Je, tunapaswa kuwa na wasiwasi kiasi gani kuhusu hantavirus?

Chanzo cha picha, Reuters
Abiria kutoka kwa meli ya watalii iliyokumbwa na mlipuko wa virusi vya hantavirus wamehamishwa na kupelekwa katika nchi zao kujitenga na kupokea matibabu ikiwa ni lazima.
Baadhi ya abiria wengine kutoka MV Hondius waliondoka kwa safari za awali za ndege au viunganishi na mawasiliano yao sasa yanatafutwa kama tahadhari.
Maafisa wanasema hatari ya maambukizi kuenea kwa umma bado ni ndogo.
Wafanyakazi na abiria sasa wanakabiliwa na kulazimika kujitenga kwa zaidi ya mwezi mmoja ili kuzuia kuenea kwa uwezekano wowote.
Abiria watatu wamekufa baada ya kusafiri kwenye meli hiyo, wawili kati yao walithibitishwa kuwa na virusi.
Kwa hivyo tunapaswa kuwa na wasiwasi gani?
'Hii sio Covid'
Katika taarifa ya siku ya Alhamisi, Dk Maria Van Kerkhove kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) alisisitiza haikuwa mwanzo wa janga, akisema: "Hii sio Covid, hii sio mafua, inaenea tofauti sana."
Tofauti na magonjwa kama vile surua, ambayo huambukiza sana na huenea kwa urahisi, aina ya Andes ya hantavirus iliyosababisha mlipuko huo sio ya kuambukiza.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Usamabasaji kutoka kwa binadamu hadi kwa binadamu unawezekana lakini hatari ya maambukizo duniani bado ni ndogo, linasema WHO.
Katika taarifa ya hivi karibuni, WHO inasema kati ya kesi tisa - saba zilizothibitishwa na vipimo - zimetambuliwa kwa watu ambao walikuwa kwenye meli.
Bado haijabainika jinsi mlipuko huo ulianza.
Hantavirus kawaida huenea kutoka kwa panya, na watu walioambukizwa kwa kupumua hewa iliyochafuliwa na chembe za virusi kutoka kwa mkojo wa panya, kinyesi, au mate.
Safari hiyo ilikuwa ikizuru maeneo ya mbali ya wanyamapori, kwa hivyo abiria angeweza kuguswa na virusi wakati huo, au kabla ya kupanda meli.
Wataalam wameona aina ya Andes ikienea kati ya wagonjwa wa binadamu katika milipuko ya hapo awali, kupitia mawasiliano ya karibu sana, na wataalam wa afya wanaamini kuwa baadhi ya maambukizo kwenye meli ya MV Hondius yanaweza kuwa kati ya watu.
Hata meli za kifahari za kusafiri baharini zina hali duni au vikwazo vya maisha, na watu hutumia kwa pamoja vyumba na maeneo ya kulia - mahali ambapo maambukizi yanaweza kuenea.
Watu wanaweza kuambukizwa kutoka kwa mtu ambaye wanakaa naye kwa muda mrefu kupitia ukaribu wa kimwili.
Vifo hivyo vitatu ni pamoja na mwanamke wa Uholanzi aliyeondoka katika meli ya MV Hondius iliposimama katika kisiwa cha St Helena tarehe 24 Aprili.
Alikuwa akitumia chumba kimoja na mumewe ambaye hapo awali alikufa kwenye meli hiyo tarehe 11 Aprili - ingawa haijulikani kwa sasa ikiwa ni moja ya kesi zilizothibitishwa za hantavirus.
Hantavirus haisambazwi katika ulimwengu wa nje kupitia mawasiliano ya kila siku ya kijamii kama vile kutembea katika maeneo ya umma, maduka, sehemu za kazi, au shule, Shirika la Usalama la Afya la Uingereza (UKHSA) linasema.
Hantavirus inaweza kusambazwa kupitia wanadamu
Dalili za kawaida huonekana kati ya wiki mbili hadi nne baada ya kuambukizwa virusi, lakini zinaweza kutokea zaidi ya mwezi mmoja baadaye, ndiyo sababu muda uliopendekezwa wa kutengwa kwa abiria ni mrefu sana.
Watu ambao wanaweza kuwa wameambukizwa - ikiwa ni pamoja na kwenye meli, hospitalini au kwenye ndege yoyote ambayo abiria walichukua - watafuatiliwa.
Kazi ya kuwatafuta watu waliogusana na walioambukizwa ambayo inaendelea imekuwa "juhudi kubwa kabisa", Prof Robin May, afisa mkuu wa kisayansi katika UKHSA ameambia BBC, na ni hatua moja ambayo "tutaendelea kufanya... kwa muda".










