Korea Kusini yadokeza kushiriki kulinda usalama wa baharini katika Mlango wa Hormuz
Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri wa Ulinzi wa Korea Kusini, Ahn Gyu-bak amesema Seoul inazingatia hatua za taratibu za kushiriki katika kulinda usalama wa njia za usafirishaji wa majini katika Mlango wa Hormuz, lakini haitajihusisha moja kwa moja kijeshi.
Akizungumza na waandishi wa habari wa Korea Kusini mjini Washington Jumatano, Ahn alisema pia aliwasilisha msimamo huo katika mkutano wake na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth Jumatatu.
Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini, Ahn alisema:
“Tutatekeleza wajibu wetu kama mwanachama anayewajibika wa jumuiya ya kimataifa katika kuhakikisha usalama wa baharini katika Mlango wa Hormuz, na hatua kwa hatua tutatafakari namna tunavyoweza kushirikiana.”
Alisema hatua zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja na kutoa uungaji mkono wa kisiasa, kupeleka wafanyakazi, kubadilishana taarifa pamoja na kutoa rasilimali za kijeshi.
Hata hivyo, alifafanua kuwa hakukuwa na mazungumzo ya kina kuhusu kuongeza ushiriki wa wanajeshi wa Korea Kusini katika eneo hilo.
Trump azua mjadala baada ya kuiita Venezuela “Jimbo la 51” la Marekani
Chanzo cha picha, Truth social
Rais wa Marekani Donald Trump ameibua mjadala mpya baada ya kuchapisha ramani ya Venezuela iliyoambatanishwa na bendera ya Marekani na maneno “State 51” kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Jumanne usiku.
Trump, ambaye yuko njiani kuelekea China kwa mkutano na Rais Xi Jinping, alichapisha picha hiyo siku moja baada ya ripota wa Fox News kusema kuwa rais huyo alimweleza kwa simu kwamba alikuwa “anafikiria” kuifanya Venezuela kuwa jimbo la 51 la Marekani.
Kauli na picha hiyo zimezua mjadala mkubwa kimataifa, hasa ikizingatiwa kuwa Trump aliwahi pia kutoa kauli zinazofanana kuhusu Canada na Greenland, hatua zilizokosolewa vikali na serikali pamoja na wananchi wa maeneo hayo.
Nollywood yaomboleza Alex Ekubo baada ya mwigizaji kufariki akiwa na miaka 40
Chanzo cha picha, Alex Ekubo/Facebook
Mwigizaji maarufu wa filamu za Nollywood Alex Ekubo amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 40, tukio ambalo limeacha tasnia ya filamu ya Nigeria katika majonzi makubwa huku wenzake wakimkumbuka kwa heshima na hisia kali kupitia mitandao ya kijamii.
Habari za kifo chake zilithibitishwa Jumanne na baadhi ya watu wake wa karibu pamoja na waigizaji wenzake akiwemo Funke Akindele, Bolanle Ninalowo na Godwin Nnadiekwe.
Akizungumzia msiba huo kupitia Instagram yake, Funke Akindele aliandika maneno ya huzuni akisema alijaribu kumtafuta ili waweze kuonana tena lakini hakufanikiwa, akimtakia pumziko la amani na kumkumbuka kama “rafiki yake wa karibu” aliyeitwa kwa upendo “Ore mi”.
Kwa upande wake, Bolanle Ninalowo aliandika ujumbe wa rambirambi akimuombea marehemu apumzike kwa amani na kuwatakia faraja familia yake pamoja na mashabiki wote.
Naye Godwin Nnadiekwe alieleza kuguswa sana na taarifa hiyo akisema ni vigumu kuamini kifo cha rafiki na msanii mwenza, akisema Nollywood imepoteza kipaji cha kipekee.
Kwa mujibu wake, msiba huo umemuumiza sana hadi kushindwa kupata maneno ya kueleza, akibainisha kuwa marehemu tayari alikuwa ameacha wosia, jambo lililoongeza uzito wa huzuni hiyo.
Alex Ekubo alijulikana sana kama mmoja wa waigizaji mahiri na wanaopendwa zaidi katika Nollywood, akiwa amejipatia umaarufu kupitia filamu za mapenzi, vichekesho na vipindi vya televisheni vilivyovutia watazamaji ndani na nje ya Nigeria.
Ronaldo akosa ushindi, Al Nassr na Al Hilal wagawana pointi katika mbio za ubingwa
Chanzo cha picha, Getty Images
Al Nassr na Al Hilal zimekutana katika mchezo uliotarajiwa kuamua hatima ya ubingwa wa ligi ya Saudi Pro League.
Jorge Jesus alianza vibaya mchezo huo baada ya kikosi chake kuzidiwa nguvu katika kipindi cha kwanza na upande wa Simone Inzaghi.
Licha ya shinikizo hiyo, bao la Mohamed Simakan lilibadilisha mwelekeo wa mchezo na kuipa Al Nassr matumaini makubwa ya karibu na ubingwa wa kwanza kwa Cristiano Ronaldo akiwa na klabu hiyo.
Katika kipindi cha kwanza, Al Hilal walitawala kwa muda mrefu wakitumia shinikizo na mpira wa pamoja uliopangwa vizuri, hatua iliyowalazimisha Al Nassr kujihami zaidi. Hata hivyo, Karim Benzema na N'Golo Kanno walikosa nafasi muhimu ambazo zingebadilisha matokeo mapema.
Baada ya bao la Simakan, Al Hilal walirudi nyuma kwa kiasi kikubwa huku Al Nassr wakianza kudhibiti mchezo.
Timu ya Jorge Jesus iliendelea kuhimili mashambulizi lakini bado haikupoteza ushindani, huku Sadio Mane akiongoza safu ya ushambuliaji kwa kiwango cha juu.
Kipindi cha pili kilishuhudia mabadiliko ya kasi, Al Nassr wakijaribu kuongeza mashambulizi na kulazimisha mchezo wa kasi zaidi.
Hali hiyo ilizifanya timu zote kugawana umiliki wa mpira, lakini Ronaldo hakuonekana sana uwanjani, huku Joao Felix akionyesha kiwango bora kwa upande wa ushambuliaji.
Wakati mchezo ukielekea kumalizika, kosa la kipa Bento Krepski liliiwezesha Al Hilal kusawazisha katika sekunde za mwisho za dakika za nyongeza (90+8), na kuhitimisha mchezo kwa sare iliyoweka mbio za ubingwa wazi zaidi.
Kidonge kipya chatajwa kusaidia kudhibiti uzito wa mwili baada ya kuacha sindano
Chanzo cha picha, Getty Images
Utafiti mpya umeonyesha kuwa kidonge kipya cha matumizi ya kila siku kinaweza kusaidia watu waliotumia sindano za kupunguza uzito kuendelea kuwa na mwili mwembamba hata baada ya kuacha matibabu hayo.
Dawa hiyo tayari inapatikana Marekani na huenda ikaanza kutumika Uingereza hivi karibuni.
Katika majaribio yaliyofanywa, wagonjwa waliotumia kidonge hicho kinachoitwa Orforglipron kila siku kwa mwaka mmoja walifanikiwa kuepuka kurejea kwa uzito mkubwa waliokuwa wameupunguza awali.
Kuongeza uzito wa mwili ni moja ya changamoto zinazowakabili watu wengi wanapoacha sindano za GLP 1 za kupunguza uzito.
Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Nature Medicine ulifadhiliwa na kampuni ya Eli Lilly ambayo pia hutengeneza sindano ya kupunguza uzito ya Mounjaro.
Wataalamu wanasema bado kuna haja ya kufanya tafiti zaidi ili kubaini mtu anatakiwa kutumia dawa hiyo kwa muda gani, huku baadhi wakisema huenda matibabu yakahitajika kwa muda mrefu au hata maisha yote.
Daktari Marie Spreckley, mtaalamu wa tafiti za kudhibiti uzito katika Chuo Kikuu cha University of Cambridge ambaye hakushiriki katika utafiti huo, amesema watu wengi wanaweza kuona ni rahisi zaidi kutumia kidonge kuliko kujidunga sindano.
Hata hivyo, ameonya kuwa bado haijulikani matokeo hayo yataendelea kwa muda gani kwa matumizi ya muda mrefu.
“Utafiti huu unaonyesha kuwa unene kupita kiasi ni tatizo sugu ambalo linaweza kurejea tena, na mara nyingi huhitaji matibabu na msaada wa kuendelea,” alisema.
Mourinho afanya mazungumzo ya kuwa kocha mpya wa Real Madrid
Chanzo cha picha, Getty Images
Kocha raia wa Ureno Jose Mourinho yuko katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kurejea kuinoa Real Madrid, miaka 13 baada ya kuondoka kwa mara ya kwanza katika dimba la Santiago Bernabeu.
Mourinho mwenye umri wa miaka 63 ndiye anayepewa nafasi kubwa zaidi ya kuchukua mikoba ya ukocha, na kwa sasa ndiye mgombea pekee ambaye Real Madrid inaendelea kufanya naye mazungumzo rasmi.
Iwapo makubaliano yatafikiwa, atamrithi Alvaro Arbeloa ambaye alichukua nafasi hiyo mwezi Januari baada ya kuondoka kwa Xabi Alonso.
Rais wa Real Madrid Florentino Perez alianza kufikiria uwezekano wa Mourinho kurejea siku mbili baada ya kuondoka kwa Xabi Alonso, kupitia mawasiliano ya awali na wawakilishi wa kocha huyo wa Ureno.
Kwa sasa Mourinho ni kocha wa Benfica baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili Septemba mwaka jana. Hata hivyo, jana alikwepa kuzungumzia mustakabali wake.
“Kuna mechi dhidi ya Estoril, na kuanzia Jumatatu nitaweza kujibu maswali kuhusu mustakabali wangu na wa Benfica,” alisema Mourinho.
Mechi ya Jumamosi dhidi ya Estoril Praia utakuwa wa mwisho kwa Benfica msimu huu.
Kuanzia Jumapili, Real Madrid itakuwa na nafasi ya kukamilisha dili hilo kwa gharama nafuu kutokana na kipengele cha mkataba kinachomruhusu Mourinho kuondoka kwa ada ya euro milioni tatu ndani ya siku 10 baada ya mechi ya mwisho ya msimu.
Katika kipindi chake cha kwanza Real Madrid kati ya mwaka 2010 na 2013, Mourinho aliiongoza klabu hiyo kutwaa taji la La Liga, Copa del Rey pamoja na Spanish Super Cup.
Baada ya kuondoka Madrid, alirejea Chelsea na kushinda taji lake la tatu la Ligi Kuu England pamoja na Kombe la EFL msimu wa 2014 hadi 2015.
Mwaka 2016 alijiunga na Manchester United ambapo alitwaa Europa League, EFL Cup na Community Shield kabla ya kutimuliwa mwaka 2018 kutokana na matokeo mabaya.
Mourinho pia amewahi kuzinoa Tottenham Hotspur, AS Roma ambako alitwaa ligi ya Europa Conference mwaka 2022, pamoja na Fenerbahce kabla ya kujiunga na Benfica mwaka jana.
Wakati huo huo, Real Madrid imemaliza msimu wa 2025 hadi 2026 bila taji lolote, huku mahasimu wao Barcelona wakitwaa ubingwa wa La Liga baada ya ushindi wa mabao 2 kwa 0 katika El Clasico na kumaliza kwa tofauti ya pointi 14.
Katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid iliondolewa robo fainali baada ya kufungwa kwa jumla ya mabao 6 kwa 4 na mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich.
Mfumo wa Trump wa ‘Golden Dome’ kugharimu dola trilioni 1.2 huku ukitiliwa shaka uwezo wake
Chanzo cha picha, Getty Images
Mfumo wa kisasa wa ulinzi wa makombora wa Rais wa Marekani Donald Trump unaojulikana kama “Golden Dome” unatarajiwa kugharimu takriban dola trilioni 1.2 za Marekani sawa na pauni bilioni 882 katika kipindi cha miaka 20 ya kuubuni, kuujenga na kuendesha, kwa mujibu wa makadirio ya Ofisi ya Bajeti ya Bunge la Marekani.
Kiasi hicho ni kikubwa zaidi kuliko makadirio ya awali ya dola bilioni 175 zilizokuwa zimetengwa kwa mradi huo.
Hata hivyo, mfumo huo uliobuniwa kuilinda Marekani dhidi ya makombora ya balistiki na makombora kutoka kwa meli za kivita huenda usiwe na uwezo wa kuhimili mashambulizi makubwa ya moja kwa moja.
Ripoti mpya ya Ofisi ya Bajeti ya Bunge imeonya kuwa “Golden Dome” inaweza kuzidiwa nguvu katika shambulizi kamili kutoka Urusi au China.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa gharama za ununuzi pekee zitazidi dola trilioni moja, ikijumuisha mifumo ya kuzuia makombora pamoja na teknolojia za anga za juu za kutoa tahadhari na kufuatilia makombora.
Kwa muda mrefu kumekuwa na mashaka kuhusu uwezo wa Marekani kujenga mfumo wa ulinzi wenye uwezo wa kulinda eneo kubwa kiasi hicho la kijiografia.
Maafisa wa Marekani pia wameonya kuwa mifumo iliyopo sasa haijaendana na maendeleo ya silaha za kisasa zinazomilikiwa na mataifa hasimu.
Licha ya gharama kubwa zinazotarajiwa, Ofisi ya Bajeti ya Bunge ilisema mfumo huo “unaweza kuzidiwa uwezo na mashambulizi makubwa yatakayofanywa na taifa lenye nguvu sawa au linalokaribia kiwango hicho.”
Amri ya kiutendaji iliyoagiza kuundwa kwa mfumo huo, ambao awali uliitwa “Iron Dome for America”, ilieleza kuwa tishio la silaha za kizazi kipya limekuwa “kubwa na tata zaidi” kadri muda unavyopita, hali inayoweza kusababisha madhara makubwa kwa Marekani.
Mwezi uliopita, SpaceX na Lockheed Martin zilipata kandarasi zenye thamani ya hadi dola bilioni 3.2 kwa ajili ya kuunda mifumo ya majaribio ya anga ya kuzuia makombora kwa mradi huo.
Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi cha Iran kimetekeleza mazoezi ya kijeshi ambayo hayakutangazwa rasmi, yaliyopewa jina la “Mashahidi wa Makamanda”.
Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kuwa mazoezi hayo yalilenga kupima uwezo wa vikosi vya kijeshi katika kukabiliana na adui pamoja na kutathmini mikakati ya operesheni za kivita.
Kwa mujibu wa Hassan Hassanzadeh, mbinu zote za kiutendaji na operesheni za vikosi maalumu pamoja na maafisa wake zilifanyiwa majaribio kwa mafanikio wakati wa mazoezi hayo.
Alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha uwezo wa mapambano na kuongeza utayari wa kijeshi dhidi ya hatua zozote zinazoweza kuchukuliwa na adui.
Pentagon: Gharama ya vita kati ya Marekani na Iran yafikia karibu dola bilioni 29
Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, imetangaza Jumanne kuwa makadirio ya hivi karibuni ya gharama ya vita dhidi ya Iran yamefikia karibu dola bilioni 29 za Marekani.
Takwimu hiyo mpya, iliyotolewa wakati wa kikao cha kujadili bajeti katika Bunge la Marekani, ni takriban dola bilioni 4 zaidi ya makadirio yaliyotolewa wiki mbili zilizopita na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth.
Pete Hegseth pamoja na Jenerali Dan Caine walikuwa wakifafanua ombi la bajeti ya dola trilioni 1.5 kwa mwaka 2027 walipoulizwa kueleza gharama ya vita dhidi ya Iran.
“Wakati wa ushuhuda huo, gharama ilikuwa dola bilioni 25,” alisema Jules Hurst, afisa mkuu wa fedha wa Pentagon ambaye pia alikuwepo katika kikao hicho, akirejelea makadirio ambayo Waziri wa Ulinzi aliwasilisha kwa Bunge Aprili 29.
Reuters: Saudi Arabia ilifanya mashambulizi ya siri dhidi ya Iran wakati wa vita
Chanzo cha picha, @modgovksa/X
Baada ya kuripotiwa jana kuwa UAE ilifanya mashambulizi ya siri ya anga dhidi ya Iran, shirika la habari la Reuters limeripoti kwamba Saudi Arabia pia ilitekeleza mashambulizi kadhaa ambayo hayakutangazwa rasmi dhidi ya Iran, ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi kufuatia mashambulizi yaliyofanywa dhidi yake wakati wa vita vya Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu wa maafisa wawili wa Magharibi wenye ufahamu wa suala hilo pamoja na maafisa wawili wa Iran, mashambulizi hayo ndiyo mara ya kwanza kwa Saudi Arabia kujulikana kuchukua hatua ya moja kwa moja ya kijeshi ndani ya ardhi ya Iran, hali inayotafsiriwa kuwa ishara ya Riyadh kuonyesha uthubutu zaidi katika kujilinda dhidi ya mpinzani wake mkuu wa kikanda.
Reuters imesema katika ripoti yake maalumu kuwa mashambulizi hayo, ambayo hayajawahi kuripotiwa hapo awali, yalifanywa na jeshi la anga la Saudi Arabia na huenda yalitekelezwa mwishoni mwa mwezi Machi.
“Hayakuwa mashambulizi ya kawaida, bali yalikuwa ya kulipiza kisasi baada ya Saudi Arabia kushambuliwa,” mmoja wa maafisa hao wa Magharibi aliliambia Reuters.
Hata hivyo, Reuters imesema haikuweza kuthibitisha maeneo mahsusi yaliyolengwa katika mashambulizi hayo.
Afisa mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia hakuzungumzia moja kwa moja madai hayo alipoulizwa na Reuters kutoa maoni, huku Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran nayo ikikataa kujibu ombi la shirika hilo la habari.
Saudi Arabia, ambayo kwa muda mrefu imekuwa na ushirikiano wa karibu wa kijeshi na Marekani, imekuwa ikitegemea ulinzi wa Marekani dhidi ya vitisho vya kikanda. Hata hivyo, vita vya wiki 10 vilivyoikumba Mashariki ya Kati vimeonekana kuiacha nchi hiyo katika mazingira hatarishi baada ya baadhi ya mashambulizi kupenya mifumo ya ulinzi inayoungwa mkono na Marekani.
Jana, gazeti la The Wall Street Journal liliripoti kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu ulifanya mashambulizi ya anga dhidi ya miundombinu ya mafuta ya Iran katika Ghuba ya Uajemi katika saa za mwanzo za tangazo la usitishaji mapigano kati ya Iran na Marekani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mashambulizi hayo yalijumuisha angalau shambulizi moja dhidi ya vituo vya Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Iran katika Kisiwa cha Lavan.
Trump: lazima tufikie makubaliano na Iran ama tutaiangamiza
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump amesema hahitaji msaada wa China katika juhudi za kumaliza vita dhidi ya Iran.
Akizungumza wakati akiondoka kuelekea ziara rasmi nchini China, Trump alisema atakuwa na mazungumzo ya kina na Rais Xi Jinping katika mkutano wao wa wiki hii.
Hata hivyo, Trump amesisitiza kuwa hahitaji msaada wa Xi Jinping katika kutatua mzozo ulioanza miezi miwili na nusu iliyopita kufuatia mashambulizi makubwa ya Marekani na Israel, ambayo baadaye yalizua mvutano mkali kuhusu udhibiti wa Mlango wa Hormuz.
“Tunazungumzia mambo mengi. Kwa kweli, siwezi kusema Iran ni mojawapo, kwa sababu tunaidhibiti Iran kikamilifu,” alisema Trump.
Kiongozi huyo wa Marekani aliongeza kuwa: “Ima tufikie makubaliano na Iran, au itaangamizwa kabisa.”
Kauli hiyo imejiri huku kukiwa na ripoti zinazoeleza kuwa China inaendelea kuisaidia Iran kupitia biashara ya mafuta na ushirikiano mwingine licha ya vikwazo vya kimataifa.
Trump, hata hivyo, alimpongeza Xi Jinping akisema kuwa “amekuwa akifanya kazi nzuri sana.”
China inaripotiwa kuwa mmoja wa washirika muhimu zaidi wa kiuchumi wa Iran, hasa kupitia ununuzi mkubwa wa mafuta ya nchi hiyo, huku Beijing ikionekana pia kuipa Tehran uungaji mkono wa kisiasa na kiuchumi.