Mcheza dansi Nigeria afukuzia rekodi ya dunia
Mcheza dansi kutoka Nigeria anajaribu kuweka rekodi mpya ya dunia kwa kucheza bila kusimama kwa siku saba mfululizo.
Benjamin Daniel, anayejulikana kama Ben Dancer, analenga kucheza kwa saa 168, ikiwa ni saa 41 zaidi ya rekodi ya sasa.
Shirika la Guinness World Records bado halijathibitisha iwapo jaribio hilo linakidhi vigezo vya kutambuliwa rasmi kama rekodi ya dunia. BBC imewasiliana na shirika hilo kwa maoni zaidi.
Katika siku za hivi karibuni, mamia ya vijana wamekuwa wakikusanyika katika uwanja wa Freedom Park jijini Lagos kumshangilia, huku wengine wakirekodi kila hatua yake na kushiriki kucheza dansi.
Mmoja wa mashuhuda, Uche Anumudu, amesema ni jambo la kufurahisha kuona jinsi Ben Dancer alivyojitahidi kufikia hatua hiyo na kwamba anajivunia mafanikio yake.
Rekodi ya sasa ya kucheza dansi kwa muda mrefu zaidi inashikiliwa na mchezaji wa India, Srushti Sudhir Jagtap, aliyefikia saa 127 mwaka 2023 akiwa na umri wa miaka 16.
Ben Dancer mwenye umri wa miaka 33 amekuwa akifanya dansi kitaaluma kwa miaka 18. Jaribio lake lilianza tarehe 22 Septemba na iwapo atakamilisha saa zote 168 zilizopangwa, anatarajiwa kufikia lengo hilo mapema Jumanne.