Spishi mpya ya nyani wenye midomo ya rangi ya chungwa yagunduliwa msituni DRC
Nyani mwenye midomo ya rangi ya waridi inayokaribia chungwa, uso mweusi na anayeishi katika misitu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) amethibitishwa kuwa spishi mpya kwa sayansi.
Nyani huyo mwenye manyoya meusi alionekana na kupigwa picha akiwa amejificha kwenye matawi ya juu ya miti katika msitu mnene wa kitropiki wa Hifadhi ya Taifa ya Lomami, iliyoko mashariki ya kati mwa DRC.
Wahifadhi wa mazingira wanaofanya kazi katika eneo hilo waliripoti kumuona mnyama huyo wa kipekee kwa mara ya kwanza mwaka 2008, lakini wakati huo walifanikiwa kupata picha moja tu isiyoeleweka vizuri.
Baada ya kuonekana tena miaka 10 baadaye, timu ya kimataifa ya watafiti ilianzisha msako wa kumtafuta na kumchunguza, na hatimaye kuthibitisha kuwa alikuwa spishi ambayo haikuwa imewahi kutambuliwa na sayansi.
Hii ni spishi ya tano pekee ya nyani barani Afrika kugunduliwa katika kipindi cha miaka 75 iliyopita.
Junior Amboko, mwanafunzi wa shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Florida Atlantic, aliongoza sehemu ya utafiti huo uliotumia kurekodi sauti, upigaji picha na uchambuzi wa kina wa vinasaba.
Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa katika jarida la kisayansi la PLoS One.
Akizungumza na BBC News, Amboko alisema ilikuwa "hisia ya kipekee" kutazama uso wa mnyama ambaye watu wachache sana duniani walijua uwepo wake.