Kwa nini tajiri wa Zimbabwe 'Sir Wicknell' alipendwa na kuchukiwa Afrika?

Chanzo cha picha, Zanu-PF
- Author, Ish Mafundikwa
- Akiripoti kutoka, Harare
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 11
Wicknell Chivayo, tajiri wa Zimbabwe aliyefariki dunia katika ajali ya helikopta pamoja na mkewe, Lucy Muteke, wiki iliyopita, alikuwa mtu aliyeibua hisia mseto wakati wa uhai wake na anaendelea kufanya hivyo hata baada ya kifo chake.
Alijiita "Sir Wicknell" - jina lililoonyesha upendo wake wa maisha ya fahari na mbwembwe - na ambalo pia lilitumiwa na baadhi ya watu kumtukuza. Akiwa na umri wa miaka 45, aliacha nyuma historia iliyojaa utata na mijadala mingi, kiasi kwamba yaliyomhusu yangeweza kutosha kusimulia maisha ya watu kadhaa.
Alipenda kujirekodi na kuweka maisha yake hadharani, akijenga taswira yake kupitia mitandao ya kijamii. Mara kwa mara alionekana akipiga picha akiwa na mabunda ya fedha taslimu na kutangaza magari pamoja na fedha alizowapa watu aliowaona kuwa wanastahili.
Chivayo pia hakusita kuonyesha uhusiano wake na viongozi wa nchi mbalimbali za Afrika na kujivunia utajiri wake. Katika video alizochapisha, alionyesha mkusanyiko wa magari yake ya kifahari, hasa aina ya Rolls-Royce zenye namba za usajili za kipekee, pamoja na saa za thamani na mamia ya viatu vya chapa maarufu.
Kwa wafuasi wake, alikuwa mfano wa mtu aliyefanikiwa na ambaye hakuwa na hofu ya kugawana utajiri wake na wengine. Kwa wakosoaji wake, alikuwa ishara ya kujionyesha kupita kiasi. Walihoji chanzo cha mali zake na ukaribu wake na wanasiasa, huku wakiona mtindo wake wa maisha kama kielelezo cha pengo kubwa kati ya matajiri na maskini.
Hata hivyo, ukosoaji huo haukuonekana kumtatiza. Kadiri utajiri wake ulivyoongezeka, ndivyo alivyozidi kuonyesha hadharani mali zake katika nchi ambayo karibu nusu ya wananchi wanaishi chini ya mstari wa kimataifa wa umaskini, kwa mujibu wa Benki ya Dunia.
"Aliwasaidia watu wachache waliokuwa wakiishi katika kisiwa cha utajiri katikati ya bahari ya umaskini," alisema Pedzisai Ruhanya, mkurugenzi wa taasisi ya utafiti ya Zimbabwe Democracy Institute, katika mahojiano na BBC, akidai kuwa ukarimu wa Chivayo uliwanufaisha zaidi watu wenye ushawishi.
Ruhanya alipuuza taswira ya Chivayo kama mfadhili wa kawaida, akisema misaada yake ilikuwa sehemu ya juhudi za kujijengea ushawishi ndani ya chama tawala cha Zanu-PF na kupata uungwaji mkono kutoka kwa wanasiasa na viongozi wa dini.
Pamoja na hayo, kifo chake kimezua wimbi kubwa la majonzi, hasa miongoni mwa wale walionufaika na ukarimu wake. Wanasiasa, viongozi wa dini na wafanyabiashara ni miongoni mwa waliotuma jumbe za rambirambi.
Miongoni mwa waliojitokeza kuomboleza katika makazi ya kifahari ya familia ya Chivayo jijini Harare kabla ya mazishi yake ya Alhamisi alikuwa Cleopas Mukungunugwa, mwanamitandao anayeunga mkono chama kikuu cha Zanu-PF na ambaye aliwahi kupewa magari mawili ya kifahari na "Sir Wicknell".
Akizungumza nje ya jumba hilo, mbele ya bango kubwa lenye picha ya wanandoa hao, Mukungunugwa alisema ameguswa sana na kifo cha mfadhili wake. Alieleza kuwa "Sir Wicknell" alikuwa akimshauri mara kwa mara kuhusu maudhui ya machapisho yake mtandaoni.
"Alikuwa akikosolewa sana mitandaoni, na jukumu letu lilikuwa kusaidia kujenga taswira yake kama mtu mwenye moyo wa kusaidia na anayejali jamii," alisema.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Chivayo aliacha shule ya sekondari akiwa na umri wa miaka 15, baada ya familia yake kushindwa kumudu ada kufuatia kifo cha baba yake alipokuwa na umri wa miaka 10.
Kazi yake ya kwanza ilikuwa ya karani wa mishahara katika kampuni ya mabasi. Baadaye alijitosa katika biashara binafsi ya kuuza simu za mkononi na kubadilisha fedha za kigeni, mara nyingi kupitia soko haramu wakati Zimbabwe ilipokuwa ikikabiliwa na mfumuko mkubwa wa bei.
Mwaka 2005, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani baada ya kupatikana na hatia ya utakatishaji fedha iliyohusisha rand 837,000 za Afrika Kusini. Alitumikia miaka mitatu katika Kuu la Chikurubi huku miaka miwili ya adhabu yake ikisitishwa.
Maelezo kuhusu shughuli zake za kibiashara baada ya kuachiwa hayako wazi, lakini baadaye aliingia katika sekta ya nishati na kujijengea sifa kama kile ambacho gazeti moja la serikali liliita "tenderpreneur" , yaani mfanyabiashara anayenufaika kwa kupata zabuni za serikali.
Aliongoza kampuni ya Intratrek Zimbabwe, iliyoshirikiana na kampuni kubwa ya umeme ya China, CHiNT Electric. Ushirikiano huo ulifanyika katika kipindi ambacho Zimbabwe ilikuwa ikitekeleza sera ya kuwahamishia wazawa Weusi sehemu ya umiliki na udhibiti wa kampuni za kigeni.
Mwaka 2014, Intratrek ilichaguliwa kujenga kituo cha kuzalisha umeme wa jua chenye uwezo wa megawati 100 mjini Gwanda, kusini mwa Zimbabwe. Mkataba wenye thamani ya zaidi ya dola milioni 170 ulitiwa saini mwaka uliofuata, lakini baadaye ukawa chanzo cha moja ya mijadala mikubwa zaidi katika shughuli zake za kibiashara.
Kampuni ya umeme ya Zimbabwe, ilitishia kusitisha mkataba huo baada ya Intratrek kushindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati. Hata hivyo, mahakama iliamua kuwa makubaliano hayo yalikuwa halali na yanastahili kuzingatiwa.
Baadaye, uchunguzi wa bunge uliitaja Intratrek kama "kampuni hewa", ukidai ilitumika zaidi kama daraja la kuvutia uwekezaji kuliko kampuni yenye uwezo wa kutekeleza mradi huo.
Chivayo mwenyewe alikiri kuwa Intratrek haikuwa na utaalamu wa kujenga mitambo ya umeme wa jua, akisema jukumu lake lilikuwa kuwa mshirika wa ndani huku CHiNT ikitoa utaalamu wa kiufundi.
Ijapokuwa kampuni hiyo ilipokea zaidi ya dola milioni tano kama malipo ya awali kwa mradi wa Gwanda, kituo hicho hakijajengwa hadi leo. Wiki chache kabla ya kifo chake, Intratrek ilikuwa imepewa kibali cha kuendelea na mradi huo na kuukamilisha ndani ya muda wa miezi 24.
Licha ya tuhuma na mabishano yaliyomzunguka, Chivayo mara nyingi alionekana kutoyumbishwa. Kwa tabasamu na haiba yake ya kuvutia, aliweza kuhimili misukosuko ya kisiasa na kibiashara, na hatimaye kujenga uhusiano wa karibu na Rais Emmerson Mnangagwa, ambaye mwanzoni hakuonekana kuvutiwa naye alipoingia madaraka.
Mwaka 2018, Mnangagwa aliutaja mradi wa Gwanda kama mfano wa hatari ya kufanya biashara na "wafanyabiashara wasioleweka wanaoibuka na kutoweka", akionya kuwa "Gereza la Chikurubi bado halijajaa". Gazeti la serikali la The Herald liliripoti kuwa kauli hiyo ilielekezwa kwa Chivayo.
Hata hivyo, ndani ya miaka michache, uhusiano kati yao ulibadilika kwa kiasi kikubwa. Katika baadhi ya picha zilizochapishwa hadharani, Chivayo alionekana akiwa ametulia kwa mazoea makubwa karibu na rais, jambo lililoonyesha ukaribu usio wa kawaida kati yao.
Ushawishi wake haukuishia ndani ya Zanu-PF pekee. Pia aliwahi kuchapisha picha akiwa na viongozi wa upinzani, akiwemo Morgan Tsvangirai marehemu na Nelson Chamisa.
Hata hivyo, kadiri miaka ilivyopita, alionekana kuwa mmoja wa watu waliokuwa karibu zaidi na Mnangagwa. Mara kwa mara alimpongeza rais huyo hadharani na hakuficha uungaji mkono wake kwa chama tawala cha Zanu-PF.
Pia alikabiliwa na tuhuma kuhusu ununuzi wa vifaa vya uchaguzi mkuu wa 2023 uliompa Mnangagwa muhula wa pili madarakani.
Uchunguzi ulidai kuwa kampuni ya Afrika Kusini ya Ren-Form ilipandisha bei kupita kiasi na baadaye ikalipa mamia ya mamilioni ya rand kwa kampuni iliyohusishwa na Chivayo. Alikanusha kuhusika na makosa yoyote, huku Tume ya Kupambana na Ufisadi ya Zimbabwe baadaye ikisema haikupata ushahidi wa kumhusisha na udanganyifu huo. Ren-Form nayo ilikanusha tuhuma hizo.
Mwezi Aprili mwaka huu, Chivayo aliwaahidi wabunge wote 360 wa Zimbabwe dola 10,000 kila mmoja, hatua iliyozua tuhuma kwamba alikuwa akijaribu kushawishi mjadala kuhusu marekebisho tata ya Katiba yaliyolenga kuongeza muda wa utawala wa Mnangagwa hadi mwaka 2030.
Kutokana na ukosoaji mkali uliofuata, alilazimika kufuta ahadi hiyo, huku akisisitiza kwamba haikuwa na lengo la kushawishi kura ya wabunge.
Miezi kadhaa baadaye, baada ya sheria hiyo kutiwa saini, Zanu-PF ilichapisha video ya Chivayo akishangilia ndani ya ndege yake ya kifahari aina ya Gulfstream G550, akiimba kwa furaha: "2030 ndeya Emmerson Baba!".

Chanzo cha picha, Zanu-PF
Ukaribu wake na viongozi wenye mamlaka ulikuwa sehemu muhimu ya taswira aliyojijengea kwenye mitandao ya kijamii. Mwezi Juni, Mfalme Mswati III wa Eswatini alimpa uraia wa nchi hiyo pamoja na pasipoti ya kidiplomasia. Picha na video zilizosambaa zilimuonyesha akipiga magoti mbele ya mfalme huyo wakati wa hafla ya kukabidhiwa hadhi hiyo.
Chivayo pia alipenda kuonyesha mahusiano yake na baadhi ya viongozi mashuhuri barani Afrika. Miongoni mwa picha alizowahi kuchapisha ni zile akiwa na Rais Bola Tinubu wa Nigeria, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, rais wa zamani wa Malawi Peter Mutharika, Rais Daniel Chapo wa Msumbiji na Rais Hakainde Hichilema wa Zambia. Mapema mwaka huu, alikuwa pia miongoni mwa ujumbe uliokutana na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini wakati wa ziara yake katika shamba la Rais Emmerson Mnangagwa.
Kwa baadhi ya viongozi, uhusiano huo ulionekana kuvuka mipaka ya mikutano rasmi. Mwezi Agosti, Chivayo na mkewe walikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria sherehe ya uchumba ya Charlene, binti ya Rais William Ruto wa Kenya, iliyofanyika nyumbani kwa familia ya rais huyo.
Baadaye, Ruto mwenyewe aliendesha gari lililowapeleka wanandoa hao hadi kwenye helikopta iliyokuwa ikiwasubiri. Chivayo alirekodi safari hiyo akiwa ameketi kwenye kiti cha abiria na, kama ilivyokuwa kawaida yake, akasema kwa kujigamba: "Ninaendeshwa na rais wa jamhuri. Mungu ni mkuu."
Baada ya kifo chake, Ruto alimuenzi kupitia mtandao wa X, akisema atakumbuka urafiki wake, uchangamfu wake na imani yake katika mustakabali wa Afrika.
Hata hivyo, nchini Kenya, ukaribu wa Chivayo na rais ulizua maswali na mijadala mikubwa, hasa kwenye mitandao ya kijamii kufuatia kifo chake.
Ingawa sehemu kubwa ya maoni hayo hayawezi kuchapishwa, baadhi ya wakosoaji walielezea wazi kutoridhishwa kwao. Mwanablogu wa Kenya, Cyprian Nyakundi, alisema: "Kama Mkenya, najitenga kabisa na sifa ambazo Rais Ruto amempa Wicknell Chivayo. Maneno hayo ya rambirambi na kumwita 'rafiki mpendwa' ni ya rais mwenyewe, si kwa niaba yangu wala ya Wakenya wote."
Ukosoaji huo ulienda mbali zaidi. Mchangiaji mmoja kwenye mtandao wa X alidai kuwa kifo cha Chivayo "kiliwaunganisha Waafrika katika kusherehekea".
Katika ujumbe mwingine ulioakisi hisia za baadhi ya wakosoaji wake, aliandika: "Kifo cha mtu kinapoleta ahueni kuliko huzuni, mwitikio huo wenyewe unasimulia hadithi nzito. Ni wakati wa wenye mamlaka kutafakari na kujitathmini upya."

Chanzo cha picha, @sir_wicknell
Hata baada ya kifo chake, mjadala kuhusu urithi wa Chivayo umeendelea kutawala mazungumzo nchini Zimbabwe. Wapo wanaoamini kuwa haifai na sio jambo la heshima kumkosoa mtu aliyefariki, wakisema ni kinyume na maadili ya Kiafrika. Lakini wengine wanasisitiza kuwa kifo hakiwezi kufuta maswali kuhusu maisha na matendo ya mtu.
Akizungumza katikati ya jiji la Harare mwishoni mwa wiki, Christabel Moyo, mhasibu mwenye umri wa miaka 42, alieleza mtazamo unaoshikiliwa na baadhi ya wakosoaji wa mfanyabiashara huyo.
"Utamaduni wa Kiafrika ni upi hasa? Kutajirika kupitia mikataba ya serikali yenye bei zilizopandishwa na kisha kutumia fedha hizo kuunga mkono Zanu-PF?" alihoji.
"Alikuwa akigawa magari na fedha taslimu kwa watu ambao tayari walikuwa na uwezo, wakati mfumo wa afya ya umma nchini Zimbabwe ukiendelea kudorora."
Hata hivyo, kampeni yake ya utoaji zawadi ndiyo huenda ikawa sehemu itakayokumbukwa zaidi katika urithi wake. Tangu karibu mwaka 2023, Chivayo alijijengea sifa kwa kuwagawia wanamuziki, wanamichezo, wafanyabiashara, wanasiasa na viongozi wa dini magari pamoja na fedha taslimu. Kwa wafuasi wake, huo ulikuwa ukarimu wa kipekee; kwa wakosoaji wake, ulikuwa mkakati wa kujenga ushawishi na kuimarisha nafasi ya chama tawala cha Zanu-PF.
Mwanzoni, zawadi hizo zilikuwa magari ya kawaida aina ya Toyota Aqua. Baadaye, thamani yake iliongezeka haraka na kujumuisha magari ya kifahari pamoja na fedha nyingi taslimu.
Miongoni mwa walionufaika zaidi alikuwa mwanamuziki maarufu Jah Prayzah, anayejulikana kwa ukaribu wake na Zanu-PF. Katika kipindi cha miaka mitatu, alipokea magari matatu ya kifahari na takriban dola 400,000 za Marekani.
Baada ya ajali ya helikopta iliyogharimu maisha ya Chivayo na mkewe, Jah Prayzah aliahirisha harusi yake iliyokuwa imepangwa kufanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
"Wicknell alikuwa zaidi ya rafiki kwetu," alisema.
Miongoni mwa watu wengine walionufaika kwa kiasi kikubwa alikuwa Askofu Nehemiah Mutendi, kiongozi wa Kanisa la Zion Christian Church, ambalo lina uhusiano wa karibu na Zanu-PF. Kanisa hilo lilipokea michango ya fedha na magari manne ya kifahari kutoka kwa Chivayo.
Mfanyabiashara huyo pia alikuwa mhudhuriaji wa mara kwa mara wa ibada za Johane Masowe weChishanu, mojawapo ya makanisa makubwa ya kitume nchini Zimbabwe, ambalo waumini wake huabudu nje wakiwa wamevalia mavazi meupe.
Kanisa hilo nalo lilinufaika kwa kupokea magari, mabasi na fedha taslimu kutoka kwake. Wakati huo huo, Chivayo alionekana kutumia ushawishi wake kuimarisha uhusiano kati ya kundi hilo kubwa la kidini na chama tawala. Juhudi hizo zilidhihirika mwezi Agosti, alipomwalika Rais Emmerson Mnangagwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano mkubwa wa kanisa hilo.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Lakini si kila mtu aliyevutiwa na ukarimu wa Chivayo. Eunor Guti, mjane wa mwanzilishi wa Zimbabwe Assemblies of God Africa (ZAOGA), Askofu Mkuu Ezekiel Guti, alikataa gari la kifahari pamoja na dola 250,000 taslimu alizopewa na mfanyabiashara huyo.
Mwaka 2024, mwanamuziki mkongwe na mkosoaji wa serikali, Thomas Mapfumo, ambaye anaishi nchini Marekani, pia alikataa zawadi ya gari la kifahari na nyumba kutoka kwa Chivayo, akisema hawezi "kuhongwa" na baadaye kudai kwa fedha hizo ni "chafu".
Hata hivyo, msimamo huo ulionekana kulegea mwaka huu alipopokea dola milioni moja ili kutumbuiza katika harusi ya Jah Prayzah na katika sherehe ya siku ya kuzaliwa ya Chivayo iliyokuwa imepangwa kufanyika mwezi Novemba.
Hatua hiyo ilizua mjadala miongoni mwa baadhi ya mashabiki wa muda mrefu wa Mapfumo. Baada ya msanii huyo mwenye umri wa miaka 81 kuwasili Harare muda mfupi kabla ya ajali ya helikopta, alikabiliwa na ukosoaji kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa waliomtuhumu kuachana na msimamo wake wa awali. Hata hivyo, alikanusha tuhuma hizo.
Ukarimu wa Chivayo haukuwalenga watu binafsi pekee. Pia alitoa magari 20 ya kubebea wagonjwa kwa mfumo wa afya wa umma wa Zimbabwe na kuchangia mabasi pamoja na misaada mingine kwa shule mbalimbali.
Watu waliokuwa karibu naye wanasisitiza kuwa matendo yake ya hisani hayakuwa ya kujionyesha tu. Wakili maarufu Wilson Manase alisema kuwa alipougua akiwa Dubai, Chivayo alisafiri kwenda kumtembelea.
Katika mahojiano na shirika la utangazaji la serikali, ZBC, Manase, ambaye alikuwa miongoni mwa watu walioahidiwa gari katika ujumbe wa mwisho wa Chivayo kwenye mtandao wa X, alimwelezea kama mtu mwenye "moyo safi" na imani kubwa ya dini.
Chivayo ameacha watoto wawili aliowapata na mke wake wa kwanza, Sonja Madzikanda. Wawili hao walitengana mwaka 2024 na walikuwa bado wanakabiliana na mgogoro wa kisheria kuhusu makubaliano ya talaka yao.
Licha ya utajiri na maisha ya fahari aliyoyaishi, Chivayo alionekana kujivunia asili yake. Siku ya kifo chake, alikuwa ametembelea kijiji cha Gandami, kusini mashariki mwa Harare, ambako alikuwa akijenga jumba la thamani ya dola milioni moja lenye vyumba vinane vya kulala.
Jumba hilo lilitarajiwa kuzinduliwa rasmi mwezi Novemba wakati wa maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa. Chivayo alikuwa akijigamba kuwa mradi huo ungeleta hadhi ya "Borrowdale Brooke hadi Gandami", akirejelea mojawapo ya maeneo ya kifahari zaidi jijini Harare.
Pia alikuwa ameahidi kutoa dola 500,000 kwa ajili ya kuboresha shule za msingi na sekondari pamoja na zahanati katika eneo hilo.
Kifo chake kinaiacha Zanu-PF bila mmoja wa watu wake mashuhuri zaidi waliokuwa wakitumia utajiri, ushawishi na umaarufu wao kuunga mkono chama hicho hadharani.
Hata hivyo, nyuma ya maisha yake ya anasa na ukarimu, bado yamebaki maswali ambayo hayajajibiwa kikamilifu. Kwa wengi nchini Zimbabwe, fumbo kubwa linaendelea kuwa jinsi alivyoibuka kutoka maisha ya kawaida na yenye changamoto hadi kuwa mmoja wa watu matajiri zaidi nchini, mwenye uwezo wa kugawa mamilioni ya dola na zawadi za gharama kubwa kwa urahisi mkubwa.
Ish Mafundikwa ni mwandishi wa habari huru anayeishi Harare.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi
































