Manchester United: Je, Carrick ndiye tatizo au uongozi wa klabu?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Mustakabali wa kocha wa Manchester United, Michael Carrick, unaendelea kuwa na mashaka baada ya timu hiyo kupokea kipigo cha mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Bournemouth, huku hasira za mashabiki zikielekezwa pia kwa wachezaji na viongozi wa klabu hiyo.

Kulikuwa na hali iliyoashiria mwisho unaoweza kuwa karibu kwa Carrick alipokuwa akizunguka uwanja wa Old Trafford baada ya kipigo hicho. Kocha huyo amekuwa akiwaaga mashabiki kwa kuwapigia makofi, lakini safari hii hali ilikuwa tofauti, baada ya timu hiyo kupitia kipindi kigumu cha matokeo.

United ilikuwa imecheza mechi nane bila ushindi, mfululizo mbaya zaidi tangu msimu wa 2015-16, huku ikipokea vipigo viwili vizito ndani ya wiki moja.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, viongozi wa klabu walikuwa katika mazungumzo mazito kuhusu mustakabali wa kocha huyo.

Hata hivyo, iwapo viongozi wa United wanaamini kuwa kumfukuza Carrick kutatosha kutatua matatizo ya klabu, mwitikio wa mashabiki uwanjani unaashiria kuwa mgogoro huo ni mpana zaidi.

Ijumaa, Carrick alikuwa amesema timu yake ingekuwa tofauti katika mchezo dhidi ya Bournemouth, baada ya kufungwa mabao 4-1 na Como.

"Tutakuwa timu tofauti Jumapili. Ni lazima tuwe timu tofauti," alisema.

Lakini United ilishindwa kuonyesha mabadiliko aliyokuwa ameahidi.

Carrick hakuweza kuthibitisha iwapo bado atakuwa kocha wa timu hiyo katika mchezo ujao dhidi ya Chelsea.

"Wajibu ni wangu. Niseme nini zaidi kwa sasa? Ninaelewa kabisa hali ilivyo. Sitarajii jambo lolote, liwe hili au lile. Ninaipenda klabu hii na nitafanya kile ninachoamini kuwa bora kwa ajili yake," alisema.

Mashabiki waigeukia timu na viongozi

Mashabiki wa United walionyesha hasira zao baada ya kipigo hicho. Walikuwa wameimba jina la Carrick, lakini mara tu alipoingia kwenye njia ya kuelekea vyumbani, waligeukia wachezaji kwa kuwazomea.

Zomeazomea iliendelea hadi mchezaji Diogo Dalot alipoondoka uwanjani.

Kwa mujibu wa makala hiyo, mashabiki wanaamini baadhi ya wachezaji hawana uwezo wa kutosha, hawajitumi ipasavyo au huenda yote mawili.

Lakini hasira zao hazikuishia hapo.

Mchezo ulikuwa haujatimia hata dakika moja wakati baadhi ya mashabiki walipoanza kuimba nyimbo za kuwapinga wamiliki wa klabu, familia ya Glazer, pamoja na Sir Jim Ratcliffe.

Familia ya Glazer imekuwa ikikosolewa na mashabiki wa United tangu ilipochukua umiliki wa klabu hiyo mwaka 2005 kupitia mpango uliohusisha mikopo.

Kwa mujibu wa hesabu za hivi karibuni zilizotajwa katika makala hiyo, deni la klabu limeongezeka hadi zaidi ya pauni bilioni 1.15. Mchambuzi wa masuala ya fedha katika soka anayejulikana kama Swiss Ramble anakadiria kuwa malipo ya riba yaliyolipwa yanafikia pauni milioni 852.

Katika mwaka wa mwisho wa fedha, malipo ya riba yalikuwa pauni milioni 37, kutoka pauni milioni 34 mwaka uliotangulia.

Baadhi ya mashabiki wanaamini fedha hizo zingetumika vizuri zaidi kuimarisha kikosi kwa kusajili wachezaji bora.

Je, Ratcliffe ameshindwa kutimiza matarajio?

Kulikuwa na matumaini kuwa Ratcliffe, ambaye ni shabiki wa muda mrefu wa United, angebadilisha mwelekeo wa klabu baada ya kufikia makubaliano na familia ya Glazer ya kununua hisa za sehemu ya klabu mnamo Desemba 2023.

Hata hivyo, maamuzi kadhaa ya uongozi wake yameibua maswali kuhusu namna anavyoisimamia klabu hiyo.

Baada ya United kushinda Kombe la FA mwaka 2024 kwa kuifunga Manchester City katika fainali, uongozi uliamua kuendelea kumuunga mkono kocha Erik ten Hag baada ya kutathmini uwezekano wa makocha wengine.

Klabu ilitumia zaidi ya pauni milioni 200 kuwasajili wachezaji, akiwemo Leny Yoro, Matthijs de Ligt na Manuel Ugarte.

Ten Hag alifukuzwa kazi Oktoba 2024.

Wiki iliyotangulia, Ten Hag aliambia gazeti la The Athletic kuwa klabu ilikiuka ahadi ya kutomuuza kiungo wa Scotland Scott McTominay, ambaye alihamia Napoli, huku United ikimleta Ugarte kutoka Paris Saint-Germain kwa ada ya pauni milioni 50.

Baadaye, United ilimshawishi Ruben Amorim kuondoka Sporting CP kabla ya mwisho wa msimu, licha ya kutaka kusubiri hadi majira ya joto.

Klabu iliendelea kumuunga mkono Amorim hata baada ya kumaliza nafasi ya 15 katika Ligi Kuu ya England, matokeo mabaya zaidi kuwahi kurekodiwa na United katika kipindi cha karibuni, na baada ya kufungwa na Grimsby Town ya Ligi ya Pili katika Kombe la EFL.

Hata hivyo, Amorim alifukuzwa Januari baada ya kutofautiana na mkurugenzi wa soka Jason Wilcox kuhusu mtindo wa uchezaji.

Carrick aliletwa kuiongoza timu hadi mwisho wa msimu, lakini baadaye akapewa nafasi hiyo kwa kudumu baada ya kuisaidia United kurejea katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kukosekana kwa miaka miwili.

Iwapo atafutwa kazi, itakuwa mara ya tatu kwa klabu hiyo kumfukuza kocha ndani ya misimu mitatu, jambo ambalo linaweza kuzua maswali zaidi kuhusu maamuzi ya viongozi.

Bango lililokuwa limeinuliwa katika sehemu ya Stretford End uwanjani Old Trafford lilionyesha picha za manahodha wa zamani wa United, Bryan Robson, Eric Cantona na Roy Keane, likiwa na ujumbe wa kuwakumbusha viongozi kuhusu viwango vya juu vilivyokuwa vikiitambulisha klabu hiyo.

Usajili, tiketi na uwanja mpya vyazidisha hasira

Mkurugenzi wa soka Jason Wilcox pia amekuwa akikosolewa na baadhi ya mashabiki kuhusu usajili wa wachezaji, licha ya bajeti ya usajili kuwekwa katika kiwango cha juu.

Wilcox, ambaye alijiunga na United akitokea Southampton baada ya Ratcliffe kuingia katika uongozi wa klabu, amekuwa akifanya kazi kwa kiasi kikubwa nyuma ya pazia. Hata hivyo, katika mchezo dhidi ya Bournemouth, mashabiki waliimba nyimbo za kumkosoa na kumtukana.

Afisa mkuu mtendaji wa klabu hiyo, Omar Berrada, ambaye aliwahi kufanya kazi Manchester City, alikuwa ameketi pamoja na Wilcox wakati United ilipokuwa ikipokea kipigo hicho.

Baadhi ya mashabiki wamekuwa na wasiwasi kuhusu viongozi hao kutokana na historia yao ya kufanya kazi katika City, ingawa Berrada hakuhusika katika mchakato wa hivi karibuni wa Ligi Kuu ya England kuhusu madai ya ukiukaji wa kanuni za kifedha dhidi ya klabu hiyo.

Mzozo mwingine uliowakasirisha mashabiki ni uchunguzi kuhusu uuzaji wa tiketi kwa bei za juu ulioanzishwa wakati wa kiangazi. Klabu ilisema ililenga kuwabaini watu wanaouza tiketi kinyume cha taratibu, lakini baadhi ya mashabiki walihisi hatua hiyo ingeweza kuwasukuma mashabiki wa kawaida nje na kutoa nafasi zaidi kwa wateja wa kampuni.

Vikundi vikuu vya mashabiki vilikosoa hatua hiyo, huku uongozi ukisisitiza kuwa haukuwa na nia ya kuwafukuza mashabiki wa kawaida.

Mipango ya kujenga uwanja mpya wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 100,000 pia imeibua mjadala.

Klabu ilisema utafiti wake ulionyesha kuwa wengi wa waliohojiwa waliunga mkono ujenzi wa uwanja mpya. Mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya pauni bilioni mbili, huku United ikitumia pauni milioni 63.5 kununua ardhi kwa ajili ya mradi huo mapema mwaka huu.

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wanatilia shaka gharama hizo, huku wengine wakipinga wazo la kuacha uwanja wa Old Trafford na kuhamia katika uwanja mpya.

Je, kubadilisha kocha kutatosha?

Ingawa Carrick amekubali kuwajibika kwa matokeo mabaya ya timu, ishara kutoka kwa mashabiki zinaonyesha kuwa matatizo ya Manchester United hayaishii katika benchi la ufundi.

Kuanzia malalamiko kuhusu wamiliki, maamuzi ya usajili, gharama za tiketi hadi mipango ya uwanja mpya, klabu hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi zinazozidi matokeo ya uwanjani.

Swali kubwa sasa ni iwapo mabadiliko ya kocha yataweza kurejesha utulivu, au kama Manchester United inahitaji mageuzi mapana zaidi katika uongozi na namna klabu inavyoendeshwa.