Tetesi za Soka Ulaya Jumanne: Arsenal yafikiria kumsajili Fofana, bado yamuwania Alvarez

.

Chanzo cha picha, SNS

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Arsenal inatathmini uwezekano wa kufanya usajili wa dakika za mwisho wa winga wa Lyon na timu ya taifa ya Ubelgiji, Malick Fofana, kabla ya dirisha la usajili kufungwa Jumanne.

Kwa mujibu wa RMC Sport, klabu hiyo ya London Kaskazini inafuatilia kwa karibu hali ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 huku ikitathmini uwezekano wa kufanikisha dili hilo katika siku za mwisho za usajili.

Wakati huo huo, Arsenal haijaondoa nia yake ya kumsajili mshambuliaji wa Atletico Madrid, Julian Alvarez. Ripoti zinaeleza kuwa viongozi wa Gunners wanaendelea kufanya kazi ya kuweka mazingira yatakayorahisisha nyota huyo wa Argentina kuhamia London.

Julian Alvarez

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Julian Alvarez iliichezea timu ya taifa ya Argentina katika fainali ya Kombe la Dunia 2026.

Arsenal bado ina matumaini ya kufanikisha uhamisho wa Alvarez, mwenye umri wa miaka 26, huku mawasiliano kati ya wawakilishi wa mchezaji huyo na klabu yakiendelea. (Teamtalk)

Liverpool imekataa ofa ya pauni milioni 30 iliyowasilishwa na Nottingham Forest kwa ajili ya kiungo chipukizi Trey Nyoni. Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya England hawana mpango wa kumuuza mchezaji huyo aliye na matumaini makubwa katika siku hizi za mwisho za dirisha la usajili.

Wakati huo huo, Borussia Dortmund inatafakari uwezekano wa kumrudisha Jadon Sancho kwa mara nyingine katika klabu hiyo ya Bundesliga.

Dortmund iko tayari kumpa fursa mpya winga huyo wa England mwenye umri wa miaka 26 ili kufufua taaluma yake. Hata hivyo, Sancho atalazimika kukubali masharti tofauti na mikataba yake ya awali, ikiwa ni pamoja na makubaliano yanayozingatia zaidi kiwango cha utendaji uwanjani pamoja na kuachana na bonasi ya kusaini mkataba. (Bild)

Jodan Sancho

Chanzo cha picha, Getty Images

Newcastle United imepiga hatua kubwa katika harakati zake za kuimarisha kikosi kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili. (Athletic- Usajili unahitajika)

The Athletic inaripoti kuwa klabu hiyo imefikia makubaliano na Lille kuhusu ada ya uhamisho wa kiungo wa Ubelgiji Matias Fernandez-Pardo. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka mitano utakaomfanya kuwa sehemu ya mpango wa muda mrefu wa Newcastle katika St James' Park.

Ajax imeonyesha nia ya kumsajili winga wa Sunderland na Ivory Coast, Simon Adingra, mwenye umri wa miaka 24.

Klabu hiyo ya Uholanzi imefanya uchunguzi kuhusu upatikanaji wa Adingra huku ikitafuta kuimarisha kikosi chake kabla ya dirisha la usajili kufungwa. (Telegraph)

Wakati huo huo, Fulham imeanza mazungumzo na Eintracht Frankfurt kuhusu uwezekano wa kumsajili kiungo wa Sweden, Hugo Larsson, mwenye umri wa miaka 22. Majadiliano kati ya pande hizo mbili tayari yameanza huku Fulham ikisaka kuongeza nguvu katika eneo la kiungo. (Fabrizio Romano)

Matias Fernandez-Pardo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Matias Fernandez-Pardo ameichezea timu ya taifa ya Ubelgiji mara tano

Newcastle United na Juventus zimefikia makubaliano ya awali kuhusu uhamisho wa mkopo wa mshambuliaji wa Ujerumani, Nick Woltemade, mwenye umri wa miaka 24.

Kwa mujibu wa mwandishi Florian Plettenberg, makubaliano hayo hayajumuishi kipengele cha kufanya uhamisho huo kuwa wa kudumu mara baada ya mkopo kumalizika.

Naye winga wa Arsenal na timu ya England chini ya miaka 21, Ethan Nwaneri, ni miongoni mwa wachezaji wanaozingatiwa na Borussia Dortmund kwa uhamisho wa mkopo katika siku za mwisho za dirisha la usajili.

Ripoti kutoka Sky Germany zinaeleza kuwa klabu hiyo ya Bundesliga inatafuta kuimarisha safu yake ya ushambuliaji na inamchukulia Nwaneri, mwenye umri wa miaka 19, kama mmoja wa malengo yake.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi