Shambulio la droni nchini Sudan lalenga msafara wa mazishi na kuua watu kadhaa

Chanzo cha picha, Los Angeles Times via Getty Images
Shambulio la ndege isiyo na rubani lililolenga msafara wa mazishi katika makaburi ya mji wa El-Obeid nchini Sudan limeua takribani watu wanne na kuwajeruhi wengine kadhaa, kwa mujibu wa makundi mawili ya kutetea haki za binadamu na huduma za afya, Sudan Doctors Network na Emergency Lawyers.
Makundi yote mawili yamelilaumu kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces (RSF) kwa kuhusika na shambulio hilo. Kundi la Emergency Lawyers limesema kuwa shambulio hilo ni sehemu ya mfululizo wa mashambulizi ya droni yaliyoanza Jumatano jioni, ambapo kwa jumla watu wasiopungua 23 wameuawa.
RSF haijatoa tamko lolote kuhusu madai hayo.
Mji wa El-Obeid, ambao kwa sasa unadhibitiwa na jeshi la Sudan, ni moja ya maeneo muhimu ya mapigano katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan vilivyoanza miaka mitatu iliyopita baada ya viongozi wa jeshi na RSF kutofautiana kuhusu mustakabali wa nchi hiyo.
Mapigano hayo yamesababisha kile kinachotajwa kuwa janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani kwa sasa, ambapo zaidi ya watu milioni 11 wamelazimika kuyahama makazi yao na watu milioni 28 wanakabiliwa na njaa kali.
Hakuna takwimu rasmi na za kuaminika kuhusu idadi kamili ya waliopoteza maisha tangu vita hivyo vianze, lakini inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 50,000 wamefariki dunia.
Unaweza kusoma;















