Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump asema Marekani imeondoa mabomu ya baharini katika Mlango wa Hormuz

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Jeshi la Wanamaji la Marekani ndilo linalodhibiti kwa sasa Mlango wa Hormuz.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Iran ilipe fidia kwa madhara iliyosababisha wakati wa vita - Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema Iran inapaswa kulipa fidia kwa watu walioathiriwa na vifo na majeraha yaliyosababishwa na matukio mbalimbali katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

    Trump amesema kauli hiyo inajibu madai ya Iran ya kutaka kulipwa fidia kwa uharibifu unaodaiwa kusababishwa na Marekani.

    “Waliomba fidia, unaweza kusema, au waliomba fedha kwa ajili ya uharibifu ambao tumesababisha. Nikasema hilo ni wazo zuri. Basi nasi tutaomba fedha kwa ajili ya uharibifu ambao wao wamesababisha kwa kipindi cha miaka 50,” Trump amesema.

    Ametaja pia shambulio la meli ya kijeshi ya Marekani USS Cole na watu waliouawa au kujeruhiwa katika matukio mbalimbali.

    Trump pia amesema familia za watu waliouawa katika maandamano nchini Iran zinapaswa kulipwa fidia.

    “Tunafikiri familia zao zinapaswa kupata fidia kwa kuuawa kwa mtu wao, mtoto wao, mama au baba yao waliokuwa wakiandamana,” Trump amesema.

    Amedai kuwa watu 52,000 waliuawa katika maandamano nchini Iran katika kipindi cha miezi minne iliyopita, ingawa kauli hiyo BBC haijathibitisha kwa uhuru.

    Trump amesema iwapo fidia italipwa, Iran ndiyo inapaswa kubeba gharama hiyo.

    Soma Zaidi Hapa:

  2. Safari ya ndege Canada yasitishwa baada ya mtoto kukataa kuketi

    Ndege kutoka Canada imeghairiwa baada ya mtoto kukataa kufunga mkanda wa usalama, hali iliyozua mjadala kuhusu usalama na taratibu za watoto wanaosafiri kwa ndege.

    Ndege ya kampuni ya Porter Airlines iliyokuwa ikijiandaa kuondoka Victoria kuelekea Toronto tarehe 6 Agosti, ilirudishwa eneo la kupandia abiria baada ya mtoto mdogo kusimama kwenye kiti chake na kukataa kufunga mkanda, kwa mujibu wa kampuni hiyo.

    Kutokana na tukio hilo, ndege hiyo haikuweza kuondoka uwanjani. Abiria walilazimika kupangiwa safari nyingine siku iliyofuata.

    Tukio hilo limeibua mitazamo tofauti kuhusu namna watoto wanavyopaswa kushughulikiwa katika mazingira kama hayo na hatua ambazo mashirika ya ndege yanapaswa kuchukua.

    Porter Airlines imesema juhudi za mzazi aliyekuwa akiandamana na mtoto huyo pamoja na wahudumu wa ndege kutatua suala hilo hazikufanikiwa.

    Kampuni hiyo imesema ndege haingeweza kuondoka katika hali hiyo kwa kuwa haikuwa salama. Kwa hiyo, wafanyakazi wa ndege waliamua kuirejesha katika eneo la kuanzia safari na kuwashusha abiria hao wawili.

  3. Trump asema itakuwa 'kosa kubwa' Infantino akiondolewa

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema itakuwa kosa kubwa sana kumuondoa Gianni Infantino katika nafasi yake ya urais wa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA.

    Kauli ya Trump imekuja baada ya UEFA, Concacaf na Shirikisho la Soka la Asia, AFC, kumshutumu Infantino kwa kuvunja uaminifu kupitia pendekezo lake lililofutwa la uekezaji linalojulikana kama Fifa Forward Enterprise, FFE.

    Pendekezo hilo lililenga kuunda kampuni mpya ya kusimamia haki za kibiashara na mauzo ya tiketi za mashindano yote ya FIFA, yakiwemo Kombe la Dunia, huku asilimia 21 ya kampuni hiyo ikiuzwa kwa kampuni binafsi ya uwekezaji.

    Trump amesema FIFA itakuwa inafanya kosa kubwa ikiwa itafikiria kumwondoa Infantino.

    “FIFA itakuwa inafanya kosa baya sana ikiwa, kwa sababu yoyote ile, itafikiria hata kumwondoa Rais Gianni Infantino,” Trump aliandika kwenye mitandao ya kijamii.

    “Yeye ni mzuri sana, kwani hivi karibuni ameongoza Kombe la Dunia lenye mafanikio makubwa zaidi kuwahi kufanyika, mara nne zaidi. Ikiwa ataondoka, halitawahi kuwa na mafanikio au faida kubwa kama hiyo tena.”

    Kombe la Dunia la mwaka 2026 liliandaliwa kwa pamoja na Marekani, Canada na Mexico msimu huu wa kiangazi, huku Hispania ikitwaa ubingwa baada ya kuifunga Argentina katika fainali.

    Alipozungumzia kwa mara ya kwanza pendekezo la FFE tarehe 31 Julai, Trump alisema hajawahi kuzungumza na Infantino kuhusu mipango hiyo.

    Thrive Eternal ilitarajiwa kuongoza kundi la wawekezaji lililopendekezwa kwa ajili ya FFE.

    Thrive ni kampuni ya Marekani ya uwekezaji wa mitaji iliyoanzishwa na Joshua Kushner, ambaye ni kaka wa Jared, mkwe wa Trump.

    Trump na Infantino wana uhusiano wa karibu.

    Infantino alimtuza Trump Tuzo ya kwanza ya Amani ya FIFA mwezi Desemba 2025.

  4. Tetemeko la ardhi Colombia lasababisha vifo vya zaidi ya watu 130

    Takriban watu 132 wamefariki baada ya tetemeko kubwa la ardhi kupiga magharibi mwa Colombia, katika tukio kubwa zaidi la aina hiyo nchini humo kwa miaka kadhaa.

    Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 7.4 kwa kipimo cha Richter lilipiga jimbo la Chocó, kati ya miji ya Medellín na Cali.

    Waokoaji wanaendelea kuwasaka manusura huku kukiwa na hofu kwamba baadhi ya watu wamenaswa chini ya majengo yaliyoporomoka. Idadi ya waliofariki inatarajiwa kuongezeka.

    Katika mji mkuu Bogotá, miti na taa za barabarani ziliyumba kwa nguvu, ingawa hakukuwa na uharibifu mkubwa ulioripotiwa.

    Tetemeko hilo pia lilihisiwa katika maeneo ya mbali, yakiwemo Venezuela, Ecuador na Panama.

    Rais wa Colombia Abelardo de la Espriella, aliyeapishwa Ijumaa, ametangaza hali ya dharura.

    Eneo la Risaralda, linalojulikana kwa uzalishaji wa kahawa, linaonekana kuathirika zaidi, huku mji wake mkuu Pereira ukiripotiwa kupata uharibifu mkubwa na nyumba kadhaa kubomoka.

    Soma Zaidi:

  5. Kenya yatuma ombi la kuandaa Mashindano ya Dunia ya Riadha 2029

    Jiji kuu la Kenya, Nairobi, imewasilisha rasmi ombi la kuandaa Mashindano ya Dunia ya Riadha mwaka 2029, ikiwa na lengo la kuwa mji wa kwanza barani Afrika kuandaa mashindano hayo makubwa ya riadha.

    Mji mkuu wa Kenya unashindana na London, Rome na Munich kuwania haki ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.

    Serikali ya Kenya imetoa dhamana ya kuunga mkono zabuni hiyo kikamilifu, ikiwemo kuboresha miundombinu, usalama na maandalizi ya kiutawala yanayohitajika kuandaa mashindano hayo.

    Kenya tayari ina uzoefu wa kuandaa mashindano makubwa ya riadha.

    Mombasa iliandaa Mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika mwaka 2007, huku Nairobi ikiwa mwenyeji wa Mashindano ya Dunia ya Riadha kwa Wanariadha walio chini ya miaka 18 mwaka 2017 na yale ya chini ya miaka 20 mwaka 2021.

    Nairobi pia iliandaa Mashindano ya Riadha ya Afrika mwaka 2010.

    Shirikisho la Dunia la Riadha, World Athletics, linatarajiwa kutangaza mji utakaokuwa mwenyeji wa mashindano ya mwaka 2029 mwezi Septemba.

  6. Zambia yaelekea uchaguzi huku Hichilema akilenga muhula wa pili

    Zambia itaelekea kwenye uchaguzi baada ya siku mbili, ambapo wananchi watapiga kura kumchagua Rais, wabunge na viongozi wa mabaraza ya serikali za mitaa.

    Uchaguzi huo umetajwa kwa kiasi kikubwa kuwa ni ushindani wa wagombea wawili wakuu, kufuatia kuibuka kwa mgombea mmoja wa muungano wa upinzani.

    Kwa mujibu wa Reuters, kura za maoni pamoja na wawekezaji wengi wanatarajia Rais Hakainde Hichilema kushinda muhula mwingine wa miaka mitano, akimshinda mpinzani wake Brian Mundubile, anayeongoza upinzani uliogawanyika.

    Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi ya Zambia inakabiliwa na moja ya mitihani yake mikubwa zaidi, huku ikisimamia uchaguzi wa kwanza unaotumia daftari jipya la wapiga kura na unaofanyika katika majimbo mapya ya uchaguzi. Masuala ya usalama wa kura, mvutano wa kisiasa na wasiwasi wa umma kuhusu uaminifu wa mchakato wa uchaguzi pia yameibua changamoto kwa tume hiyo.

    Uchaguzi huo wa Agosti 13 umejikita katika ushindani kati ya miungano miwili mikuu ya kisiasa.

    Muungano unaoongozwa na chama tawala cha United Party for National Development, UPND, unaungwa mkono na vyama vidogo 15.

    Upande wa pili ni Tonse Pamodzi Alliance, unaoongozwa na mgombea urais Brian Mundubile na mgombea mwenza Makebi Zulu.

    Muungano huo unajumuisha vyama vidogo visivyo na uwakilishi bungeni pamoja na sehemu kubwa ya miundo iliyosalia ya chama cha Patriotic Front, PF.

    Mundubile aliwahi kuwa mwanachama wa PF, chama kilichoondolewa madarakani katika uchaguzi wa mwaka 2021.

    Kwa mujibu wa sheria za Zambia, miungano ya kisiasa haiwezi kusajiliwa kama vyombo vya uchaguzi. Hivyo, wagombea wa miungano hiyo hulazimika kugombea kupitia chama kimoja, huku wakiungwa mkono na muungano usio rasmi.

    Kuundwa kwa miungano ya upinzani si jambo jipya nchini Zambia. Takriban kila uchaguzi umekuwa ukishuhudia mazungumzo ya kuunganisha vyama vya upinzani, ingawa ni miungano michache iliyofanikiwa kudumu hadi wakati wa uchaguzi.

    Mwaka huu, vyama vya upinzani viliungana katika hatua za mwisho za maandalizi ya uchaguzi, vikidai kukabiliwa na kile vinachokiita kuingiliwa kwa kiasi kikubwa na serikali.

    Licha ya changamoto hizo, upinzani unasema una matumaini ya kushinda uchaguzi.

    Jumla ya wagombea 14 wanawania urais, ingawa ni vyama vichache vinavyotambulika kwa kiasi kikubwa na wapiga kura.

    Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30, hakuna chama chochote kilichowahi kuwa madarakani kinachowakilishwa kwenye karatasi ya kura ya urais. Soma Zaidi:

  7. Trump asema atamjibu Netanyahu kuhusu mpango wa amani wa Gaza

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema hivi karibuni atajibu kauli ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ya kuukataa mpango wa amani wenye vipengele 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

    Trump, akijibu maswali ya waandishi wa habari ndani ya Ikulu ya Marekani, amesema atachapisha majibu yake kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social.

    “Nitachapisha jibu langu huko. Nina jibu, ni jibu zuri, nitalichapisha huko,” Trump amesema.

    Amesema pia uhusiano wake na Netanyahu bado ni “mzuri sana.”

    Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na kusitishwa kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, angalau kwa kiwango fulani, jambo ambalo Hamas ililitaka wakati ilipokubali mpango wa vipengele 15 unaoungwa mkono na Marekani.

    Pia kuna dalili nyingine kwamba Israel iko tayari kuendeleza mpango wa amani wa Rais wa Marekani Donald Trump kwa Gaza, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya kupelekwa kwa Kikosi cha Kimataifa cha Kuleta Utulivu (ISF). Kikosi hicho kinaundwa na wanajeshi kutoka nchi mbalimbali, na mpango ni kwamba watashirikiana na kikosi kipya cha polisi wa Palestina katika kuhakikisha usalama wa eneo hilo.

    Ujenzi wa kituo cha kwanza cha ISF bado unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu, miongoni mwa magofu ya Rafah, kusini mwa Gaza, kwa mujibu wa redio ya umma ya Israel, Kan News. Hatua hiyo itawezesha hatimaye kuanza kwa ujenzi upya wa eneo hilo.

    Soma Zaidi Hapa:

  8. Wahouthi washambulia mji wa Mukha nchini Yemen

    Vikosi vinavyoiunga mkono serikali ya Yemen vimesema wapiganaji wa Houthi wameushambulia mji wa bandari wa Mukha.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa jeshi la Yemen kwenye mtandao wa X, jeshi hilo limesema Wahouthi walifyatua makombora ya balistiki kuelekea mji huo uliopo katika pwani ya Bahari ya Shamu.

    Jeshi hilo pia limesema maeneo na vituo kadhaa katika bandari ya Mukha vililengwa katika mashambulizi hayo.

    Pia Unaweza kusoma:

  9. Trump asema Marekani imeondoa mabomu ya baharini katika Mlango wa Hormuz

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema vikosi vya Marekani vimeondoa mabomu ya baharini katika Mlango wa Hormuz na kuifanya njia hiyo kuwa salama kwa usafiri wa meli.

    Trump amesema Jeshi la Wanamaji la Marekani ndilo linalodhibiti kwa sasa Mlango wa Hormuz.

    “Angalia, kwa sasa ni Jeshi la Wanamaji la Marekani pekee ndilo linalodhibiti Mlango wa Hormuz,” aliwaambia waandishi wa habari katika Ofisi ya Oval ya Ikulu ya Marekani.

    Aidha Trump amesema Marekani imeweka kizuizi imara katika njia hiyo na inaruhusu kupita meli ambazo inataka.

    “Tumeweka kizuizi kinachofanya kazi kikamilifu na kisichoweza kupenywa, kama ukuta wa chuma.”

    Trump pia amesema baadhi ya mabomu ya baharini huwekwa katika njia hiyo, lakini vikosi vya Marekani huyagundua na kuyaondoa.

    “Ni jambo gumu kidogo, bila shaka, kwa sababu wakati mwingine wanaweka mabomu ya baharini, lakini sisi tunayagundua. Unajua, tumeondoa mabomu mangapi katika njia hii yote ya majini,” Trump alisema.

    Soma Zaidi Hapa:

  10. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 11/08/2026.