Kwa nini mawasiliano ya binadamu yanapungua kila mwaka, na kwa nini wataalamu wana wasiwasi?

g
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Utafiti mpya unaonyesha kwamba katika jamii za Magharibi, ambapo watu wanapendelea upweke, watu sasa hawazungumzi sana kuliko hapo awali.

Watafiti walifuatilia mazungumzo ya kila siku ya karibu watu 2,000 wa rika zote, wanaoishi katika nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Marekani, Mexico, Australia, na nchi kadhaa za Ulaya. Baada ya kuchanganua data hizo kwa miaka 17, waligundua mwelekeo dhahiri ulioonyesha kupungua kwa idadi ya maneno yaliyotumika: watu walipunguza maneno 300 kila siku katika mawasiliano yao ikilinganishwa na mawasiliano yao ya awali.

Ikiwa nambari hii itaongezwa pamoja, itakuwa takriban maneno 110,000 kwa mwaka, ambayo ni sawa na maneno yanayoweza kuandika kitabu cha hadithi fupi.

Valeria Pfeiffer na Matthias Mehl, waandishi wa utafiti huo, walisema utafiti wao haukuundwa kubaini chanzo cha hili. Hata hivyo, kuenea kwa kasi kwa simu za mkononi, intaneti, na mitandao ya kijamii katika miongo ya hivi karibuni huenda kumechangia kupungua kwa mawasiliano baina ya watu.

Zaidi ya hayo ni kuibuka kwa janga la COVID-19, ambalo limewalazimisha watu wengi kujitenga kijamii. Hali hii imezidishwa na kuenea kwa kazi za mbali na kuongezeka kwa teknolojia na huduma zinazopunguza hitaji la watu kukutana ana kwa ana.

Hata hivyo, Mehl anakubali kwamba kuna jamii "zilizounganishwa", jamii ambazo haziko katika mpangilio ulioonekana katika utafiti huu na zinajumuisha zaidi ya watu elfu mbili.

Kulingana na Mehl, njia ya kuzuia hali hii na kupambana na "ugonjwa wa upweke" ambao nchi nyingi zinakabiliwa nao inaweza kuwa rahisi kama kuwa na ujasiri wa kuzungumza na "wageni"; na wageni wakati mwingine huwa karibu nasi kama majirani zetu.

Alizungumza na Mwandishi Maalum wa BBC Katie Kay kuhusu matokeo ya utafiti huo.

g

Unagunduaje kwamba kila mwaka watu huzungumza kidogo?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tulichapisha utafiti mwaka wa 2007 ambao ulionyesha kwamba hakukuwa na tofauti kubwa kati ya wanaume na wanawake katika idadi ya maneno waliyozungumza kwa siku, na kwamba makundi yote mawili yalizungumza kwa kiwango sawa. Hata hivyo, watu wengi walisema kwamba idadi ya watu tuliotegemea utafiti wetu ilikuwa ndogo sana.

Kwa hivyo, miaka 17 baadaye, tulifanya utafiti tena kwa kutumia idadi ya watu mara nne zaidi, zaidi ya watu 2,000. Dkt. Pfeiffer alipoona matokeo, alisema, "Matokeo yamekamilika, na inaonekana kwamba watu huzungumza kama maneno 12,000 kwa siku."

Nami nikasema, "Hili linaonekana si sahihi, haiwezekani. Lazima liwe na maneno kama 16,000, kwa sababu hiyo ndiyo idadi tuliyokuwa nayo wakati huo."

Lakini aliangalia tena nambari hizo, na ikawa kwamba zilikuwa sahihi tangu mwanzo. Kwa hivyo, ilishangaza sana kuona kwamba katika kipindi cha takriban miaka 17, idadi ya maneno ambayo watu husema kwa siku imepungua kwa karibu maneno 4,000.

k
Maelezo ya picha, Katie Kay anamhoji Matthias Mehl

Ubashiri wangu wa kwanza ni kwamba simu za mkononi zimebadilisha jinsi tunavyozungumza, tunatumia vidole gumba vyetu zaidi, tunatuma ujumbe mfupi zaidi, na tunazungumza kidogo. Je, unajua hilo?

Hatukuangalia hili moja kwa moja katika utafiti huu. Hata hivyo, tunaamini kwa dhati kwamba tumebadilisha maneno mengi yanayozungumzwa na maneno yaliyoandikwa. Kwa kweli, hatutashangaa kama jumla ya maneno tunayotumia imeongezeka tangu wakati huo, tunapoandika zaidi katika barua pepe, ujumbe mfupi, na mitandao ya kijamii.

Lakini kinachovutia zaidi, na muhimu zaidi, ni hiki: ikiwa kupungua huku kwa usemi kunasababishwa na matumizi ya vifaa vya kidijitali, swala linatokea kuhusu kama vizazi vichanga vinapoteza maneno haya zaidi kuliko vingine.

Tuliweza kuchunguza hili. Ili kufanya hivyo, tuliwagawanya washiriki wa utafiti katika makundi mawili: wale walio chini ya umri wa miaka 25 na wale walio zaidi ya umri wa miaka 25.

Kama ilivyotarajiwa, tuligundua kuwa kupungua kwa mazungumzo kulikuwa kubwa zaidi katika kundi la vijana. Kwa wastani, idadi ya maneno yaliyotumika kwa siku ilipungua kwa 338. Lakini kwa washiriki walio chini ya umri wa miaka 25, kupungua kulikuwa maneno 451 kwa siku, ikilinganishwa na maneno 314 yaliyorekodiwa katika kundi la wazee.

Matokeo haya yanaonyesha kwamba matumizi ya vifaa vya kidijitali yanaweza kuhusishwa na kupungua kwa usemi wa kila siku.

Je, una taarifa zaidi kuhusu maneno mahususi tunayokosa, na aina za mazungumzo tunayoweza kukosa?

Kile ambacho pengine tumepoteza ni sehemu kubwa ya mazungumzo mafupi ambayo tulikuwa tukifanya kila siku. Sababu ni kwamba muundo wa mahusiano ya kijamii umebadilika, na kusababisha fursa chache za mazungumzo ya maneno machache na watu wanaoshiriki kile wanasayansi wanachokiita "mahusiano dhaifu."

g

Data zetu ni za kuanzia mwaka wa 2019, wakati kabla ya janga la Covid-19 ambapo kufanya kazi kwa mbali kulikuwa jambo la kawaida sana. Kwa hivyo, una wazo lolote kuhusu nini kimetokea kwenye mazungumzo yetu tangu mlipuko ulipotokea? Je, yameongezeka au yamepungua?

Kwa sasa tunafanya utafiti ambao tunaweza kuuchambua katika miaka michache ijayo. Kwa hivyo hatuna data za moja kwa moja, lakini sina sababu ya kufikiria kwamba mwelekeo huu umekoma, kwa sababu janga hilo lilikuwa tukio lililosababisha kutengwa sana.

Ilikuwa ni uzoefu ambapo hatukuweza kufanya mazungumzo haya ya hiari kwa sababu tulilazimika kudumisha umbali wa kijamii.

Baada ya janga hili, watu wengi waliripoti aina ya uvivu wa kijamii, kana kwamba mwingiliano wa kijamii umekuwa mgumu zaidi na kuwakaribisha marafiki au kutoka nje kulionekana kuwa vigumu zaidi. Kwa hivyo nadhani kunaweza kuwa na kurudi nyuma kutokana na mdororo wa uchumi, lakini kwa ujumla, ningeshangaa sana ikiwa tungeweza kudhibiti mwenendo huu kweli.

g

Unafikiri mabadiliko haya yanaweza kusimamishwa au kubadilishwa vipi?

Sina suluhisho zuri kwa hili, lakini nilizungumzia watafiti wawili, Gillian Sandstrom na Nicholas Appley. Waliandika vitabu viwili, Once Upon a Time, a Stranger na A Little More Social. Nilisoma vitabu hivyo baada ya utafiti wetu kuonyesha kwamba tulikuwa tunakosa mazungumzo ya aina hii.

Kwa muhtasari wa walichosema, ujumbe wao ni: Jaribu; anza mwingiliano na mazungumzo zaidi. Nimejiwekea lengo hili: kila ninapojiuliza, "Labda naweza kuzungumza na mtu huyu sasa hivi," mimi hufanya hivyo mara moja.

Lakini kuna upande mwingine ambao ulinichukua muda mrefu kuelewa. Tulizungumzia kuhusu nyakati ndogo za kuwa sehemu ya wengine, na ndivyo ninavyopata kutokana na mazungumzo haya. Hata hivyo, naamini kwamba jamii kwa ujumla inafaidika zaidi kutokana na mazungumzo haya kuliko mtu binafsi.

Kwa maoni yangu, wakati ambapo tunakabiliwa na si tu tatizo la kutengwa kijamii, bali pia changamoto ya migawanyiko mikubwa ya kijamii, mazungumzo haya rahisi yanaweza kuwa fursa ya kutuleta karibu zaidi.