Kwa nini msichana huyu wa miaka sita anafanana na bibi wa miaka 80?

- Author, Nandini Velasamy
- Akiripoti kutoka, BBC Tamil
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
"Kwa nini mnatoka naye nje? Si mngemweka nyumbani?" Hayo ni baadhi ya maneno ambayo mama yake Aiza, Anjali, amekuwa akisikia kutoka kwa watu.
Lakini Anjali huwa na jibu moja tu:
"Huyu ni mwanangu yuko hivi, lakini anapaswa kutoka nje na watu wamwone."
Anjali na mumewe Akhil wanaishi Mananthavady, kijiji kilichoko jimboni Kerala nchini India. Binti yao mwenye umri wa miaka sita, Aiza maarufu kama Thaku, anaishi na ugonjwa nadra wa kurithi unaoitwa Cutis Laxa.
Kutokana na ugonjwa huo, ngozi yake imelegea na kukunjamana kiasi kwamba watu wengi humfananisha na mtu mwenye umri wa miaka 70 au 80.
Licha ya changamoto hizo, Aiza ana ndoto kubwa. Anataka kuwa daktari siku moja, na wazazi wake wanafanya kila wawezalo kuhakikisha ndoto yake inatimia.
Ugonjwa uliogundulika akiwa na miezi sita

Mama yake Anjali anasema walianza kugundua mikunjo isiyo ya kawaida kwenye ngozi ya Aiza akiwa na miezi sita, na kuamua kumpeleka hospitalini.
"Daktari alitushauri tufanye uchunguzi wa vinasaba ili kubaini tatizo halisi. Mwezi mmoja baadaye, tulipewa majibu kuwa ana ugonjwa adimu unaoitwa Cutis Laxa, kwa Kiingereza," anasema Anjali.
Cutis Laxa ni ugonjwa nadra unaofanya ngozi kupoteza uwezo wake wa kujikaza na kurudi katika hali yake ya kawaida. Hivyo ngozi huonekana kuwa imelegea, imekunjamana au kunyauka.
Kwa baadhi ya wagonjwa, ugonjwa huo huathiri pia mapafu, moyo na viungo vingine vya ndani ya mwili.
Alifanyiwa upasuaji akiwa na miaka miwili na nusu
Kutokana na hali yake, Aiza huugua mara kwa mara mafua, kikohozi na homa, jambo linalomfanya kulazwa hospitalini mara kadhaa kila mwezi.
"Tunalazimika kwenda hospitali angalau mara mbili au tatu kila mwezi," anasema mama yake.
Anasema pia Aiza alifanyiwa upasuaji mara mbili akiwa na miaka miwili na nusu kutokana na tatizo la ngiri pamoja na hitilafu katika moja ya macho yake.
Daktari wake, Anjana, anasema watu wanaoishi na ugonjwa huo wanaweza kukumbwa na matatizo ya mfumo wa kupumua na magonjwa ya moyo.
"Matarajio ya maisha ya wagonjwa hutegemea kiwango ambacho viungo vya ndani vinaathirika. Kwa sasa hakuna tiba inayoweza kuponya ugonjwa huu kabisa," anasema daktari huyo.
Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la misaada la Cutis Laxa International, watu wapatao 400 duniani kote wanaishi na ugonjwa huo, sawa na mtu mmoja kati ya milioni mbili.
Nchini India, wagonjwa saba pekee ndio wanaojulikana kuwa na hali hiyo.
'Ilikuwa vigumu sana kukubali'

Baba yake Aiza, Akhil, ambaye ni mlinzi katika kampuni binafsi, anasema mwanzo ulikuwa mgumu sana kwa familia yao.
"Hatukuwahi kusikia wala kuona ugonjwa kama huu. Ilituumiza sana. Ilikuwa kama unaona bibi wa miaka 70 au 80 katika mwili wa mtoto mdogo," anasema.
Anasema pia changamoto ya gharama za matibabu imekuwa kubwa kutokana na kipato chake.
"Tumepunguza matumizi mengine mengi ili kugharamia matibabu yake. Matibabu yake mengi yanafanyika Kerala," anasema.
Hata hivyo, Akhil anasema anajivunia ndoto ya binti yake kuwa daktari.
Changamoto shuleni
Kwa sasa Aiza yuko darasa la kwanza katika shule ya serikali karibu na nyumbani kwao.
Somo analolipenda zaidi ni hesabu.
Mama yake anasema Aiza bado haelewi kikamilifu hali yake, lakini wakati mwingine huuliza maswali yanayoumiza moyo.
"Kwa nini watu wote hunitazama hivi? Kwa nini hakuna anayetaka kuwa rafiki yangu?"
Mwanzoni, baadhi ya wanafunzi walikuwa wakimdhihaki kwa kumwita "Mama".
Baada ya wazazi wake kuzungumza na uongozi wa shule, hali ilibadilika.
'Ni mwanafunzi mwenye akili sana'

Mwalimu wake, Aishwarya, anasema Aiza ni miongoni mwa wanafunzi wenye bidii na akili darasani.
"Yuko vizuri katika kila kitu. Anawasaidia marafiki zake na watu wengine pia. Mwanzoni watoto walimdhihaki, lakini sasa wote ni marafiki zake," anasema.
Mwalimu huyo anasema Aiza mara nyingi huwaambia watu:
"Nataka kuwa daktari nitakapokua ili niweze kuwasaidia watoto wengine walio kama mimi."
"Sikiliza maneno hayo, naomba kwa moyo wote ndoto yake itimie," anaongeza.
Umaarufu kwenye mitandao ya kijamii
Aiza pia ana zaidi ya wafuasi 25,000 kwenye Instagram.
Ndugu yao Arjun ndiye aliyependekeza video zake ziwekwe mtandaoni baada ya kuona anavyopenda kucheza muziki, kuimba na kuchora.
Mwanzoni familia ilikabiliwa na maoni mengi mabaya kutoka kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii.
"Watu walitoa maoni mengi ya kuumiza. Nilikuwa nayaondoa haraka kabla wengine hawajayaona," anasema Arjun.
Kadri muda ulivyopita, watu wengi walianza kumkubali Aiza jinsi alivyo na kumtia moyo.
Wakati mmoja, Aiza alisema kwa utani:
"Sasa nimekuwa maarufu sana, nahitaji mlinzi wa kunilinda kazini."
Ndoto ya kuwa daktari
Hata hivyo, wataalamu wa saikolojia wameonya kwamba matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii yanaweza kuleta msongo wa mawazo kwa mtoto mdogo anayekabiliwa tayari na changamoto za kiafya.
Pamoja na hilo, wazazi wa Aiza wanaamini kuwa uwepo wake mtandaoni unasaidia kubadilisha mitazamo ya watu kuhusu ugonjwa wake na kupunguza unyanyapaa.
Anjali anasema:
"Anataka kuwa daktari atakapokua, na tutafanya kila tuwezalo kumpatia elimu bora."
Baba yake Akhil hupata hisia kali anapozungumzia binti yake.
"Binti yangu ndiyo maisha yangu," anasema huku machozi yakimlengalenga.
Imefasiriwa na Asha Juma






























