Kombe la Dunia: Argentina yafuzu fainali kwa shangwe, England yaondoka kwa majonzi
Chanzo cha picha, Getty Images
Argentina imefuzu fainali kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuiondoa England katika mchezo wa nusu fainali ulioshuhudia hisia tofauti kwa timu hizo mbili.
Baada ya filimbi ya mwisho, wachezaji wa Argentina walipiga magoti uwanjani wakisherehekea ushindi na tiketi ya kuelekea fainali, huku wachezaji wa England wakijilaza uwanjani kwa huzuni baada ya ndoto yao ya kutwaa ubingwa kuyeyuka.
Argentina sasa itachuana na Uhispania katika fainali itakayopigwa Jumapili mjini New Jersey, ikilenga kutwaa taji hilo.
Kwa upande wa England, itaelekeza nguvu zake katika pambano la kuwania nafasi ya tatu dhidi ya Ufaransa, baada ya kushindwa tena kufika fainali.
Shirika la habari la Fars: Makombora ya Marekani yamedondoka karibu na hospitali ya watoto wenye saratani.
Chanzo cha picha, Tasnim
Shirika la habari la Iran, Fars News Agency, limesema makombora ya Marekani yamedondoka karibu na hospitali inayowahudumia watoto wenye saratani katika mji wa Ahvaz, kusini magharibi mwa nchi.
Kwa mujibu wa shirika hilo, milipuko kadhaa ilisikika katika maeneo mbalimbali ya mji huo katika saa za hivi karibuni.
Fars ilisema baadhi ya makombora hayo yalidondoka karibu na Hospitali ya Baghaei, ambayo hutoa huduma za tiba ya kemikali kwa wagonjwa wa saratani, hasa watoto.
"Katika moja ya mashambulizi hayo, makombora kadhaa yalidondoka karibu na Hospitali ya Baghaei, inayotoa huduma za tiba ya saratani kwa watoto," ilisema Fars.
BBC haijaweza kuthibitisha kwa njia huru madai hayo kutokana na ukosefu wa fursa ya kupata taarifa moja kwa moja kutoka ndani ya Iran.
Trump asema Iran itashindwa vitani huku Marekani ikiongeza mashambulizi
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump amesema Iran “inataka sana” kufikia makubaliano na Marekani, lakini akasisitiza kuwa Washington ndiyo itakayoamua iwapo mazungumzo hayo yataendelea.
Akizungumza Jumatano mjini Carlisle, Pennsylvania, Trump alisema pia kuwa Iran “itashindwa karibuni,” bila kutoa maelezo zaidi kuhusu kauli hiyo.
Kauli yake imejiri wakati mvutano wa kijeshi kati ya Marekani na Iran ukiendelea kuongezeka.
Jeshi la Marekani lilisema limeanzisha wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya malengo ya kijeshi ya Iran, likidai yamelenga kupunguza uwezo wa Tehran wa kutishia meli zinazopita katika Mlango wa Hormuz.
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema mashambulizi hayo yalianza saa 19:00 GMT na yalilenga miundombinu ya kijeshi inayohusishwa na vitisho dhidi ya usafiri wa baharini katika eneo hilo.
Wakati huo huo, shirika la habari la Mehr la Iran liliripoti kuwa milipuko ilisikika katika mji wa Bandar Abbas, kusini mwa Iran, na baadaye likasema makombora ya Marekani yaligonga eneo karibu na mji huo.
Iran haikuwa imetoa taarifa rasmi kuhusu kiwango cha uharibifu au idadi ya walioathiriwa kufikia wakati wa kuchapishwa kwa taarifa hii.
Marekani yaanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran huku Trump akiionya Tehran kuishi kwa nidhamu
Chanzo cha picha, CENTCOM,
Marekani imesema imeanzisha wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya Iran ikiwa ni usiku wa tano mfululizo, huku Rais Donald Trump akiionya Tehran kwamba "ni vyema ikaishi kwa nidhamu".
Jeshi la Marekani limesema mashambulizi hayo yalilenga uwezo wa kijeshi wa Iran uliokuwa ukitumiwa kutishia meli zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz. Pia limesema lilishambulia meli iliyodaiwa kujaribu kuvunja marufuku mpya ya usafirishaji kupitia bandari za Iran.
Hatua hiyo imekuja baada ya Iran kudai kuwa ilishambulia maeneo ya kijeshi ya Marekani katika eneo la Ghuba, yakiwemo Bahrain na Kuwait, huku siku ya tano ya mapigano mapya ikizidi kuhatarisha makubaliano ya awali yaliyolenga kumaliza vita.
Mjadala mkuu wa Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, ameiambia vyombo vya habari vya serikali kuwa Tehran "haina sababu" ya kuendelea kuheshimu makubaliano hayo ikiwa hayatakuwa na manufaa kwa nchi hiyo.
Jumanne usiku, Trump alitishia kushambulia madaraja na miundombinu ya uzalishaji wa umeme nchini Iran iwapo Tehran haitarejea kwenye mazungumzo wiki ijayo.
Alipoulizwa na waandishi wa habari Jumatano usiku iwapo angeweka muda wa mwisho kabla ya kuchukua hatua hiyo, Trump alisema:
"Sipendi kuweka muda wa mwisho, lakini wanafahamu hali ilivyo. Ni vyema wakaishi kwa nidhamu."
Baadaye, akihutubia mkutano wa viongozi wa masuala ya ulinzi, Trump alisema Iran haijafurahishwa na hali ya sasa.
"Wanataka kufikia makubaliano kwa udi na uvumba. Hawafurahishwi na kile tunachofanya. Tutaona kama tutafikia makubaliano nao au kama tutamaliza suala hili kabisa," alisema.