Tiba ya kutema maji "ya baraka": Uhaba wa huduma za afya unavyowasukuma Waafghanistan kwa waganga

Chanzo cha picha, BBC via Getty
Kwenye viunga vya mji wa Kandahar kusini mwa Afghanistan, makumi ya watu hukusanyika mbele ya nyumba.
Wamekuja wakitumaini kupata majibu, na nafuu kutokana na magonjwa yanayotishia maisha yao.
Katika moja ya vyumba, kilichopambwa kwa rangi ang'avu, wanaume, wanawake na watoto wengi wagonjwa huonekana wamekaa au wamelala chini.
Lakini si wote waliopo hapa wanakufa au wanaougua.

Katika kona moja ameketi Neda Mohammad Qadri, mtu ambaye wote wamekuja kumuona. Akiwa amevaa kilemba cheupe na ndevu ndefu nyeusi, anajiita pir, yaani mganga au mponyaji wa kiroho.
Qadri hunywa maji kutoka kwenye chupa, kisha huyatema, akiwanyunyizia watu walioko mbele yake.
Anadai kuwa, kupitia Mungu, kitendo hiki rahisi kimewasaidia watu wengi wanaougua saratani na thalassemia, ugonjwa wa damu unaoweza kusababisha kushindwa kufanya kazi kwa viungo vya mwili.
Qadri hana elimu rasmi ya dini, wala mafunzo yoyote ya kitabibu.
Miaka michache iliyopita, alikuwa akifanya kazi kama mpishi, lakini hata wakati huo, anasema watu walikuwa wakimfuata ili wapate hirizi, vitu vidogo vinavyoaminika na baadhi ya watu kuwa na nguvu za kiasili.
Anasema kadiri hali za wagonjwa zilivyoanza kuimarika, idadi ya watu waliomtembelea iliongezeka sana, hasa wagonjwa wa saratani.

Chanzo cha picha, Habib Ullah
Mfumo wa afya uko chini ya shinikizo kubwa
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, kuna zaidi ya wagonjwa 24,000 wa saratani nchini Afghanistan kila mwaka, na takribani vifo 17,000 husababishwa na ugonjwa huo kila mwaka.
Wataalamu wanasema huenda idadi halisi ni kubwa zaidi kwa sababu wagonjwa wengi hawapati uchunguzi rasmi kutokana na ukosefu wa hospitali na kliniki, pamoja na madaktari na wauguzi wa kutosha kuzihudumia.
Nchini Afghanistan, watu wanazidi kukimbilia kwa wanaoitwa waganga wa kiroho kutokana na uhaba wa vituo vya afya vya kutosha na gharama kubwa za kupata huduma katika vituo vichache vya kitabibu, kama vile hospitali maalum ya saratani iliyojengwa hivi karibuni na serikali ya Taliban huko Kabul.
Wataalamu pia wanasema Afghanistan ina viwango vya juu vya saratani katika eneo hilo kutokana na sababu za mtindo wa maisha, ikiwa ni pamoja na matumizi makubwa ya vyakula vyenye chumvi nyingi na tumbaku ya kutafuna inayojulikana kama naswar, pamoja na viwango vya juu visivyo vya kawaida vya uchafuzi wa mazingira.
Baada ya Taliban kuidhibiti Afghanistan 2021, misaada ilipungua kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano, Shirika la Msalaba Mwekundu lilisimamisha msaada wake kwa Hospitali ya Mirwais huko Kandahar, kituo kikuu cha huduma za afya katika eneo hilo, ikitaja changamoto za ufadhili.

Chanzo cha picha, Bilal Guler/Anadolu Agency via Getty Images
Kwa ufadhili mdogo na usio wa kudumu kutoka Taliban, hospitali hiyo sasa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa rasilimali, hali inayowalazimu wagonjwa kununua hata dawa na vifaa vya msingi wao wenyewe.
Athari za upungufu huu mkubwa zilipunguzwa kwa kiasi fulani, hasa kusini mwa Afghanistan, kupitia huduma za afya za kuvuka mpaka kwenda Pakistan.
Hadi takribani miezi 18 iliyopita, wakazi wa Kandahar waliweza kuvuka mpaka bila viza, wakisafiri kwenda hospitali zilizo na vifaa bora zaidi kwa matibabu, hata kwa magonjwa madogo.
Hata hivyo, hali hiyo sasa imekoma. Mipaka katika eneo la Chaman–Spin Boldak imekuwa ikifungwa mara kwa mara kufuatia mapigano kati ya Afghanistan na Pakistan, na udhibiti mkali umewekwa kwa dawa zilizokuwa zikiingizwa kutoka Pakistan, bidhaa ambazo eneo hilo linazitegemea sana.
Hali hii yote imeweka mzigo mkubwa zaidi kwa mfumo wa afya wa Afghanistan ambao tayari uko katika hali dhaifu.
Vikwazo vya huduma za matibabu
Mke wa Nazir Ahmad Maiwandwal, Shukriya, alianza kupata maumivu makali ya kichwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Alisafiri naye kwenda Pakistan, ambako alifanyiwa upasuaji baada ya kugunduliwa kuwa na uvimbe wa ubongo.
"Baada ya upasuaji, hali ya mke wangu ilianza kuimarika," anasema Maiwandwal. "Aliongezeka uzito kidogo, na kwa miezi sita kila kitu kilionekana kuwa sawa. Hata hivyo, afya yake ilianza kudhoofika tena polepole."
Kwa kukata tamaa, wanandoa hao waliamua kurudi Pakistan baada ya kushauriwa na madaktari kuwa ni muhimu, lakini kufikia wakati huo mpaka ulikuwa umefungwa kwa usafiri wa bure.
"Niliomba visa ya Pakistan mara tatu, lakini kila mara ilikataliwa," anasema Maiwandwal. "Nilienda Kabul, lakini hata huko, kituo cha matibabu ya saratani hakikuwa na huduma ya mionzi. Nilirudi nyumbani nikiwa nimekata tamaa."
Shukriya alifariki mwezi Machi. Alikuwa na umri wa miaka 24 tu.
Kurudi kwenye ile nyumba huko Kandahar, Qadri anasema watu wanaendelea kufika mlangoni kwake. Wengi wanatafuta tumaini la mwisho.
"Wagonjwa wa saratani wanakuja kwangu kutoka kila pembe ya Afghanistan, kati ya watu 250 hadi 300, na hata kufikia 400 hutembelea kila siku," anasema.
Mtoto wa Habibullah, Assad, alikuwa mmoja wao.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Habibullah aliweza kufika nchi jirani ya Pakistan akitafuta matibabu kwa ajili ya mwanawe, lakini aliambiwa hakuna chochote kingeweza kufanywa. Alishauriwa amrudishe Assad nyumbani ili atumie muda wake uliobaki na familia yake.
Akiwa hataki kukata tamaa, na akitafuta angalau "faraja ya moyoni", Habibullah alirudi Afghanistan na kumpeleka Assad kwa Qadri baada ya kusikia kutoka kwa marafiki kwamba aliwaponya watu wengi waliokuwa na saratani.
Lakini hata huko hakukuwa na matumaini.
"Walichukua picha ya mwanangu na kumwambia aihifadhi, kwamba baada ya siku kumi uso wake ungeweza kubadilika na hata asingejitambua," anasema Habibullah.
Badala yake, hali ya Assad ilizidi kuwa mbaya na alifariki akiwa njiani kuelekea hospitalini.
"Nilimpoteza mwanangu. Ameacha watoto watano na mjane," analalamika Habibullah.
"Mwanangu alidanganywa kwa ahadi zisizo na msingi. Alitoa pesa na hirizi lakini hakupata nafuu kutokana na saratani," anasema.
Habibullah anadai kuwa licha ya kumpa kondoo kama malipo, Qadri pia alidai kiasi kikubwa cha pesa "kama sadaka na kwa ajili ya usafiri".
Kwa mujibu wake, Qadri ni "tapeli."

Mkazi mwingine wa Kandahar ambaye hakutaka kutajwa jina, anasema alitembelea maeneo mengi ya ibada na waganga wa kiroho, akiwemo Qadri, akitafuta matibabu ya saratani ya ngozi.
"Qadri aliniambia nisiende Pakistan au mahali pengine popote, na nilete kondoo. 'Mungu akipenda utapona kabisa,'" anakumbuka.
Anaongeza kuwa alienda kwa Qadri kwa siku saba kwa ajili ya maombi na pia alipewa sindano za ceftriaxone pamoja na vidonge vya co-amoxiclav na Augmentin.
Hizi ni antibiotiki zenye nguvu ambazo kwa kawaida hutumika kutibu maambukizi mbalimbali ya bakteria.
"Licha ya yote haya, hali yangu haikubadilika; nilijua muda ulikuwa unapotea, hivyo nililazimika kwenda kutibiwa katika Shaukat Khanum Memorial Cancer Hospital & Research Centre huko Lahore, Pakistan."
Hatimaye alipona baada ya kupata matibabu ya kitabibu huko.

Chanzo cha picha, Hamid Sabawoon/Anadolu via Getty Images
Mohammad Aziz Saeedi, mkazi wa Nangarhar, anasema mapacha wake wa kike walikuwa na thalassemia na walihitaji kupatiwa damu kila mwezi ili waendelee kuishi.
Anasema kwamba kwa ushauri wa baadhi ya ndugu, aliwapeleka watoto wake kwa waganga wa kiroho, lakini hali yao ilizidi kuwa mbaya.
"Baadhi walitupatia masharti ya lishe na wengine wakatupa maji yaliyobarikiwa," anasema Saeedi. "Lakini hakukuwa na mabadiliko; baadaye tulianza matibabu ya kitabibu na sasa hali yao ni nzuri sana."
Wataalamu wanatahadharisha kwamba maombi na tiba za kiroho zinaweza kutoa msaada wa kisaikolojia na faraja kwa watu wanaoishi na magonjwa sugu na hatari, lakini havipaswi kuchukua nafasi ya matibabu ya kitabibu.
Hili linaweza kuwa ushauri mgumu kusikia kwa wagonjwa wanaosubiri kwa subira nje ya ile nyumba ya kawaida huko Kandahar, wakisukumwa na matumaini yanayofifia na karibu hakuna kingine cha kuwategemea.













