Trump aanzisha kituo kipya cha habari huku vyombo vya habari vikichukua hatua
Ikulu ya Marekani imezindua kituo cha televisheni mtandaoni kinachoitwa Trump TV, hatua inayokuja saa chache baada ya mitandao mikubwa ya televisheni nchini humo kusitisha kwa pamoja matangazo yao kutoka Ikulu.
Hatua hiyo ya vyombo vya habari imekuja baada ya Rais Donald Trump kuzuia CNN, MS NOW na Politico kuingia Ikulu, akivituhumu kwa kusambaza taarifa za uongo. Vyombo hivyo vimefungua kesi dhidi ya utawala wa Trump, vikidai hatua hiyo inakiuka haki zao za kikatiba za uhuru wa vyombo vya habari.
Tovuti ya Ikulu imeeleza Trump TV kuwa “kituo muhimu cha kupata taarifa muhimu”.
Katika taarifa yake, utawala wa Trump umesema kupata fursa ya kufanya kazi Ikulu ni “upendeleo, si haki” kwa kila mtu. Pia umesema rais halazimiki kuruhusu kile ilichokiita chombo cha habari chenye uhasama kufanya kazi ndani ya Ikulu.
Wakati huo huo, mitandao mingine mikubwa ya televisheni, ikiwemo ABC, CBS, NBC na Fox News, imesitisha matangazo ya matukio ya rais kwa kutumia mfumo wa pamoja wa kuripoti Ikulu, kufuatia kuzuiwa kwa CNN.
CNN, MS NOW na Politico zimesema zitapinga hatua hiyo mahakamani, zikidai kuwa inalenga kuzuia kazi yao ya uandishi wa habari na inakiuka uhuru wa vyombo vya habari.