Tahadhari ya Ebola: Uganda yaweka masharti mapya ya usafiri
Uganda imewawekea karantini ya siku 21 raia wake wanaorejea kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku ikiongeza hatua za tahadhari dhidi ya Ebola.
Hatua hiyo inakuja wakati DRC ikiendelea kukabiliwa na mlipuko mkubwa wa ugonjwa huo, pamoja na kuibuka kwa wasiwasi baada ya watu wawili waliowahi kupita nchini Uganda kubainika baadaye kuwa na Ebola nchini Kenya na Nigeria.
Wizara ya Afya ya Uganda imesema wasafiri waliotembelea DRC hawataruhusiwa kwa sasa kutumia Uganda kama njia ya kupita kwenda nchi nyingine. Vilevile, raia wa Uganda wanaorejea kutoka DRC watalazimika kugharamia na kukamilisha karantini ya siku 21.
Mamlaka za afya pia zimeimarisha uchunguzi wa wasafiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe, mipaka ya nchi kavu na vituo maalumu vya ukaguzi vilivyowekwa kwenye baadhi ya barabara.
Waziri wa Afya wa Uganda, Chris Baryomunsi, amesema ni wasafiri wa huduma muhimu pekee kutoka DRC watakaoruhusiwa kuingia nchini, lakini chini ya hatua kali za afya ya umma.
Alisema hatua hizo zinalenga kuzuia Ebola kuingia nchini na kuhakikisha Uganda inaendelea kuwa huru dhidi ya ugonjwa huo.
Wakati huohuo, Wizara ya Afya imesema watu 60 waliokuwa wakifuatiliwa baada ya kuhusishwa na mgonjwa wa Ebola nchini Kenya wameondolewa kwenye uangalizi baada ya kukamilisha kipindi cha ufuatiliaji bila kuonesha dalili za maambukizi.
“Hatua hizi zote zinalenga kuhakikisha Uganda inaendelea kuwa huru dhidi ya Ebola,” amesema Waziri wa Afya, Chris Baryomunsi.
Tangu wagonjwa waiwili wa Ebola kuthibitishwa nchini Kenya na Nigeria mwezi huu, Uganda imeendelea kusisitiza kuwa hakuna kisa chochote cha maambukizi kilichoripotiwa ndani ya mipaka yake.
Uganda ilithibitisha kuwa watu 20 wameabukizwa Ebola na vifo viwili kabla ya kutangazwa kuwa huru dhidi ya ugonjwa huo mwezi Agosti.
Hata hivyo, wasiwasi umeendelea kuibuka baada ya wasafiri wawili waliopitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe siku moja kubainika baadaye kuwa na Ebola nchini Kenya na Nigeria.
Maelezo zaidi: