alisema kumekuwa na maendeleo yaliyopatikana katika majadiliano kuhusu kupeleka meli zaidi kupitia njia hiyo na Iran na Oman.
"Kumepatikana maendeleo katika mazungumzo hayo, lakini bado hayajakamilika. Tunatumai hilo litatokea hivi karibuni," aliwaambia waandishi wa habari katika Wizara ya Mambo ya Nje.
Bessent alisema makubaliano ya kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz yanaweza kuafikiwa siku ya Jumanne au Jumatano.
Meli ya India yazama baada ya kupigwa kombora karibu na maji ya Yemen
Waziri wa Usafirishaji wa India anasema meli ya India ilipigwa na kitu kilichorushwa, na kusababisha ipinduke na kuzama karibu na maji ya Yemen.
Alisema: "Wanamaji wote 14 waliokuwa kwenye meli hiyo waliokolewa salama na Kikosi cha Walinzi wa Pwani cha Yemen."
Wizara ya Mambo ya Nje ya India ililaani shambulio hilo "vikali" katika taarifa yake.
"Tunalaani shambulio dhidi ya meli ya kibiashara yenye bendera ya India, MSV Faiz Noor Alia, ambayo ilizama katika Bahari ya Shamu karibu na pwani ya Yemen mnamo Agosti 4, 2026. Raia wote 13 wa India wameokolewa," wizara hiyo ilisema katika taarifa..
Bloomberg: Iran inazingatia kuruhusu Ulaya kushiriki katika kuondoa mabomu ya baharini yaliotegwa katika Mlango-bahari wa Hormuz
Shirika la habari la Bloomberg liliripoti, likinukuu wanadiplomasia wenye taarifa za ndani, kwamba Iran inafikiria kuonyesha utayari kwa nchi za Ulaya kushiriki katika shughuli za kuondoa mabomu yaliotegwa baharini katika Mlango-bahari wa Hormuz; hatua ambayo inaweza kuwa sehemu ya makubaliano ya kurejesha hali ya kawaida ya usafirishaji katika njia hiyo ya maji na kurahisisha mazungumzo ya amani na Marekani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Iran imesisitiza mara kwa mara katika misimamo yake ya hadharani kwamba haitaruhusu nchi za kigeni kushiriki katika shughuli za kuondoa mabomu hayo katika njia hiyo muhimu ya kimkakati kwa usafirishaji wa mafuta na gesi asilia.
Hata hivyo, kulingana na wanadiplomasia waliozungumza na Bloomberg kwa sharti la kutotajwa majina kutokana na unyeti wa suala hilo, Tehran imelainisha msimamo wake kiasi katika mikutano ya faragha katika wiki za hivi karibuni na inazingatia uwezekano wa nchi za Ulaya kushiriki katika operesheni hiyo.
Bloomberg iliripoti siku ya Jumanne kwamba iwapo mabadiliko hayo yatatekelezeka, hatua hiyo inaweza kuwa sehemu ya juhudi za kidiplomasia za kurejesha usalama wa usafirishaji katika Mlango-bahari wa Hormuz na kupunguza mivutano kati ya Iran na Marekani
CBS: Marekani imetumia karibu akiba yake yote ya makombora ya masafa marefu katika vita dhidi ya Iran
Vyanzo viwili vimeiambia CBS News - mshirika wa BBC nchini Marekani - kwamba Marekani imetumia karibu akiba yake yote ya dunia nzima ya makombora ya masafa marefu yenye usahihi wa hali ya juu wakati wa vita dhidi ya Iran.
Kulingana na ripoti hii, Marekani imetumia karibu makombora yake yote ya aina ya *Army Tactical Missile System* (ATACMS) na makombora ya kushambulia kwa usahihi (*Precision Strike Missiles*) katika Operesheni Epic Fury.
Awali, Reuters iliripoti kuwa Marekani ilikuwa imetumia "karibu makombora yote" ya masafa marefu yenye usahihi wa hali ya juu katika operesheni hii.
CBS iliripoti hapo awali kuwa akiba ya Marekani ya makombora ya kuzuia mashambulizi (*interceptor missiles*) na makombora ya masafa marefu imepungua sana, na jambo hili limekuwa changamoto ya ndani kwa serikali.
Kulingana na ripoti hiyo, Marekani haiwezi kuendelea na mwenendo huu kwa kasi ileile iliyotumika kumaliza akiba ya silaha hizo mwanzoni mwa vita dhidi ya Iran.
Maafisa wa Marekani wamesema kuwa akiba ya makombora haya ni finyu, lakini suala la dharura zaidi ni idadi ya makombora ya kuzuia mashambulizi ya aina ya Patriot na THAAD, ambayo yanatumika kwa kasi kubwa kuliko uwezo wa viwanda vya ulinzi vya Marekani wa kuyazalisha.
Sean Parnell, msemaji mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon), alisema katika taarifa kwa CBS:
"Jeshi la Marekani ndilo jeshi lenye nguvu zaidi duniani na lina kila kitu kinachohitajika kutekeleza majukumu yake wakati wowote na mahali popote ambapo rais ataamua. Tumefanya operesheni kadhaa zilizofanikiwa katika maeneo mbalimbali huku tukihakikisha kuwa jeshi la Marekani lina akiba kubwa ya uwezo wa kulinda watu na maslahi ya taifa."
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegsett, hapo awali alitupilia mbali wasiwasi kuhusu kupungua kwa akiba ya silaha za Marekani. Aliambia CBS mnamo Julai 14:
"Hii ni habari ya kubuni ambayo vyombo vya habari vinataka kuisambaza. Hatimaye, akiba yetu iko katika hali nzuri na inaendelea kuimarika zaidi."
Ripoti hii inakuja wakati matumizi makubwa ya makombora ya kuzuia mashambulizi na silaha zenye usahihi wa hali ya juu katika vita vya hivi karibuni yamechochea mijadala mjini Washington kuhusu uwezo wa uzalishaji wa viwanda vya ulinzi vya Marekani na utayari wake kwa mzozo wa muda mrefu.