Watu watano wauawa huku Urusi ikianzisha mashambulizi mapya ya anga kote nchini Ukraine

Raia wa tano wa Ukraine ameripotiwa kuuawa katika mashambulizi ya Urusi yaliyofanyika usiku kucha.

Moja kwa moja

Abdalla Seif Dzungu

  1. Riccardo Calafiori, Kai Havertz na Martin Odegaard waisaidia Arsenal kuilaza Man City

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mabingwa watetezi Arsenal walionyesha mchezo wa kiwango cha hali ya juu katika mchezo wa Community Shield, kwa kuichapa Man City mabao 3-0 jijini Cardiff na kutuma ujumbe wa onyo kwa wapinzani wao wote wa Ligi Kuu ya Uingereza.

    Vijana hao wa Arsenal (The Gunners) waliwashangaza City na kocha wao mpya Enzo Maresca sekunde 23 tu baada ya mchezo kuanza, pale pasi safi ya Myles Lewis-Skelly ilipomfikia Riccardo Calafiori, ambaye alimalizia kwa utulivu na kufunga bao la kwanza.

    Baadaye, Christos Tzolis—mchezaji aliyesajiliwa na Arsenal kwa pauni milioni 34 katika dirisha la usajili la majira ya joto alihusika katika mabao mawili yaliyofuata; kwanza kwa kupiga mpira wa kichwa kuvuka lango ambao ulimfanya Kai Havertz kufunga bao la pili licha ya juhudi za kipa Gianluigi Donnarumma, na kisha kumpa pasi nahodha Martin Odegaard aliyefunga bao la tatu dakika tatu tu baada ya mapumziko katika Uwanja wa Principality.

  2. Kamanda wa jeshi la Iran atangaza zawadi ya dola 30,000 hadi 60,000 kwa ajili ya "kuua au kuwakamata" wanajeshi wa Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Hatami

    Amir Hatami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema kuwa jeshi hilo limeandaa mpango mpya ambapo yeyote atakayemuua au kumkamata na kumkabidhi askari wa Marekani atapokea "zawadi yenye thamani ya dola 30,000 au tomans bilioni tano."

    Amesema kuwa kiasi cha zawadi kwa ajili ya wanawake kitakuwa mara mbili ya kile cha wanaume, yaani dola 60,000.

    Alitoa kauli hizo katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Waandishi wa Habari iliyofanyika katika Shirika la Itikadi ya Kisiasa la Jeshi.

    Kamanda huyo wa jeshi la Iran aliendelea kusema, "Silaha ya mtu yeyote atakayefanikiwa kumuua mvamizi wa Marekani itanunuliwa kwa bei mara mbili ya thamani yake na atapewa silaha mpya.

    Silaha ya mtu huyo pia itawekwa katika makumbusho yaliyopangwa maalum."

    Soma zaidi:

  3. Arsenal vs Manchester City

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mabingwa wa ligi ya England Arsenal wanajibwaga uwanjani hii leo dhidi ya Manchester City katika kombe la Community Shield

    Wachezaji wa Arsenal watakaoanza: Raya, White, Mosquera, Gabriel, Calafiori, Lewis-Skelly, Guimaraes, Odegaard, Madueke, Tzolis, Havertz

    Wachezaji wa ziada: Arrizabalaga, Hincapie, Zubimendi, Merino, Rice, Eze, Dowman, Saka, Gyokeres

    Enzo Maresca amemuweka Elliot Anderson katika safu ya kati huku Erling Haaland akiongoza safu ya mashambulizi. Jack Grealish ametajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wa akiba wa City.

    Wachezaji wa Manchester City wanaoanza XI: Donnarumma, Khusanov, Dias, Guardiol, O'Reilly, Kovacic, Anderson, Semenyo, Foden, Doku, Haaland

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

  4. Tanzania yapinga kutuma watu kuingilia uchaguzi wa Zambia

    ..

    Serikali ya Tanzania imepinga madai yaliotolewa na mgombea wa urais wa Zambia Brian Mandubile kwamba Tanzania ilituma watu kwenda kuingilia uchaguzi mkuu wa taifa hilo uliofanyika hivi karibuni.

    Mgombea huyo wa urais wa Zambia, aliwaonya Watanzania anaodai wamehusika katika siasa za Zambia, akiwataka kuondoka nchini humo.

    Lakini katika taarifa iliotumwa katika mitandao ya kijamii, Tanzania imejibu kupitia barua kwa ubalozi wake nchini Zambia ikitaka maelezo ya kina kuhusu sababu za mgombea huyo kuzua madai kama hayo.

    Tanzania imesena inachukulia tuhuma hizo kwa uzito na kwamba inawahakikishia Watanzania na jamii ya kimataifa kwamba haijatuma mtu yeyote Zambia kuvuruga uchaguzi wa taifa hilo.

    ‘’Kama ilivyo nchi zingine za Jumuiya ya Maendeleo , kusini mwa Afrika SADC, Tanzania inao uwakilishi wa waangalizi wa uchaguzi nchini Zambia wanaofanya kazi kulingana na miongozo ya waangalizi wa uchaguzi wa SADC sambamba na waangalizi wengine waliopo Zambia na sio kuingilia Uchaguzi kama ilivyotuhumiwa na bwana Mandubile’’.

    Bwana Mandubile alinukuliwa akisema kwamba

    Zambia si Tanzania na kwamba mbinu za kisiasa zinazoweza kufanya kazi Tanzania haziwezi kutumika nchini Zambia.

    Alisema: "Ndugu zangu Watanzania ambao mmekodiwa, tafadhali tokeni katika nchi yetu."

    Alisema chama tawala cha UPND hakiwezi kushinda uchaguzi huo na kukituhumu kutumia kile alichokiita "mbinu ya Tanzania" ili kupata ushindi.

    "UPND hawawezi kushinda uchaguzi huu, hakuna muujiza. Sasa wameamua kutumia mbinu ya Tanzania. Zambia si Tanzania. Hii ni Zambia. Wale wanaofikiri wanaweza kuingiza katika nchi hii mbinu inayofanya kazi Tanzania, hawawezi kufanikiwa kamwe."

    Kauli ya Mundubile imekuja wakati mchakato wa kuhesabu kura katika uchaguzi wa Zambia ukiendelea chini ya ulinzi mkali, baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zambia kusimamisha kwa muda zoezi hilo kufuatia taarifa za mashambulizi dhidi ya maafisa wa uchaguzi na kuibwa kwa kura.

    Tume hiyo imesisitiza kuwa wagombea hawapaswi kujitangaza washindi kabla ya matokeo rasmi kutangazwa.

    Mundubile, ambaye ni mmoja wa wagombea wakuu wa upinzani, tayari amejitangaza mshindi wa uchaguzi huo, licha ya Tume ya Uchaguzi ya Zambia kutokuwa imetangaza matokeo ya mwisho.

  5. Jeshi la Israel limetangaza kuuawa kwa kamanda mkuu wa Kikosi cha Hezbollah

    Jeshi la Israel limetangaza kuuawa kwa Abu Hassan Alaa, kamanda mkuu wa Kikosi cha Badr cha Hezbollah.

    Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, jeshi la Israel lilisema kuwa lilimuua kamanda huyo mkuu ikiwa ni jibu kwa vitendo vya Hezbollah dhidi ya vikosi vya jeshi la Israel katika eneo la usalama.

    Ujumbe wa jeshi la Israel unasema: "Hassan Alaa alishiriki katika kupanga na kutekeleza mashambulizi mengi dhidi ya vikosi vya jeshi la Israel vilivyokuwa vikifanya operesheni katika eneo la usalama, ikiwa ni pamoja na kurusha ndege zisizo na rubani zilizobeba vilipuzi dhidi ya vikosi vya jeshi la Israel kusini mwa Lebanon."

  6. Habari za hivi punde, Urusi yazindua wimbi la mashambulizi dhidi ya Ukraine huku Kyiv ikishambulia kampuni kubwa karibu na Moscow

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Raia wa tano wa Ukraine ameripotiwa kuuawa katika mashambulizi ya Urusi yaliyofanyika usiku kucha.

    Meya wa Kryvyi Rih anasema mwanamume mwenye umri wa miaka 44, ambaye awali aliripotiwa kupotea, amepatikana akiwa amefariki dunia chini ya vifusi.

    Mtu mwingine aliuawa na wafanyakazi 14 wa kiwanda cha chuma walijeruhiwa. Urusi inasema eneo hilo lilikuwa likitengeneza vipuri vya silaha.

    Watu wawili wenye umri wa miaka ya 60 walifariki dunia baada ya nyumba kuharibiwa huko Zaporizhzhia.

    Idara za huduma za dharura zinasema moto uliokuwa ukiwaka katika soko moja jijini Kyiv umezimwa, baada ya soko hilo kushambuliwa usiku kucha.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anasema watu sita wamejeruhiwa jijini humo kufuatia mawimbi manne ya mashambulizi ya anga yaliyofanyika usiku na asubuhi ya leo.

    Rais alitaja kifo cha tano kilichotokea jana jioni huko Sumy, ambapo gari moja lilishambuliwa.

    Urusi inasema mashambulizi yake dhidi ya Kyiv usiku uliopita yalilenga kituo kilichokuwa kikizalisha vipuri vya makombora ya Ukraine aina ya Flamingo, pamoja na kiwanda kilichokuwa kikizalisha vipuri vya ndege zisizo na rubani (drones).

    Wizara ya Ulinzi ya Urusi inasema kuwa katika eneo la Poltava, ilishambulia kiwanda cha kusafisha mafuta cha Kremenchuk, ambacho inasema kinasambaza mafuta kwa jeshi la Ukraine.

    Urusi inasema ilishambulia meli ya mizigo karibu na Odesa, ikidai kuwa ilikuwa imebeba vifaa vya kijeshi.

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

  7. Idadi ya waliofariki katika ajali ya boti nchini Zimbabwe yapanda hadi 68 huku miili zaidi ikipatikana

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mtu anayesaidia kubeba jeneza anasimama karibu na majeneza wakati wa ibada ya ukumbusho kwa wahanga wa kivuko cha abiria cha Shirika la Maendeleo ya Miundombinu Vijijini (RIDA) kilichopinduka katika Ziwa Kariba, katika Uwanja wa Nyamhunga mjini Kariba, Zimbabwe, tarehe 13 Agosti 2026. Boti hiyo ilipinduka siku ya Jumanne na kusababisha vifo vya watu kadhaa.

    Miili mingine 22 imepatikana kufuatia ajali ya boti katika ziwa nchini Zimbabwe, polisi walisema Jumamosi, na hivyo kufanya idadi ya waliofariki kufikia 68.

    Boti hiyo ilipinduka tarehe 11 Agosti katika Ziwa Kariba.

    Uchunguzi unaonyesha kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba watu au mizigo kupita kiasi wakati ilipopinduka kutokana na upepo mkali.

    Jeshi la Polisi la Zimbabwe lilithibitisha idadi hiyo mpya ya waliofariki kupitia mitandao ya kijamii.

  8. Kamanda wa CENTCOM ahitimisha ziara yake Mashariki ya Kati baada ya kutembelea nchi sita na meli moja

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Kamanda wa Centcom Admirali Brad Cooper

    Kamanda wa Kamandi Kuu ya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati (CENTCOM) ameondoka eneo hilo baada ya ziara ya siku 10.

    Katika ziara hiyo, Admirali Brad Cooper alitembelea nchi sita na meli ya kubeba ndege za kivita ya Jeshi la Wanamaji la Marekani inayofanya kazi katika Bahari ya Uarabuni.

    Wakati wa ziara yake, alikutana na maafisa wa ngazi ya juu wa kiraia na kijeshi nchini Bahrain, Iraq, Israel, Jordan, Saudi Arabia, na Falme za Kiarabu, na pia alikutana na vikosi vya Marekani vilivyopo katika eneo hilo.

    Zaidi ya wanajeshi 50,000 wa Marekani wanatekeleza misheni mbalimbali kote Mashariki ya Kati.

    Kamanda huyo wa CENTCOM alikutana na mabaharia pamoja na wanajeshi wa 'Marines' waliopo kwenye meli ya kubeba ndege za kivita ya *Abraham Lincoln* kwa mara ya pili mwaka huu wakati wa ziara yake.

    Awali, aliitembelea meli hiyo mwezi Februari akiwa na Steve Whittaker, mjumbe maalum wa Marekani kwa ajili ya misheni za kulinda amani, na Jared Kushner, mkwe wa Donald Trump.

    "Kikosi cha Mashambulizi cha Lincoln (Lincoln Strike Group) ni timu imara ya Wamarekani wachapakazi na wenye mafanikio makubwa, ambao wanajivunia sana na kuwa na imani na mafanikio yao.

    Historia itaandika kupelekwa kwa kikosi hiki kama mojawapo ya vipindi vikali na muhimu zaidi vya operesheni katika nyakati za kisasa," aliwaambia wanajeshi wote wa meli ya Lincoln wakati wa ziara yake ya hivi karibuni.

    Meli ya *Abraham Lincoln*, ambayo kituo chake kikuu kiko San Diego, ilitumwa eneo hilo mwezi Novemba na kuwasili Mashariki ya Kati mwezi Januari.

    Kikosi hicho cha mashambulizi kimefanya maelfu ya safari za ndege za kivita kikiunga mkono Operesheni Epic Fury, katika vita dhidi ya Iran, na misheni za usalama wa kikanda, pamoja na hatua inayoendelea ya Marekani ya kuweka kizuizi cha majini dhidi ya Iran.

  9. Iran yataka kutumwa kwa timu ya wataalamu kufuatia Qatar kukanusha madai ya "kushikiliwa" kwa marubani wake

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mohammad Bagherzadeh, kamanda wa Kamati ya Kutafuta Watu Waliopotea chini ya Makao Makuu ya Jeshi, akijibu hatua ya Qatar kukanusha madai ya "kushikiliwa" kwa marubani wa Iran, aliitaka Doha kuandaa mazingira ya kutumwa kwa timu ya wataalamu wa Jeshi la Anga la Iran nchini humo.

    Alisema kuwa wataalamu wa Jeshi la Anga la Iran wamekuwa wakisubiri kwa miezi kadhaa kuingia Qatar na kufanya uchunguzi wa kina kuhusu suala hilo, lakini "vitendo vya hujuma na ucheleweshaji wa mara kwa mara unaofanywa na mamlaka za Qatar" vimezuia marubani hao kurejea nchini mwao hadi sasa.

    Bw. Bagherzadeh alisisitiza kuwa badala ya kupinga suala hilo, Qatar inapaswa kuruhusu timu ya wataalamu na wachunguzi wa Jeshi la Anga kwenda nchini humo.

    Kamanda huyo wa Kamati ya Kutafuta Watu Waliopotea pia alitoa wito kwa Shirika la Msalaba Mwekundu kufuatilia suala hilo mara moja.

    Pia alionya kuhusu hatima ya raia wanne wa Iran ambao alisema wanashikiliwa nchini Kuwait, akibainisha kuwa mamlaka za Kuwait bado hazijatoa taarifa kuhusu hali zao.

    Majid Ansari, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, jana alikanusha vikali madai ya Iran kuhusu "kushikiliwa" kwa marubani watatu wa Iran nchini Qatar, akisema alishangazwa sana na "kauli za kupotosha katika kipindi hiki," ikizingatiwa juhudi za kidiplomasia zinazoendelea kupunguza mivutano katika eneo hilo.

    Bw. Ansari aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba aliwasiliana na marubani hao wa Iran baada ya anga ya Qatar kukiukwa mwezi Machi na kuthibitisha njia waliyokuwa wakifuata.

    Alisema kuwa baada ya marubani hao kutojibu ujumbe uliotumwa, Qatar ilichukua hatua za kulinda eneo lake "kwa mujibu wa sheria za migogoro na matakwa ya sheria za kimataifa."

    Pia alisema kuwa timu za utafutaji na uokoaji za Qatar zilifanya operesheni ya kuwatafuta marubani hao na kwamba serikali ya Qatar imewasiliana na Iran ili kukabidhi mabaki ya mmoja wa marubani hao aliyepatikana.

  10. Jumuiya ya Nchi za Kiarabu: Mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon yanaongeza hatari ya vita kusambaa

    Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ililaani mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya Lebanon, ikiyataja mashambulizi ya jana—ambayo yalisababisha vifo vya watu 11—kuwa "ongezeko hatari la uhasama" linaloweza kuharibu juhudi za kusitisha mapigano na kufikia suluhisho.

    Msemaji wa Jumuiya hiyo alisema kuwa sera na vitendo vya Israel "vinaonyesha wazi nia ya wavamizi hao ya kuendeleza mgogoro, kukwamisha mazungumzo, na kulazimisha hali mpya ardhini, jambo ambalo halikubaliki kabisa na linapingwa vikali."

    Alionya kuhusu uwezekano wa migogoro hiyo kusambaa, akisema kuwa iwapo jumuiya ya kimataifa, na hasa Washington, haitazuia "mashine ya vita" ya Israel na kuilazimisha nchi hiyo kutii Azimio namba 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hali hiyo itaendelea kuzidi kuwa mbaya.

    Azimio hilo, lililopitishwa mwaka 2006, linataka kusitishwa kabisa kwa uhasama kati ya Israel na Hezbollah na kusisitiza kukomeshwa mara moja kwa mashambulizi yote ya Hezbollah pamoja na operesheni zote za kijeshi za mashambulizi zinazofanywa na Israel.

  11. Waokoaji wanawatafuta manusura wa tetemeko kubwa la ardhi nchini Indonesia

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Vikosi vya uokoaji nchini Indonesia vimekuwa vikiwatafuta manusura wa tetemeko kubwa la ardhi la siku ya Jumamosi ambalo limesababisha vifo vya watu wasiopungua 47.

    Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 7.7 katika kipimo cha Richter lilikumba kisiwa cha Flores muda mfupi kabla ya saa 05:00 asubuhi (saa 22:00 GMT siku ya Ijumaa) na kitovu chake kilikuwa katika kina cha kilomita 15, kulingana na taarifa ya shirika la hali ya hewa na jiolojia la Indonesia.

    Ripoti za awali zilionyesha kuwa zaidi ya nyumba 900 na mamia ya majengo mengine yaliathirika vibaya kutokana na tetemeko hilo pamoja na mitetemo 341 iliyofuata, shirika la kitaifa la usimamizi wa majanga (BNPB) lilisema.

    Hata hivyo, ukubwa kamili wa janga hilo bado haujajulikana, na taarifa za tetemeko la pili lenye ukubwa wa 6.9 katika upande mwingine wa Indonesia zilitumika kama ukumbusho wa sababu inayofanya eneo hili kuitwa "Pete ya Moto" (Ring of Fire).

    Mitetemo kutoka kwa tetemeko hilo kali la Jumamosi iliripotiwa kuhisiwa na wakazi hadi maeneo ya magharibi katika Wilaya na Jiji la Bima, BNPB ilisema, lakini jimbo la Manggarai ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi.

    Takwimu za awali zinaonyesha kuwa vifo 24 viliripotiwa huko, huku vifo 17 vikiripotiwa katika jimbo la Manggarai Mashariki, vitatu katika jimbo la Sikka, na angalau kifo kimoja katika kila moja ya majimbo ya Ngada, Ende na Manggarai Magharibi.

    Angalau watu wengine wawili walijeruhiwa vibaya na 11 walipata majeraha madogo.

    BNPB ilisema kuwa zaidi ya watu 5,000 bado wako katika vituo vya muda vya kuhifadhi waathirika na vifurushi 10,500 vya misaada vimepelekwa katika maeneo yaliyoathirika.

  12. Qatar yakanusha kuwakamata marubani watatu wa Iran baada ya kutungua ndege za kivita

    .

    Chanzo cha picha, UK MOD

    Iran imetoa wito wa kuachiwa huru kwa marubani watatu ambao ilisema walitekwa na Qatar baada ya ndege zake mbili za kivita kupigwa na mifumo ya ulinzi wa anga wakati wa operesheni ya kijeshi mwanzoni mwa vita kati ya Marekani na Iran.

    Katika barua kwa mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), Brigedia Jenerali wa Iran Mohammad Bagherzadeh alisema marubani hao - Javad Salehi, Abdul Majid Dashtian na Imran Behroshian - walikuwa wakishikiliwa mateka kwa miezi sita.

    Alisema mwili wa rubani wa nne, Majid Kazemi, ulikuwa umerejeshwa baada ya kuuawa katika operesheni hiyo hiyo mnamo tarehe 2 Machi 2026 - siku ya tatu ya vita.

    Qatar "ilikanusha vikali" madai ya Iran na kusema ilikuwa "imeshangazwa na kauli hizi za kupotosha".

    Jenerali Bagherzadeh alisema marubani hao watatu walitekwa na Qatar baada ya kuruka nje ya ndege zao wakati wa operesheni ya kivita iliyolenga kambi ya kijeshi ya Qatar.

    Katika barua hiyo kwa mkuu wa ICRC Mirjana Spoljaric, iliyochapishwa na vyombo vya habari vya Iran, aliishutumu Qatar kwa kukiuka "haki zisizoweza kuondolewa za wafungwa hawa, kinyume na sheria na kanuni zote za kimataifa".

    Barua hiyo pia ilidai kuwa marubani hao watatu hawakuruhusiwa kukutana au kuwasiliana na familia zao.

    Msemaji wa mambo ya nje wa Qatar, Majed Mohammed Al Ansari, alisema mawasiliano yalifanywa na marubani hao "baada ya kukiuka anga ya Qatar", lakini kwamba hawakupata majibu.

    "Hatua stahiki zilichukuliwa kulinda eneo letu kwa mujibu wa sheria za kimataifa," aliongeza katika taarifa kwenye mtandao wa X.

    Al Ansari alisema timu za utafutaji na uokoaji za Qatar "zilitekeleza majukumu yake kikamilifu katika kutafuta mabaki ya marubani hao".

    Alisema Qatar iliwasiliana na Iran ili "kuratibu makabidhiano ya mabaki ya mmoja wa marubani hao yaliyopatikana" na kwamba Tehran bado haijajibu mwaliko wa kupitia maelezo ya operesheni hiyo ya utafutaji na uokoaji.

    Soma zaidi:

  13. Natumai hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja