Ni vita gani vilivyo na athari kubwa zaidi kwa bei ya dizeli — vya Iran au vya Ukraine?

    • Author, Ben Chu
    • Nafasi, Policy and analysis correspondent, BBC Verify
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Rais wa Marekani Donald Trump amelaumu mashambulizi ya Ukraine dhidi ya viwanda vya kusafisha mafuta vya Urusi kwa kupungua kwa mauzo ya dizeli duniani na kupanda kwa bei kote duniani, akisema Rais Volodymyr Zelensky "anataka kuleta matatizo kwa dunia".

"Ni lazima aache mara moja," alisema Trump, kabla ya kupendekeza kuwa Ukraine inapaswa "kupata kiongozi mpya anayeweza kufikia makubaliano".

Hata hivyo, wengine wameelekeza lawama kwenye mzozo kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran kwa kusababisha kupungua kwa mauzo ya mafuta yaliyosafishwa kutoka eneo la Ghuba.

Baada ya Trump kutangaza mpango wenye utata wa kununua dizeli kutoka Urusi - akiahidi "bei nafuu kwa Wamarekani" - kitengo cha BBC Verify kimechunguza mambo yaliyoathiri upatikanaji wa mafuta hayo katika miezi na miaka ya hivi karibuni.

Takwimu zinaonyesha kuwa ingawa migogoro ya Ukraine na Iran yote imepunguza kwa kiasi kikubwa mauzo ya dizeli duniani, kupungua kwa usambazaji kutoka nchi za Ghuba kutokana na vita dhidi ya Iran kumekuwa kukubwa zaidi.

Ni nini kimetokea kwa bei za dizeli duniani?

Ingawa kupanda kwa gharama ya dizeli kunawaathiri moja kwa moja madereva, kuna wasiwasi mkubwa zaidi kutokana na matumizi yake katika malori, magari ya kubeba mizigo na meli ambazo huunda uti wa mgongo wa minyororo ya usambazaji duniani. Ongezeko lolote la gharama za usafiri linaweza kuwafikia watumiaji kwa njia ya bei za juu.

Wastani wa bei za dizeli za rejareja za Marekani mnamo Oktoba 5 zilikuwa $6.20 (£4.69) kwa lita, chini ya rekodi ya $6.50 kwa lita iliyoonekana mnamo Septemba 21, kulingana na takwimu za hivi karibuni kutoka kwa Utawala wa Habari za Nishati wa Marekani.

Kabla ya vita na Iran lita ya dizeli nchini Marekani iligharimu karibu $3.50.

Vile vile, wastani wa bei za dizeli za Uingereza kwa sasa zinafikia viwango vya juu vya rekodi, huku data kutoka Idara ya Usalama wa Nishati na Net Zero ikionyesha kuwa mnamo Oktoba 5 lita moja iligharimu 199p.

Mnamo mwaka wa 2025, takriban mapipa milioni 6.8 ya dizeli kwa siku yalikuwa yakisafirishwa kwenda kwenye soko la kimataifa, kulingana na takwimu kutoka kampuni ya data ya usafirishaji wa baharini ya Kpler.

Mauzo hayo ya nje yanachangia takriban robo moja ya jumla ya matumizi ya dizeli duniani; kiasi kilichosalia kinatokana na uzalishaji wa ndani wa nchi mbalimbali.

Mnamo Septemba 2026, mauzo ya nje ya kimataifa yalikuwa yameshuka hadi mapipa milioni 5.8 kwa siku ikiwa ni upungufu wa takriban mapipa milioni moja kwa siku.

Baadhi ya nchi, hasa Marekani, zimeongeza mauzo yake ya dizeli nje ya nchi katika mwaka uliopita, lakini kwa ujumla, mauzo halisi ya kimataifa yamepungua.

Wachambuzi wanasema kuwa kupungua huko ndiko kulikosababisha kupanda kwa bei ya rejareja ya dizeli.

Ni kiasi gani cha usambazaji kimepungua kutoka Urusi?

Mwaka wa 2025, Urusi ilikuwa ikisafirisha nje takriban mapipa 810,000 ya dizeli kwa siku, lakini kufikia Septemba 2026, kiwango hicho kilishuka hadi takriban mapipa 140,000 kwa siku ikiwa ni upungufu wa takriban mapipa 670,000 kwa siku.

Jonathan Leader Maynard, kutoka Chuo cha King's College London, anasema kuwa "wachambuzi wengi" wangetazama kushuka huko kwa mauzo ya nje ya bidhaa za mafuta ya Urusi, ikiwemo dizeli, kama jambo linalotokana "hasa ​​na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Ukraine" badala ya vikwazo vya kimataifa.

Ni kiasi gani cha usambazaji kimepungua kutoka Mashariki ya Kati?

Mbali na kuwa muuzaji mkuu wa mafuta ghafi, Mashariki ya Kati pia ni kitovu muhimu cha kimataifa cha uzalishaji wa dizeli.

Mnamo mwaka wa 2025, nchi za Ghuba, Saudi Arabia, Falme za Kiarabu (UAE), Kuwait, Bahrain na Oman, zilikuwa zikisafirisha takriban mapipa milioni 1.4 ya dizeli kwa siku.

Kufikia mwezi wa Septemba 2026, kiwango hicho kilikuwa kimeshuka hadi takriban mapipa 670,000 kwa siku.

Kushuka huko kwa kasi kumesababishwa na athari za vita kati ya Marekani na Iran kwenye mtiririko wa usafirishaji wa dizeli iliyosafishwa kutoka nchi za Ghuba kupitia Lango la Bahari la Hormuz.

Mzunguko wa meli katika njia hiyo ya maji umevurugwa vibaya na mashambulizi ya Iran dhidi ya meli za mafuta pamoja na hatua ya Marekani ya kuzingira bandari za Iran.

Ingawa makadirio kutoka kwa kampuni zinazofuatilia meli yanaonyesha kuwa mtiririko wa mafuta ghafi kupitia njia hiyo ulirejea karibu na viwango vya kabla ya vita mwezi uliopita, kwa kiasi fulani kutokana na msaada wa jeshi la wanamaji la Marekani katika kulinda usafiri wa meli, mtiririko wa dizeli iliyosafishwa kutoka Mashariki ya Kati umebaki chini sana ikilinganishwa na viwango vya kabla ya vita.

Ni mgogoro upi unaostahili lawama zaidi?

Takwimu zinaashiria kuwa mzozo na Iran umekuwa na athari kubwa zaidi katika kushuka kwa kiasi cha mauzo ya dizeli duniani kuliko vita vya Ukraine.

Mauzo ya nje kutoka Urusi yamepungua kwa takriban mapipa 670,000 kwa siku, ikilinganishwa na upungufu wa takriban mapipa 810,000 kutoka Mashariki ya Kati;

Ingawa wachambuzi wanasisitiza kuwa matukio yote mawili ni muhimu.

"Mgogoro kati ya Marekani na Iran ulisababisha mshtuko mkubwa katika masoko ya nishati duniani mwaka wa 2026, lakini mgogoro unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine sasa unaongeza shinikizo hilo kwa kusababisha kusimama kwa shughuli za viwanda vya kusafisha mafuta nchini Urusi," Paul de Leeuw, mkurugenzi wa Taasisi ya Mabadiliko ya Nishati katika Chuo Kikuu cha Robert Gordon, aliambia BBC Verify.

Maoni yake yaliungwa mkono na Rory Johnson, mchambuzi wa masuala ya mafuta katika kampuni ya Commodity Context, ambaye alisema kuwa mashambulizi ya Ukraine "yanafikisha madhara ya vita ndani kabisa ya ardhi ya Urusi na kwa kiasi kikubwa kuathiri pakubwa soko la nchi hiyo ambayo ni muuzaji wa pili kwa ukubwa duniani wa dizeli".

Taarifa za ziada zimetolewa na Nicholas Barrett na Joshua Cheetham

Chati na kuandaliwa na Erwan Rivault