Kwa nini Tanzania inatajwa kama mfano wa mageuzi ya elimu Afrika, licha ya changamoto zake?

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Ripoti mpya ya Mastercard Foundation kuhusu elimu ya sekondari barani Afrika inaitaja Tanzania miongoni mwa nchi ambazo uzoefu wake katika kuboresha elimu unaweza kutoa mafunzo kwa mataifa mengine yanayotafuta namna ya kuwaandaa vijana kwa maisha na soko la ajira.

Ripoti hiyo, Secondary Education in Africa: Expanding Pathways to Work, Livelihoods, and Lifelong Learning, iliyozinduliwa mjini Accra, Ghana, inaeleza kuwa mabadiliko ya mtaala wa Tanzania yameanza kuleta mwelekeo mpya wa ufundishaji, unaosisitiza zaidi mafunzo ya vitendo, fikra tunduizi na uhusiano kati ya elimu na shughuli za kiuchumi.

Tanzania ni miongoni mwa nchi saba zilizofanyiwa uchunguzi wa kina katika ripoti hiyo, pamoja na Ethiopia, Ghana, Malawi, Rwanda, Senegal na Sierra Leone. Uchunguzi huo ulihusisha tafiti maalumu na mashauriano na vijana ili kuelewa namna mifumo ya elimu inavyoweza kukidhi mahitaji ya kizazi kipya.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tangu kuanza kutekelezwa kwa mtaala ulioboreshwa mwaka 2023, baadhi ya wanafunzi na walimu nchini Tanzania wameripoti mabadiliko kutoka kwenye mfumo wa kukariri masomo kuelekea mijadala, kujifunza kwa vitendo na kuhusisha maarifa ya darasani na fursa za kujipatia kipato.

Hata hivyo, ripoti hiyo haioneshi kuwa Tanzania imekwishaondoa changamoto zinazokabili elimu ya sekondari. Badala yake, inaeleza mafanikio yaliyoanza kupatikana pamoja na mapungufu ambayo bado yanahitaji kushughulikiwa, huku ikiweka uzoefu wa nchi hiyo katika muktadha mpana wa changamoto za elimu barani Afrika.

Kilichoipaisha Tanzania

.

Moja ya mambo yaliyotajwa katika ripoti hiyo ni mabadiliko ya namna wanafunzi wanavyofundishwa na kile wanachotarajiwa kufanya baada ya kumaliza shule.

Mtaala ulioboreshwa umeanzisha mbinu za ufundishaji zinazomweka mwanafunzi katikati ya mchakato wa kujifunza, ikiwemo mafunzo yanayotegemea miradi, elimu ya ujasiriamali, somo la Biashara na mifumo mipya ya upimaji wa wanafunzi.

Ripoti inasema baadhi ya wanafunzi na walimu wameanza kuona mabadiliko kutoka kwenye mfumo wa kukariri kwenda kwenye mijadala, fikra tunduizi na kujifunza kwa vitendo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Somo la Biashara, ambalo limeingizwa katika mtaala wa sekondari, limetajwa na wanafunzi kuwawezesha kuona uhusiano kati ya wanayojifunza darasani na uwezekano wa kuanzisha shughuli za ujasiriamali.

Mwalimu mmoja wa somo hilo mkoani Morogoro aliwaambia watafiti kuwa mbinu za kufundisha kwa vitendo zinawasaidia wanafunzi kuelewa dhana mbalimbali na kushiriki kikamilifu zaidi darasani.

Lakini ripoti haijabainisha mabadiliko ya mtaala pekee. Pia imetambua nafasi ya programu za kuwaendeleza walimu kazini, ikiwemo MEWAKA, chini ya SEQUIP na mafunzo elekezi ya kitaifa kwa walimu.

Hatua hizo zimetajwa kusaidia kuziba pengo kati ya sera na utekelezaji wake kwa kuwapa walimu mafunzo na fursa za kubadilishana uzoefu.

Kingine ambacho kinatajwa ni kwamba Tanzania pia imeanza kuunganisha elimu ya sekondari na mafunzo ya ufundi. Wanafunzi wanaochagua mkondo huo wanaweza kumaliza Kidato cha Nne wakiwa na cheti cha elimu ya sekondari pamoja na cheti cha ujuzi kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).

Mabadiliko hayo yanaendana na hoja kuu ya ripoti kwamba elimu ya sekondari haipaswi kuwaandaa vijana kwa njia moja tu ya maisha, kama kuendelea na elimu ya juu au kutafuta ajira rasmi.

"Shule ya sekondari haiwezi tena kupangwa kwa kuzingatia dhana kwamba wanafunzi wote wanaelekea kwenye njia moja au kwamba kuna mabadiliko yanayotabirika kutoka shuleni moja kwa moja kwenda kazini," anasema Daniel Hailu, Kaimu Afisa Mkuu wa Programu wa Mastercard Foundation.

Kwa upande wake, Rais na Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Sewit Ahderom, anasema elimu ya sekondari ni muhimu kwa kuwa kwa vijana wengi barani Afrika ndiyo fursa ya mwisho kwa mfumo rasmi wa elimu kuwafikia kwa kiwango kikubwa.

"Kwa vijana wa leo, hasa katika ngazi ya sekondari, elimu lazima iwe na mwelekeo na iwawezeshe kufikia mahali fulani. Kwa vijana wengi wa Afrika, shule ya sekondari ndiyo fursa ya mwisho kwa mfumo wa elimu kuwafikia kwa kiwango kikubwa," anasema Ahderom.

Changamoto zimekwisha?

.
Maelezo ya picha, Wanafunzi wa kike wakiwa na mwalimu wao katika shule ya sekondari ya Jambiani huko Zanzibar, Tanzania

Pamoja na hatua hizo, takwimu zilizowasilishwa katika ripoti zinaonesha kuwa Tanzania bado ina safari ndefu katika kuhakikisha mageuzi ya elimu yanawanufaisha wanafunzi wengi zaidi.

Kwa mfano, katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne wa mwaka 2023, kiwango cha ufaulu kilikuwa takribani asilimia 25 katika somo la Hisabati, asilimia 69 katika Kiingereza na asilimia 97 katika Kiswahili.

Aidha, ni takribani robo tu ya wanafunzi wanaoendelea na elimu ya sekondari ya juu, huku wanafunzi wanaojiunga na mikondo ya ufundi na ufundi stadi wakichangia takribani asilimia 0.5 tu ya wanafunzi wote wa sekondari.

Hali hiyo inaibua swali kuhusu kasi ya kupanua fursa za elimu inayohusisha ujuzi wa vitendo, hasa wakati mabadiliko ya mtaala yanapolenga kuwaandaa vijana kwa njia mbalimbali za kujipatia kipato.

SHIRIKA la HakiElimu Tanzania liliwahi kusema kuwa licha ya serikali kuboresha sekta ya elimu, lakini bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto ikiwemo mlundikano wa wanafunzi darasani.

Shirika hilo lilirejea kitabu cha takwimu za elimu Tanzania (BEST) 2021 ambacho kinaonyesha uwiano wa darasa shule za msingi ni 1:74 badala ya 1:45 huku yale madarasa ya awali ukiwa ni 1:75 badala ya 1:40 unaotakiwa.

Changamoto nyingine ni tofauti za upatikanaji na ukamilishaji wa elimu kati ya maeneo mbalimbali. Ripoti inasema tofauti za kiwango cha wanafunzi wanaomaliza elimu ya sekondari ya chini kati ya halmashauri zenye kipato cha juu na zile zenye kipato cha chini zinafikia wastani wa karibu asilimia 50.

Pia, theluthi mbili ya vijana walioajiriwa nchini Tanzania wanafanya kazi katika sekta ya kilimo, wakati ajira rasmi zinachangia asilimia tano pekee ya ajira kwa vijana.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa hata kama vijana watapata maarifa na ujuzi kupitia mtaala mpya, bado wanahitaji mazingira yatakayowawezesha kuutumia ujuzi huo katika shughuli za kiuchumi.

Suala jingine ni maandalizi ya walimu na mifumo ya upimaji. Ikiwa mtaala unasisitiza ubunifu na mafunzo ya vitendo, lakini mitihani inaendelea kuthamini zaidi uwezo wa kukariri, kuna hatari ya malengo ya mabadiliko hayo kutofikiwa.

Serikali inakiri kwamba changamoto katika sekta ya elimu hazijakwisha, na ianzishughulikia kwa uwezo wake.

Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba akiwasilisha Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2026/2027 alisema jumla ya sh. trilioni 1.77 zinahitajika kwa ajili ya kuboresha elimu hasa sekondari

Alisema fedha hizo ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, maabara, ajira mpya za walimu, ruzuku ya mitihani, ya vitabu na uendeshaji kwa wanafunzi zaidi ya milioni tatu wanaotarajiwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2028.

Changamoto ni za Afrika

Changamoto zinazokabili Tanzania ni sehemu ya tatizo pana zaidi katika mifumo ya elimu barani Afrika, ambayo inakabiliwa na ongezeko kubwa la vijana wanaohitaji elimu na fursa za ajira.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya vijana milioni 10 wanaingia katika soko la ajira barani Afrika kila mwaka, lakini ni takribani ajira rasmi milioni tatu tu zinazotarajiwa kuundwa kila mwaka.

Hali hiyo inatarajiwa kuwa na athari kubwa zaidi katika miaka ijayo. Ripoti inakadiria kuwa zaidi ya vijana milioni 330 kutoka kusini mwa Jangwa la Sahara watafikia umri wa kufanya kazi ifikapo mwaka 2035.

Wakati huohuo, karibu asilimia 90 ya ajira za vijana barani Afrika zipo katika sekta isiyo rasmi, jambo linaloonesha kuwa mifumo ya elimu inahitaji kuandaa vijana kwa ajira, kujiajiri, ujasiriamali na shughuli nyingine za kiuchumi.

Katika ngazi ya bara, ni asilimia 35.4 pekee ya wanafunzi wanaokamilisha elimu ya sekondari ya juu. Aidha, Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara inahitaji walimu wengine wa sekondari wapatao milioni 10.7 ifikapo mwaka 2030.

Waziri wa Elimu wa Ghana, Haruna Iddrisu, anasema upatikanaji wa elimu peke yake hautoshi kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa yanayohitajika, akisisitiza umuhimu wa walimu katika kufanikisha mageuzi.

"Upatikanaji wa elimu kuleta matokeo katika ujifunzaji unategemea kwa kiasi kikubwa rasilimali yetu muhimu zaidi – walimu. Ripoti hii inaweka wazi kuwa kujenga nguvu kazi yenye ujuzi, motisha na uwezo wa kufanya maamuzi ni jambo muhimu kwa mageuzi," anasema.

Ripoti inapendekeza nchi za Afrika kuanza na masomo ambayo hayahitaji gharama kubwa na yanaweza kubadilishwa kulingana na mazingira ya eneo husika, kama ujasiriamali, kilimo na teknolojia ya habari na mawasiliano, kabla ya kupanua mikondo ya ufundi inayohitaji uwekezaji mkubwa zaidi.

Paul Kasanga, mmoja wa wadau wa elimu Afrika, anasema maendeleo yaliyopatikana yanapaswa kutambuliwa, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya.

"Hayo ni maendeleo ya kweli. Lakini pia ni ukumbusho wa wazi kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanya," anasema.

Nchi ya Tanzania , uzoefu wake uliotambuliwa katika ripoti hiyo unaweza kuwa sehemu ya mafunzo kwa nchi nyingine za Afrika, licha ya uwepo wa changamoto lukuki zinazotofautiana nchi na nchi. Lakini kubwa zaidi ambalo liliwahi kusemwa na Dkt. Calvin Swai msomi kutoka Tanzania kwamba elimu inapaswa kujenga ubunifu na ujuzi wa kukabiliana na changamoto.