Watoto waliozaliwa wakati wa vita Sudan wanavyokosa utambulisho kisheria

    • Author, Ethar Shalaby
    • Nafasi, BBC News Arabic
    • Author, Patricia Whitehorne
    • Nafasi, BBC Africa
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Onyo: Habari hii ina maelezo ambayo baadhi ya wasomaji wanaweza kuyaona kuwa ya kusikitisha au ya kutatiza.

Msichana wa Sudan mwenye umri wa miaka 17 amembeba mtoto mchanga mikononi mwake kwa utulivu mkubwa usioendana na umri wake, huku akihofia mustakabali wa maisha ya mtoto huyo.

"Mwanangu huyu hana baba, hana cheti cha kuzaliwa wala namba ya utambulisho wa taifa," anaiambia BBC. Amira (si jina lake halisi, limebadilishwa kwa ajili ya kulinda utambulisho wake).

Akimtazama mtoto wake, Amira anazungumza kwa utaratibu, kana kwamba bado anajaribu kuelewa yote yaliyompata tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipozuka nchini Sudan.

Yeye na familia yake waliishi katika maeneo ya mashariki mwa mji wa el-Fasher, ambao ulikuwa umezingirwa na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF). RSF imekuwa ikipambana vikali na jeshi la Sudan tangu Aprili 2023.

El-Fasher ulikuwa ngome ya mwisho ya jeshi la Sudan katika eneo la magharibi la Darfur, hadi ulipoangukia mikononi mwa RSF na wanamgambo washirika mwezi Oktoba mwaka jana, baada ya kuzingirwa kwa miezi 18.

Kwa makumi ya maelfu ya raia waliokuwa wamenaswa ndani ya mji huo, hali ilikuwa ya kutisha kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara, mapigano makali na uhaba mkubwa wa chakula.

Hatimaye, mwanzoni mwa mwaka 2025, Amira na familia yake waliamua kukimbia wakitafuta usalama.

Hata hivyo, walipokuwa wakitoroka kupitia barabara ya kusini-magharibi mwa el-Fasher, Amira anasema alitekwa nyara na wanaume watatu wenye silaha wa RSF na kuwekwa mateka.

"Waliniziba macho na kunipeleka eneo la Tabit, kusini mwa el-Fasher. Nilifungiwa ndani ya chumba kwa miezi miwili, na kila siku mmoja wao alinibaka kwa zamu," anasimulia kwa sauti ya chini.

Baada ya wiki kadhaa akiwa mateka, aligundua kuwa alikuwa mjamzito na afya yake ilianza kuzorota.

Amira anasema wanaume hao walipoamua kumuachia, walimtelekeza karibu na eneo alikotekwa.

Kwa msaada wa watu wengine waliokuwa wakikimbia el-Fasher, alipelekwa kupata matibabu.

Miezi kadhaa baadaye, katika kituo cha misaada ya kibinadamu kilichokuwa nje ya udhibiti wa RSF, alijifungua katika hospitali inayosimamiwa na International Medical Corps.

Akiwa hospitalini, alipata msaada kutoka shirika la misaada la Sudan liitwalo Nada Al-Azhar Foundation for Disaster Prevention and Sustainable Development.

Shirika hilo pia lilifanikiwa kuipata familia yake, ambayo ilikuwa imekimbilia katika kambi inayohifadhi mamia ya maelfu ya wakazi waliokimbia el-Fasher.

Ingawa kuungana tena na familia yake kulikuwa faraja kubwa, bado wanakabiliwa na changamoto nyingi. Mojawapo ni kwamba, miezi minane baada ya kujifungua, Amira bado ameshindwa kumsajili mtoto wake.

"Hata kupata taarifa ya kuzaliwa kutoka hospitalini kunahitaji taarifa ambazo sina," anasema, akieleza kuwa hawezi kutoa maelezo yoyote kuhusu baba wa mtoto huyo.

Kutokana na hali hiyo, hawezi kupata utambulisho rasmi wa kisheria kwa mtoto wake.

"Siwezi kumpatia chanjo, wala kumwandikisha kwenye chekechea au shule," anasema.

"Nina hofu kuhusu mustakabali wake kwa sababu hajasajiliwa kabisa. Hali yangu ya kiuchumi ni mbaya sana, siwezi kumudu matibabu wala kumlea ipasavyo. Siwezi hata kwenda kufanya kazi kwa hofu ya kukumbwa tena na ukatili."

Kwa mujibu wa shirika la Nada, simulizi la Amira si tukio la kipekee, bali ni sehemu ya hali inayowakumba wanawake na wasichana wengi katika maeneo yaliyoathiriwa na vita nchini Sudan.

Hali hii inatokana na ukweli kwamba watoto wengi wanazaliwa katika mazingira magumu, mara nyingi bila kufahamika baba zao, jambo linalofanya iwe vigumu kuwasajili rasmi, anaeleza Abu Bakr Yousif Yaqoub, mkurugenzi wa programu za ulinzi katika shirika la Nada.

"Usajili wa mtoto unahitaji taarifa za utambulisho wa wazazi, namba ya taifa na cheti cha kuzaliwa. Lakini baba anapokuwa hayupo au hajulikani, mchakato huo unakuwa mgumu sana," aliiambia BBC kutoka mji wa el-Fasher.

Anaongeza kuwa mara nyingi mama hubaki peke yake, na wakati mwingine yeye mwenyewe ni mtoto anayehitaji uangalizi, jambo linalopunguza uwezo wake wa kumlea mtoto.

"Pia kuna changamoto za kiafya kutokana na kukosekana kwa ufuatiliaji wa chanjo muhimu ambazo huanza kutolewa tangu mtoto anapozaliwa na kuendelea katika miaka yake ya mwanzo," alisema.

Yaqoub anaonya kuwa tatizo hilo haliishii katika utoto pekee, bali linaweza kuathiri maisha ya mtoto baadaye, ikiwemo kupata elimu, kusafiri au kupata nyaraka rasmi za utambulisho akiwa mtu mzima.

Si rahisi kupata takwimu sahihi kuhusu idadi ya watoto waliozaliwa kutokana na ubakaji nchini Sudan.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa shirika la Nada, Shaza Ahmed, sababu kubwa ni unyanyapaa wa kijamii unaowafanya wahanga wengi kutoripoti matukio hayo.

"Wanawake wanaopitia ukatili wa kijinsia hawajisikii huru kuripoti yaliyowapata," aliiambia BBC akiwa mjini Port Sudan, ambao unadhibitiwa na jeshi la Sudan.

"Cha kusikitisha ni kwamba, akina mama wengi wa watoto hawa ni watoto wenyewe, wasichana walio chini ya umri wa miaka 18. Hawawezi kwenda mahakamani au polisi kuripoti rasmi bila kuandamana na mlezi wao."

Ahmed anasema kuwa asilimia 90 ya kesi zilizorekodiwa na shirika lake zinahusisha familia zinazokataa kuruhusu matukio ya ubakaji yaliyopelekea ujauzito yaripotiwe rasmi.

"Kama mwanamke wa Sudan, hofu yangu kubwa ni kwamba tunashuhudia kizazi kizima cha watoto kitakachoishi chini ya unyanyapaa, hofu na hatari," alisema.

"Watoto hawa hawatapewa heshima inayostahili katika jamii, ustawi wao hautalindwa ipasavyo, na zaidi ya yote, watanyimwa huduma muhimu pamoja na haki zao."

Kwa mtazamo wake, watoto hao hawatendewi kama "binadamu kamili", licha ya sheria za Sudan kutambua haki ya kila mtoto kupata utambulisho rasmi.

Wakili wa Sudan, Majida Idris, anaeleza kuwa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2010 inaruhusu watoto waliozaliwa nje ya ndoa kusajiliwa.

Hata hivyo, mchakato huo unategemea mama kuwa tayari kutoa taarifa rasmi kwamba alifanyiwa ukatili wa kingono, kwa kuwa hatua hiyo ndiyo huanzisha taratibu za usajili.

Baada ya taarifa hiyo kutolewa, kesi hupelekwa kwa idara za ustawi wa jamii kwa ajili ya uhakiki na nyaraka, kabla ya kuwasilishwa kwa ofisi ya usajili wa raia, ambapo mtoto husajiliwa kwa jina la mama yake na kupewa jina kamili la kisheria kulingana na taratibu zilizowekwa.

Hata hivyo, wakili Majida Idris anasema hali halisi wakati wa vita ni tofauti kabisa, hasa katika eneo la Darfur, ambako mapigano yanayoendelea yamesababisha huduma nyingi za serikali kusambaratika na ofisi za usajili wa raia kufungwa, na kuwaacha maelfu ya watoto bila kusajiliwa.

"Kukosekana kwa nyaraka si kukosa karatasi tu; kunamaanisha kumnyima mtoto haki ya kupata elimu, huduma za afya na kutambuliwa kisheria," aliiambia BBC.

Idris anasema ni muhimu sana kufungua tena ofisi za usajili wa raia katika maeneo yanayoweza kufikika na kuimarisha juhudi za kisheria ili kuhakikisha watoto wote wanapata haki yao ya utambulisho na kutambuliwa rasmi na sheria.

Kwa sasa, Amira na mtoto wake bado wanaishi Darfur, hali inayomaanisha wanaendelea kukosa utambulisho rasmi na huduma muhimu zinazotegemea usajili wa kisheria.

Mama yake Amira anakiri kuwa kutokuwepo kwa nyaraka za mjukuu wake kunamsumbua sana.

Hata hivyo, kwa sasa familia hiyo inasema jambo muhimu zaidi ni kwamba wamefanikiwa kuungana tena baada ya kutengana kwa muda mrefu.

Amira pia ameanza kupokea ushauri nasaha pamoja na huduma za msaada wa kisaikolojia kutoka kwa shirika la Nada, jambo ambalo limeipa familia hiyo faraja na matumaini.

"Nilikuwa na hofu kubwa sana hadi nilipompata. Nilikuwa siwezi kula wala kunywa," mama yake Amira aliiambia BBC.

Aliongeza:

"Kuungana tena naye kulikuwa kama muujiza kutoka kwa Mungu. Kumwona binti yetu amerudi na kukaa tena pamoja nasi ni zawadi na baraka ambayo hatuwezi kuishukuru vya kutosha."