Watoto wanavyohimili milipuko ya makombora kutafuta elimu Yemen

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kila asubuhi saa kumi na mbili, Rafif mwenye umri wa miaka 10 na mdogo wake hujiandaa kwenda shuleni wakiwa wamevalia sare zao za rangi ya krimu na kahawia.

Rafif husubiri kwa hamu kukutana na marafiki zake darasani na kujifunza masomo mbalimbali, ikiwemo hisabati, Kiarabu na masomo ya Kiislamu. Pia anafurahia matarajio ya kuanza kujifunza Kiingereza mwaka ujao.

Lakini safari yake ya kwenda shule inakabiliwa na changamoto kubwa zaidi kuliko kuvuka barabara au kuchelewa basi.

Shule ya Rafif iko katika mji wa Taiz, kusini-magharibi mwa Yemen, juu ya mlima unaotazama bonde linalojulikana kama "eneo lisilomilikiwa na upande wowote". Eneo hilo liko mstari wa mbele wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea kati ya vikosi vinavyoiunga mkono serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa, inayoungwa mkono na Saudi Arabia, na wapiganaji wa kundi la Houthi Ansar Allah wanaoungwa mkono na Iran.

Upande mmoja wa shule hiyo kuna maeneo yanayodhibitiwa na vikosi vya serikali, huku upande wa pili kukiwa na maeneo yanayoshikiliwa na wapiganaji wa Houthi, wakiwemo wapiga-risasi wa mbali (snipers). Hali hiyo inamaanisha kuwa wanafunzi kama Rafif hulazimika kusoma kila siku wakiwa karibu na mstari wa mapambano.

Nyumba ya Rafif iko chini ya mteremko wa mlima, hivyo kila siku hulazimika kupanda njia ya mlima kuelekea shuleni.

Lakini safari hiyo si ya kawaida. Kila anapoelekea shuleni, mgongo wake hubaki wazi kuelekea maeneo yanayoaminika kuwa wapiganaji wa kundi la Houthi.

"Nahisi uwoga," anasema Rafif.

Licha ya hofu hiyo, kama watoto wengi wa Yemen wanaoishi karibu na maeneo ya mapigano, Rafif huendelea na safari yake ya kila siku kwenda shule, akihatarisha maisha yake ili kupata elimu.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), takriban watoto milioni 3.2 nchini Yemen walikuwa nje ya mfumo wa elimu hata kabla ya kuongezeka kwa mapigano mwezi uliopita.

Mzozo wa miaka mingi nchini humo umeathiri pakubwa sekta ya elimu, huku mamilioni ya watoto wakikosa fursa ya kwenda shule kutokana na mapigano, umaskini, uharibifu wa miundombinu na kuhama kwa familia kutoka maeneo yao.

Kwa watoto kama Rafif, changamoto si tu kupata nafasi ya kusoma, bali pia kufika shuleni salama katikati ya mazingira yaliyozungukwa na vita.

Shirika hilo linasema kuwa maelfu ya watoto wameuawa au kupata ulemavu tangu vita vilipozuka mwaka wa 2014, huku maelfu wengine wakisajiliwa kupigania makundi yenye silaha kutoka pande zote mbili za mzozo huo.

Licha ya hatari hizi, Rafif anasema hataki kuacha kwenda shuleni kwa sababu anapenda kuwaona marafiki zake, na kwa kuwa shule ndiyo fursa yake pekee ya kujumuika nao. Kisha anaanza kutaja majina ya watoto wa darasani mwake.

Kwenda shuleni ndiyo wakati pekee ambao wazazi wa Rafif humruhusu kutoka nje ya nyumba, na wanatamani sana apate elimu na fursa ya maisha bora zaidi.

Rafif ana ndoto ya kua daktari baadaye maishani.

Ganda la kombora lilianguka kutoka mahali tusipopajua

Familia ya Rafif ilihamia mji wa Taiz kutoka Hodeidah miaka tisa iliyopita wakitafuta usalama baada ya Wahouthi kuudhibiti mji huo. Hata hivyo, Taiz nayo imeendelea kugubikwa na mapigano makali.

Rafif anakumbuka tukio la miaka miwili iliyopita wakati kombora la mizinga lilipoanguka karibu na nyumba yao.

"Kila mtu alikuwa nje isipokuwa mimi na kaka yangu. Ghafla kombora lilianguka kutoka sehemu tusiyoijua. Vipande vyake vilipenya mlango na kuingia ndani ya nyumba," alisema.

Katika shambulio hilo, Rafif alivunjika mkono na hadi leo bado ana kovu la jeraha alilopata.

Katika siku za karibuni, mapigano yamezidi kushika kasi. Jumapili iliyopita, Wahouthi walikata njia muhimu ya usafirishaji inayounganisha Taiz na Aden, hatua iliyoongeza hofu ya kuzingirwa kwa mji huo. Wakazi waliiambia BBC kuwa wana wasiwasi Wahouthi wanaweza kuuteka Taiz wakati wowote.

Wakati huo huo, vikosi vya serikali vinadaiwa kupata mafanikio katika maeneo mengine, vikirejesha udhibiti wa maeneo ya kimkakati katika Mlango Bahari wa Bab al-Mandab na kuanzisha mashambulizi ya kujaribu kuurejesha mji mkuu, Sanaa.

Nyumba nyingi za Taiz zimejengwa kwenye miteremko ya milima, lakini baadhi sasa zimesalia mahame baada ya familia nyingi kukimbia mapigano.

BBC ilijaribu kutembelea eneo analoishi Rafif mara mbili, lakini viongozi wa jamii walionya kuwa ni hatari sana. Katika ziara ya kwanza, wakazi waliripoti watu watatu kupigwa risasi na wadunguaji, huku ziara ya pili ikikatizwa baada ya kuripotiwa tukio jingine la ufyatuaji risasi.

Katika Shule ya Rafeef, mwalimu Abdul Raqeeb Al-Obaidi aliwaonyesha waandishi wa habari maeneo ya milimani ambayo alisema yanatumika kama kambi za kijeshi, ngome na vituo vya wadunguaji wa Wahouthi.

Walipokuwa juu ya paa la shule, mshauri wa usalama aliyekuwa akiandamana nao aliwataka warejee ndani haraka, akionya kuwa walikuwa wakionekana kutoka maeneo hayo na wangeweza kulengwa kwa risasi.

Abdul Raqeeb alisema shule hiyo imewahi kushambuliwa hapo awali.

"Hali inaweza kulipuka wakati wowote. Tunaweza kuwa darasani, shuleni, barabarani au hata usingizini, lakini hatujui kesho itakuwaje," alisema.

Kwa Abdul Raqeeb na wakazi wengi wa Taiz, hatari imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku, jambo linaloonyesha namna vita vilivyoathiri maisha ya kawaida ya wananchi.

Taiz imekuwa kwa muda mrefu moja ya maeneo makuu ya mapigano katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Yemen.

Baada ya Wahouthi kuiondoa serikali madarakani katika mji mkuu, Sanaa, mwaka 2015, walijaribu kuudhibiti mji wa Taiz. Hata hivyo, makundi ya wapiganaji wa eneo hilo yaliwafurusha kutoka sehemu kubwa ya mji huo.

Kuidhibiti Taiz kungeipa harakati ya Wahouthi udhibiti kamili wa kaskazini mwa Yemen. Katika mashambulizi yao ya hivi karibuni, wameongeza matumizi ya ndege zisizo na rubani pamoja na silaha nyingine za kivita.

Mara nyingi, raia ndio wanaobeba gharama kubwa ya mapigano hayo.

Jioni ya siku hiyo, BBC ilipigiwa simu kutoka hospitali iliyoko karibu na shule hiyo, ikiarifiwa kuwa watoto wawili walikuwa wamejeruhiwa vibaya baada ya kombora la mizinga kulipuka.

Waandishi wa habari walipofika Hospitali ya Al Rawda, walimkuta muuguzi amesimama nje ya chumba cha wagonjwa mahututi akiwa ameshika jozi ndogo ya viatu vya plastiki vya mtoto, vilivyokuwa vimetapakaa damu.

Viatu hivyo vilikuwa vya Ahmed, mvulana mwenye umri wa miaka mitatu aliyefariki baada ya kombora kuanguka kwenye karakana ya kutengeneza magari mjini humo.

Tukio hilo linaangazia athari za vita vinavyoendelea Yemen, ambavyo vimegeuza maisha ya raia, hasa watoto, kuwa katika hatari ya kila siku.