Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Msemaji wa IRGC: Ikiwa Marekani itafanya shambulio jipya, tutatumia silaha zitakazoishangaza dunia

Hossein Mohebbi, msemaji wa Walinzi wa Mapinduzi, alionya kwamba iwapo Marekani itafanya shambulio jipya dhidi ya Iran, Iran itatumia "silaha mpya" na kushambulia maeneo ambayo hayajalengwa hadi sasa

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid & Abdalla Seif Dzungu

  1. Xhaka achunguzwa kuhusiana na cheti bandia cha Covid-19

    Nahodha wa Uswizi, Granit Xhaka, anachunguzwa na waendesha mashtaka wa Uswizi kufuatia madai kuwa alipata cheti bandia cha chanjo ya Covid-19.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 anadaiwa kupata cheti hicho mwaka wa 2022, wakati ambapo kilikuwa sharti nchini Uswizi kwa ajili ya safari fulani za kwenda nje ya nchi.

    Ofisi ya mwendesha mashtaka wa umma wa jiji la Lucerne ilithibitisha kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini iwapo kulikuwa na kitendo chochote cha uhalifu katika kupata cheti hicho "kisicho sahihi au ghushi".

    Kiungo huyo wa Sunderland, ambaye wakati huo alikuwa akiichezea Arsenal, alitoa taarifa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumatatu akisema alikuwa na "mashaka" kuhusu chanjo hiyo na kwamba alikuwa "ameathiriwa na hofu na kutokuwa na uhakika".

    Alisema: "Katika hali hiyo ya kuchanganyikiwa kifikra, nilipata cheti cha chanjo badala ya kutafuta majibu sahihi ya maswali yangu ambayo hayakupata ufafanuzi.

    "Leo naona wazi kuwa njia hiyo haikuwa sahihi. Ilikuwa ni makosa. Samahani.

    "Ninachukua jukumu la uamuzi huu, nitashiriki katika mchakato wa kubaini ukweli na kushirikiana kikamilifu na mamlaka husika."

    Ofisi ya Afya ya Umma ya Uswizi ilithibitisha kuwa, ingawa hakukuwa na sheria ya jumla inayolazimisha kupata au kuwa na cheti hicho, kilikuwa kikihitajika ili kushiriki katika shughuli mbalimbali, kuingia maeneo fulani na kusafiri; hivyo basi, ushiriki ulizuiwa kwa yeyote ambaye hakuwa nacho.

    Hatua hizo nchini Uswizi zilitekelezwa hadi majira ya kuchipua ya mwaka wa 2022.

    Baada ya hapo, vyeti vya Covid-19 viliendelea kutolewa, hasa ili kuwawezesha wananchi kukidhi masharti ya kuingia nchi nyingine wakati wa kusafiri nje ya nchi.

    Shirikisho la Soka la Uswizi lilisema kuwa Xhaka mchezaji aliyechezea timu ya taifa mara nyingi zaidi kuliko mwingine yeyote nchini humo, akiwa na rekodi ya mechi 152 alijiondoa katika kambi ya timu ya taifa kwa ajili ya mechi zijazo za Ligi ya Mataifa (Nations League) dhidi ya Scotland, Macedonia Kaskazini na Slovenia kufuatia taarifa yake.

  2. Washington Post: Idadi ya wanajeshi wa Marekani waliouawa katika vita dhidi ya Iran ni zaidi ya inayoripotiwa

    Idadi ya vifo vya wanajeshi wa Marekani katika vita dhidi ya Iran imezidi takwimu za Pentagon kwa angalau watu wanne

    Gazeti la Washington Post liliripoti siku ya Ijumaa, likinukuu maafisa sita wa Marekani, kwamba idadi ya vifo vya wanajeshi wa Marekani katika vita dhidi ya Iran ni kubwa kuliko takwimu zilizotangazwa hadharani na Pentagon.

    Gazeti hilo, likinukuu maafisa watano wanaofahamu takwimu za ndani za Wizara ya Ulinzi kuhusu wanajeshi waliouawa, lilisema kuwa angalau wanajeshi 22 walikuwa wameuawa idadi inayozidi ile iliyo katika hifadhidata ya umma ya Pentagon kwa watu wanne.

  3. Poland yajiunga na muungano wa Ukraine wa " kuzuia makombora ya balistiki"

    Waziri Mkuu wa Poland, Donald Tusk, alitangaza Ijumaa kuwa nchi hiyo, pamoja na Ukraine na washirika wengine, imejiunga na muungano wa kukabiliana na makombora ya balistiki.

    "Kuanzia leo, Poland ni sehemu ya mradi huu mkubwa... Tumekubaliana kuhusu namna na mfumo wa ushirikiano huu," Bw. Tusk alisema katika video iliyowekwa kwenye mtandao wa X.

    Habari hizi zinakuja baada ya Bw. Tusk kuhudhuria mkutano wa viongozi wa kundi jipya la kikanda la nchi nane katika Milima ya Carpathian, uliofanyika magharibi mwa Ukraine kwa mpango wa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky.

    Mnamo mwezi Julai, Ukraine na nchi tisa za Ulaya zilitangaza kuundwa kwa muungano wa ulinzi wa anga unaohusisha uundaji wa pamoja wa mfumo mpya wa kukabiliana na makombora ya balistiki, ukiwa mbadala wa gharama nafuu zaidi kuliko mfumo wa Patriot wa Marekani.

    Waziri Mkuu huyo wa Poland alitangaza katika mkutano na waandishi wa habari kuwa nchi yake imeandaa kifurushi kipya na "muhimu" cha msaada kwa Ukraine, lakini hakutoa maelezo zaidi.

    Pia alisema: "Poland lazima iunge mkono Ukraine katika mapambano dhidi ya uchokozi wa Urusi... Historia haiwezi kututenganisha na Urusi."

  4. Gary Neville aiita Man Utd 'ya kusikitisha' - lakini Carrick adumisha imani

    Gary Neville alivuta pumzi ndefu baada ya bao la kujifunga la Lisandro Martinez kuipa Fulham uongozi wakati mchezo ukiwa umepita zaidi ya saa moja huku Manchester United ikionyesha kiwango duni na cha kusikitisha kisha akatoa tathmini yake.

    Nahodha huyo wa zamani wa United huwa haishiwi na maneno makali ya ukosoaji, lakini hata kwa viwango vyake, kauli hii ilikuwa ya kulaumu sana.

    "Nimekuwa nikiiangalia Manchester United tangu nikiwa na umri wa miaka mitano na hizo ndiyo dakika 15 mbaya zaidi kuwahi kuziona," alisema. "Ni mhcezo wa kusikitisha na wa aibu.

    "Sijawahi kuona ukosefu wa juhudi kama huu. Je, [Michael] Carrick anawaza nini?"

    Ili kuweka mambo katika muktadha, Neville alikuwa sehemu ya kikosi cha United kilichofungwa mabao 3-1 na wapinzani wao wa Jumapili, Fulham, katika uwanja wa Old Trafford mnamo Oktoba 2003.

    Katika siku za hivi karibuni, pia wamepoteza kwa mabao 7-0 dhidi ya Liverpool na 6-1 wakiwa nyumbani mara mbili, dhidi ya Tottenham na Manchester City.

    Maneno hayo ya Neville yalikuja baada ya kipindi kibaya cha dakika 15 kuanzia mwanzoni mwa kipindi cha pili hadi wakati huo wa kujifunga kwa Martinez kabla ya United kufanikiwa kupata sare ya 1-1 kutokana na shuti la Matheus Cunha lililobadili mwelekeo baada ya kugonga mchezaji mwingine katika dakika ya 89.

  5. Zaidi ya watu milioni 1.6 watakiwa kuhama huku kimbunga kikali kikitishia Japan

    Zaidi ya watu milioni 1.6 wameambiwa kuhama makazi yao kutokana na Kimbunga Dujuan.

    Wizara ya Mambo ya Ndani ya Japan inasema kuwa watu 1,674,084 katika maeneo ya Ibaraki, Chiba, Tokyo, Kanagawa na Shizuoka wamehusishwa na amri za kuhama.

    Uhamishaji huo si wa lazima.

    Shirika la Hali ya Hewa la Japan linasema "kuna uwezekano mkubwa sana kwamba aina fulani ya maafa tayari imetokea katika maeneo yaliyo hatarini kupata maporomoko ya ardhi na maeneo mengine yanayofanana na hayo," na linawasihi watu kuhakikisha usalama wao "mara moja," huku likionya kuwa "kuna tishio la karibu kwa maisha."

  6. Msemaji wa IRGC: Ikiwa Marekani itafanya shambulio jipya, tutatumia silaha zitakazoishangaza dunia

    Hossein Mohebbi, msemaji wa Walinzi wa Mapinduzi (IRGC), alionya kuwa iwapo Marekani itafanya shambulio jipya dhidi ya Iran, Iran itatumia "silaha mpya" na "kubadili jiografia ya vita" kwa kushambulia maeneo ambayo hayajalengwa hadi sasa.

    Alisema kuwa Marekani ikishambulia, Iran itatumia silaha mpya zitakazo "ishangaza" dunia.

    Alieleza kuwa Iran imetengeneza silaha na kuimarisha uwezo wake wa kijeshi kwa njia ambazo hazijatumika katika hatua ya sasa ya vita.

    Alizitaja silaha hizo kuwa ni za "kimkakati" ambazo zitatumika "ikiwa ni lazima" na kwamba "dunia itaona kitakachotokea." Kuhusu kubadilika kwa jiografia ya vita, msemaji huyo wa IRGC pia alisema, "Vita sasa vimekuwa vya kikanda, lakini kwa kuwa eneo hilo ni kubwa sana, bado kuna nafasi ya vita hivi kupanuka kijiografia." Alisema jeshi linajiandaa kwa ajili ya "vita vya muda mrefu."

    Onyo hilo la msemaji wa IRGC linakuja baada ya Makao Makuu ya Kati ya Khatam al-Anbiya kutoa taarifa ikisema kuwa Marekani inakusudia kuanza upya hatua zake kwa "idhini" (taa ya kijani) kutoka kwa baadhi ya nchi za eneo hilo.

    Makao Makuu ya Khatam al-Anbiya, ambayo ni taasisi ya juu zaidi ya kijeshi ya Iran wakati wa vita, yalisema kuwa Iran imepata taarifa kwamba Marekani na Israel zilishiriki katika mkutano uliofanyika katika nchi ya Ulaya pamoja na nchi kadhaa za eneo hilo.

  7. Trump anasema atawazuia waandishi wa habari wa CNN kuingia Ikulu ya Marekani

    Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza siku ya Ijumaa, katika hatua isiyo na kifani, kwamba atawazuia waandishi wa habari kutoka vyombo vitatu vya habari—CNN, MSNBC, na Politico kuingia Ikulu ya Marekani (White House) kutokana na kile alichokiita "habari za uongo."

    Donald Trump aliandika katika chapisho kwenye mtandao wa Truth Social siku ya Ijumaa kwamba vyombo hivyo vya habari "huandika au kuripoti mara kwa mara habari au uongo" kuhusu utawala wake, ingawa hakutoa mifano yoyote.

    Bado haijafahamika wazi iwapo wafanyakazi wa vyombo hivyo vya habari watakatazwa kuingia katika eneo la Ikulu ya Marekani.

    CNN ilijibu haraka hatua hiyo, ikilaani kitendo hicho kama "shambulio lisilo halali" dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Marekani.

    Donald Trump alijibu maswali ya waandishi wa habari katika Ofisi ya Oval muda mfupi baada ya tangazo hilo, akisema kuwa "wengine wanaweza kuungana nao," lakini hakutaja chombo chochote mahususi cha habari.

    Pia alikiri kwamba changamoto za kisheria zinaweza kujitokeza kufuatia tangazo hilo, akisema, "Nadhani ni vyema kuweka hili wazi, iwe hatua hii itadumu au la."

  8. Waokoaji wasaka manusura baada ya mgodi kuporomoka Sudan

    Operesheni ya uokoaji inaendelea kuwatafuta manusura walionaswa chini ya ardhi baada ya mgodi kuporomoka na kuua watu 11 na kujeruhi wachimbaji wasiopungua 30 katika jimbo la Bahari ya Shamu, Sudan.

    Kwa mujibu wa wachimbaji waliozungumza na shirika la habari la Associated Press, ajali hiyo ilitokea Jumamosi usiku katika eneo la Oni, katika ukanda wa uchimbaji madini wa Jebeit, takriban kilomita 300 kutoka Port Sudan.

    Taarifa zinaeleza kuwa migodi minne iliporomoka, ingawa bado haijafahamika ni watu wangapi walionaswa chini ya vifusi.

    Wachimbaji na waokoaji wanaendelea kuchimba katika eneo lililoanguka kujaribu kuwafikia manusura.

    Hata hivyo, baadhi ya wachimbaji wameiambia AFP kuwa hakuna operesheni rasmi ya uokoaji inayoendeshwa katika eneo hilo. Wamesema wachimbaji wenyewe wanajaribu kuwafikia walionaswa wakitumia zana za jadi.

    Kampuni ya serikali ya Sudan ya Rasilimali za Madini imethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, lakini haikutoa idadi ya waliofariki au kujeruhiwa.

    Ajali hiyo ni ya pili kubwa katika mgodi wa dhahabu usio rasmi nchini Sudan ndani ya wiki moja. Takriban watu 82 walifariki katika ajali nyingine ya mgodi katika eneo la West Kordofan.

    Ajali za migodi ni za kawaida nchini Sudan, mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa dhahabu barani Afrika, ambako shughuli nyingi za uchimbaji hufanyika bila rasmi na viwango vya usalama havitekelezwi ipasavyo.

    Dhahabu pia inahusishwa kwa karibu na uchumi wa vita nchini Sudan. Umoja wa Ulaya unasema uchimbaji wa dhahabu ni chanzo kikuu cha mapato kwa Jeshi la Sudan (SAF) na kikosi cha kijeshi cha Rapid Support Forces (RSF), hivyo kusaidia kuendeleza vita nchini humo.

    Mnamo Julai 2026, Umoja wa Ulaya ulipiga marufuku ununuzi, uagizaji na uhamishaji wa dhahabu inayotoka Sudan, huku pia ukiweka vikwazo kwa usafirishaji wa zebaki na sianidi kwenda nchini humo.

    Uingereza pia imewawekea vikwazo watu na kampuni zinazodaiwa kutumia dhahabu na mitandao ya kifedha kuunga mkono vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, wakiwemo wafadhili wanaohusishwa na RSF na kampuni za serikali za uchimbaji madini.

  9. Taliban yadai Pakistan imeua watu watatu Afghanistan

    Serikali ya Taliban nchini Afghanistan imedai kuwa mashambulizi ya Pakistan katika majimbo ya Kunar na Paktika yamewaua watu watatu.

    Msemaji wa Taliban, Zabihullah Mujahid, alisema katika mtandao wa X kuwa jeshi la Pakistan lilishambulia maeneo ya makazi usiku wa kuamkia leo.

    Amesema watu watatu, wakiwemo mwanamke mmoja na wanaume wawili, waliuawa na wengine wanne, wakiwemo wanawake wawili, walijeruhiwa.

    Mujahid amesema waliouawa na kujeruhiwa ni raia na wakazi wa maeneo hayo.

    Amesema nyumba moja na duka moja vilishambuliwa katika jimbo la Paktika, lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo.

    Serikali ya Pakistan bado haijajibu madai hayo.

    Mujahid amelaani mashambulizi hayo, akiyataja kuwa ni “uchokozi na ukatili” na kusema yanaendeleza kile alichokiita uhalifu wa zamani.“Uongozi wa kijeshi wa Pakistan umefanya tena uhalifu wa aina hii kwa lengo la kugeuza mawazo kutoka kwa kushindwa kwake kukabiliana na changamoto za usalama nchini humo. Waafghanistan watatoa jibu linalostahili, Mungu akipenda.”

  10. Marekani yaondoa vikwazo dhidi ya Eritrea huku mvutano ukiongezeka Bab al Mandab

    Utawala wa Rais Donald Trump umetangaza kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Jeshi la Ulinzi la Eritrea na baadhi ya taasisi za nchi hiyo. Marekani ilitangaza uamuzi huo Ijumaa iliyopita.

    Ofisi ya Marekani ya Udhibiti wa Mali za Kigeni (OFAC) imesema Marekani imeziondoa Jeshi la Ulinzi la Eritrea, chama tawala cha PFDJ, pamoja na baadhi ya kampuni na watu binafsi, kwenye orodha yake ya vikwazo.

    Hatua hiyo inachukuliwa wakati vita katika Mashariki ya Kati vikizidi kushika kasi, huku macho ya dunia yakielekezwa kwenye Bahari ya Shamu.

    Eritrea ina mwambao mrefu katika Bahari ya Shamu, mkabala na Saudi Arabia.

    Kwa mujibu wa wachambuzi, mwambao huo mrefu na eneo la Eritrea kwenye mojawapo ya njia kuu za usafirishaji wa kibiashara duniani, Bahari ya Shamu, umeongeza umuhimu wa kimkakati wa nchi hiyo.

    Wachambuzi pia wanasema hatua hiyo inaweza kufungua njia mpya kwa Marekani kuboresha uhusiano wake na Eritrea.

    Vikwazo vya Marekani dhidi ya Eritrea vilihusishwa na ushiriki wa nchi hiyo katika vita vya miaka miwili katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia, vilivyoanza mwaka 2020.

    Serikali ya Marekani chini ya Rais wa zamani Joe Biden ilichukua hatua za kumaliza vita kati ya Eritrea na Ethiopia mwaka 2021. Wakati huo, vikosi vya Eritrea viliunga mkono serikali ya Ethiopia na kupigana dhidi ya vikosi vya serikali ya eneo la Tigray.

    Baadaye Marekani iliweka vikwazo dhidi ya jeshi la Eritrea na maafisa kadhaa wa serikali, akiwemo viongozi wa chama tawala.

    Hatua ya Marekani inakuja wakati hali ya usalama katika Mashariki ya Kati ikizidi kuwa tete.

  11. Ethiopia: Makundi 7 yenye silaha yaungana kuipinga serikali

    Makundi saba yenye silaha nchini Ethiopia yametangaza kuunda muungano wenye lengo la kuipindua serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed.

    Muungano huo umejiita Alliance for Survival, yaani Muungano wa Kujiokoa.

    Makundi hayo yamesema serikali ya Abiy Ahmed imepoteza uhalali wa kuongoza nchi na haina utayari wa kufanya mazungumzo na makundi yenye silaha.

    Tangazo hilo linakuja miezi miwili baada ya ripoti kuibuka kwamba makundi yanayopinga serikali yalikuwa yakijiandaa kuunda muungano mpana.

    Makundi hayo yamesema yanalenga kupambana na serikali mjini Addis Ababa na kushinikiza kuundwa kwa serikali ya mpito. Yameonya kuwa Ethiopia inaweza kusambaratika iwapo matatizo ya nchi hiyo hayatapatiwa suluhisho.

    Serikali ya Ethiopia bado haijatoa maoni kuhusu tamko hilo.

    Ethiopia imekuwa ikikabiliwa na mapigano kwa miaka kadhaa katika maeneo ya Oromia na Amhara. Mvutano pia umeongezeka tena katika siku za hivi karibuni katika eneo la Tigray, kaskazini mwa nchi hiyo.

    Wataalamu wanakadiria kuwa vita vya miaka miwili vya Tigray vilisababisha vifo vya mamia ya maelfu ya watu.

    Mamlaka za Tigray zimeishutumu serikali kwa kushindwa kutekeleza kikamilifu makubaliano ya amani ya mwaka 2022 yaliyomaliza vita hivyo.

  12. Mlipuko mkubwa watikisa ghala la silaha Syria

    Mlipuko mkubwa umetokea katika ghala la silaha lililoko viunga vya kusini mwa mkoa wa Aleppo, kaskazini mwa Syria, na kujeruhi watu wasiopungua wanne, kwa mujibu wa taarifa.

    Televisheni ya taifa ya Syria, Al Ikhbariya, pamoja na mashirika mengine ya habari, imeripoti kuwa milipuko hiyo ilitokea karibu na mji wa Al Ais, kusini mwa Aleppo, ambako kwa mujibu wa vyanzo vya eneo hilo kuna ghala la silaha linalohusishwa na Wizara ya Ulinzi ya Syria.

    Shirika la habari la taifa la Syria, SANA, pia limeripoti kuwa milipuko hiyo ilitokea alfajiri katika kituo cha jeshi la Syria karibu na Al Ais.

    Chanzo cha milipuko hiyo bado hakijajulikana. Hata hivyo, baadhi ya vyanzo vimedai kuwa ilisababishwa na mashambulizi ya anga ya Israel, yakilenga ghala lililotumika kuhifadhi silaha za kijeshi zinazoungwa mkono na Uturuki.

    Mamlaka za eneo hilo zimewaagiza wananchi kujiepusha na eneo hilo.

  13. Tetesi za Soka Jumatatu: Spurs walenga kumsajili Gibbs White kwa £125m

    Tottenham Hotspur wameweka lengo la kumsajili kiungo wa Nottingham Forest Morgan Gibbs White, 26, kwa kitita cha hadi pauni milioni 125 katika dirisha la Januari, baada ya kukaribia kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa England katika dirisha la majira ya kiangazi 2025. (Football Insider)

    Manchester United wanamfuatilia kiungo wa Lens, Mezian Mesloub, 16, ambaye ni mchezaji wa kimataifa wa vijana wa Ureno, huku klabu hiyo ikilenga kuimarisha kundi lake la vipaji chipukizi. (Teamtalk)

    Manchester United pia bado wanataka kumbakiza mshambuliaji kijana wa England JJ Gabriel, 15, ambaye amehusishwa na uwezekano wa kujiunga na Real Madrid au Barcelona. Chelsea sasa wamejiunga na mbio za kumsajili kinda huyo. (Teamtalk)

    Manchester United pia wanamfuatilia kocha wa Italia Antonio Conte, 57, kama mmoja wa wanaoweza kuchukua nafasi ya kocha wa sasa Michael Carrick endapo nafasi ya kocha huyo wa zamani wa England katika klabu hiyo itakuwa hatarini. (Hard Tackle)

    AC Milan na Juventus pia wanamfuatilia Conte, ambaye anasubiri fursa inayofaa kuanza mradi wake mpya baada ya kuondoka Napoli mwishoni mwa msimu wa kiangazi.(Calciomercato - in Italian)

    Atletico Madrid wamehuisha nia yao ya kumsajili kinda wa Bayer Leverkusen Ibrahim Maza, 20, huku wakitafuta kuimarisha safu yao ya kiungo. (Goal)

    Liverpool, Manchester City, Fulham na Tottenham ni miongoni mwa klabu kadhaa za Ligi Kuu England zinazomfuatilia beki wa Real Sociedad na timu ya taifa ya Venezuela, Jon Aramburu, 24.

    Liverpool imefanya mazungumzo ya awali na Monaco kuhusu uwezekano wa kumsajili kiungo wa Senegal Lamine Camara, 22, katika dirisha la Januari. (Caughtoffside)

    Arsenal wanamnyatia mshambuliaji wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Ujerumani, Maximilian Beier, 23. (Teamtalk)

    Newcastle United wanakabiliwa na ushindani kutoka Barcelona katika mbio za kumsajili kiungo wa Djurgarden na timu ya taifa ya Norway, Bo Hegland, 22. (Football Insider)

    Soma Pia:

  14. Museveni asema Uganda imepata mpango mpya wa uagizaji mafuta uliopunguza gharama

    Rais wa Uganda Yoweri Museveni amefafanua kauli yake kuhusu mikataba ya serikali kwa serikali, akisema mwanasiasa wa Kenya anayemtaja kwa jina la Jirongo ndiye aliyemweleza kuhusu kile alichodai kuwa kulikuwa na utata katika mpango wa uagizaji wa mafuta kati ya Kenya na Uganda.

    “Ilikuwa Seneta wa Kenya anayejulikana kama Jirongo aliyeniambia kuhusu hili mwaka 2019. Mara moja nilimpa jukumu Waziri wa wakati huo Irene Muloni kushughulikia suala hilo,” Museveni alisema katika ujumbe kwenye mtandao wa X Jumapili jioni.

    Museveni amesema taarifa hiyo ilimfanya kusitisha mfumo huo na kuanza kununua mafuta kwa wingi moja kwa moja.

    Hata hivyo, amesema Uganda haikubadilisha mfumo wake wa ununuzi wa mafuta hadi mwaka 2023, ilipoanza kufanya kazi na kampuni ya kimataifa ya mafuta ya Vitol.

    Museveni amesema mpango huo ulipunguza gharama ya mafuta nchini Uganda. Bei ya dizeli ilishuka kutoka dola 118 hadi dola 83 kwa tani, huku petroli ikishuka kutoka dola 97.5 hadi dola 61.5.

    “Nataka kumshukuru Mheshimiwa Ruto kwa sababu aliwashinda baadhi ya watu nchini Kenya waliokuwa wakipinga. Hivyo ndivyo tulivyopata mpango wetu mpya, na Serikali ya Kenya imeturuhusu kusafirisha bidhaa zetu kupitia bomba la mafuta la Kenya, ambapo Serikali ya Kenya imeturuhusu kuwa na hisa za asilimia 20.15,” alisema.

    Kauli hiyo ilifuatia matamshi ya Museveni Alhamisi, ambapo alisema Uganda ilikuwa ikinunua bidhaa za mafuta kupitia madalali nchini Kenya, badala ya kununua moja kwa moja kutoka serikalini kama ilivyokuwa imeainishwa katika mfumo wa serikali kwa serikali.

    “Jamhuri ya Uganda ilikuwa inanunua bidhaa za mafuta kupitia madalali nchini Kenya. Hebu fikiria hilo. Na mtu wa kwanza kuniamsha kuhusu suala hilo alikuwa seneta kutoka Kenya,” Museveni alisema.

    Wakati huo huo, Wizara ya Nishati ya Kenya imekanusha madai ya kuwepo kwa utata katika uagizaji na usambazaji wa mafuta chini ya mpango wa serikali kwa serikali.

    Waziri wa Nishati Opiyo Wandayi amesema Kenya iliwezesha makubaliano ya uagizaji mafuta na kampuni binafsi mwaka 2023 ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa dola.

    Chama cha Waendesha Magari Kenya, MAK, kimeitaka serikali kufanya ukaguzi maalumu wa mpango wa uagizaji mafuta wa serikali kwa serikali kufuatia kauli za Museveni kuhusu matumizi ya madalali.

  15. Marekani yawaonya raia wake dhidi ya kusafiri Iran

    Ubalozi wa Marekani nchini Iran kupitia tovuti yake umewaonya raia wake kutosafiri kwenda Iran kwa sababu yoyote, ukisema hali ya usalama Mashariki ya Kati bado ni tete na inaweza kubadilika bila kutarajiwa.

    Taarifa hiyo iliyotolewa Jumapili, Septemba 20, imewataka raia wa Marekani waliopo Mashariki ya Kati kuwa waangalifu zaidi na kujiandaa kwa uwezekano wa kughairiwa kwa safari za ndege, kufungwa kwa anga na usumbufu wa usafiri.

    Ubalozi huo umesisitiza: “Kwa sababu yoyote, msisafiri kwenda Iran. Raia wa Marekani wanapaswa kuondoka Iran mara moja.”

    Katika kipindi cha mwaka uliopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetoa maonyo kama hayo kwa raia wake kuhusu kusafiri katika maeneo ya Asia Magharibi na nchi zinazohusika katika vita kati ya Marekani, Israel na Iran, ikiwataka kutathmini upya safari zao na kuchukua tahadhari zinazohitajika.

    Pia Unaweza Kusoma:

  16. Iran yaionya Marekani dhidi ya mashambulizi mapya, mapigano yaendelea Yemen

    Iran imesema imepata taarifa kwamba Marekani huenda inapanga kufanya mashambulizi mengine, na kuonya kwamba italipiza kisasi “bila vikwazo” iwapo Washington itatekeleza mpango huo.

    Kwa mujibu wa Reuters, Iran imesema kuwa washirika wa Marekani katika Mashariki ya Kati watahusishwa kwa mzozo huo iwapo Tehran itashambuliwa upya.

    Kwa upande mwingine, Rais wa Marekani Donald Trump amesema chaguo pekee zilizopo kuhusu vita hivyo ni “kuangamiza Iran, kuiacha ididimie kiuchumi, au kufikia makubaliano.”

    Rais Trump ameonya kwamba Iran itakabiliwa na kushindwa kiuchumi au viongozi wake kuangamizwa ikiwa haitakubali makubaliano. Jeshi la Iran nalo limesema litajibu vikali mashambulizi yoyote mapya.

    Mzozo huo umeonekana kukwama kwa miezi kadhaa, huku kukiwa hakuna dalili kwamba upande wowote uko tayari kufanya makubaliano.

    Wakati huohuo, mzozo huo umeongeza changamoto katika nishati duniani, umeathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa Iran na kusababisha kuongezeka kwa mvutano katika maeneo mengine ya Mashariki ya Kati.

    Soma pia:

  17. Hujambo na karibu kwa habari zinazochipuka kote duniani.