Je, Elon Musk kuwa trilionea wa kwanza duniani?

Chanzo cha picha, Manuel Mazzanti / NurPhoto / Getty Images
Kampuni ya Elon Musk, Space X, imetangaza bei ya hisa ya kampuni hiyo kabla ya kufungua hisa hizo kwa umma.
Ikiwa wataweza kufikia bei lengwa, kampuni hiyo itakuwa ya kwanza kuuza hisa kubwa kwa umma kuwahi kutokea katika historia.
Kulingana na taarifa ya kampuni hiyo iliyotolewa tarehe 3 mwezi Juni, hisa za space x zitauzwa dola 135, na itailetea kampuni hiyo kipato cha dola trillioni 1.75.
Si kawaida kutangaza kipato cha kampuni kabla ya hisa kuuzwa.
Taarifa ya kampuni hiyo si hakikisho kuwa hisa hizo zitauzwa kwa makadirio hayo, bali inategemea na uamuzi wa wanunuzi. Bei hiyo inaweza kupanda au kushuka.
Akivunja rekodi hiyo, Je Musk atakuwa Trillionea?
Space X ambayo hujenga roketi na vifaa vingine vya angani na pia inamiliki XAi na Starlink, imechukua hatua isiyo ya kawaida ya kutangaza bei ya hisa kwa umma kabla ya kuanza kuuza kwa umma wiki moja baadaye.
Kwa kawaida kampuni nyingi hutangaza bei yao siku moja kabla ya kuanza kuuza hisa.
Hisa za Space X zinatarajiwa kuanza kuuzwa katika soko la hisa la NewYork la Nasdaq kuanzia tarehe 12 mwezi Juni, na kuifanya kuwa kampuni ya kwanza kwenye historia kutoa makadirio ya bei ya hisa kabla ya kuanza kuuza.
Kampuni hiyo inalenga kupata mtaji wa dola billioni 75 kupitia uuzaji wake wa kwanza wa hisa kwa umma, hii ikiwa rekodi mpya ya juu.
Rekodi ya awali inashikiliwa na kampuni ya mafuta ya Saudi Aramco ambayo ilipata mtaji wa dola billioni 25.6 mwaka wa 2019.

Chanzo cha picha, Reuters
Iwapo hisa za kamuni hiyo zitauzwa zaidi ya dola 135, space X itakuwa mojawapo ya makampuni tajiri duniani. Hilo likitokea na Musk ambaye anamiliki 80% ya Space X anaweza kuwa trilionea.
Mapato ya dola bilioni 18.6, hasara ya dola bilioni 4.9
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mujibu wa takwimu za kampuni ya utafiti wa masoko ya Dealogic, karibu nusu ya kampuni zote zilizotoa hisa zao kwa umma,katika kipindi cha miaka 30 iliyopita zimepoteza thamani tangu zilipoanza kuuza kwenye soko la hisa.
Samuel Kerr, mtendaji wa kampuni ya Mergermarket alisema kuhusu SpaceX kuwa "Bila shaka thamani yake imepandishwa kwa kiwango cha juu sana."
Thamani ambayo SpaceX imejiwekea ikilinganishwa na mauzo yake ni kubwa zaidi kuliko ile ya kampuni nyingine yoyote katika kundi la kampuni kubwa za teknolojia linalojulikana kama "Mag 7", linalojumuisha, Amazon, Apple, Meta, Nvidia, Microsoft na Tesla.
Kerr aliongeza kuwa, "Hata hivyo, SpaceX inathaminiwa kwa kuzingatia mapato na faida zinazotarajiwa siku zijazo badala ya hali yake ya sasa, hivyo baadhi ya wawekezaji wanaweza kupuuza hali hiyo."
Mwaka uliopita, kampuni ya Space Exploration Technologies (SpaceX) ilipata mapato ya dola bilioni 18.6 lakini ikarekodi hasara ya dola bilioni 4.9.
Katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu, kampuni hiyo ilifanya mauzo ya dola bilioni 4.7 lakini ikapata hasara ya dola bilioni 4.3.
Taarifa yake ya kifedha inaonyesha kuwa ina mali zenye thamani ya dola bilioni 102, zikiwemo roketi na vifaa vingine, lakini pia ina madeni yenye thamani ya dola bilioni 60.5.
Maabara ya Akili Mnemba
Mapema mwaka huu, kampuni ya SpaceX ilinunua xAI, kampuni nyingine inayomilikiwa na Elon Musk inayojulikana kwa chatbot yake ya Grok.
xAI, ambayo ilianzishwa kwa kutumia rasilimali za X zamani Twitter, ilitumia data kutoka kwenye jukwaa hilo kufundisha teknolojia yake ya akili mnemba.
Musk kwa muda mrefu amekuwa akiamini kuwa, kutokana na nafasi na rasilimali kuwa finyu duniani, njia bora ya kupata nguvu na miundombinu inayohitajika kuendesha akili mnemba ni kuendeleza miundombinu hiyo angani.
Kampuni hiyo imeweka mipango ya kuzindua satelaiti zaidi na hatimaye kujenga vituo vya kuhifadhi na kuchakata data katika obiti ya dunia.
Akizungumza na BBC, Laurence Pevsner, mshirika wa kampuni ya uwekezaji wa mtaji wa ubia ya Lux Capital, alisema:
"SpaceX zamani ilikuwa biashara rahisi, ilikuwa kampuni ya kurusha roketi na pia kutoa huduma za intaneti kupitia satelaiti. Lakini sasa ni kampuni ya mitandao ya kijamii na maabara ya akili mnemba."
Aliongezea kuwa "Nadhani kitengo cha akili mnemba ndicho kilichochangia zaidi kupanda kwa thamani ya kampuni hiyo"
Utoaji wa kwanza wa hisa za SpaceX kwa umma unakuja wakati ambapo makampuni mengine makubwa ya teknolojia yanatafuta fedha zaidi ili kufadhili matumizi yao makubwa katika maendeleo ya akili mnemba.












