Zaidi ya watu 900 wakamatwa katika maandamano dhidi ya wahamiaji Afrika Kusini
Zaidi ya watu 900 wamekamatwa kufuatia maandamano ya kitaifa dhidi ya wahamiaji yaliyofanyika Jumanne nchini Afrika Kusini, ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa ya amani lakini katika baadhi ya maeneo yaligeuka kuwa ya vurugu na kusababisha uporaji wa maduka.
Naibu Kamishna wa Kitaifa wa Polisi, Tebello Mosikili, amesema maandamano 108 kati ya 120 yaliyofanyika nchini yalikuwa ya amani, huku maandamano 12 yakihitaji polisi kuingilia kati.
Amesema sababu za kukamatwa kwa watu hao zinajumuisha ukiukaji wa sheria za uhamiaji, kufanya vurugu hadharani, kuwaficha wahamiaji wasio na nyaraka halali na wizi.
Polisi pia wamesema mtu mmoja alipigwa risasi na kuuawa usiku wa Jumanne katika kitongoji cha Alexandra, mjini Johannesburg, ambako wakazi walikuwa wakipora maduka madogo maarufu kama spaza shops yanayomilikiwa na raia wa kigeni.
Mamlaka zilisambaza askari wa ziada katika majimbo matano kati ya tisa ya nchi hiyo usiku kucha, huku wanajeshi wakipelekwa katika eneo la Hillbrow katikati mwa Johannesburg, ambako watu wawili walijeruhiwa kwa kupigwa risasi.
Katika mji wa bandari wa Durban, polisi wameanza uchunguzi kuhusu kifo cha raia mmoja wa kigeni ambaye inadaiwa alijirusha kutoka ghorofa ya nane ya jengo moja usiku kabla ya maandamano, akiamini alikuwa analengwa.
Maandamano ya Jumanne yaliandaliwa kuashiria mwisho wa muda uliowekwa na kundi linalopinga wahamiaji, lililokuwa limetaka wahamiaji wasiokuwa na vibali halali vyaondoke Afrika Kusini.
Unaweza kusoma;