Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini wanawake wa nchi hii hupenda kuvaa mavazi ya kiume?
Msimu wa joto ulipokaribia, Kexin aligundua mabadiliko alipopanga kabati lake: Nguo za "kiume" zilikuwa nyingi kuliko za wanawake. Hanunui tena mashati, fulana, na kaptula kwa ajili ya mpenzi wake au baba yake, bali anajinunulia mwenyewe.
Kexin hayuko peke yake. Idadi inayoongezeka ya wanawake vijana wa Kichina, katika mzunguko wake wa marafiki na mtandaoni, wanasema wanageukia mavazi ya kiume kwa sababu moja ya ubora wake, bei ya nafuu, sio sana watu kuzungumzia muonekano wa mwili wako unapovalia.
Lakini mtindo huu unatokana na nini hasa?
Kexin anakumbuka alianza kubadilisha mavazi yake mwaka wa 2023, wakati ukurasa wake wa mapendekezo wa Douyin (toleo la China la TikTok) ulionyesha matangazo yake ya moja kwa moja ya T-shirt za wanaume zikiuzwa.
Mwanzoni, ilimchanganya. Hakuwahi kumnunulia baba au mpenzi wake, kwa hivyo kwa nini kanuni hiyo ingependekeza maudhui kama haya kwake?
Kexin alifikiri ilikuwa hitilafu ya mfumo, hadi siku moja, alipokuwa akienda bafuni, aliacha simu yake kwa bahati mbaya kwenye matangazo ya moja kwa moja ya uuzaji wa nguo.
Wasichana wanaweza kununua nguo hii kwa ukubwa mdogo na kuvaa wenyewe." "Nguo hii haina jinsia; wanawake wanaweza kuvaa pia."
Kauli hizi zilirejelewa mara kwa mara nadni ya dakika chache
Ikilinganishwa na matangazo ya moja kwa moja yanayowalenga wanawake—ambayo mara nyingi husisitiza kuwafanya waonekane wembamba zaidi, kuficha kasoro wanazodhaniwa kuwa nazo, au kuonyesha taswira ya upole na kuw amujibu wa jinsia yao—tangazo hili lilijikita katika ubora wa kitambaa na vifaa vilivyotumika.
"Jambo hilo lilinivutia sana," anasema. "Sijawahi kuelewa kwa nini mavazi ya wanawake huendelea kusisitiza viwango vya kawaida vya urembo, hasa ikizingatiwa kuwa miundo yake mara nyingi huwa haistareheshi."
Bei pia ilikuwa sababu muhimu: mashati mengi yaligharimu chini ya yuan 100 (dola 14 au pauni 11). Hata kama ingebidi ayarudishe, hakuchukulia hatua hiyo kama kuwa hatari kubwa sana.
Alinunua shati lake la kwanza la "wanaume" na alishangazwa sana na matokeo. Lilikuwa zuri zaidi, zito zaidi, na hafifu kuliko mashati ya wanawake aliyokuwa akinunua awali na bei ilikuwa mara tatu zaidi.
Muda mfupi baadaye, alianza kununua nguo zaidi za wanaume, na ule usumbufu aliohofia kupata kwa kuzivaa haukutokea kamwe.
Anasema kuwa kadiri muda ulivyopita, nguo hizo zilianza kuwa sehemu kubwa ya mavazi yake.
Punguza gharama
Mwelekeo huu pia unakuja huku hali ya kiuchumi yaa watumiaji nchini China ukiwa dhaifu tangu vikwazo vya Covid vilipomalizika mwishoni mwa 2022.
Kwa wafanyakazi kama Kexin, ambaye anafanya kazi kwa ratiba ngumu ya "996" huko Shanghai (saa 9 asubuhi hadi 9 jioni, siku sita kwa wiki), amekuwa muangalifu sana linapokuja suala la matumizi fedha.
Ana uwezekano mdogo wa kubadilisha kazi na pia hayuko tayari kugharamika sana kwa mahitaji ya msingi kama vile mavazi.
Katika hali kama hizo, baadhi ya watumiaji wamegeukia mitindo inayojulikana kama "matumizi yenye tija," ikimaanisha wanapendelea thamani na uimara kuliko mitindo ya haraka.
"Ikiwa kitu hakifai, ni rahisi kukirudisha," anasema Kexin. "Sioni sababu yoyote ya kutumia pesa nyingi kwa mavazi. Mimi kwa kawaida sivai nguo kwa zaidi ya msimu mmoja."
Tatizo la ukubwa
Kwa wengi, mabadiliko sio kutoa maoni kuhusu jinsia pekee bali inahusu vitendo. Ukubwa wa nguo ni mojawapo ya vipengele vinavyokosolewa zaidi kuhusu mavazi ya wanawake nchini China.
Kwenye mitandao ya kijamii kama Douyin na Xiaohongshu, watu wenye ushawishi mdogo mara nyingi huonyesha kwamba hata kile kinachoitwa saizi kubwa ni vigumu kuzifaa. Nguo zilizoandikwa XL (kubwa sana) hazipiti hata paja, au mifumo ya ukubwa inayowaweka wanawake wembamba katika kategoria ndogo zaidi. Wakati huo huo, wanawake warefu huelekezwa haraka kwenye saizi kubwa zaidi.
Katika moja ya video zinazotazamwa zaidi, mwanablogu anamvisha sweta kubwa mbwa wake na vazi hilo linamtosha kikamilifu.
Bi. Li, wakili na mkaazi wa Shanghai ambaye aliomba kutambuliwa kwa jina lake la ukoo pekee, anasema aligeukia mavazi ya wanaume tangu ukiwa mdogo kwa sababu mavazi ya wanawake ni nadra sana kumtosha. Ana urefu wa sentimita 170 na ana mabega mapana.
Anasema hakujua hilo hadi alipoenda Ulaya kwa masoma ndipo alipogundua kuwa saizi ya kawaida ya wastani inaweza kuwa saizi yake kamili.
"Nguo za wanawake hapa hazionekani kutengenezwa kwa ajili ya watu wenye umbo la mwili wangu," anasema.
Pia anaangazia umuhimu wa mavazi ya wanaume: suruali ya wanaume iliyo na ukubwa wa kati inaweza kutoshea kibao cha inchi 11 na kitabu mifukoni mwao bila kuathiri umbo la vazi.
"Ni nguo gani za wanawake ziko hivyo? Hata kupaka lipstiki kunaweza kukufanya uonekane mkubwa," anasema.
Changamoto zinazokumba tasnia ya mitindo
Kulingana na Wang, mbunifu katika chapa ya nguo ya ukubwa wa kati, masuala ya ukubwa na ubora yanaonyesha shinikizo kubwa katika tasnia.
Sekta ya nguo ya China imepungua sana tangu janga hili, huku uzalishaji na mauzo ya nje yakishuka. Ukuaji wa soko la rejareja pia umepungua sana, ukiongezeka kwa sehemu ndogo sana ya asilimia mwaka wa 2024, ikilinganishwa na takriban asilimia 15 mwaka wa 2023.
Kampuni sasa zinazalisha miundo mipya michache, na watumiaji ambao tayari wanamiliki nguo nyingi pia wamepunguza ununuzi wao.
Ili kupunguza gharama, baadhi ya chapa sasa zinanunua mifumo iliyotengenezwa tayari kutoka Asia ya Kusini-mashariki badala ya kubuni yao wenyewe.
Lakini miundo hii mara nyingi haiendani na umbo la mwili la Wachina, na hivyo kusababisha ukubwa na kuenea kwa nguo za wanawake zinazoitwa "za ukubwa wa watoto".
Chaguo za miundo pia huathiriwa na masuala ya kiuchumi. Nguo za miili nyembamba ni za bei nafuu na rahisi kutengeneza, huku zile kubwa zikihitaji kukata na kushona tena kwa gharama ya juu zaidi.
"Ikiwa itagharimu kiasi cha kuuza nguo 20 za ukubwa wa juu kama vile kuuza nguo 200 za ukubwa wa wastani, makampuni bila shaka yataacha kutengeneza nguo za ukubwa wa juu," Bi. Wang anasema.
Anaongeza kuwa kutokana na ongezeko kubwa la gharama ya kitambaa, watengenezaji wanakabiliwa na changamoto nyingine, akionya kwamba matokeo yake yanaweza kuwa nguo nyembamba zaidi mwaka ujao.
Kwa wanunuzi kama Kexin, hii inaweza kuharakisha tu mwenendo ambao tayari unabadilisha yaliyomo kwenye kabati lake.