Arsenal na Atletico zatoka sare ligi ya mabingwa Ulaya
Chanzo cha picha, Getty Images
Arsenal na Atletico Madrid walifunga penalti kila
mmoja katika sare ya mkondo wa kwanza iliyojaa matukio ambayo yalisawazisha
nusu fainali yao ya Ligi ya Mabingwa.
Viktor Gyokeres alishinda na kufunga mkwaju wa
penalti kwa wageni dakika moja tu kabla ya kipindi cha mapumziko baada ya
kuangushwa katika eneo hatari na beki David Hancko.
Lakini Julian Alvarez alisawazisha bao hilo dakika
11 baada ya kipindi cha pili baada ya Ben white kuunawa mpira katika eneo la
ulinzi wa Arsenal
Mchezaji wa akiba Eberechi Eze alifikiria
kujishindia penalti alipokanyagwa na beki wa wa Atletico Madrid Hancko ndani ya
eneo hatari lakini uamuzi huo
ulibatilishwa baada ya ukaguzi wa VAR.
Mchezo huo ulianza kwa kishindo huku kukiwa hakuna
upande wowote unaotaka kuona lango la mwenzake
Lakini baada ya Gyokeres kuweka The Gunners mbele,
Atletico Madrid walianza kipindi cha pili kwa kuzidisha presha.
Ademola Lookman alimlazimisha David Raya kuokoa
kabla ya Gabriel Magalhaes kuokoa shambulio laAntoine Griezmann huku wenyeji wakitafuta bao la kusawazisha.
Atletico walipata penalti wakati mkwaju wa Marcos
Llorente kutoka pembeni mwa eneo la goli ulipogonga mguu wa Ben White na kugusa
mkono wake.
Habari za hivi punde, 'Milipuko kadhaa' yaripotiwa kisikika Tehran
Vahid Online, Jukwaa maarufu la habari za kidijitali linaloendeshwa na mwanaharakati wa Iran na mwanablogu Vahid, muda mfupi uliopita limechapisha jumbe kadhaa zinazoripoti milipuko ya kusikia mjini Tehran.
Walioshuhudia tukio hiloi wameiambia mtandao huo wa habari kwamba milipuko hiyo ilisikika katika sehemu ya mashariki ya mji mkuu, katika wilaya za Tehran-Pars na Hakimiyah.
Baadhi ya watu walieleza milipuko hiyo kama "shughuli za kupambana na ndege za kivita."
BBC haijafanikiwa kuthibitisha usahihi wa ripoti hizo.
Shambulio dhidi ya wanaume wawili wa Kiyahudi mjini London ni ugaidi- Polisi
Chanzo cha picha, UGC
Wanaume wawili Wayahudi wamechomwa visu katika eneo la Golders Green, kaskazini mwa London, katika tukio lililotangazwa na polisi kuwa la kigaidi.
Wanaume hao wawili, waliotajwa kama Shilome Rand na Moshe Shine, walipatiwa matibabu katika eneo la tukio na sasa wako katika hali thabiti hospitalini, kulingana na Polisi.
Polisi wamesema mwanaume mwenye umri wa miaka arobaini na mitano, raia wa Uingereza aliyezaliwa Somalia, alipigwa kwa bunduki ya umeme yaani Taser na polisi kabla ya kukamatwa kwa tuhuma za jaribio la mauaji. Mshukiwa huyo kwa sasa yuko rumande.
Waziri Mkuu Keir Starmer amesema shambulio hilo la chuki dhidi ya Wayahudi ni la kusikitisha sana, akiongeza kuwa “Mashambulizi dhidi ya jamii yetu ya Kiyahudi ni mashambulizi dhidi ya Uingereza.”
Polisi wamesema maafisa wao waliitikia tukio hilo Jumatano baada ya kupokea taarifa kuwa watu walikuwa wamechomwa visu.
Mshukiwa huyo pia alijaribu kuwachoma visu maafisa waliokuwa wamefika eneo la tukio, lakini hakuna aliyejeruhiwa.
Polisi walitoa picha za tukio hilo kutoka kamera zilizovaliwa na maafisa, ambapo wanasikika wakimwamrisha mshukiwa mara kadhaa alale chini kabla ya kumshambulia kwa Taser, na kisha kumuamuru aachie kisu.
Imeelezwa kuwa mshukiwa huyo alikuwa na historia ya vurugu kubwa na matatizo ya afya ya akili.
Wachunguzi wanaamini mshukiwa huyo huyo alihusika katika tukio jingine la awali katika eneo hilo.
Mkuu wa Polisi wa Kupambana na Ugaidi nchini Uingereza, Laurence Taylor, baadaye alitangaza rasmi tukio hilo kuwa la kigaidi.
Rabbi Mkuu Ephraim Mirvis, ambaye anawakilisha jamii kubwa zaidi ya Wayahudi nchini Uingereza, amesema tukio hilo “linathibitisha kuwa ukiwa Myahudi unaoonekana wazi, hauko salama na hatua zaidi zinahitajika.”
Shambulio hilo linakuja chini ya wiki moja baada ya jaribio la uchomaji moto dhidi ya ukuta wa kumbukumbu eneo la Golders Green, na zaidi ya mwezi mmoja tangu magari ya wagonjwa yanayoendeshwa na shirika la matibabu la Kiyahudi Hatzola kuchomwa moto.
Comey ajisalimisha kufuatia madai ya kumtishia Trump maisha katika chapisho la Instagram
Chanzo cha picha, Getty Images
Mkurugenzi wa zamani wa shirika la upelelezi la Marekani, FBI, James Comey, amejisalimisha kwa mamlaka ili kukabiliana na mashtaka yanayodai kuwa picha aliyosambaza kwa muda mfupi kwenye mitandao ya kijamii ilikuwa tishio kwa maisha ya Rais wa Marekani Donald Trump.
Kesi hiyo inatokana na chapisho la mwaka 2025 kwenye Instagram lililowekwa na Comey, lililokuwa na picha ya magamba ya baharini yaliyopangwa kuunda maneno “86 47”. ni istilahi ya mtaani inayomaanisha “kuondoa”, na waendesha mashtaka wanadai kuwa inahamasisha vurugu dhidi ya Trump, rais wa 47.
Comey alikanusha mashtaka akisema hakujua maana ya namba hizo, na ameshutumu upande wa mashtaka kwa kuwa na nia za kisiasa.
Hii ni mara ya pili kwa Wizara ya Sheria kumfungulia mashtaka ya jinai Comey, ambaye ni mkosoaji wa muda mrefu wa Trump.
Comey hakuweka ombi la kujitetea wala kuzungumza wakati alipofikishwa mahakamani kwa muda mfupi katika jimbo la Virginia.
Wakili wake, Patrick Fitzgerald, alisema mkurugenzi huyo wa zamani atataka kesi ifutwe kwa misingi ya mashtaka ya kuchagua na yenye nia ya kulipiza kisasi — akidai alilengwa kwa sababu ya kuzungumza dhidi ya Trump.
Jaji Fitzpatrick alikataa juhudi za Wizara ya Sheria kuweka masharti ya kuachiliwa kwa Comey, akisema hayakuwa ya lazima, kwa mujibu wa CBS News.
Waendesha mashtaka wamemshtaki Comey kwa kujua na kwa makusudi kutoa tishio la kuondoa maisha ya — na kusababisha madhara ya kimwili kwa — rais, na pia kusambaza tishio hilo kati ya majimbo.
Kila shtaka lina adhabu ya juu ya hadi miaka 10 jela.
Katika taarifa ya video Jumanne, Comey alisema ana nia ya kupambana na mashtaka hayo.
Chapisho lake la awali la Mei 2025 lilikuwa na picha ya magamba ya baharini ufukweni yaliyopangwa kuonyesha “86 47”, likiwa na maelezo: “Mpangilio mzuri wa magamba ya baharini wakati wa matembezi yangu ufukweni.”
Comey alifuta picha hiyo baada ya malalamiko ya umma.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mashtaka dhidi ya Comey Jumatano, Trump alimuita “mtu fisadi”.
“Niseme yeyote anayejua kuhusu uhalifu, anajua 86. Ni istilahi ya magenge ya uhalifu inayomaanisha muue. Magenge hutumia neno hilo wanapotaka kumuua mtu, wanasema ‘86 huyo’.
Watu kama Comey ni tishio kubwa sana, nadhani, kwa wanasiasa na wengine,”
Baadhi ya wataalamu wa sheria — pamoja na wabunge — wamehoji uzito wa mashtaka hayo.
Comey alifutwa kazi na Trump katika muhula wake wa kwanza baada ya kuanzisha uchunguzi kuhusu uingiliaji wa Urusi katika uchaguzi wa urais wa Marekani wa 2016.
Tangu wakati huo, Trump amekuwa akitaka mara kwa mara kufunguliwa mashtaka dhidi yake — na mashtaka ya sasa ni jaribio la pili la utawala kufanya hivyo.