Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Niligundua nina saratani mwanangu aliponipiga teke kwenye korodani'
Ben Lidgey alikuwa akicheza na mwanawe katika bustani na kufurahia wakati alipopigwa teke kwa bahati mbaya sehemu za siri, lakini tukio hilo huenda liliokoa maisha yake.
Baada ya maumivu kuendelea kwa wiki nzima, alitafuta msaada wa kimatibabu na kugundulika kuwa na saratani ya korodani.
Ripoti mpya kutoka kwa shirika la hisani la wanaume la Movember imesema kuwa theluthi moja ya wanaume nchini Wales, Uingereza, hufariki kabla ya kufikisha umri wa miaka 75, na imetoa wito kwa serikali ya Wales kuandaa mpango maalum wa kuboresha afya ya wanaume.
Serikali imesema kuwa mikakati yake ya sasa ya kuzuia kujiua na kujidhuru, pamoja na ile inayoshughulikia afya ya akili na saratani, inasaidia kukabiliana na baadhi ya changamoto za kiafya zinazowakabili wanaume.
Onyo: Makala hii inazungumzia kujiua
Ben Lidgey kutoka Cardiff alisema korodani zake zilivimba sana na kuwa ngumu "kama mpira wa kriketi" baada ya mwanawe kuzipiga teke. Hata hivyo, alisita kwenda kumuona daktari, akidhani tatizo hilo lingepotea lenyewe.
"Ni mojawapo ya mambo ya kawaida yanayowapata wanaume, kwa hivyo unalipuuza tu na kufikiri, 'litapita'," alisema.
"Nilikuwa na maisha ya familia yenye shughuli nyingi, nilikuwa na watoto wawili wadogo, na kulikuwa na mambo mengine mengi yaliyopewa kipaumbele."
Baada ya kuhakikishiwa kuwa saratani haijarudi au imepona, Ben alikabiliwa na changamoto nyingine.
Alisema: "Nilijihisi vizuri, lakini miaka mitano baadaye mke wangu aliniambia, 'Sidhani kama uko sawa. Nadhani unahitaji kuzungumza na mtu.'
"Aliona kana kwamba nimekuwa mtu mwenye hasira zaidi, anayependa kubishana, asiyevumilia watu, na kwamba sikuwa tena yule mtu niliyekuwa hapo awali."
Baada ya kupata ushauri nasaha wa kisaikolojia, Ben aliona mabadiliko chanya na maendeleo yanayoonekana. Sasa anahamasisha kuongezwa kwa msaada kwa wanaume na wavulana, ili waweze kupata huduma za kimatibabu na kisaikolojia wanapozihitaji.
End of Pia unaweza kusoma
Kwa nini wanaume hufariki wakiwa na umri mdogo?
Kusita kwa wanaume kwa ujumla kutafuta msaada wa kimatibabu iwe wa kimwili au wa kiakili mara nyingi hutajwa kuwa sababu inayofanya wanaume kufariki wakiwa na umri mdogo zaidi kwa wastani.
Ripoti ya Movember ilionyesha kuwa karibu wanaume 7,000 watafariki kabla ya kutimiza umri wa miaka 75 mnamo mwaka wa 2024. Kiwango cha vifo vya mapema kwa wanawake ni cha chini zaidi, kikiwa katika kiwango cha 28%.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa wanaume wengi hufariki kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika au matatizo ya kiafya ambayo yanaweza kutibika kwa urahisi yakigunduliwa na kutibiwa mapema; mfano wake ni aina fulani za saratani, magonjwa ya moyo, mapafu na ini, matatizo yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya na pombe, pamoja na kujiua.
Mahali anapoishi mwanaume pia kuna athari kubwa kwa afya na muda wake wa kuishi. Kwa mfano, kiwango cha vifo vya mapema kwa wanaume katika eneo la Blaenau Gwent, Uingereza, ni takriban asilimia 60 juu zaidi kuliko kwa wanaume wa eneo la Powys.
Vilevile, wanaume wanaoishi katika jamii maskini zaidi wanatarajiwa kuishi kwa wastani wa miaka 7.5 ikilinganishwa na wale wanaoishi katika jamii zenye utajiri mkubwa.
Uchambuzi wa ripoti hiyo pia unaonyesha kuwa visababishi vikuu vitano vya vifo vya mapema kwa wanaume huigharimu uchumi wa Wales kiasi kinachokadiriwa kuwa pauni bilioni 1.4 kwa mwaka.
Jonathan Scourfield, profesa wa ustawi wa jamii katika Chuo Kikuu cha Cardiff, alisema: "Vijana wa kiume, hasa, wako katika hatari kubwa zaidi ya kupata majeraha au kufa kutokana na hatari wanazochukua. Pia kuna matarajio ya kijamii kwamba wanapaswa kuonyesha nguvu za kimwili."
Alisema baadhi ya wanaume pia hupuuza umuhimu wa kujenga mtandao wa kijamii wa marafiki na watu wa kuwapa sapoti, au hutegemea wenzi wao wa kike kushughulikia jambo hilo.
"Wanapowapoteza wenzi wao au kustaafu, hukabiliwa na changamoto kubwa ya upweke," alisema.
"Lishe ni suala muhimu sana. Vyakula vyenye afya kama vile matunda na mboga wakati mwingine havionekani kama vitu vinavyohusishwa hasa na uanaume.
Kwa upande mwingine, tabia zinazodhuru afya kama vile unywaji wa pombe kupita kiasi wakati mwingine huonekana kama ishara ya mvulana kugeuka kuwa mwanaume."
Scourfield alisema kuwa licha ya kupungua kwa ajira za viwanda vizito na kazi zinazohitaji nguvu za mwili, taswira na mawazo ya jadi kuhusu "uanaume" bado huathiri vijana wa kiume, yakisambaa kupitia mitandao ya kijamii na watu wenye ushawishi katika jamii.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa, iwapo itatekelezwa, mpango mahususi wa afya ya wanaume ungekamilishana na mpango wa afya ya wanawake uliotolewa mwaka wa 2024.
Pia inabainisha kuwa hatua hii haitakuwa mabadiliko makubwa ya kimsingi, kwani mashirika mengi tayari yanajitahidi kuboresha huduma na uungaji mkono kwa ajili ya wanaume.
Hivyo, mpango huo wa afya ya wanaume unatarajiwa kuunganisha juhudi zilizopo na kuimarisha mikakati ya kuboresha afya na huduma kwa wanaume.