Xhaka achunguzwa kuhusiana na cheti bandia cha Covid-19

Chanzo cha picha, Getty Images
Nahodha wa Uswizi, Granit Xhaka, anachunguzwa na waendesha mashtaka wa Uswizi kufuatia madai kuwa alipata cheti bandia cha chanjo ya Covid-19.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 anadaiwa kupata cheti hicho mwaka wa 2022, wakati ambapo kilikuwa sharti nchini Uswizi kwa ajili ya safari fulani za kwenda nje ya nchi.
Ofisi ya mwendesha mashtaka wa umma wa jiji la Lucerne ilithibitisha kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini iwapo kulikuwa na kitendo chochote cha uhalifu katika kupata cheti hicho "kisicho sahihi au ghushi".
Kiungo huyo wa Sunderland, ambaye wakati huo alikuwa akiichezea Arsenal, alitoa taarifa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumatatu akisema alikuwa na "mashaka" kuhusu chanjo hiyo na kwamba alikuwa "ameathiriwa na hofu na kutokuwa na uhakika".
Alisema: "Katika hali hiyo ya kuchanganyikiwa kifikra, nilipata cheti cha chanjo badala ya kutafuta majibu sahihi ya maswali yangu ambayo hayakupata ufafanuzi.
"Leo naona wazi kuwa njia hiyo haikuwa sahihi. Ilikuwa ni makosa. Samahani.
"Ninachukua jukumu la uamuzi huu, nitashiriki katika mchakato wa kubaini ukweli na kushirikiana kikamilifu na mamlaka husika."
Ofisi ya Afya ya Umma ya Uswizi ilithibitisha kuwa, ingawa hakukuwa na sheria ya jumla inayolazimisha kupata au kuwa na cheti hicho, kilikuwa kikihitajika ili kushiriki katika shughuli mbalimbali, kuingia maeneo fulani na kusafiri; hivyo basi, ushiriki ulizuiwa kwa yeyote ambaye hakuwa nacho.
Hatua hizo nchini Uswizi zilitekelezwa hadi majira ya kuchipua ya mwaka wa 2022.
Baada ya hapo, vyeti vya Covid-19 viliendelea kutolewa, hasa ili kuwawezesha wananchi kukidhi masharti ya kuingia nchi nyingine wakati wa kusafiri nje ya nchi.
Shirikisho la Soka la Uswizi lilisema kuwa Xhaka mchezaji aliyechezea timu ya taifa mara nyingi zaidi kuliko mwingine yeyote nchini humo, akiwa na rekodi ya mechi 152 alijiondoa katika kambi ya timu ya taifa kwa ajili ya mechi zijazo za Ligi ya Mataifa (Nations League) dhidi ya Scotland, Macedonia Kaskazini na Slovenia kufuatia taarifa yake.
















