Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump atishia kushambulia miundombinu ya Iran isiporejea katika mazungumzo

Tehran yasema mashambulizi mapya ya Marekani yamefuta msingi wa maelewano kati ya pande hizo mbili.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Ripoti yasema Kenya iko katika hatari kubwa ya kushuhudia vurugu za uchaguzi wa 2027

    Kenya inakabiliwa na uwezekano wa asilimia 84.1 wa kutokea kwa aina fulani ya vurugu zinazohusiana na uchaguzi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Taasisi ya Kofi Annan.

    Ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia hiyo ni tathmini ya kiwango cha hatari na si uhakika kwamba vurugu zitatokea. Hivyo, inatoa wito kwa serikali, viongozi wa kisiasa, asasi za kiraia na wananchi kuchukua hatua mapema ili kuimarisha juhudi za kudumisha amani na kuzuia vurugu kabla hazijatokea.

    "Takwimu hizi ni tathmini ya hatari, si uhakika wa kitakachotokea. Zinapaswa kuwa mwito wa kuchukua hatua mapema ili kuimarisha juhudi za amani na kuzuia vurugu kabla hazijatokea," imeongeza ripoti hiyo.

    Kwa mujibu wa Taasisi ya Kofi Annan, uchaguzi unaweza kuwa fursa ya kuimarisha demokrasia, lakini pia unaweza kuongeza mvutano iwapo kutakuwa na mgawanyiko wa kisiasa, taasisi dhaifu au kupungua kwa imani ya wananchi katika mchakato wa uchaguzi.

    Ripoti hiyo imeeleza kuwa Kielezo cha Hatari ya Uchaguzi kinatumia viashiria vya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutawala kutathmini mazingira ya uchaguzi na kutoa tahadhari ya mapema kwa watunga sera, wasimamizi wa uchaguzi na wadau wengine.

    Kenya ni miongoni mwa nchi 10 zilizofanyiwa uchambuzi wa kina katika ripoti hiyo, ambao unachanganya tathmini ya takwimu na uchambuzi wa mazingira ya kisiasa, changamoto za uchaguzi na hatua zinazoweza kuchukuliwa kupunguza hatari ya vurugu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

  2. Majaribio ya dawa ya kuzuia Ebola yaanza DR Congo na Uganda

    Shirika la Afya Duniani, WHO, limetangaza kuanza kwa majaribio ya kwanza ya kitabibu ya dawa ya kuzuia Ebola kwa watu waliokaribiana na walioambukizwa virusi hivyo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda.

    Majaribio hayo, yanayojulikana kama EBO PEP, yanalenga kutathmini uwezo wa dawa ya obeldesivir kuzuia maambukizi ya aina ya Bundibugyo Ebola kwa watu waliowahi kukutana na wagonjwa waliothibitishwa kuwa na virusi hivyo.

    Dawa hiyo ya majaribio, inayotengenezwa na kampuni ya Marekani ya Gilead Sciences na kutumiwa kwa njia ya kumeza, imeonyesha matokeo ya kutia matumaini katika tafiti za awali.

    Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kuanza kwa majaribio hayo ni hatua muhimu katika juhudi za kukabiliana na Ebola.

    "Kila mafanikio huanza na matumaini. Ikiwa dawa hii itathibitika kuwa na ufanisi kwa watu walio katika hatari kubwa baada ya kuathiriwa, inaweza kuwa hatua kubwa mbele katika kuzuia maambukizi ya Ebola," alisema Tedros.

    WHO imesema iwapo dawa hiyo itafanikiwa, inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuwalinda wahudumu wa afya, wanafamilia na jamii wakati wa milipuko ya Ebola.

  3. Rwanda yasaini mkataba wa udhamini na Aston Villa kupitia kampeni ya Visit Rwanda

    Klabu ya Aston Villa imetangaza kampeni ya utalii ya Visit Rwanda kuwa mdhamini mkuu wa jezi za nyumbani kwa msimu wa 2026 hadi 2027 wa Ligi Kuu ya England.

    Chini ya makubaliano hayo, nembo ya Visit Rwanda itaonekana mbele ya jezi za timu za wanaume, wanawake na vijana.

    Aidha, kampeni hiyo itakuwa mshirika wa utalii wa klabu hiyo pamoja na msambazaji wa kahawa.

    Mkurugenzi wa Biashara wa Aston Villa, Francesco Calvo, amesema ushirikiano huo unaashiria kuendelea kwa ukuaji wa klabu hiyo.

    “Huu ni ushirikiano mkubwa kwa Aston Villa. Kuna fursa nyingi za kushirikiana, kujifunza na kuleta ubunifu. Tunafurahia kufanya kazi na Visit Rwanda kuanzisha shughuli zenye manufaa kupitia utalii, uwekezaji na maendeleo ya michezo.”

    Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda, Jean Guy Afrika, amesema ushirikiano huo utaiwezesha Rwanda kujitangaza kwa mamilioni ya watu duniani.

    “Ushirikiano huu unatupa fursa kubwa ya kuisogeza Rwanda karibu na mamilioni ya watu duniani, kwa kuwaalika kutembelea, kuwekeza, kufanya biashara na kugundua fursa zilizopo nchini mwetu.”

    Mkataba huu unakuja baada ya ushirikiano wa Visit Rwanda na Arsenal kumalizika mwishoni mwa msimu uliopita.

    Makubaliano hayo yalikuwa yamekumbwa na ukosoaji kutoka kwa baadhi ya mashabiki wa Arsenal kutokana na madai ya kuhusika kwa Rwanda katika mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, madai ambayo Rwanda imekuwa ikiyakanusha.

    Aston Villa ilimaliza msimu uliopita wa Ligi Kuu ya England katika nafasi ya nne.

  4. Trump: Iran isiporejea kufanya mazungumzo, tutashambulia mitambo ya umeme na madaraja

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema jeshi lake litalenga mitambo ya kuzalisha umeme na madaraja nchini Iran wiki ijayo ikiwa Tehran haitarejea kwenye meza ya mazungumzo.

    Akizungumza katika mahojiano na kituo cha Fox News, Trump amesema hatua hiyo itachukuliwa iwapo Iran haitakubali kuendelea na mazungumzo.

    "Ikiwa Iran haitarejea kwenye meza ya mazungumzo, tutalenga mitambo yao ya umeme na madaraja wiki ijayo," alisema Trump.

    Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuanzisha operesheni ya vikosi vya ardhini, Trump hakutoa jibu la moja kwa moja.

    "Sitazungumzia hilo kwa undani. Wakati mwingine operesheni ya ardhini inahitajika, lakini kuna watu wengine watakaoitekeleza kwa niaba yetu," alisema.

    Kauli hiyo imekuja wakati mvutano kati ya Marekani na Iran ukiendelea kuongezeka, huku pande zote zikiendeleza mashambulizi na vitisho vya kijeshi.

    Soma Zaidi Hapa:

  5. Hispania yafuzu fainali baada ya kuichapa Ufaransa

    Beki wa Hispania na mchezaji bora wa mechi, Pedro Porro, amesema kufuzu kwa timu yake ni ndoto aliyokuwa akiisubiri kwa muda mrefu.

    "Hii ni ndoto iliyotimia kwangu. Ilikuwa ndoto yangu kubwa zaidi. Nina furaha sana kwa timu. Tulicheza vizuri kuanzia mwanzo hadi mwisho na leo tulifanya kila tulichoweza ili kufuzu," alisema Porro.

    Akizungumzia ushindi dhidi ya Ufaransa, Porro alisema walijua wangekutana na mpinzani mgumu lakini walitekeleza mpango wao ipasavyo.

    "Tulijua tunakutana na timu ngumu sana. Huu ni ushindi wa timu nzima, si wangu pekee. Nawapongeza wachezaji wote kwa kiwango walichoonyesha."

    Kuhusu jinsi walivyowadhibiti Wafaransa, Porro alisema umiliki wa mpira ulikuwa sehemu muhimu ya mkakati wao.

    "Tulijua kumiliki mpira kungetusogeza karibu na ushindi. Mashambulizi yao ya kushtukiza ndiyo silaha yao kubwa, na kuyazuia ilikuwa jambo muhimu."

    Porro pia alisema alitolewa uwanjani baada ya kuhisi hangeweza kuendelea kuchangia zaidi, akisisitiza kuwa ushindi huo ulitokana na mchango wa kikosi kizima.

    "Nilihisi siwezi kuchangia zaidi. Ushindi huu umeletwa na wachezaji wote 26. Sasa tunaelekeza nguvu zetu kwenye fainali."

    Alimalizia kwa kusema kuwa licha ya uchovu, Hispania itajipanga upya na kupambana kwa nguvu zote katika mchezo wa fainali.

    Soma Zaidi:

  6. Maseneta wa Democratic wazuia muswada wa ulinzi wa Marekani kupinga vita na Iran

    Maseneta wa Chama cha Democratic nchini Marekani wamekwamisha kupitishwa kwa Muswada wa Mwaka wa Sera ya Ulinzi, wakionyesha kupinga kuendelea kwa vita dhidi ya Iran.

    Muswada huo, unaojulikana kama National Defense Authorization Act (NDAA), umeshindwa kusonga mbele baada ya kuungwa mkono na maseneta 50 huku 46 wakipinga.

    Ingawa bado unahitaji hatua nyingine kabla ya kuwa sheria, matokeo hayo yanaonyesha mgawanyiko mkubwa katika Seneti kuhusu sera ya Marekani dhidi ya Iran na athari zake kwa bajeti ya Wizara ya Ulinzi.

    Seneta Richard Blumenthal, mwanachama wa chama cha Democratic na kiongozi wa upinzani katika Kamati ya Seneti ya Huduma za Kijeshi, alisema muswada huo kwa sasa unaendeleza ufadhili wa vita dhidi ya Iran.

    "Kwa mtazamo wangu, sheria hii inaendeleza ufadhili wa vita, huku utawala wa sasa ukikosa uwajibikaji," alisema.

    Blumenthal alisema hataunga mkono muswada huo hadi utawala wa Rais Donald Trump utoe mkakati wazi kuhusu Iran na upate idhini ya Bunge kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Vita.

    Naye Seneta Tammy Duckworth alisema asingepigia kura muswada huo kusonga mbele isipokuwa marekebisho aliyopendekeza yapitishwe, yakilenga kuzuia fedha zaidi kutumika kufadhili operesheni za kijeshi za kushambulia Iran.

    Soma Zaidi Hapa:

  7. Trump afuta pendekezo la tozo ya asilimia 20 kwa meli zinazopita Hormuz

    Rais wa Marekani Donald Trump ameondoa pendekezo lake la kutoza ada ya asilimia 20 kwa mizigo yote inayopitia Mlango wa Bahari wa Hormuz, akisema badala yake atategemea mikataba mikubwa ya biashara na uwekezaji kutoka mataifa ya Ghuba.

    Hatua hiyo imekuja saa chache kabla ya Jeshi la Marekani kupitia Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) kurejesha kizuizi dhidi ya bandari za Iran na kuanzisha duru mpya ya mashambulizi dhidi ya malengo ya Iran.

    CENTCOM ilisema mashambulizi hayo yanalenga kudhoofisha uwezo wa Iran wa kushambulia meli za kibiashara zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.

    Mashambulizi hayo yanafuatia mapigano mapya kati ya Marekani na Iran, ambayo yamesababisha bei ya mafuta kupanda huku shughuli za usafirishaji wa mafuta kupitia Hormuz zikipungua kwa kiasi kikubwa.

    Iran ilisema imelenga vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Bahrain na Jordan, baada ya awali kushambulia meli mbili za Umoja wa Falme za Kiarabu.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema:

    "Nimeamua kuondoa tozo ya asilimia 20 ya Marekani na badala yake mataifa ya Ghuba yatawekeza na kufanya mikataba mikubwa ya biashara nchini Marekani."

    Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi kuhusu mpango huo.

    Trump pia alisema Mlango wa Bahari wa Hormuz utaendelea kuwa wazi kwa meli zote isipokuwa zile zinazofanya biashara na Iran.

    Baadaye, akizungumza mjini Washington, Trump alisema hakupendelea wazo la kutoza ada kwa meli zinazopita Hormuz, lakini akaongeza kuwa si haki kwa Marekani kubeba jukumu la kulinda njia hiyo muhimu ya baharini kwa manufaa ya dunia nzima.

    Kwa upande wake, Iran imesema itaendelea kusimamia Mlango wa Bahari wa Hormuz licha ya hatua za Marekani.

    Unaweza kusoma;

  8. Iran yasema makubaliano ya kusitisha mapigano na Marekani yamevunjika

    Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa masuala ya kisheria Iran Kazem Gharibabadi amesema hakuna tena kinachoitwa Makubaliano ya Islamabad kati ya Tehran na Washington, akidai kuwa mashambulizi mapya ya Marekani yameharibu kabisa msingi wa maelewano yaliyokuwapo.

    Kauli hiyo imekuja baada ya Marekani kuanzisha mashambulizi mapya katika pwani ya kusini mwa Iran na Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) kutangaza kurejesha kizuizi cha majini dhidi ya bandari za Iran.

    "Hakuna tena kinachoitwa Makubaliano ya Islamabad. Msingi wa maelewano kati ya Iran na Marekani umeharibiwa kabisa," alisema Naibu Waziri huyo.

    Mapema Jumatano, milipuko kadhaa iliripotiwa katika maeneo ya kusini mwa Iran kufuatia mashambulizi ya Marekani.

    Kwa kujibu mashambulizi hayo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na jeshi la Iran yalisema yamelenga vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Kuwait, Bahrain na Jordan kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani.

    Mvutano kati ya Iran na Marekani umeendelea kuongezeka huku pande zote zikiendeleza mashambulizi na hatua za kijeshi katika eneo la Ghuba.

    Soma Zaidi:

  9. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.