Iran yajibu pendekezo la Trump la ushuru wa Hormuz

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amejibu pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump la kutoza ushuru wa asilimia 20 kwa meli za kibiashara zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, akisema kiwango hicho ni kikubwa mno huku akisisitiza kuwa Iran imekuwa mlinzi wa njia hiyo muhimu ya baharini.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Araghchi alionekana kujibu kwa kejeli pendekezo la Trump.
“Rais wa Marekani yuko sahihi kabisa. Yeyote anayehakikisha meli za kibiashara zinapita kwa usalama katika Mlango wa Bahari wa Hormuz anapaswa kulipwa kwa huduma hiyo'', aliandika kwa ukurasa wake.
Vile vile akaendelea kusisitiza msimamo wa Iran kuhusu njia hiyo ya kimkakati kwa kusema, “Iran imekuwa mlinzi wa Mlango wa Hormuz siku zote na itaendelea kuwa hivyo milele.”
Akirejelea moja kwa moja pendekezo la Trump, Araghchi aliongeza, “Asilimia 20 bila shaka ni kubwa mno. Tutatoza ada za bei nafuu.”
Kauli hiyo imekuja baada ya ripoti kwamba Rais Trump alipendekeza kutozwa ushuru wa asilimia 20 kwa meli za mizigo zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, ambao ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa bidhaa duniani.
Mlango huo hupitisha sehemu kubwa ya mafuta ghafi na gesi asilia inayosafirishwa duniani, hivyo ukiwa na umuhimu mkubwa kwa biashara na usalama wa nishati duniani.
Kauli za Araghchi zinaweza kuongeza mvutano kati ya Tehran na Washington kuhusu usalama na udhibiti wa njia hiyo muhimu ya baharini.
Hadi sasa, Marekani haijatoa tamko rasmi kujibu kauli za Araghchi, lakini mabadilishano hayo yanaonyesha kuendelea kwa mvutano kati ya mataifa hayo mawili kuhusu Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Soma Zaidi:






















