Walipokonywa Taji, Wakalirejesha Mahakamani: Safari ya Senegal ya AFCON 2025

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Na Asha Juma
- Nafasi, Mwandishi wa BBC
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Hebu fikiria hali hii: unashinda fainali ya AFCON mbele ya maelfu ya mashabiki, unainua kombe la ubingwa na taifa zima linaanza kusherehekea. Kisha, miezi miwili baadaye, unaambiwa wewe si bingwa tena. Taji unaloliamini umelishinda uwanjani linakabidhiwa kwa mpinzani wako.
Hiyo ndiyo hali iliyowakumba Senegal baada ya kuibuka mabingwa wa AFCON 2025 kwa kuifunga Morocco kwa bao 1-0 mjini Rabat. Kilichoanza kama shangwe za ubingwa kiligeuka kuwa moja ya migogoro mikubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia ya soka la Afrika. CAF iliubatilisha ushindi huo na kuipa Morocco ushindi wa mezani wa mabao 3-0, lakini Senegal haikukubali uamuzi huo.
Badala ya kukata tamaa, iliwasilisha rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) nchini Uswisi, na kuanzisha vita ya kisheria iliyodumu kwa miezi kadhaa. Hatimaye, tarehe 24 Novemba 2026, CAS ilitoa uamuzi wake wa mwisho na kuirejeshea Senegal ubingwa wa Afrika.
Lakini nini hasa kilitokea hadi mabingwa wa Afrika wakanyang'anywe taji lao? Morocco iliupataje ubingwa huo mezani? Na ni sababu zipi zilizoifanya CAS kubadili kabisa uamuzi wa CAF?
Fuatilia mtiririko wa matukio unaonyesha jinsi Senegal ilivyopokonywa na kurejeshewa ubingwa kuanzia dakika za mwisho za fainali ya Rabat hadi hukumu iliyobadili historia ya AFCON 2025.
18 JANUARI 2026 – FAINALI YA KIHISTORIA
Senegal wanakutana na wenyeji Morocco katika fainali ya AFCON 2025, kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah, Rabat.
Mchezo unakuwa mkali, dakika 90 zinaisha bila bao wakati huo Morocco wanataka kutwaa ubingwa wao wa kwanza tangu mwaka 1976, huku Senegal wakisaka taji lao la pili.
DAKIKA ZA NYONGEZA – CHECHE ZAANZA KUWAKA!
Senegal wanaamini wamepata bao kupitia Ismaila Sarr, lakini mwamuzi Jean-Jacques Ndala alikuwa ameshapuliza filimbi kuashiria faulo ya Morocco.
Muda mfupi baadaye, VAR inaingilia kati na Morocco wanapewa penalti.
Hapo ndipo hasira zinapolipuka!

Chanzo cha picha, Getty Images
DAKIKA 90 NA NYONGEZA – SENEGAL WATOKA UWANJANI!
Kocha Pape Thiaw anaongoza baadhi ya wachezaji wake kuelekea vyumbani kupinga uamuzi wa penalti.
Hapa ndipo chanzo cha mgogoro wa kisheria kinapoanzia.
Mchezo unasimama kwa takribani dakika 14. Mashabiki wanachafukwa na roho, vurugu zinatokea na fainali inayotazamiwa na dunia nzima inageuka kuwa tafrani.
MCHEZO UNAENDELEA TENA – MOROCCO WAKOSA PENALTI!

Chanzo cha picha, Getty Images
Senegal wanarejea uwanjani baada ya mwamuzi kuruhusu mchezo kuendelea.
Brahim Diaz anachukua jukumu la kupiga penalti, lakini anajaribu mtindo wa Panenka na kipa Edouard Mendy anaokoa!
Morocco wanapoteza nafasi ya dhahabu ya kutwaa ubingwa.
DAKIKA YA 124 – PAPE GUEYE AUA MCHEZO! SENEGAL WAPATA USHINDI
Senegal wanapata bao la ushindi kupitia Pape Gueye katika muda wa ziada.
Mwisho wa mchezo, Senegal wanashinda 1-0 na kutangaza mabingwa wa Afrika kwa mara ya pili katika historia yao.
Mashabiki wanashangilia. Wachezaji wanainua kombe. Inaonekana kila kitu kimekwisha.
BAADA YA FAINALI - MOROCCO YAWASILISHA MALALAMIKO CAF
Mara baada ya fainali, Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) linawasilisha malalamiko rasmi kwa CAF.
Morocco inadai kuwa Senegal ilikiuka kanuni za mashindano baada ya baadhi ya wachezaji wake kuondoka uwanjani wakati wa dakika za nyongeza wakipinga penalti iliyotolewa kwa Morocco.
28 JANUARI 2026 - CAF YATUPILIA MBALI MALALAMIKO YA MOROCCO
Kamati ya Nidhamu ya CAF inakataa malalamiko ya Morocco na kuthibitisha matokeo ya uwanjani yaliyoiwezesha Senegal kushinda ubingwa kwa bao 1-0.
Hata hivyo Morocco hairidhiki na uamuzi huo na kuamua kuukata rufaa.
FEBRUARI 2026 - MOROCCO YAKATA RUFAA CAF
FRMF inawasilisha rufaa kwa Bodi ya Rufaa ya CAF, ikisisitiza kuwa Senegal ilipaswa kuadhibiwa kwa kuondoka uwanjani kinyume cha kanuni za mashindano.
17 MACHI 2026 - MOROCCO YASHINDA RUFAA
Bodi ya Rufaa ya CAF inakubaliana na hoja za Morocco, inabatilisha uamuzi wa awali wa Kamati ya Nidhamu na kuitangaza Senegal kuwa imepoteza mchezo kwa kufuta matokeo ya uwanjani.
CAF inaipa Morocco ushindi wa mabao 3-0 na kuitangaza bingwa mpya wa AFCON 2025.
SENEGAL WAENDA CAS
Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) linapinga uamuzi huo na kukata rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), iliyopo Lausanne, Uswisi.
Senegal wanataka uamuzi wa CAF ubatilishwe.
8 OKTOBA 2026 – KESI YASIKILIZWA
Jopo la wasuluhishi watatu wa CAS linasikiliza kesi hiyo kwa faragha mjini Lausanne.
Kiini cha hoja kinakuwa mamlaka ya mwamuzi kuamua kama mchezo unaweza kuendelea baada ya wachezaji kurejea uwanjani.
24 NOVEMBA 2026 – CAS YATOA UAMUZI
CAS inabatilisha uamuzi wa CAF uliokuwa umeipa Morocco ushindi wa 3-0.
Mahakama inaeleza kuwa uamuzi wa mwamuzi kuendelea au kusimamisha mchezo ni mamlaka yake ya mwisho katika mazingira hayo.
Matokeo ya uwanjani yanabaki: Senegal 1-0 Morocco.
Na hiyo ndiyo safari ndefu ya Senegal katika vita ya kutetea ubingwa wa AFCON 2025! Kutoka kwenye ushindi wa uwanjani, kunyimwa taji na CAF, hadi kupigania haki yao katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo, CAS.
Mwisho wa yote, Senegal wanarejeshewa ubingwa, huku Morocco wakipoteza taji walilopewa kupitia uamuzi wa mezani.
Lakini simulizi hii inatuachia swali kubwa: Je, katika soka, matokeo yanapaswa kuamuliwa na kile kinachotokea ndani ya dakika 90 uwanjani, au kanuni zinapaswa kuchukua nafasi hata pale mchezo unapokuwa umekwisha?
Jambo moja lililowazi ni kwamba, fainali hii haitakumbukwa kwa bao la Pape Gueye pekee, bali pia kwa mgogoro ulioifikisha soka la Afrika hadi mahakamani.
Senegal walishinda uwanjani, wakapoteza mezani, lakini mwisho wa safari wakarejeshewa taji lao!
Kombe linaweza kubadilishwa mezani, lakini historia ya kile kilichotokea uwanjani haiwezi kufutwa!



























