Mwanamke anayeokoa nyoka dhidi ya binadamu

Dhamira ya Okikiola ni kuokoa nyoka

Chanzo cha picha, Adesola Ikulajolu/BBC

Maelezo ya picha, Dhamira ya Okikiola ni kuokoa nyoka
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Nyoka huchukuliwa kuwa hatari kubwa, waerevu na mara nyingine hata kuhusishwa na imani potofu na uchawi katika baadhi ya jamii za Kiafrika.

Kwa kawaida nyoka anakuwa juu ya orodha ya mambo ambayo mtu anaogopa maishani mwake.

Kwa mfano, Nigeria, tatizo la kung'atwa na nyoka linaendelea kuwa tishio kubwa la afya ya umma, hasa katika maeneo ya vijijini ambako visa vingi haviripotiwi. Hata hivyo, Taiwo Okikiola, mwanamke anayejihusisha na utafiti wa wanyama watambaao, amejitolea kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu nyoka na kuhamasisha uhifadhi wao.

Kwa wengi, kukutana na nyoka ni jambo la kutisha. Katika mataifa mengi ya Afrika, ambako dawa za kuondoa sumu ya nyoka bado ni adimu, watu wengi huamua kuwaua nyoka mara tu wanapowaona.

Lakini kwa Okikiola, nyoka si viumbe wa kuogopwa pekee, bali ni sehemu muhimu ya mfumo wa ikolojia na chanzo muhimu cha maendeleo ya tiba mbalimbali.

Anajitambulisha kama mtaalamu wa wanyama watambaao na amejitolea kuwaokoa nyoka wanaokaribia kuuawa na binadamu kwa kuwakamata na kuwarejesha katika makazi yao ya asili.

Takwimu za Kituo cha Utafiti wa Kung'atwa na Nyoka nchini Nigeria zinaonyesha kuwa takribani watu 20,000 hung'atwa na nyoka kila mwaka. Kati yao, karibu watu 2,000 hupoteza maisha kutokana na ukosefu wa dawa za kuondoa sumu ya nyoka.

Kwa Okikiola, kulinda nyoka si suala la uhifadhi wa viumbe pekee, bali pia ni hatua muhimu katika kuokoa maisha ya binadamu kupitia maendeleo ya dawa zinazotokana na sumu ya nyoka.

"Nyoka ni chanzo muhimu cha tiba"

Katika sehemu nyingi za Afrika, hususan Tanzania, nyoka bado wanahusishwa na imani za ushirikina, mikosi na nguvu za giza. Mtazamo huo umechangia hofu kubwa dhidi ya viumbe hao.

Hata hivyo, Okikiola alichagua njia tofauti. Aliamua kujifunza kuhusu nyoka, tabia zao na mchango wao katika mazingira na afya ya binadamu.

Ingawa watu wengi husita kumkaribia nyoka, Okikiola ana lengo moja: anataka watu wawe na mtazamo chanya dhidi ya nyoka kwa sababu ni viumbe wa tiba.

"Watu wengi huona nyoka kama tishio pekee, lakini ukweli ni kwamba ni viumbe wanaotafuta chakula na makazi kama wanyama wengine. Wanapokaribia makazi ya watu mara nyingi huwa wanatafuta mazingira ya kuishi," anasema.

Anasisitiza kuwa nyoka wana mchango mkubwa katika sekta ya tiba kutokana na matumizi ya sumu zao katika utafiti na utengenezaji wa dawa mbalimbali.

Kwa zaidi ya miaka mitano sasa, amekuwa akifanya tafiti kuhusu aina tofauti za nyoka na tabia zao.

Safari hiyo haijakosa changamoto

"Baadhi ya watu huniita mchawi, wengine hudhani nina matatizo ya akili. Lakini ninaelewa ninachofanya na ninaamini kazi hii ni kwa manufaa ya jamii," anasema.

Licha ya kutetea uhifadhi wa nyoka, Okikiola anakiri kuwa baadhi ya aina zenye sumu kali zinaweza kuwa hatari kwa binadamu na zinahitaji kushughulikiwa kwa tahadhari kubwa.

''Sitaki tu kuwalinda nyoka, nataka kubadili mtazamo wa watu, lakini wale wenye sumu kali, wanaoua watu nchini Nigeria, ni hatari," alisema mwanadada huyo.

Okikiola aliamua kuchunguza tabia za nyoka

Chanzo cha picha, Adesola Ikulajolu/BBC

Maelezo ya picha, Okikiola aliamua kuchunguza tabia za nyoka

"Dawa ya kuondoa sumu ya nyoka inapaswa kupatikana kila hospitali"

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mbali na shughuli zake za uhifadhi, Okikiola pia anahamasisha utafiti na utengenezaji wa dawa za kuondoa sumu ya nyoka nchini Nigeria.

Mjadala kuhusu suala hilo ulipamba moto mwezi Januari 2026 baada ya kifo cha mwimbaji kijana Ifunanya Nwagene, maarufu kama Nanyah.

Ripoti zilieleza kuwa msanii huyo mwenye umri wa miaka 26 alifariki baada ya kung'atwa na nyoka huku akishindwa kupata matibabu stahiki kwa wakati.

Tukio hilo lilizua maswali mengi kuhusu upatikanaji wa dawa za kuondoa sumu ya nyoka katika hospitali za Nigeria.

Kwa mujibu wa Okikiola, aina tofauti za nyoka huzalisha sumu tofauti, jambo linalomaanisha kuwa matibabu lazima yaendane na aina ya nyoka aliyesababisha jeraha.

"Ili kumpatia mgonjwa tiba sahihi, ni muhimu kwanza kubaini aina ya nyoka aliyemng'ata," anasema.

Anaeleza kuwa ukosefu wa dawa hizo katika hospitali nyingi, hasa za maeneo ya vijijini, unaendelea kuhatarisha maisha ya maelfu ya watu kila mwaka.

"Inasikitisha kwamba mwaka 2026, taifa kubwa kama Nigeria bado linapoteza watu kutokana na kung'atwa na nyoka ilhali dawa za kuondoa sumu hiyo hazipatikani kwa urahisi katika vituo vya afya vya karibu na wananchi," anasema.

Mwaka 2017, Nigeria ilitenga dola 192,000 kwa ajili ya programu za kukabiliana na tatizo la kung'atwa na nyoka. Hata hivyo, wengi wanaamini kiasi hicho hakilingani na ukubwa wa tatizo hilo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, zaidi ya watu milioni 5.4 hung'atwa na nyoka kila mwaka duniani, huku zaidi ya watu 81,000 wakifariki kutokana na madhara ya sumu ya nyoka.

Kwa Okikiola, suluhisho la tatizo hilo halipo tu katika kuongeza upatikanaji wa dawa, bali pia katika kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu nyoka na umuhimu wao kwa maisha ya binadamu.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid