Maharamia wa Somalia waua wafanyakazi wa meli ya mafuta
Wafanyakazi watano wa meli ya mafuta ya MT Honer 25 waliuawa na maharamia kabla ya vikosi vya usalama vya Puntland kuanzisha operesheni ya kuikomboa meli hiyo, naibu waziri wa habari wa Puntland ameambia BBC.
Bile Qabowsade amesema vikosi vya Puntland vilianzisha operesheni ya kuirejesha meli hiyo chini ya udhibiti wa serikali, lakini maharamia walikuwa tayari wamewaua watu watano waliokuwa ndani yake.
"Kwa bahati mbaya, maharamia walikuwa tayari wamewaua watu watano waliokuwa ndani kabla ya operesheni kuanza," alisema.
Qabowsade alikanusha madai kwamba wafanyakazi hao waliuawa wakati wa mapigano kati ya maharamia na vikosi vya Puntland wakati wa operesheni hiyo.
Kwa mujibu wa mamlaka za Puntland, waliofariki ni raia watatu wa Pakistan, mmoja wa India na mmoja wa Myanmar.
Wafanyakazi wengine wanne walijeruhiwa, wakiwemo raia watatu wa Pakistan na mmoja wa India.
Mamlaka za Puntland zilisema operesheni hiyo imekamilika na kwamba meli hiyo sasa iko salama chini ya udhibiti wa vikosi vya serikali.
Maharamia 16 walikamatwa huku wengine wakitoroka na kuendelea kusakwa.
Qabowsade pia alikanusha madai kuwa baadhi ya maharamia walisaidiwa kutoroka na vikosi vya Puntland.
Vifo vya wafanyakazi hao vinaonekana kuwa vya kwanza vinavyohusishwa na maharamia wa Somalia katika zaidi ya miaka 10, kulingana na taarifa za mamlaka za Puntland. Serikali imekanusha madai kwamba waliuawa katika makabiliano kati ya vikosi vya usalama na maharamia wakati wa operesheni ya uokoaji.
Pia unaweza kusoma