Indonesia yasaka watu 36 baada ya moto kiwandani kuua watatu

Chanzo cha picha, Reuters
Waokoaji nchini Indonesia wanaendelea na juhudi za kuwatafuta wafanyakazi 36 ambao hawajulikani walipo, kufuatia moto mkubwa uliotokea katika kiwanda cha kutengeneza pipi na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine wanne kujeruhiwa.
Moto huo ulizuka Jumamosi jioni katika kiwanda kilichopo Cikande, wilayani Serang, mkoani Banten, magharibi mwa kisiwa cha Java.
Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka, watu 15 waliweza kunusurika katika tukio hilo, huku wanne kati yao wakipelekwa katika vituo vya matibabu kwa ajili ya kupata huduma.
Timu za uokoaji zinaendelea kukagua maeneo mbalimbali ya jengo lililoharibiwa na moto, wakiamini huenda baadhi ya wafanyakazi waliokuwa ndani wamenasa kwenye vifusi.
Hadi mapema leo Jumapili, wazima moto walikuwa bado wakifanya kazi ya kupoza maeneo ya kiwanda hicho baada ya kubaini kuwa baadhi ya sehemu bado zilikuwa na mabaki ya moto na joto kali.
Mamlaka bado hazijatoa taarifa kuhusu chanzo cha moto huo.

