Wachunguzi Zanzibari wasema mwanamitindo wa Marekani Ashlee alijiua
Polisi huko Zanzibar wamehitimisha kuwa mshawishi wa mitandao ya kijamii kutoka Marekani, Ashley Robinson, mwenye umri wa miaka 31, alifariki kwa kujiua kufuatia msongo wa mawazo, baada ya uchunguzi kuhusu kifo chake katika hoteli moja visiwani humo.
Bi Robinson, ambaye pia alijulikana kama Ashlee Jenae, alifariki baada ya tukio lililotokea katika hoteli moja kisiwani huko tarehe 8 mwezi wa Aprili.
Akitoa taarifa kuhusu matokeo ya uchunguzi huo Alhamisi, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Zuberi Chembera, alisema wachunguzi wamebaini bila shaka kwamba kifo cha Bi Robinson kilitokana na kujiua na kwamba hakuna mtu mwingine aliyehusika.
"Kupitia maelezo ya mashahidi na uchunguzi wa vifaa vya mawasiliano vya marehemu na mchumba wake, tulibaini kuwa alikuwa na msongo wa mawazo. Ujumbe waliotumiana ulionyesha malalamiko ya mara kwa mara kuhusiana na hali ya maisha yake," Chembera aliwaambia waandishi wa habari mjini Zanzibar.
Tukio hilo lilizua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuibuka kwa taarifa zinazokinzana kuhusu mazingira ya kifo chake.
Katika matokeo yake ya awali, polisi walisema Robinson alijitoa uhai kufuatia kutofautiana na mchumba wake, Joseph McCann, 45. Hata hivyo, ripoti zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa huenda ndiye aliyemuua.
Polisi baadaye walianzisha uchunguzi kamili na kuchukua pasipoti ya McCann na kumhoji kama sehemu ya taratibu za kawaida.
Kulingana na wachunguzi, McCann na Bi Robinson waliingia katika jumba la kifahari la Zuri Hotel tarehe 6 Aprili na kutoelewana kulitokea kati ya wanandoa hao karibu saa sita mchana tarehe 8 Aprili, na kusababisha mzozo ambao haujatatuliwa.
Wasimamizi wa hoteli waliarifiwa na kumhamisha McCann hadi Villa 65 huku juhudi zikiendelea kushughulikia hali hiyo.
Polisi walisema alipatikana akiwa amejilingalinga kwenye chuma cha kutundika nguo kwa kutumia mkanda wa nguo unaotolewa kwa kawaida kwa wageni katika vyumba vya hoteli.
Familia ya mshawishi na McCann hazijatoa maoni kuhusu matokeo ya polisi wa Zanzibar.
Bi Robinson na McCann walikuwa wamesafiri hadi Tanzania kwa likizo na kusherehekea siku yake ya kuzaliwa tarehe 5 Aprili.
Alimchumbia siku hiyo hiyo, siku nne kabla ya kifo chake.
Mwili wa Bi Robinson baadaye ulirudishwa Marekani tarehe 24 Aprili, na ibada ya mazishi yake ilifanyika Mei 05 huko New Jersey.
Soma zaidi: