Kenya yajibu madai ya 'chuki dhidi ya wageni'
Serikali ya Kenya imesema hakuna agizo lolote lililotolewa linalowataka raia wa kigeni kuondoka nchini, kufuatia mjadala uliozuka baada ya kauli za Rais William Ruto kuhusu ushiriki wa wageni katika biashara ndogo ndogo.
Katika mahojiano maalum na BBC, Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Lee Kinyanjui, alisema serikali inachukua hatua za kuwatuliza raia wa kigeni na wawekezaji waliopata wasiwasi kutokana na tafsiri mbalimbali za matamshi ya rais.
Kinyanjui pia alipuuza madai yanayolinganisha hali ya sasa nchini Kenya na matukio ya chuki dhidi ya wahamiaji yaliyoshuhudiwa Afrika Kusini.
“Hakuna ulinganisho kati ya hali ya Kenya na ile ya Afrika Kusini. Tutahakikisha suala hili halipelekwi nje ya muktadha wake. Kenya inaendelea kuwa nyumbani kwa Waafrika wote wanaotaka kuja hapa. Tuko tayari kufanya biashara na yeyote, mradi afuate sheria,” alisema.
Alisisitiza kuwa utekelezaji wa maelekezo ya rais utakuwa jukumu la serikali pekee na si wananchi, akionya kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayechukua sheria mkononi, awe Mkenya au raia wa kigeni.
Kwa mujibu wa Kinyanjui, baadhi ya taarifa kuhusu suala hilo zimekuwa zikipewa uzito usio wa lazima na kuchochewa kwa sababu za kisiasa.
“Rais hakutoa agizo la mtu yeyote kuondoka nchini leo au wakati mwingine wowote. Badala yake, alielekeza timu kutoka Bunge na Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda kuchunguza suala la raia wa kigeni wanaojihusisha na biashara au ajira bila vibali vinavyohitajika. Maelekezo hayo yalitokana na malalamiko na maandamano ya wafanyabiashara,” alisema.
Aliongeza kuwa ripoti ya kina kuhusu suala hilo inatarajiwa kutolewa ndani ya wiki hii.
Kauli za Rais Ruto zimezua mjadala mpana nchini Kenya. Wakati baadhi ya wafanyabiashara wamezipokea kwa matumaini, wakisema zitalinda nafasi za biashara za wenyeji, wakosoaji wameonya kuwa zinaweza kuchochea hisia za chuki dhidi ya wageni.
Wakati huo huo, mamia ya watu walijitokeza katika ubalozi wa Burundi mjini Nairobi kutafuta nyaraka za safari baada ya ubalozi huo kutangaza utoaji wa hati za dharura kwa raia wake wanaotaka kurejea nyumbani.
Hata hivyo, Kinyanjui alisisitiza kuwa maelekezo hayo hayakulenga raia wa Burundi wala wananchi wa nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Raia wa Burundi na wa mataifa mengine wanapaswa kuelewa kuwa Kenya inaongozwa na utawala wa sheria. Kutakuwa na mfumo rasmi wa kuhakikisha kuwa utekelezaji wa maelekezo haya hauathiri kwa njia isiyo ya haki kundi lolote la watu,” alisema.
Serikali imeeleza kwamba hatua zozote zitakazochukuliwa zitalenga kuhakikisha sheria za biashara na uhamiaji zinafuatwa, huku ikisisitiza kuwa Kenya inaendelea kuwa taifa linalokaribisha wageni, wawekezaji na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali.