Mtu aliyeishi siku 555 bila moyo

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Mwili wa binadamu una uwezo wa ajabu wa kustahimili hali ngumu, kama inavyoonyeshwa na visa vingi vya watu walioendelea kuishi licha ya kupoteza baadhi ya viungo vyao.

Historia ya tiba inaonesha kwamba mwili wa binadamu kwa wastani una uwezo mkubwa wa kustahimili hali ngumu kuliko tunavyoweza kudhani. Kuna visa vya ajabu vilivyoandikwa, kama vile mwanaume mmoja wa Ufaransa aliyegundulika mwaka 2007 kuwa anaishi bila takribani asilimia 90 ya ubongo wake.

Mtu huyo mwenye umri wa miaka 44 alikuwa akiishi maisha ya kawaida wakati madaktari walipogundua kwamba alikuwa na hali kali ya haidrocefalia, ambapo tishu za ubongo hubadilishwa kwa kiasi kikubwa na maji ya ubongo na uti wa mgongo (cerebrospinal fluid).

Hiki ni kielelezo cha kushangaza cha uwezo wa mwili kujibadilisha na kukabiliana na upungufu wa tishu. Tishu za ubongo zilizobaki zinaweza kwa kiasi fulani kuchukua majukumu ya tishu zilizopotea, katika hali hii, kupitia mchakato unaojulikana kama neuroplasticity, yaani uwezo wa ubongo kujipanga upya na kubadilisha jinsi unavyofanya kazi.

Jambo kama hilo linaweza kutokea pia katika viungo vinavyokuja kwa jozi, kama vile mapafu, figo au korodani. Ikiwa kimoja kitapotea, kiungo kilichobaki kinaweza kuchukua jukumu la viungo vyote viwili.

Katika hali nyingine, teknolojia ya ajabu ya kitabibu huwasaidia watu kuendelea kuishi baada ya kupoteza viungo muhimu vya mwili.

Kwa mfano, kijana mmoja wa Marekani alibeba moyo bandia unaofanya kazi ndani ya mkoba kwa siku 555, baada ya moyo wake mwenyewe kuondolewa lakini kabla ya kupata nafasi ya kupandikiziwa moyo mwingine.

Katika hali zinazoitwa "empty chest cases", madaktari wa upasuaji huondoa moyo na mapafu ya mgonjwa, na kazi za viungo hivyo hubadilishwa na mfumo wa kusaidia maisha unaoitwa extracorporeal membrane oxygenation (ECMO).

Pia kuna mifano ya watu walioishi bila viungo vingi vya mwili.

Baadhi ya wagonjwa wenye saratani ya tumbo huhitaji kuondolewa viungo kadhaa vya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula, ambavyo vinaweza kujumuisha tumbo lote, wengu, kongosho, utumbo mwembamba na utumbo mpana.

Katika hali hizi, wagonjwa wanaweza kuendelea kuishi kwa kutumia mchanganyiko wa dawa za kurejesha vimeng'enya, lishe iliyorekebishwa na lishe inayotolewa kwa njia ya mshipa, pamoja na insulini ya kuchukua nafasi ya ile ambayo mwili hauwezi tena kuzalisha.

Viungo vingine vya ndani vya mwili ambavyo mtu anaweza kuishi bila kuwa navyo ni kibofu cha nyongo, kibofu cha mkojo, tezi ya thyroid na appendix.

Haijulikani wazi ikiwa kuna kikomo cha idadi ya viungo ambavyo mtu anaweza kuishi bila kuwa navyo kwa wakati mmoja, ingawa kupoteza viungo kadhaa katika tukio moja kunaweza kusababisha kifo kutokana na kupoteza damu nyingi, maambukizi au majeraha makubwa ya mwili.