'Nilinusurika mashambulizi ya makombora Hormuz, lakini rafiki yangu hajapatikana'

Chanzo cha picha, Sunil Puniya
- Author, Kayleen Devlin
- Nafasi, BBC Verify
- Author, Phoebe Keane
- Nafasi, BBC News
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
"Nilisikia meli nzima ikitikisika. Mwanzoni nilidhani injini imekumbwa na hitilafu. Lakini Lakini mara tu nilipotoka nje ya chumba changu, kulikuwa na mlipuko mwingine."."
Sunil Puniya, 26, alikuwa kwenye kazi yake ya kwanza baharini wakati kombora lilipoipiga meli ya mafuta ya Skylight mapema tarehe 1 Machi.
Meli hiyo iliyokuwa chini ya vikwazo vya Marekani ilikuwa safarini kutoka Dubai na ilikuwa inakaribia Mlango-Bahari wa Hormuz - mojawapo ya njia za meli zenye shughuli nyingi zaidi duniani. Skylight ilikuwa meli ya kwanza ya kibiashara kushambuliwa baada ya vita vya Marekani, Israel na Iran kuzuka katika eneo hilo.
Wakati wa shambulio hilo, Sunil alikuwa amelala kwenye chumba chake katika ghorofa ya tatu. Alizunduka na kupata hali ya machafuko ndani ya meli hiyo. Kombora lilikuwa limepiga chumba cha injini, na kusababisha moto ambao ulienea kwa kasi kwenye chombo.
"Kulikuwa na umme, lakini moshi ulikuwa umeenea kila mahali," alisema. "Kila mtu alikuwa anapata shida kupumua."
"Kuna baadhi ya mabaharia kutoka India Kusini ambao walikuwa wakilia na kupiga simu nyumbani kwa hofu . Niliwaambia waache kupiga simu na kuwasaidia kuwapandisha sehemu ya juu ya meli."
Lakini walipofika juu moto ulikuwa tayari umetanda.
"Mafuta yalikuwa yametapakaa kila mahali," Sunil alisema. "Moto ulikuwa unatujia hivyo tukaamua hivo tukaruka baharini."
'Alikua kama kaka yangu'

Chanzo cha picha, Family of Dalip Rathore
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jeshi la Wanamaji la Oman lilianzisha operesheni ya uokoaji ndani ya saa moja baada ya shambulio hilo na kuwatoa manusura kutoka majini. Lakini sio kila mtu alipatikana.
"Mara tu nilipogundua kuwa Dalip hayupo, ndipo uhalisia wa kilichotokea ulinijia," Sunil alisema. "Nilianza kuingiwa na hofu. Niliendelea kuwaza: nitaiambia nini familia yake?"
Dalip Rathore, 25, alikuwa amejiunga na Skylight siku moja baada ya Sunil. India ni mojawapo ya wasambazaji wakuu wa mabahariausafiri wa meli duniani kote lakini Dalip na Sunil waligundua kuwa wanatoka vijiji jirani vya Rajasthan na hivi karibuni wakawa marafiki wa karibu.
"Kulikuwa na changamoto ya mtandao kwenye meli, kwa hivyo hatukuweza kupiga simu nyumbani mara kwa mara," Sunil alisema. "Katika nyakati hizo, Dalip alikuwa akinijali. Alikuwa kama kaka."
Saa chache kabla ya shambulio hilo, Dalip alikuwa amechukua saa ya Sunil kwenye chumba cha injini - eneo lililopigwa na kombora.
Dalip na nahodha wa meli, Ashish Kumar, waliuawa katika shambulio hilo. Ingawa mwili wa nahodha ulipatikana, mwili wa Dalip haujawahi kupatikana.
Kukwama katika Mlango-Bahari wa Hormuz
Hadithi yao ni sehemu ya mgogoro mpana ambao umekuwa ukishuhudiwa katika Mlango-Bahari wa Hormuz. Mwanzoni mwa vita, Tehran ilijibu haraka mashambulizi kwa kufunga Mlango huo wa Bahari na njia muhimu kwa 20% ya usafirishaji wa mafuta na gesi duniani.
Kampuni ya ujasusi ya baharini ya Kpler iliiambia BBC Verify kwamba meli 38 za kibiashara zimeshambuliwa ndani na karibu na Hormuz tangu kuanza kwa mzozo huo. Takwimu zao zinaonyesha meli 24 zilishambuliwa na Iran, nne na Marekani, na zingine hazijathibitishwa.
Vita hivyo vimefanya mamia ya meli kushindwa kupita kwenye mlango huo wa bahari. Zaidi ya mabaharia 20,000 kwa sasa wamekwama katika Ghuba, kulingana na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini.
Chini ya sheria za baharini, wamiliki wa meli wanatakiwa kuwwajibikia kwa ustawi na kurejesha wafanyikazi wao. Ikiwa wamiliki wa meli watashindwa kuchukua hatua, jukumu linaweza kuangukia kwenye bendera ya meli na, hatimaye, mamlaka ya bandari.
Wamiliki wengi wa meli wamekuwa wakiandaa vifaa kwa ajili ya wafanyakazi wao ambao wamekwama kwenye mlango bahari wa Hormuz, wakitumia boti ndogo kupeleka chakula na vitu vingine vya msingi kwa meli zinazotia nanga.
Tangu mzozo huo kuzuka, Shirikisho la Kimataifa la Wafanyakazi wa Uchukuzi (ITF), chama cha wafanyakazi kinachosaidia mabaharia walio katika dhiki, linasema kuwa limepokea zaidi ya simu 2,000 za kuomba msaada kutoka kwa watu wa aina mbalimbali za meli za kibiashara ambazo zimenasa ndani na karibu na Mlango wa Bahari.
Matatizo hayo ni pamoja na mishahara ambayo haijalipwa, migogoro ya mikataba, ugumu wa kurudi nyumbani, na uhaba wa vifaa vya msingi kama vile chakula na maji.
Mohamed Arrachedi, mratibu wa mtandao wa ITF Arabuni na Iran, anasema baadhi ya wafanyakazi wamekwama baharini.
Aliwasilisha kwaBBC ujumbe wa sauti kutoka kwa mabaharia watatu waliotia nanga baharini na sasa wanaishi kwenye boti ndogo kwenye pwani ya Oman.
Katika ujumbe huo wanaume wanaomba msaada, wakisema wanapungukiwa na mahitaji ya msingi na hawajapata mawasiliano yoyote kutoka kwa mwenye meli kwa miezi kadhaa.
"Kwa bahati mbaya, tasnia kwa ujumla wake haijafanikiwa kutokomeza tatizo hili sugu la mabaharia kutelekezwa," alisema Arrachedi.
ITF inafafanua hili kama hali ambapo wamiliki wa meli huwatelekeza wafanyakazi, kuwaacha bila malipo wakiwa wamekwama, na bila mahitaji muhimu kama vile chakula, maji au huduma ya matibabu.
Jumla ya mabaharia 6,223 walitelekezwa katika meli 409 mwaka jana. Ni sehemu ndogo ya meli 100,000 za meli za wafanyabiashara zinazofanya kazi kote duniani, lakini umoja huo unasema ni hali inayotia wasiwasi.

Chanzo cha picha, Rex Pereira
David Loosley kutoka Bimco, mojawapo ya mashirika makubwa ya kimataifa ya usafiri wa meli, alisema kuwa wakati sekta hiyo inafanya kazi chini ya kanuni za kimataifa, kuna "matukio ya kipekee ambapo viwango havizingatiwi kikamilifu, na madhara makubwa kwa ustawi wa baharini".
"Migogoro ya kijiografia na kisiasa huongeza kwa kiasi kikubwa hatari zinazowakabili wale walio baharini," aliongeza.
Wakati mabaharia wengi waliokwama katika eneo hilo hawajatelekezwa, mzozo huo umefanya hali ambayo tayari ni hatarishi kuwa hatari zaidi kwa wale walio.
Rex Pereira, 28, kutoka Mumbai, hakuwa kwenye Skylight lakini aliajiriwa na mawakala sawa na Sunil.
Alisema alivumilia hali mbaya baharini kwa zaidi ya miezi minne kabla ya vita kuanza. Alisema maji yao ya kunywa yalikuwa yamechafuliwa na dizeli, chakula walichokuwa wakila kilikuwa kimeisha muda wake wa matumizi, na kusambaza picha za maji machafu ya rangi ya kahawia ambayo alisema wafanyakazi waliambiwa waoge nayo.
Licha ya ombi lake la kuondoka kwenye chombo ndani ya siku chache baada ya kupanda, hakupokea majibu ya simu zake za kuomba msaada.

Chanzo cha picha, Rex Pereira
Badala yake, alizuiliwa baharini kwa miezi kadhaa. Vita vilipoanza aliwekwa kando ya pwani ya Iraq na kushuhudia makombora yakirushwa karibu.
Tuliweza kuiona Iran kutoka tulipokuwa," alisema, na kuongeza kuwa makombora "yalikuwa yanaruka kila mahali".
Meli isiyo na mwenyewe

Kwa upande wa Skylight, ni vigumu kutambua nani alihusika na chombo hicho.
Jukwaa la ufuatiliaji wa usafiri wa baharini MarineTraffic linaorodhesha mmiliki wa meli kama Usimamizi wa Meli ya Bahari ya Shamu, kampuni iliyoko Dubai.
BBC ilipojaribu kuwasiliana na kampuni hiyo, simu kwa nambari iliyounganishwa na kampuni hiyo hazikupokelewa, huku barua pepe iliyotolewa kwa kampuni hiyo ikijirudia.
Kampuni pia inaonekana haina tovuti inayofanya kazi.
Sunil na familia ya Dalip wanasema hawajafanikiwa kuwasiliana na mmiliki wa meli hiyo tangu iliposhambuliwa.
Wachambuzi wa masuala ya baharini wanasema vikwazo vimebadilisha jinsi baadhi ya meli zinavyofanya kazi, huku meli zikizidi kutegemea muundo wa umiliki usio wazi, kubadilisha bendera na bima, na mitandao iliyochangamana ya usimamizi ili kuendelea kufanya biashara.
Wataalamu wanasema mfumo huo unaweza kufanya iwe vigumu zaidi kutambua ni nani anayewajibikia chombo mambo yakienda mrama.
Skylight iliwekewa vikwazo na Marekani mwezi Disemba mwaka jana kwa kusafirisha mafuta ya Iran. Kufuatia hatua hiyo ilipoteza bima yake na haikusajiliwa tena kwa nchi - inayojulikana kama serikali ya bendera - ambayo ina jukumu la kutekeleza viwango vya usalama na kisheria kwenye meli ya kibiashara.
Hapo awali ilikuwa imewekewa bima na Hydor, lakini msemaji wa kampuni hiyo aliiambia BBC kuwa mkataba wao ulivunjika wakati Marekani ilipoiwekea vikwazo meli hiyo. ITF ilithibitisha kuwa hakuna bima iliyosajiliwa kwa meli baada ya hapo.
Tumeona pia mawasiliano kutoka Palau - jimbo la bendera lililohusishwa hapo awali na meli - ikisema kwamba kufuatia vikwazo vya Marekani, Skylight ilifutiwa usajili na haikuendesha tena shughuli zake kwa kutumia alama ya nchi hiyo

Chanzo cha picha, Sunil Pereira
Wakati iliposhambuliwa, Skylight haikuwa na bima na wa uraia.
"Kwa sababu haina bima, hakutalipiwa fidia," anasema Michelle Bockmann, mchambuzi wa masuala ya bahari huko Windward.
"Umeachwa mikononi mwenye meli. Je, unaweza kupata mmiliki wa meli akiamumu kukutelekeza? Kawaida katika kesi hizi, wanatoweka na hawaonekani popote. Wanapanga umiliki wa meli kwa makusudi kupitia makampuni katika nchi ambazo ni vigumu sana kutambua ni nani hatimaye nyuma ya meli."
Kwa familia ya Dalip, ukosefu wa bima unaweza kuwa na matokeo mabaya.
Chini ya sheria za baharini, meli za kibiashara zinatakiwa kuwa na bima ili kufidia vifo na majeraha ya wafanyakazi. Bila hivyo, familia zinaweza kuhangaika kupata fidia.
Kwa mujibu wa Sunil, kabla ya kupanda Skylight, aliambiwa na wakala wa kuajiri nchini India kwamba meli hiyo ilikuwa na bima.
"Niliambiwa hati zote zipo na kuna bima," alisema.
Kuweka mabaharia kwenye meli isiyo na bima ni uvunjaji wa sheria ya baharini.
Alipowasiliana na BBC, mmoja wa maajenti waliohusika katika kumsajili Sunil alisema: "Hatuna taarifa zozote kwamba hakuna bima." Alidai jukumu lilikuwa la wakala mwingine aliyeko Dubai. Tulipiga simu na kutuma ujumbe kwa wakala huyo wa Dubai lakini hakupokea wala kujibu ujumbe wetu.
Sunil anasema hatarudi tena kufanya kazi baharini.
"Sijaweza kupata ujasiri wa kwenda kuona familia ya Dalip," alisema.
"Nikiona nyumbani kwake... nitahisi uwepo wake na kushindwa kuhimili majonzi. Ninamkosa sana."














