Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Bowen: Trump na Netanyahu walitaka kubadilisha mwelekeo wa Mashariki ya Kati - sasa wanakabiliwa na tishio
- Author, Jeremy Bowen
- Nafasi, Mhariri wa Kimataifa
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Donald Trump na Benjamin Netanyahu wanaamini ushindi dhidi ya Iran kutabadilisha muelekeo wa Mashariki ya Kati.
Eneo hilo linabadilika. Lakini sio kwa jinsi walivyotarajia. Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran haijasalimu amri. Hatari inayowakodolea macho sasa kuibuka kwa mzozo wa mara kwa mara.
Utawala wa Iran umedhihirisha wazi kwamba sio rahisi kuusambaraisha kama walivyodhani Trump and Netanyahu. Mtazamo wao haukuwa sahihi na sasa wameshindwa kudhibiti matokeo ya hatua yao dhidi ya taifa hilo.
Tukio la hivi punde ni la Iran kuangusha helikopta ya Marekani aina ya Apache. Hii inaashiria kuwa watawala wa Iran bado wanaweza kuwadhuru Wamarekani bila kulegeza msimamo wao katika juhudi za kuibuka washindi katika mgogoro unaoendelea.
Rais na majenerali wake watajaribu kujibu hatua ya Iran, ili kuonyesha kwamba hatakubali kuhangaishwa, huku wakijizatiti wakidumisha mchakato wa kidiplomasia usio na tija. Wahudumu wa Apache walinusurika. Laiti wangeuawa, jibu la Marekani huenda lingelikuwa kali zaidi.
Trump amekuwa akitegemea makubaliano na Iran ya kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz na kukubaliana na masharti ya mazungumzo ya muda mrefu kuhusiana na masuala makubwa, ikiwa ni pamoja na hifadhi ya urani iliyorutubishwa ya Iran na mipango yake ya nyuklia.
Wamarekani wanapinga vikali vita hivyo, sasa Trump anataka kujiondoa kwa kutafuta njia ambayo anaweza kuiwasilisha kama ushindi. Hii inaonekana kuwa changamoto kubwa.
Trump na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wamepata funzo la zamani.
Tangu wanadamu walipogundua vita, viongozi wamebaini kwamba ni rahisi kuanzisha vita kuliko kumaliza vita kwa ushindi wa moja kwa moja.
Walipoyaelekeza mataifa yao kwenye vita dhidi ya Iran siku ya mwisho ya mwezi Februari, wawili hao walitoa taarifa za video kwa kutumia maneno yaliyoakisi dhana kwamba wakati wa mabadiliko ya kihistoria unawadia. Utawala ambao umekuwa umadarakani nchini Iran tangu kupinduliwa kwa Shah mnamo 1979 ulikuwa unaelekea kuondolewa mamlakani.
"Kwa watu watukufu wa Iran, Ninasema usiku wa leo kwamba wakati uhuru wanu inanukia. Endelea kujikinga. Msiondoke majumbani mwenu. Nje ni hatari sana. Babomu yatadondoshwa kila mahali. Tutakapomaliza, chukueni serikali yenu. Hii huenda ikawa furasa ya kipekee kwa vizazi vijavyo."
Asubuhi iliyofuata, Netanyahu alisimama kwenye mwanga wa jua juu ya paa la Kyria, jumba la wizara ya ulinzi ya Israel lililopo katikati mwa jiji la Tel Aviv, ili kurekodi hotuba yake. Sawa na alivyofanya Trump, alizungumza kana kwamba ana hakika ya kuibuka mshindi katika vita hivyo.
"Muungano huu wa kijeshi unatuwezesha kufanya kile ambacho nimekuwa nikitamani kufanya kwa miaka 40: kuushinda utawala wa kigaidi. Hili ndilo nililoahidi - na hili ndilo tutakalo lifanya."
Katika maisha yake yote ya kisiasa, Netanyahu amedai Iran nindio tishio halisi kwa Israel, wala sio Wapalestina au nchi za Uarabuni. Alikuwa ameshindwa kuwashawishi marais wengine wa Marekani kuungana naye kuishambulia Iran. Trump alikuwa tofauti.
Kwa zaidi ya miaka miwili, tangu Hamas iliposhambulia Israel tarehe 7 Oktoba 2023, Netanyahu alikuwa amewaambia Waisraeli kwamba nguvu za jeshi lao, kwa ushirikiano na Marekani, zingewashinda maadui zao. Alisitiza nguvu pekee ndio jibu, sio diplomasia.
Netanyahu alikuwa na hisia ya mtu ambaye wakati wake wa kifahari ulikuwa umewadia. Alipoonekana teka mbe ya kamera baada ya Trump kumuomba aahirishae mipango yake ya kuishambulia Beirut siku ya Jumatatu, mwandishi mkuu wa gazeti la Israel Ben Caspit alisema alionekana kama puto iliyopasuka.
Caspit ni mmoja wa wakosoaji wengi wa waziri mkuu. Lakini ni wazi kuwa mkakati wa Netanyahu wa kutumia nguvu kudhibiti eneo hilo kwa maslahi yake umefeli.
Trump alitarakia ushindi wa haraka. Alifuatilia kwa tabasamu jinsi jeshi la Marekani lilivyomteka rais wa Venezuela na mke wake, na kuwapeleka katika jela la New York na kuweka madarakani mrithi anayetii huko Caracas. Aliamini utawala wa kubuni vitabuni ni bora zaidi kuliko vita vya milele vilivyopiganwa na watangulizi wake huko Iraqi na Afghanistan. Iran itafuata kwenye orodha hiyo.
Viongoz hao wawili wanajiuliza ni nini kilichoenda mrama. Marekani inasifikwa duniani kwa kuwa na jeshi lenye nguvu duniani. Israel ni nchi yenye nguvu zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Trump na Netanyahu waliona serikali ya Tehran inakabiliwa na mzozo wa kiuchumi uliosababishwa na vikwazo, usimamizi mbaya na ufisadi. Israel ilikuwa imewalemaza washirika wake kama vile Hamas huko Gaza na Hezbollah nchini Lebanon. Mshirika wake mwingine muhimu, Bashar al Assad aliondolewa madarakani kama rais wa Syria na kukimbilia Moscow. Mnamo mwezi Januari utawala huo ulivunja maandamano makubwa dhidi yake kwa kuwaua maelfu ya raia wa Iran.
Walipuuza uthabiti, ukatili na hila za utawala wa Kiislamu. Waliamini kwamba kuua kwa kiongozi wake mkuu na waandamizi wake kungeisambaratisha serikali.
Walitegemea sana ufanisi wa nguvu za kijeshi dhidi ya serikali ambayo ilikuwa imekabiliwa na vitisho vya mara kwa mara kwa takribani miaka 50, ilikuwa imejipanga kukabiliana na shambulio lolote kuzingatia usalama wa kitaifa unayoungwa mkono na imani zake za kidini na itikadi kali.
Mataifa Ghuba yenye utajiri wa mafuta, na washirika wa Marekani, kama vile Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain pia hawakusazwa. Wamepoteza mapato kutoka kwa kemikali za petroli na bidhaa zake, kama mbolea. Wamejenga mustakabali wao na kujinadi kama kitovu cha biashara ya mabilioni ya dola katika eneo la Ghuba. Wawekezaji watarajiwa, na watalii, wanahisi vita hivyo vinageuza mtazamo huo.
Utawala wa Iran unaamini kwamba utanusurika kwa kuvuruga uchumi wa dunia kwa kufunga Mlango-Bahari wa Hormuz. Hatua yake ya kushambulia majirani zake wa Uarabuni ni mbinu ya muda mrefu yakukabiliana na Marekani na Israel.
Utawala uliochukua nafasi ya viongozi wa zamani wa Iran waliouawa na Israel na Marekani wana itikadi kali sawa na watangulizi wao lakini wako tayari kuchukua hatua kali zaidi katika kile wanachoona kama kitisho. Wanaamini kuwa maneno pekee hayatazuia mashambulizi ya siku zijazo kutoka kwa Marekani au Israel. Badala yake, wanataka kuonyesha kwamba mashambulizi zaidi dhidi ya Iran yatakuwa na athari kubwa.
Sehemu muhimu ya mkakati wake ni kuunganisha vita vya Lebanon na vita vya Ghuba. Ujumbe wa utawala huo kwa Trump ni kwamba asitarajie makubaliano ya aina yoyote ikiwa Israel itaendelea kuishambulia Lebanon kwa mabomu na kujaribu kuiangamiza Hezbullah, wanamgambo wanaoendesha harakati za kisiasa ambayo imekuwa ikiikuza tangu miaka ya 1980 kama mtetezi wake dhidi ya Israel.
Kwa kuzuia mipango ya Israel ya kuishambulia Beirut, kwa madai kuwa makubaliano yalikuwa karibu kufikiwa (madai ambayo aliwahi kuyatoa hapo awali, kimakosa), Trump ameonyesha wazi kwamba anathibitisha uhusiano wa kile kinachotokea Lebanon na kile kinachofanyika katika eneo la Ghuba.
Siku ya Jumatatu, Netanyahu alisema hatakubali mpango huo. Ilikuwa alisema, "Hili kamwe halitakubalika." Hofu yake ni kwamba Trump atatanguliza maslahi ya kuvimaliza vita hivyo badala ya azma ya Netanyahu ya kuendelea na mapigano hadi pale atakapofaikiwa kuangamiza utawala wa Tehran.
Netanyahu aliahirisha mashambulizi aliyopanga dhidi ya Beirut, lakini tangu wakati huo jeshi la Israel, IDF, limeendelea kushambulia vibaya maeneo kusini mwa Lebanon.
Wakati Mlango wa Bahari wa Hormuz ulipofungwa mwezi Machi, onyo lilitolewa kwamba uchumi duniani utaathirika vibaya kutokana na mzozo huo kufikia mwezi Juni. Bila kufikiwa kwa makubalino ya kidiplomasia, huenda ikawa vigumu njia hiyo muhimu kufunguliwa tena hivi karibuni.