Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vitu vinavyoathiri Wi-Fi yako na jinsi ya kuiboresha
Alex Hills ni mvumbuzi, aliyekuwa mmoja wa watu wa kwanza ulimwenguni kuangazia shida za muunganisho wa Wi-Fi.
Katika kitabu chake "Wi-Fi and The Bad Boys of Radio" anaelezea kwamba nyumba yako inaweza kuwa imejaa vitu ambavyo vinakatiza mawimbi ya Wi-Fi.
Kutambua matatizo haya kunaweza kusaidia kurekebisha muunganisho wako na hata kubadilisha jinsi unavyotumia mojawapo ya teknolojia muhimu zaidi maishani mwako.
Baadhi ya vitu hivyo ni:
Microwave
Kwa miaka 17, mawimbi ya redio yasiojulikana yaliwashangaza wanaastronomia nchini Australia.
Baadhi waliyahusisha na miale ya jua huku umma ukishuku viumbe wa nje ya dunia.
Hatimaye, walibaini yalipotokea. Darubini yao ilikuwa ikipatana mawimbi ya nishati kutoka kwa microwave ya ofisi wakati wa chakula cha mchana.
Darubini sio teknolojia pekee ambayo inaweza kuathiriwa na kuingiliwa na mawimbi ya microwave, walibaini kuwa microwave pia inaweza kuathiri utendaji wa mtandao wako wa Wi-Fi.
WiFi, kama vile teknolojia nyingi za mawasiliano zisizotumia waya, husambaza habari kwa kutumia mawimbi ya redio.
Serikali huhifadhi masafa mengi ya redio kwa madhumuni mahususi, kama vile utekelezaji wa sheria, udhibiti wa trafiki hewani, na utangazaji wa redio za masafa ya AM na FM. Hata hivyo, baadhi ya masafa yanapatikana kwa matumizi ya umma bila leseni.
Kwa mfano, mawimbi ya bendi ya 2.4 GHz ni mojawapo ya masafa yanayotumika sana na mitandao ya Wi-Fi na vifaa vya Bluetooth. Cha kushangaza ni kwamba pia ni masafa ambayo microwave hutumia kupasha joto chakula.
Tanuri za microwave zimefunikwa ili kuweka microwave zinazopasha joto chakula ndani. Hata hivyo, ikiwa una microwave ya zamani, iliyochakaa, au ukifungua mlango kabla ya mzunguko wa kupasha joto kukamilika, Hills anasema kwamba hii inaweza kuingiliana na mawimbi ya Wi-Fi.
"Microwave si tatizo sana siku hizi," Hills anasema. Zimetengenezwa vizuri zaidi, na Wi-Fi inaweza kufanya kazi kwenye bendi ya 5 GHz badala ya bendi ya 2.4 GHz.
Hata hivyo, ikiwa una Wi-Fi au microwave ya zamani, kupasha joto chakula kunaweza kukatiza matumizi yako ya mitandao.
Tangisamaki
Ikiwa unafuga Samaki au wanyama wengine wa majini nyumbani, hii inaweza kusababisha matatizo.
"Mawimbi ya redio hudhoofika kiasili kwa umbali," Hills anaelezea. "Lakini wakati mwingine hupita kwenye kitu kinachopunguza mawimbi. Inayoitwa 'athari ya kivuli'."
Wi-Fi na maji hazichanganyiki. Miongoni mwa matatizo mengine, molekuli za maji zinaweza kuwa kama sumaku ndogo zinazonyonya nguvu ya mawimbi ya redio. Ikiwa kuna tanki la samaki kati yako na kipanga njia chako, inaweza kuhitilafiana na Wi-Fi.
Athari ya kivuli ndiyo tatizo kuu linalowakabili watumiaji wa mitandao ya wifi, Hills anasema, na si tu kwa sababu ya matangi ya samaki.
Mawimbi ya redio yanaweza kupita kwenye vifaa fulani, kama vile mbao , kwa urahisi. Hata hivyo, kuta zilizotengenezwa kwa vifaa vizito, kama vile matofali au zege, hutoa matatizo makubwa zaidi.
"Fikiria mstari ulionyooka unaounganisha kipanga njia chako kwenye kifaa unachotaka kuhudumia," anasema Hills. Mawimbi yanaweza kuruka kuzunguka chumba na kuzunguka vikwazo kwa kufuata njia tofauti; hata hivyo, kadiri vikwazo vinavyozidi kuwa njiani, ndivyo athari inavyozidi kuwa ngumu.
Ufupi pia huboresha utendaji wa Wi-Fi. Kuweka router katikati ya nyumba na juu iwezekanavyo ni hatua nzuri za kwanza.
Ikiwa hiyo haitoshi, unaweza kujaribu kutumia kiunganishi cha Wi-Fi ili kuongeza mawimbi, au ubadilishe kipanga njia na mtandao unaosambaza muunganisho katika nafasi nzima kwa kutumia vifaa kadhaa vidogo.
Kwa njia hiyo hautalazimika kuwasumbua Samaki au Wanyama wako wa majini unaowafuga nyumbani.
Vioo
Tatizo lingine la Wi-Fi ni kurudishwa mwanga kwa vioo.
Mawimbi ya redio ni aina nyingine ya mwanga. Na, kama vile mwanga unavyoruka kutoka kwenye sehemu zinazorudisha mwanga kama vioo, ndivyo vivyo hivyo katika mawimbi ya Wi-Fi.
Sehemu yoyote tambarare, inayorudisha mwanga, kama vile televisheni, unaweza kusababisha tatizo hili vile vile. Unaweza pia kupata tatizo hili ikiwa kuta za nyumba yako zina karatasi za chuma katika vifaa vyao vya ujenzi.
Ikiwa una eneo lililo wazi nyumbani, fikiria mstari ulionyooka kati yako na kipanga njia na ufikirie kama kuna kioo au televisheni kubwa ambayo inaweza kuwa inapotosha mawimbi kwa kuirusha.
Unaweza kufikiria kusogeza kifaa hicho, au ikiwa hutaki kubadilisha mpangilio wa nyumba yako, hili ni tatizo lingine ambalo viunganishi vya Wi-Fi vinaweza kusaidia kutatua.
Msimu wa baridi
Mvua haipaswi kutatiza muunganisho wako wa Wi-Fi, isipokuwa wakati unatumia mtandao ulio kando jengo tofauti katika eneo lililo wazi. Hata hivyo, matatizo yanaweza kutokea wakati hali ya hewa inazidi kuwa mbaya.
Theluji inaweza kuwa tatizo kwa miundombinu katika maeneo yaliyo na nyumba, au hata mji mzima, iwe ni kutokana na baridi kali inayoharibu sehemu za chuma au nyaya na kuzuia mawimbi ya setilaiti.
Joto linaweza kusababisha matatizo kama hayo. Na, ingawa hali ya hewa inaweza isiwe chanzo cha moja kwa moja, mitandao inaweza kupungua kasi wakati kila mtu yupo ndani na anatazama mitandao ya YouTube kwa wakati mmoja.
Hii ina maana kwamba usumbufu katika kuenea kwa meme unaweza kuwa matokeo mengine ya mabadiliko ya hali ya hewa. Suluhisho? Mbali na kutekeleza wajibu wako, unaweza kuzishinikiza kampuni za mawasiliano ya simu na mamlaka za mitaa kuchukua hatua za haraka.
Kuhusu Alex Hills, kwa sasa anaishi Alaska, ambapo amejitolea muda mwingi wa kazi yake kusaidia miji na vijiji vya mbali kuunganishwa kwenye intaneti.
Hii ni tafsiri ya ripoti ya Kihispania iliyochapishwa na BBC Future.