Marekani yaongeza vikwazo dhidi ya mtandao wa kifedha wa Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Utawala wa Rais Donald Trump umeiwekea Iran vikwazo vipya, ikilenga watu na taasisi kadhaa ambazo Marekani inazituhumu kuhusishwa na mfumo wa kifedha wa siri wa Iran, unaojulikana kama “Shadow Banking System”, kulingana na taarifa iliyochapishwa hapo jana kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha ya Marekani.
Wizara ya Fedha ya Marekani imewaongeza watu wanane wenye uhusiano na Iran pamoja na taasisi 22 zilizoko Iran, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Uturuki na Hong Kong kwenye orodha ya waliowekewa vikwazo.
Wizara hiyo imesema kuwa Mtandao wa Utekelezaji wa Uhalifu wa Kifedha (FinCEN) umebaini shughuli za kifedha zenye thamani ya takribani dola bilioni 14.7 kati ya Januari 2025 na Agosti 2026, ambazo zinaaminika kuhusishwa na mfumo huo wa kifedha wa siri wa Iran.
Taarifa hiyo pia imesema kuwa Kituo cha Ubadilishanaji wa Fedha na Dhahabu cha Iran, kilichoanzishwa takribani miaka mitatu iliyopita kwa idhini ya Benki Kuu ya nchi hiyo, kimeongezwa kwenye orodha ya waliowekewa vikwazo.
Kulingana na Wizara ya Fedha ya Marekani, mfumo wa kifedha wa siri wa Iran hutumika kuhamisha fedha zinazotokana na biashara ya kimataifa ya nchi hiyo, huku Kituo cha Ubadilishanaji wa Fedha cha Iran kikifanya kazi kama mpatanishi na kuwezesha rasilimali hizo za kifedha kufika kwenye maeneo yanayokusudiwa ndani ya Iran.
Vikwazo hivyo vya kiuchumi vya Marekani, ambavyo vimekuwa vikiongezwa katika miezi ya hivi karibuni, ni sehemu ya kampeni inayoendelea ya kuitenga Iran kiuchumi, ili kudhibiti maslahi yake ya kifedha pamoja na mitandao yake ya kifedha katika mataifa mbalimbali duniani.
Soma pia:

