Saudi Arabia yaanza uchunguzi kubaini jinsi Wahouthi walivyofanikiwa kuishambulia

Maafisa wanasema uchunguzi huo pia unalenga kubaini sababu zilizofanya mifumo ya ulinzi wa anga ya Saudi Arabia ishindwe kutoa tahadhari ya mapema.

Muhtasari

Ruka Video uendelee
  • xx
  • Wicknell Chivayo
  • Kijanangoma
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx

Moja kwa moja

Na Dinah Gahamanyi & Faidha Ngaga

  1. Tunakomea hapo kwa leo. Kwaheri.

  2. Ndege ya British Airways yavunja safari baada ya dirisha kupasuka angani

    .

    Ndege ya British Airways iliyokuwa ikielekea Faro nchini Ureno ililazimika kurejea Uwanja wa Ndege wa Gatwick baada ya dirisha lake kuripotiwa kupasuka ikiwa angani.

    Ndege hiyo ya Airbus A321, nambari BA2660, ilibadilisha mwelekeo katika anga ya kaskazini-magharibi mwa Ufaransa na kutua salama Gatwick. Wakati wa tukio hilo, ilitoa ishara ya dharura ya "7700", inayotumika kuashiria hitilafu ya kiufundi.

    British Airways imesema ndege hiyo illivunja safari kutokana na "tatizo dogo la kiufundi" na kwamba abiria wamepangiwa kuendelea na safari yao baadaye.

    Tukio hilo limejiri siku chache baada ya ndege nyingine ya shirika hilo iliyokuwa ikielekea Chicago kulazimika kurejea Uwanja wa Ndege wa Heathrow kufuatia tahadhari ya dharura, huku barakoa za oksijeni zikishuka na abiria kukiripoti mitikisiko mikali wakati wa safari.

    Mwezi Agosti, raia wa Serbia Ljubisa Karović alijeruhiwa vibaya baada ya sehemu ya mwili wake kuvutwa nje kupitia dirisha la ndege ya Ryanair. Shirika hilo lilisema huenda dirisha hilo liliharibiwa na kitu kutoka nje ya ndege.

  3. Saudi Arabia yaanza uchunguzi kubaini jinsi Wahouthi walivyofanikiwa kuishambulia

    .

    Saudi Arabia imeripotiwa kuanzisha uchunguzi ili kubaini jinsi mifumo yake ya ulinzi wa anga ilivyoshindwa kuzuia makombora na ndege zisizo na rubani zilizorushwa na wapiganaji wa kundi la Wahouthi kutoka Yemen, ambazo zilisababisha mashambulizi matatu yaliyosababisha vifo vya watu katika uwanja wa ndege wa Riyadh.

    Shirika la habari la Associated Press (AP) limeripoti kuwa maafisa wawili wa eneo hilo wamesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa wapiganaji wa Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran walianza kwa kurusha idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani ili kukwepa mifumo ya ulinzi, kabla ya kushambulia uwanja huo wa ndege.

    APimeongeza kuwa mmoja wa maafisa hao amesema uchunguzi huo pia unalenga kubaini sababu zilizofanya mifumo ya ulinzi wa anga ya Saudi Arabia ishindwe kutoa tahadhari ya mapema kuhusu shambulizi hilo.

    Unaweza pia kusoma:

  4. 'Nilipoteza ndugu zangu wawili': Manusura wa ajali ya boti Djibout

    .

    Mhamiaji wa Ethiopia aliyenusurika ajali mbaya ya boti iliyopinduka katika pwani ya Djibouti amesema alipoteza ndugu zake wawili katika mkasa huo uliohusisha mamia ya watu waliokuwa wakielekea Yemen.

    Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema watu wasiopungua 139, wakiwemo watoto 15, walifariki dunia wakati boti iliyokuwa imewabeba wahamiaji 305 ilipopinduka karibu na eneo la Guehere, kaskazini mwa Obock, usiku wa Oktoba 8 na 9. Watu 82 waliokolewa baada ya ajali hiyo.

    Miongoni mwa manusura ni Abdullah Hussein, mhamiaji kutoka Gelemso katika eneo la West Hararghe, jimbo la Oromia nchini Ethiopia. Abdullah alikuwa akielekea Yemen kabla ya kuendelea na safari ya kwenda Saudi Arabia katika jaribio lake la pili la kutafuta maisha bora.

    Hata hivyo, safari hiyo iligeuka maafa baada ya dada yake kuwa miongoni mwa waliopoteza maisha.

    “Sitajaribu tena kwenda Saudi Arabia,” alisema Abdullah, akiongeza kuwa marafiki zake wengi pia walifariki katika ajali hiyo.

    Alisema manusura wengi, akiwemo mtoto mwenye umri wa miaka 13, wamebaki bila ndugu na jamaa zao baada ya mkasa huo.

    Abdullah, ambaye alikuwa ameishi Djibouti kwa miezi saba, alisema alifahamu hatari zinazohusiana na njia ya uhamiaji kupitia Yemen. Hata hivyo, anadai alishawishiwa na dalali aliyemhakikishia kuwa safari hiyo ilikuwa salama. Baada ya kulipa faranga 30,000 za Djibouti, alipanda boti hiyo akiamini angefanikiwa kufika Yemen na baadaye kupata kazi.

    “Madalali walituambia njia hiyo ilikuwa salama na kutupandisha boti. Tuliamini walichotuambia,” alisema.

    Manusura mwingine kutoka Ethiopia, Deribe, alisema alikuwa ameondoka Raya Qobo katika eneo la Amhara kuelekea Saudi Arabia. Alisafiri pamoja na mabinti wawili wa binamu zake na mjomba wake.

    “Dakika 20 hadi 30 baada ya kuondoka, boti ilipinduka,” alisema.

    Mabinti hao wawili pamoja na mjomba wake walikuwa miongoni mwa waliofariki.

    “Nilipoteza ndugu zangu wawili. Wengi wa waliofariki walikuwa wanawake. Kulikuwa na giza, na ilikuwa vigumu kwa watu kusaidiana,” alisema.

    Kwa mujibu wa manusura hao, boti hiyo iliondoka muda mfupi baada ya saa tatu usiku kabla ya kukumbwa na ajali iliyosababisha vifo vya watu wengi katika moja ya majanga mabaya zaidi kuwahi kurekodiwa kwenye njia ya uhamiaji kati ya Pembe ya Afrika na Yemen.

  5. Rwanda kuwa mwenyeji wa mbio za kwanza za langalanga(F1) barani Afrika tangu mwaka 1993

    Uwanja mpya wa mbio karibu na Kigali umebuniwa kwa kutumia kikamilifu mandhari ya asili ya Rwanda.
    Maelezo ya picha, Uwanja mpya wa Formula 1 karibu na Kigali umebuniwa kwa kutumia kikamilifu mandhari ya asili ya Rwanda.

    Rwanda imesaini mkataba wa miaka 10 na Formula 1 ili kuwa mwenyeji wa mbio hizo katika nchi hiyo ya Afrika, kuanzia "mapema miaka ya 2030".

    Mashindano hayo – yatakayoitwa African Grand Prix – yatafanyika kwenye uwanja mpya maalum utakaojengwa eneo la Bugesera, kilomita 40 kusini mwa mji mkuu Kigali na karibu na uwanja mpya wa ndege wa kimataifa wa jiji hilo.

    Hii itakuwa mbio ya kwanza ya F1 barani Afrika tangu mwaka 1993.

    Katika hafla ya utiaji Saini, Rais wa Rwanda, Paul Kagame alisema: "Kwa zaidi ya miongo mitatu, mashindano makuu ya magari duniani yamekuwa yakindeshwa bila bara hili, na jambo hilo linabadilika kupitia makubaliano haya. "Rwanda inajivunia kuwa mwenyeji wa Formula 1 African Grand Prix, na kushiriki wakati huu na zaidi ya mashabiki milioni 100 kote Afrika, wengi wao wakiwa ni vijana ambao wanastahili kuuona mchezo huu nyumbani na kujiona wao wenyewe ndani yake: kama wahandisi, mafundi, wajasiriamali na, siku moja, madereva."

    Aliongeza kusema kuwa:"Uwanja uliopo Bugesera, kando ya uwanja mpya wa ndege wa kimataifa, utaleta ajira, ujuzi, utalii na biashara mpya katika nchi yetu na ukanda wetu kwa miongo mingi ijayo, kwa sababu lengo letu halikuwa kamwe kuwa na wikendi moja tu ya mbio, bali faida ya kudumu kwa watu wetu.

    Rais wa F1, Stefano Domenicali alisema mkataba huo mpya ulikuwa "wakati wa kihistoria kwa F1", ambao ulimaanisha kuwa mchezo huo utakuwa ukifanya mbio "katika kila bara linalokaliwa na watu". Domenicali aliongeza: "Afrika imekuwa sehemu ya mustakabali wa Formula 1 kila wakati, na tangu mwanzo tulikuwa tumedhamiria kurejea kwa njia sahihi, tukiwa na mshirika sahihi, ahadi ya muda mrefu na maono ya wazi ya kuleta athari yenye maana."

    Taarifa kutoka F1 ilisema mradi huo umekuja kama matokeo ya miaka mingi ya ushirikiano ili kuhakikisha misingi sahihi, ‘’tukiwa na mshirika bora’’, ipo tayari ili kuleta mashindano ya grand prix yenye mafanikio, endelevu na ya kiwango cha kimataifa kwa vizazi vijavyo".

    Uwanja huo, ulioundwa na aliyekuwa dereva wa F1 Alex Wurz, umeundwa ili kwenda sambamba na mazingira asilia, ukitumia mabadiliko ya miinuko ya eneo hilo kutengeneza uzoefu wa kipekee na wenye changamoto wa mashindano huku ukitoa fursa ya kipekee ya utazamaji kwa mashabiki, taarifa hiyo iliongeza.

    F1 inatumai kuwa mbio hizo zitatoa fursa kwa mchezo huo kupanua wasifu wake barani Afrika, soko ambalo halijachunguzwa sana ikilinganishwa na Ulaya, Asia, na Amerika.

    Bado haijafahamika ni wapi mbio hizo zinaweza kufaa zaidi katika ratiba ya mwaka.

    Mbio hizo zina uwezekano wa kuzua utata kwani Rwanda imewahi kushutumiwa hapo awali kwa kutumia michezo kusafisha taswira yake.

    Mchezo huo una uwezekano wa kutaka kuepuka kuandaa mbio hizo katika msimu mkuu wa mvua wa mwezi Machi hadi Mei.

    Kuna msimu mwingine mfupi wa mvua usio na usumbufu mkubwa kuanzia mwezi Oktoba hadi Novemba. F1 imejitolea kuhakikisha msimu unakuwa na mbio zisizozidi 24.

  6. Mtu anayeshukiwa kuwa na Ebola awekwa karantini Somalia

    .

    Serikali ya Somalia imetangaza kumuweka karantini raia wa nchi hiyo aliyesafiri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, anayeshukiwa kuwa na Ebola.

    Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya imesema kuwa mtu huyo amethibitishwa kusafiri pamoja na mtu aliyefariki dunia kutokana na Ebola.

    Wizara hiyo imeongeza kuwa mtu huyo amepelekwa katika Kituo cha Karantini na Matibabu ya Ebola katika Hospitali ya Forlarnini, jijini Mogadishu, kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.

    Hatua hiyo inafuatia tangazo la serikali ya Kenya siku ya Jumapili kuhusu kifo cha raia wa nchi hiyo aliyekuwa amerejea kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuambukizwa ugonjwa huo.

    Kenya ilithibitisha kisa chake cha kwanza cha Ebola, kilichomhusisha raia wa nchi hiyo ambaye alikuwa akiishi DR Congo kwa miaka saba iliyopita.

    Waziri wa Afya wa Kenya, Aden Duale, alisema mgonjwa huyo alianza kuugua mwezi mmoja uliopita na alitibiwa katika hospitali kadhaa nchini DR Congo kabla ya kufariki dunia siku chache baada ya kuwasili Nairobi, mji mkuu wa Kenya.

    Duale alisema mgonjwa huyo alipanda ndege na kufanyiwa ukaguzi wa kawaida wa afya katika uwanja mkuu wa ndege jijini Nairobi kabla ya kupelekwa hospitalini na mmoja wa ndugu zake.

    Wizara ya Afya ya Kenya imesema tangu wakati huo imeimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huo katika viwanja vya ndege na vituo vya kuvukia mipaka.

    Zaidi ya watu 4,000 wamefariki dunia kutokana na Ebola nchini DR Congo mwaka huu, katika mlipuko ambao ni wa pili kwa kusababisha vifo vingi zaidi miongoni mwa milipuko inayojulikana ya ugonjwa huo.

    Unaweza pia kusoma:

  7. Ilhan Omar: Mbunge wa Marekani mwenye asili ya Somali azungumza kuhusu msako wa nyumba yake Washington, D.C

    g

    Mbunge wa chama cha Democrats katika jimbo la Minnesota,Ilhan Omar, ameelezea msako uliofanywa na maafisa wa shirikisho katika nyumba yake huko Washington, D.C. kama "jaribio la kuwalenga maadui wa kisiasa na kuwapa silaha maafisa wa kutekeleza sheria wa shirikisho."

    Mbunge huyo wa Somalia mwenye asili ya Marekani ni mkosoaji mkubwa wa Rais Donald Trump na hapo awali ameshtakiwa kwa kashfa.

    "Niko sawa. Usifanye makosa kuhusu hilo: hili ni jaribio la kumlenga adui wa kisiasa, kwa kutumia vyombo vya sheria vya shirikisho kama silaha. Kwa muongo mmoja, Trump amenilenga kwa uongo usio na msingi na kampeni za kashfa. Hii ni hatua ya hivi karibuni katika kampeni yake ya vitisho vya kisiasa. Sitanyamazishwa," Ilhan aliandika kwenye ukurasa wake wa X.

    Ofisi yake pia ilitoa taarifa inayozungumzia uchunguzi huo.

    "Shambulio hili la DHS ya Trump ni matumizi mabaya ya madaraka na ongezeko kubwa la silaha kwa vyombo vya kutekeleza sheria vya shirikisho kuwalenga maadui wa kisiasa.Kwa muongo mmoja, Donald Trump amekuwa akimlenga Mbunge Ilhan Omar bila kuchoka kwa maneno ya uchochezi, akimlenga mara kwa mara. Sasa, mashambulizi hayo yameongezeka hadi kuwa mashambulizi yasiyo na maana ya shirikisho. Ilhan hakufanya kosa lolote. Hakuna rais aliye na mamlaka ya kutumia nguvu ya serikali ya shirikisho kuwatisha maadui zake wa kisiasa," taarifa hiyo ilisema.

    Unaweza pia kusoma:

  8. Papa Leo XIV kulazwa Roma leo kwa ajili ya kuondolewa uvimbe mdogo kwenye mapafu

    Papa Leo

    Papa Leo XIV alitarajiwa kulazwa katika hospitali ya Roma Jumanne kwa ajili ya kuondolewa uvimbe kwenye mapafu katika upasuaji ambao wataalam wanasema utaamua kama uvimbe huo unaweza kutolewa na ikiwa matibabu mengine zaidi yanahitajika.

    Leo ametoa uwazi wa nadra kuhusu tatizo kubwa la kwanza la kiafya kumuhusu hadharani tangu alipochaguliwa kuwa Papa miezi 17 iliyopita.

    Alifichua kuhusu ugunduzi wa uvimbe huo mdogo wakati wa sala yake ya Jumapili adhuhuri na kutangaza kwamba anataka uondolewe.

    Mamlaka ya Vatican ilisema Papa Leo XIV angelazwa katika hospitali ya Gemelli Jumanne asubuhi, lakini hakukuwa na taarifa kuhusu muda wa upasuaji wenyewe.

    Upasuaji huo, ambao kwa kawaida hufanywa mtu akiwa amepigwa ganzi ya jumla (mwili mzima), utahitaji kukaa hospitalini kwa wiki moja na Vatican siku ya Jumatatu ilifuta mikutano ya hadhila ya Papa hadi Oktoba 20.

    "Haya ni mambo ambayo yanaweza kutibiwa vizuri sana, ikiwa maneno aliyotumia yanaakisi hali ya kimatibabu," alisema Dkt. Lorenzo Spaggiari, mkurugenzi wa upasuaji wa kifua katika Taasisi ya Ulaya ya matibabu ya saratani (EIO), ambaye hahusiki na Matibabu ya Papa lakini anayeifahamu timu ya madaktari ya hospitali ya Gemelli.

    Teknolojia ya roboti inaweza kutumika katika uchunguzi wa uvimbe kabla ya upasuaji

    Spaggiari alisema anatarajia timu ya Gemelli ingefanya uchunguzi wa biopsy ili kubaini kama Leo ana saratani ya mapafu ikifuatiwa na kuondolewa kwa sehemu ya mapafu iliyo na uvimbe.

    Uchunguzi wote unaweza kufanywa kwa kutumia mbinu za roboti, na unaweza kufanywa mfululizo, huku mgonjwa amepigwa sindano ya ganzi, na timu tofauti za wataalamu, Spaggiari alisema.

    Unaweza pia kusoma:

  9. Nini kilichomo katika makubaliano ya dizeli kati ya Putin na Trump?

    Putin na Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump ameongeza juhudi zake za kupunguza bei ya dizeli ya Marekani kwa kuondoa vikwazo kwa mauzo ya nje ya dizeli ya Urusi na kutangaza kusitisha mapigano dhidi ya miundombinu ya nishati kati ya Urusi na Ukraine.

    Kupanda kwa bei ya dizeli nchini Marekani kunawaumiza madereva wa malori na wakulima wa Marekani, na ni wasiwasi kwa wapiga kura na vyama vya siasa kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Novemba 3 .

    Bei za Marekani zilishuka kwa 0.5% Jumatatu kufuatia matangazo ya Trump.

    Trump alisema Ijumaa kwamba Urusi itasambaza mara moja zaidi ya tani 300,000 za dizeli (mapipa milioni 2.25) kwenye masoko ya Marekani na kimataifa.

    Hii ni chini ya usambazaji wa siku moja kwa sekta ya uchukuzi ya Marekani pekee, kulingana na data ya mamlaka inayotoa taarifa kuhusu nishati nchini Marekani, ambayo inaonyesha matumizi ya kila siku ya takriban mapipa milioni 2.94 kwa siku.

    Trump alisema Urusi ingesambaza tani nyingine 500,000 mwezi Novemba na tani milioni 1 zaidi "mara moja baada ya hapo", ambayo ni chini ya mahitaji ya siku nne ya usafiri wa Marekani.

    Marekani imeondoa vikwazo kwa mauzo ya nje ya dizeli ya Urusi, lakini bado haijulikani ni meli gani za mafuta zinaweza kutumika kusafirisha mafuta hayo kutokana na vikwazo kwa wengi, na hali ya viwanda vya kusafisha mafuta vya Urusi ikoje kutokana na mashambulizi ya hivi karibuni ya Ukraine dhidi yake.

    Unaweza pia kusoma:

  10. Joseph Kabila atangazwa kuwa kiongozi wa vuguvugu jipya la upinzani la kisiasa na kijeshi DRC

    g

    Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila, ametajwa kuwa kiongozi wa vuguvugu jipya la kisiasa na kijeshi, kulingana na tamko lililosomwa Jumatatu katika mji wa Goma, mashariki mwa nchi hiyo.

    Kundi hilo, linalojulikana kama Front for the Refoundation of the Nation (FRN), linasema liliundwa na watu walioafikiana kuunganisha nguvu na rasilimali zao chini ya mfumo wa pamoja wa utendaji. Katika taarifa iliyosomwa na Claude Ibalanky, aliyekuwa mshauri mkuu na balozi maalum wa Rais Félix Tshisekedi ambaye sasa amejiunga na vuguvugu hilo, waanzilishi walisema lengo lao ni "kukomboa" nchi.

    Tamko hilo lilitaja Ibara ya 64 ya Katiba ya Kongo, inayosema kuwa raia wana wajibu wa kupinga mtu yeyote au kundi lolote linalochukua madaraka kwa nguvu au kutumia madaraka hayo kwa kukiuka katiba.

    FRN lilijielezea kama vuguvugu la kisiasa na kijeshi lenye lengo la kuratibu kile ilichokiita "vikosi vya upinzani" ili kukomesha kile lilichokitaja kuwa udhalimu na kuweka mfumo mpya wa kisiasa nchini. Taarifa hiyo ilisema vuguvugu hilo litafuatilia lengo hilo "kwa njia zote, yakiwemo matumizi ya nguvu".

    Waanzilishi wake pia walitangaza muundo wa uongozi wa mpito na kumteua kwa kauli moja Bw. Kabila, rais wa zamani, kuwa kiongozi wa FRN wakati wakisubiri kukamilika kwa uundaji wa taasisi za shirika hilo.

    Tangazo hilo linakuja siku tatu baada ya Bw. Kabila kutoa hotuba iliyorushwa kitaifa, ambapo alisema ataelezea katika siku na wiki zijazo jinsi wananchi wa Kongo wanavyopaswa kuchukua hatua ili "kuokoa" nchi yao. Aliwaambia watazamaji kuwa taifa hilo lina "historia" na kuishutumu serikali ya Rais Tshisekedi kwa kupuuza mapendekezo aliyotoa mwezi Mei 2025, ikiwemo hatua za kulenga kumaliza mgogoro mashariki mwa DRC.

    Katika hotuba hiyo, Bw. Kabila pia aliishutumu serikali kwa kudhoofisha utawala wa kikatiba, kusimamia vibaya uchumi na kushindwa kuboresha usalama. Aidha, alidai kuwepo kwa ukamataji holela wa wapinzani wa kisiasa na maafisa wa jeshi. Serikali haijatoa majibu ya hadharani kuhusu madai hayo.

    Tamko la Jumatatu ndilo ishara ya wazi zaidi hadi sasa ya kuhusika moja kwa moja kwa Bw. Kabila katika vuguvugu lenye silaha linalopinga serikali ya Kinshasa. Bw. Kabila aliongoza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuanzia mwaka 2001 hadi Januari 2019, wakati Bw. Tshisekedi alipoingia madarakani kufuatia uchaguzi uliogubikwa na utata. Katika miaka ya hivi karibuni, rais huyo wa zamani amekuwa haonekani sana hadharani, lakini amekuwa akionyesha upinzani mkali dhidi ya utawala wa mrithi wake.

    Mamlaka mjini Kinshasa hazijatoa tamko lolote kuhusu kuundwa kwa FRN.

    Unaweza pia kusoma:

  11. 'Nadhani Putin anataka makubaliano zaidi ya Zelensky' - Trump

    g

    Akitoa maoni yake kuhusu utekelezwaji wa mkataba wa "usitisha mapigano ya nishati" alioutangaza kati ya Urusi na ukraine, Rais wa Marekani Donald Trump alijibu: "Wao [Zelensky na Putin] walikubaliana. Unajua ni kwa nini? Kwa sababu niliwaambia, 'Mnakubali.' Ndiyo maana"

    Aliongeza pia kwamba kwa maoni yake, Vladimir Putin ana nia zaidi ya kufikia makubaliano kuliko Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

    "Nadhani Putin anataka makubaliano zaidi ya Zelensky. Nadhani Putin anataka makubaliano, na tunahitaji kumshawishi Zelensky kutaka makubaliano," Trump alisema.

    Alipoulizwa kama Urusi ilikiuka "mkataba wa kusitisha mapigano ya nishati" aliyokuwa ametangaza, Trump alijibu kwamba "kulikuwa na ukiukwaji wa sheria kwa pande zote mbili."

    "Putin na Zelensky wanataka kufanya makubaliano, lakini hawajui jinsi gani. Lakini tutawalazimisha kufanya makubaliano," rais wa Marekani aliongeza.

    Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuondoka kwenda kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi wa kati kati ya muhula katika jimbo la Ohio.

    Unaweza pia kusoma:

  12. Mashirika ya ndege ya Qatar na Falme za Kiarabu yasimamisha safari za ndege kwenda Saudi Arabia

    h

    Shirika la Ndege la Etihad limesema limesimamisha safari zote za ndege kati ya Abu Dhabi na miji ya Saudi Arabia ya Riyadh, Jeddah na Dammam hadi wiki ijayo.

    Shirika la ndege la Qatar Airways pia limesimamisha kwa muda safari zake zote za ndege kwenda Saudi Arabia.

    Wahouthi wa Yemen wameonya nchi nyingine dhidi ya kusafiri kwa ndege kwenda Saudi Arabia.

    Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Riyadh umefungwa kufuatia mashambulizi ya Wahouthi katika siku za hivi karibuni, ambayo yamesababisha vifo vya watu kadhaa.

    Unaweza pia kusoma:

  13. Wahouthi waionya Marekani kuhusu majibu 'machungu sana' iwapo itaingilia kati vita Yemen

    g

    Kulingana na shirika la habari la AFP, Saudi Arabia imeiomba Washington msaada kwa ajili ya kukabiliana na Wahouthi.

    Mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Houthi Mohammed al-Bakhiti, aliliambia shirika hilo: "Ikiwa Marekani itajiunga na uvamizi dhidi ya Yemen, hatutasita kuamua kuhusu majibu yetu. Tutatoa majibu ya haraka na yenye uchungu, ambayo yatailenga Marekani na maslahi yake yote katika eneo hilo."

    Pia aliwaonya wafanyakazi wa vituo vya mafuta na viwanja vya ndege vya Saudi Arabia kukaa mbali na maeneo hayo, akisema yamekuwa malengo halali ya mashambulizi.

    Jumatatu usiku, mlipuko mwingine uliripotiwa huko Riyadh, lakini Saudi Arabia ilisema ulizuiliwa na kombora lililofyatuliwa na Wahouthi.

    Kufuatia shambulio la Wahouthi kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Riyadh siku ya Jumamosi, ambalo liliwaua watu 13, Rais wa Marekani Donald Trump alisema anafikiria kama Marekani itajiunga na mashambulizi ya Saudi Arabia dhidi ya Wahouthi.

    Hatua hiyo inakuja licha ya ripoti kwamba Trump hapo awali alikataa maombi ya usaidizi kutoka kwa Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman.

    Unaweza pia kusoma:

  14. Maeneo sita ya nishati ya Ukraine yameshambuliwa na Urusi tangu Trump atangaze kusitisha mapigano- Zelensky

    g

    Urusi imeshambulia vituo sita vya nishati vya Ukraine saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutangaza kwamba nchi hizo mbili zimekubaliana kusitisha mapigano ya nishati, Volodymyr Zelensky amesema.

    Licha ya Trump kusema Jumapili kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano yataanza "kutekelezwa mara moja", rais wa Ukraine alisema Urusi imeshambulia "vituo vyetu vya mafuta, miundombinu ya nishati, na vifaa vingine".

    Kulikuwa na kukatika kwa umeme katika jiji la Izyum baada ya mashambulizi ya Urusi kuharibu mitambo ya umeme, shirika la habari la serikali la Ukraine Ukrinform lilisema, huku miundombinu ya nishati na reli magharibi mwa Ukraine pia vikilengwa na mashambulizi usiku kucha.

    Unaweza pia kusoma:

  15. Hujambo na karibu kwa matangazo haya ya mubashara ya leo tarehe 13.10.2026