Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Walimu walijua mpango wa kuchoma shule ulioua watoto 16 Kenya - Waziri

Idara ya upelelezi wa makosa ya jinai kwa sasa inawashikilia na kuwahoji wanafunzi wanane ambao wanashukiwa kuasha moto huo.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid & Beldeen Waliaula

  1. Trump asema Marekani itaondoa kizuizi cha kijeshi katika Mlango bahari wa Hormuz

    Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa amesitisha uwepo wa kizuizi cha kijeshi katika mlango Bahari wa Hormuz, na kusema kuwa meli zilizokwama eneo hilo pamoja na wafanyakazi wake wanapaswa kujiandaa kurudi nyumbani.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social hii leo, amesema masuala mengi yamekubaliwa kati yao na Iran.

    “Sasa ninaelekea kwenye mkutano wa dharura na nitafanya uamuzi wa mwisho,” aliandika Trump

    Aidha Trump amesema Iran lazima ikubali kutowahi kutengeneza silaha za nyuklia na kufungua mlango bahari wa Hormuz mara moja.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Visa zaidi vya Ebola vyaripotiwa Uganda

    Wizara ya Afya ya Uganda imethibitisha visa viwili vipya vya ugonjwa wa Ebola katika mji mkuu wa Kampala.

    Visa vya Ebola vilivyothibitishwa nchini Uganda kufikia sasa vimefika tisa.

    Katika taarifa iliyotolewa na wizara ya afya ya Uganda, maambukizi hayo mapya ni kutoka kwa raia wa DRC, ambao kwa sasa wako chini ya uangalizi wa madaktari.

    Siku ya Jumatano, mamlaka za Uganda zilitangaza kufunga kwa muda vivuko vya mpakani kati ya taifa hilo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kama sehemu ya kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo.

    Uganda pia imepiga marufuku mikusanyiko ya watu wengi na kuimarisha ukaguzi wa watu mipakani ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo wa Ebola.

    Pia unaweza kusoma:

  3. UNICEF yakashifu mauaji ya watoto nchini Lebanon

    Watoto 11 huuawa au kujeruhiwa kila siku nchini Lebanon katika kipindi cha wiki moja iliyopita, shirika la umoja wa mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF imesema.

    Israel imeendelea kutanua mashambulizi yake nchini Lebanon, licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Israel imekuwa ikilenga maeneo ya kusini mwa Lebanon pamoja na mji wa Beirut.

    Jumla ya watoto 77 wameuawa au kujeruhiwa katika siku saba zilizopita, kulingana Wizara ya Afya ya Umma ya Lebanon.

    Tangu makubaliano ya kusitisha mapigano kuafikiwa tarehe 16 mwezi Aprili, watoto 55 wameuawa huku 212 wakijeruhiwa, kwa mujibu wa shirika la UNICEF.

    Msemaji wa UNICEF Ricardo Pires, ametoa wito kwa pande zote mbili zinazo zozana kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano.

    “Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, watoto pamoja na miundombinu ya kiraia lazima zilindwe,” alisema Pires.

    Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotangazwa na Washington yalilenga kusimamisha mapigano kati ya wanajeshi wa Israel na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, ambayo yamekuwa yakiendelea tangu tarehe 2 mwezi Machi.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Balozi wa Urusi afukuzwa Romania

    Romania imemfukuza balozi wa Urusi kutoka nchini humo, na kufunga ubalozi wa Urusi, baada ya ndege mbili zisizo na rubani za Urusi kushambulia eneo la makazi nchini Romania.

    Watu wawili wamejuruhiwa katika shambulio hilo mashariki mwa mji wa Galati.

    Romania imemtaja balozi wa Urusi nchini humo kama “mtu asiyekubalika”

    Msemaji wa rais wa Urusi amesema Vladimir Putin anafahamu kuhusu ajali ya ndege zisizo na rubani iliyotokea Romania.

    Vyombo vya habari vya Urusi vimesema taifa hilo litajibu hatua ya Romania ya kumfukuza balozi wa taifa hilo kutoka nchini humo.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Wazazi waendelea kufika katika shule ya Utumishi Girls kuwatafuta watoto wao

    Wazazi wameendelea kufika katika shule ya upili ya wasichana ya Utumishi Girls nchini Kenya, kutaka kujua waliko watoto wao baada ya mkasa wa moto kwenye bweni moja shuleni humo.

    Wanafunzi 16 wamefariki kutokana na mkasa huo, 79 wakiendelea kuuguza majeraha.

    Tazama kwa picha jinsi wazazi walivyofika katika shule hiyo wakiwaulizia watoto wao

  6. Walimu wawili walijua kuhusu mpango wa kuchoma shule, asema waziri wa elimu Kenya

    Walimu wawili katika shule ya wasichana ya Utumishi, eneo la Gilgil nchini Kenya, waliarifiwa kuhusu mpango wa kuchoma bweni, uliokuwa umepangwa na kundi la wanafunzi wa kidato cha tatu, Waziri wa Elimu Julius Ogamba amesema.

    Katika taarifa yake, waziri huyo amesema walimu hao hawakuchukua hatua stahiki kabla ya tukio hilo la moto kutokea, licha ya kupewa taarifa hiyo mapema.

    Waziri huyo amesema uchunguzi umebaini kuwa moto uliochoma bweni la shule hiyo, uliashwa kimakusudi.

    Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa sasa inawashikilia na kuwahoji wanafunzi wanane ambao wanashukiwa kuasha moto huo.

    “Uchunguzi utaweka wazi majukumu ya kila mmoja katika kupanga na kutekeleza kitendo hiki cha kikatili,” alisema Waziri wa Elimu

    Ameongeza kuwa watakaobainika kuhusika na mkasa huo wa moto watafunguliwa mashtaka.

    Waziri huyo aidha amesema kuwa , shule hiyo haikuzingatia kikamilifu miongozo ya usalama shuleni iliyowekwa na wizara ya elimu.

    Wanafunzi 79 wanauguza majeraha.

    Wanafunzi saba bado wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta, huku wengine wakipewa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

    Miili ya wanafunzi waliopoteza maisha yao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Naivasha kwa ajili ya utambuzi wa vinasaba vya DNA.

    Idadi ya wanafunzi waliopoteza maisha katika mkasa huo wa moto imefikia 16.

    Pia unaweza kusoma:

  7. NATO yakashifu hatua ya Urusi ya kuishambulia Romania

    Rais wa Romania, Nicușor Dan, ameitisha kikao na baraza kuu la ulinzi wa taifa hilo, kufuatia kile alichokieleza kuwa ni “tukio kubwa zaidi” kuwahi kuathiri taifa la Romania tangu vita kati ya Urusi na Ukraine kuanza.

    Kikao hicho kinatarajiwa kujadili hatua watakazozichukua baada ya shambulizi la Urusi.

    Watu wawili wamejeruhiwa baada ya ndege isiyo na rubani ya Urusi kugonga jengo la ghorofa katika mji wa Galati nchini Romania, karibu na mpaka wa Ukraine,hii ni kulingana na wizara ya ulinzi ya Romania.

    Rais huyo ameomba washirika wa nchi hiyo kuwapa msaada wa ziada wa kukabiliana na ndege zisizo na rubani za Urusi.

    Urusi bado haijatoa tamko lolote kuhusu tukio hilo.

    Katibu Mkuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO Mark Rutte, amelaani “tabia ya kutojali ya Urusi” akisema kuwa ni “hatari kwa kila mtu”.

    Rutte amemhakikishia Rais wa Romania Nicușor Dan, kuwa NATO “iko tayari kulinda kila eneo la washirika wake”.

    Rutte amesema NATO itaendelea kuimarisha ulinzi wake na kuendelea kuiunga mkono Ukraine dhidi ya uchokozi wa Urusi.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Rais Ruto wa Kenya afanya mazungumzo na Marco Rubio kuhusu Ebola

    Serikali ya Marekani imeahidi kutoa dola milioni 13.5 takriban Shillingi billioni 1.75 za Kenya, kuisaidia taifa hilo kujiandaa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.

    Raia wa Marekani walioambukizwa ugonjwa wa Ebola walikuwa wapendekezwa kutibiwa nchini Kenya.

    Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Marco Rubio amefanya mazungumzo na Rais wa Kenya William Ruto kwa njia ya simu kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Ebola na juhudi zinazoendelea za kudhibiti ugonjwa huo.

    “Tunanuia kutoa dola milioni 13.5 kwa ajili ya kuimarisha maandalizi ya Kenya dhidi ya Ebola, na tayari tumeahidi kutoa dola milioni 112 kama msaada kwa nchi mbili ili kukabiliana na mlipuko huo wa kikanda,” ilisema taarifa ya wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Wanafunzi 8 wanazuiliwa na polisi kuhusu mkasa wa moto shuleni, nchini Kenya

    Idara ya jinai na upelelezi nchini Kenya, imeanzisha uchunguzi wa kina kuhusu mkasa wa moto uliotokea katika shule ya bweni ya wasichana ya Utumishi Girls Secondary School eneo la Gilgil, kaunti ya Nakuru.

    Timu ya pamoja ya uchunguzi imeundwa, kufanya uchunguzi wa kisa cha moto katika bweni hiyo pamoja na uchunguzi wa vinasaba kutambua miili ya wanafunzi 16 waliofariki katika mkasa huo.

    Maafisa wa polisi wamewahoji wanafunzi, walimu na wafanyikazi katika shule hiyo pamoja na kuangalia kamera za cctv.

    Wanafunzi wanane wametambuliwa kuwa washukiwa wa mkasa huo, kwa sasa wamekamatwa na kuzuiliwa na polisi.

    Maafisa wa polisi wanaendelea kuandikisha taarifa kuhusu mkasa huo, ili kubaini motisha ya kuchoma bweni hilo.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Cambodia yakanusha kuwaamuru Waafrika waondoke nchini humo

    Serikali ya Cambodia imekanusha kuwa imewaamuru raia wote wa Afrika, wakiwemo raia wa Kenya, Ghana, Cameroon na Uganda, kuondoka nchini humo ifikapo Mei 31, 2026.

    Kwenye mitandao ya kijamii notisi iliyosambaa ilidai kuwa watakaokiuka amri hiyo watakabiliwa au kukamatwa na kushtakiwa chini ya sheria za uhamiaji.

    Katika taarifa yake ya Mei 29, Idara Kuu ya Uhamiaji ya Cambodia (GDI) ilisema taarifa hizo ni za uongo na kwamba taarifa rasmi hutolewa tu kupitia tovuti yake ya www.immigration.gov.kh au kupitia nambari yake ya simu ya huduma kwa wateja (+855) 78 38 66 99.

    Ufafanuzi huo umefuatia taarifa zilizochapishwa na vyombo vingine vya habari vya Afrika, vilivyodai kuwa Cambodia ilikuwa imewaagiza raia wa Afrika waliomaliza muda wa msamaha wa ukaazi kuondoka nchini humo kabla ya Mei 31.

    Taarifa hizo zilidai hatua hiyo ingewahusu raia kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo Ghana, Kenya, Cameroon na Uganda. Pia zilidai kuwa wale watakaobaki Cambodia baada ya Juni 1 wangekabiliwa na faini na kuzuiliwa kabla ya kuruhusiwa kuondoka nchini humo.

    Madai hayo kuhusu kufukuzwa kwa wahamiaji Waafrika yameibuka wakati Cambodia ikiendelea na operesheni dhidi ya mitandao ya utapeli wa mtandaoni.

    Kwa mujibu wa Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Uhalifu wa Mtandao nchini humo, karibu watu 19,000 wamefukuzwa nchini baada ya kubainika kuhusika katika shughuli za utapeli wa mtandaoni.

    Ingawa makala hizo zilikuwa na kile kilichoelezwa kuwa notisi rasmi ya GDI, mamlaka ya uhamiaji yalisema hati hiyo imefanyiwa uchunguzi na kubainika kuwa ya kughushi.

    Soma zaidi:

  11. Iran na Marekani wafikia makubaliano ya kuongeza muda wa usitishaji mapigano

    Marekani na Iran zimefikia makubaliano ya kuongeza muda wa usitishaji mapigano na kuondoa vikwazo vya usafirishaji kupitia Mlango wa Hormuz, kwa mujibu wa vyanzo vilivyonukuliwa na Reuters, ingawa Rais wa Marekani Donald Trump bado hajayaidhinisha, huku vyombo vya habari vya serikali ya Iran vikisema makubaliano hayo bado hayajakamilishwa.

    Kwa mujibu wa vyanzo vinne vinavyofahamu suala hilo, makubaliano hayo yangepanua usitishaji mapigano kwa siku 60 zaidi na kuruhusu usafirishaji katika njia hiyo muhimu ya baharini, wakati mazungumzo yakiendelea kushughulikia masuala magumu kama mpango wa nyuklia wa Iran.

    Iwapo yataidhinishwa na uongozi wa Washington na Tehran, hatua hiyo itakuwa maendeleo makubwa zaidi kuelekea amani tangu mzozo ulipoanza Februari 28.

    Habari za uwezekano wa makubaliano hayo zimekuja baada ya mashambulizi ya kulipizana kati ya mataifa hayo mawili, ikiwa ni tukio la hivi karibuni tangu usitishaji mapigano ulipoanza mapema Aprili.

    Trump bado hajatoa idhini ya makubaliano hayo, vyanzo vimesema.

    Iran bado haijatoa maoni kuhusu taarifa za makubaliano hayo yaliyopendekezwa, ambayo yaliripotiwa kwa mara ya kwanza na Axios.

    Shirika la habari la Tasnim la Iran, likinukuu chanzo kilicho karibu na timu ya mazungumzo, limesema maandishi ya makubaliano hayo bado hayajakamilishwa wala kuthibitishwa.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Mahakama yasitisha kwa muda kufunguliwa kwa hospitali ya ebola ya Marekani nchini Kenya

    Mahakama ya Kenya imetoa amri za muda kusitisha kuweka wa kituo cha karantini cha Ebola kinachohusishwa na Marekani nchini Kenya, na kuzuia serikali kupokea au kuwaruhusu wamarekani walioambukizwa na virusi vya Ebola, hadi shauri lililowasilishwa na Katiba Institute litakaposikilizwa.

    Amri za muda za mahakama zilitolewa baada ya Mahakama kuthibitisha ombi la Katiba Institute kuwa la dharura.

    Ombi hilo linapinga mpango unaodaiwa kuwepo kati ya Kenya na serikali za kigeni, ikiwemo Marekani, kuhusu namna ya kushughulikia visa vya Ebola.

    Mahakama ilielekeza kuwa amri hizo zitabaki kuwa na nguvu hadi usikilizwaji wa pande zote mbili (inter partes hearing) wa maombi hayo utakapofanyika.

    Wakati huohuo, mlalamishi alielekezwa kuwasilisha kwa njia ya moja kwa moja Notisi ya Ombi na hati ya msingi kwa washtakiwa wote ndani ya saa 24.

    Washtakiwa pia waliagizwa kuwasilisha na kutoa majibu yao kuhusiana na ombi hilo ndani ya saa 48 baada ya kupokea nyaraka hizo.

    Shauri hilo linatarajiwa kutajwa tena mahakamani kwa ajili ya maelekezo zaidi baada ya pande husika kutekeleza ratiba zilizowekwa na mahakama.

    Kwa sasa, amri hizo za muda zinasitisha mipango yoyote ya serikali ya kuanzisha vituo vya karantini, vya kutenga wagonjwa au vya matibabu vinavyohusiana na Ebola, au kuwezesha kuingia kwa watu waliokumbana na au walioambukizwa Ebola nchini, chini ya mpango unaopingwa, hadi mahakama itakapowasikiliza pande zote.

    Amri hiyo imekuja baada ya serikali ya Marekani kutangaza kuwa imejizatiti kutoa dola milioni 13.5 (takriban shilingi bilioni 1.75 za Kenya) kusaidia juhudi za Kenya za kujiandaa dhidi ya Ebola, huku Washington na Nairobi zikiongeza ushirikiano katikati ya mlipuko unaoendelea katika kanda na taarifa kwamba Wamarekani waliokumbana na virusi hivyo huenda wakafuatiliwa na kutibiwa nchini Kenya.

    Kwa mujibu wa taarifa inayotajwa kutoka kwa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Tommy Pigott, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alifanya mazungumzo na Rais William Ruto kuhusu mlipuko huo na juhudi zinazoendelea za kukabiliana na afya ya umma.

    Taarifa hiyo ilieleza kuwa:

    “Serikali ya Marekani inanuia kuchangia dola milioni 13.5 katika juhudi za Kenya za kujiandaa dhidi ya Ebola, na tayari imejizatiti kutoa msaada wa bilioni 112 za dola za Marekani katika usaidizi wa nchi mbili kwa majibu ya kikanda.”

    Viongozi hao wawili pia walijadili juhudi za kupata vifaa muhimu vya kitabibu kwa Kenya na kuimarisha uwezo wa nchi hiyo katika kukabiliana na uwezekano wa visa vya Ebola.

    Soma zaidi:

  13. Meta yazindua mipango ya usajili wa kulipia kwa Facebook, Instagram na WhatsApp

    Kampuni ya Meta imetangaza rasmi kuzindua mipango ya usajili wa kulipia kwa Facebook, Instagram na WhatsApp, hatua inayobadilisha kwa kiasi kikubwa namna kampuni hiyo itakavyopata mapato zaidi ya matangazo.

    Mipango hiyo mipya ya “Plus” inaleta vipengele vya ziada kama filamu za hadithi za muda mfupi (Stories) zilizoongezwa muda wa kuonekana, kuongezwa kwa uonekano wa machapisho, ikoni maalumu za programu, stika za kipekee na uwezo wa kutazama hadithi bila kujitokeza kwenye orodha ya waliotazama.

    Hatua hii inakuja wakati Meta inaongeza kwa kasi uwekezaji katika miundombinu ya akili unde (AI), ambapo inakadiriwa kutumia hadi dola bilioni 145 mwaka huu pekee kwa vituo vya data za AI na miundombinu husika.

    Instagram Plus na Facebook Plus zitagharimu dola 3.99 kwa mwezi kila moja, huku WhatsApp Plus ikigharimu dola 2.99 kwa mwezi.

    Meta imesema huduma hizi za usajili zinalenga watumiaji wanaotaka zana zaidi za kubinafsisha akaunti zao, kuongeza ushirikiano na hadhira, na kusimamia akaunti zao kwenye programu hizo.

    Instagram Plus itakuwa na vipengele kama hesabu ya mara ambazo filamu za hadithi za muda mfupi (Instagram Stories) imetazamwa tena, orodha zisizo na kikomo za hadhira, muda mrefu wa kuonekana kwa Story zaidi ya saa 24, uangalizi wa siri wa Story, pamoja na kuangaziwa kwa filamu za hadithi za muda mfupi (Instagram Stories) kila wiki. Wateja pia watapata zana za kubinafsisha wasifu kama fonti maalumu, ikoni za programu, pini za ziada za wasifu na miitikio ya uhuishaji ya “Super Heart”.

    Facebook Plus itakuwa na vipengele vinavyofanana, ikilenga zaidi ubinafsishaji wa wasifu na ushirikishwaji wa hadhira.

    WhatsApp Plus inalenga zaidi ujumbe na ubinafsishaji, ambapo watumiaji watapata sauti maalumu za arifa, mandhari za programu, stika za hadhi ya juu, uwezo wa kubandika mazungumzo zaidi na zana za kupanga orodha za mawasiliano.

    Mipango hiyo mipya ya Plus haitachukua nafasi ya Meta Verified, huduma ya sasa ya kulipia inayolenga uthibitisho wa utambulisho, ulinzi dhidi ya kujifanya mtu mwingine na huduma kwa wateja.

    Wakati huo huo, kampuni hiyo inajaribu mpango mwingine wa usajili unaoitwa “Meta One” unaolenga watengenezaji wa maudhui, biashara na watumiaji wa Meta AI. Hatua hiyo inaifanya Meta kujiunga na kampuni kama Snapchat na X ambazo tayari zina huduma za usajili wa kulipia, ingawa mkakati wake unachanganya huduma za watumiaji, zana za wabunifu wa maudhui na huduma za AI katika mfumo mmoja mpana wa usajili.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Hospitali ya muda ya Ebola ya Marekani yafunguliwa rasmi Kenya Ijumaa

    Hospitali ya muda inayojengwa na jeshi la Marekani katikati mwa Kenya kwa ajili ya kuwahifadhi Wamarekani waliokumbana na virusi vya Ebola itaanza kufanya kazi Ijumaa ikiwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 50, maafisa wa serikali ya Marekani walisema Alhamisi huku wakitetea uamuzi wa kutowarejesha Marekani raia wanaoambukizwa Ebola kwa matibabu.

    Kituo hicho kinachojengwa katika Kambi ya Jeshi la Anga ya Laikipia na kusimamiwa na jeshi la Marekani kitahudumiwa na maafisa wa Huduma ya Afya ya Umma ya Marekani. Lengo lake ni kuwaweka karantini raia wa Marekani wanaoshukiwa kukumbana na virusi hivyo wakati wa mlipuko mkubwa wa Ebola unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Mamlaka zinasema visa vinavyoshukiwa vya Ebola sasa vimevuka 1,000 huku takriban watu 250 wakihofiwa kufariki.

    Hadi sasa hakuna Mmarekani aliyethibitishwa kupelekwa katika kituo hicho nchini Kenya, lakini ndege zimewekwa tayari kuwahamisha raia waliokumbana na virusi hivyo “wakati wowote,” kwa mujibu wa afisa mmoja mwandamizi wa serikali aliyekuwa akizungumza na wanahabari kwa masharti ya kutotajwa jina.

    Maafisa hao walisema awamu ya kwanza ya kituo hicho ambayo ni sehemu ya karantini yenye vitanda 50 itakuwa tayari kuanza kazi Ijumaa, ingawa hawakufafanua iwapo kitakuwa tayari kupokea wagonjwa mara moja. Kituo hicho pia kinatarajiwa kupanuliwa baadaye na kuwa na uwezo wa vitanda 250.

    Awamu ya pili inayotarajiwa kuanza wiki ijayo itaongeza vyumba maalumu vya kutenga wagonjwa na mifumo ya kudhibiti maambukizi, vitakavyosafirishwa kutoka Marekani kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa watakaoonyesha dalili au kuthibitishwa kuwa na Ebola.

    Operesheni hiyo nchini Kenya inahusisha zaidi ya maafisa 30 wa huduma ya afya ya umma waliopatiwa mafunzo ya siku tatu katika Kituo cha Kijeshi cha Joint Base Andrews, Maryland, kuhusu huduma za Ebola, taratibu za karantini na matumizi ya vifaa vya kujikinga kabla ya kuondoka kuelekea Kenya Jumatano usiku.

    Baadhi yao waliwahi kuhudumia wagonjwa wa Ebola wakati wa mlipuko wa mwaka 2014 hadi 2015 nchini Liberia.

    Kundi jingine la maafisa linatarajiwa kupata mafunzo mwishoni mwa wiki hii kabla ya kupelekwa Kenya wiki ijayo.

    Afisa huyo alisema kituo hicho kitakuwa na vyumba vitatu vya kutenga wagonjwa vyenye uwezo wa kuhifadhi wagonjwa wanne kila kimoja pamoja na vyumba viwili vya juu vya kudhibiti maambukizi vyenye uwezo wa kuhifadhi wagonjwa wawili kila kimoja.

    Hospitali hiyo ya muda ipo Laikipia, takriban kilomita 190 kaskazini mwa Nairobi. Eneo hilo lina kambi ya jeshi la anga na makazi ya wanajeshi yanayoweza kutumika kuwahifadhi wahudumu. Pia eneo hilo lina kituo cha mafunzo cha Jeshi la Uingereza nchini Kenya, ambacho ni miongoni mwa vituo vikubwa zaidi vya kijeshi vya Uingereza barani Afrika.

    Shirika la Madaktari wa Magonjwa ya Kuambukiza la Marekani limesema kituo hicho kipya nchini Kenya kinaibua maswali makubwa kuhusu rasilimali, muda wa maandalizi na ubora wa huduma watakazopata Wamarekani watakaopelekwa huko.

    “Katika kipindi ambacho mlipuko huu bado ni changamoto kuudhibiti, maamuzi yanapaswa kuongozwa na sayansi, uwazi na kile kilicho bora kwa wagonjwa pamoja na afya ya umma,” shirika hilo lilisema katika taarifa.

    Shirika hilo liliongeza kuwa Wamarekani wanaokumbana na ugonjwa hatari wanastahili kuwa na uhakika kwamba maamuzi kuhusu matibabu yao yanafanywa kwa kuzingatia ushahidi wa kisayansi, maandalizi ya kutosha na usalama wa wagonjwa wakati wa mlipuko unaoendelea.

    Kwa sasa hakuna chanjo wala tiba iliyoidhinishwa rasmi kwa aina hii ya virusi vya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo.

    Madaktari bingwa wa magonjwa ya kuambukiza waliowahi kuhudumia wagonjwa wa Ebola wanasema tiba kuu ni kubaini maambukizi mapema, kutenga wagonjwa kwa ufanisi na kutoa huduma za hali ya juu za kusaidia mwili. Wanasema maambukizi yanaweza kusababisha viungo vya mwili kushindwa kufanya kazi ndani ya siku chache.

    Iwapo wagonjwa wataugua kabla ya kuhamishwa, maafisa walisema kituo cha Kenya kitakuwa na uwezo wa kutoa dawa za kingamwili pamoja na dawa ya kuzuia virusi aina ya remdesivir, ambayo haijaidhinishwa rasmi kutibu Ebola lakini hutumiwa mara nyingi kwa matumizi maalumu. Wagonjwa pia watapatiwa maji mwilini na msaada wa kupumua ndani ya kituo hicho.

    Soma zaidi:

  15. Madaktari wapinga mpango wa karantini ya Ebola Kenya, watoa notisi ya saa 48 kugoma

    Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya (KMPDU), Davji Bhimji Atellah, amehoji sababu za Kenya kuripotiwa kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa kito cha karantini na matibabu ya Ebola kwa watu waliokumbana na virusi hivyo, katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Laikipia.

    Katika taarifa iliyotolewa Mei 28, Atellah alieleza hasira yake kuhusu mpango huo na kuishutumu serikali kwa kile alichosema ni kuweka maslahi ya mataifa ya kigeni mbele ya usalama wa raia wa Kenya.

    “Kama walinzi wakuu wa mfumo wa afya wa Kenya, tunasikitishwa sana na utayari unaoonekana wa serikali kuhatarisha usalama wa kibaolojia wa taifa na maisha ya wananchi wake kwa ajili ya misaada ya kigeni,” chama hicho kilisema.

    KMPDU sasa inamtaka Waziri wa Afya, Aden Duale, pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje kueleza kwa nini Kenya ilichaguliwa badala ya nchi zilizo karibu zaidi na kitovu cha mlipuko wa Ebola.

    “Hatutakaa kimya tukitazama Kenya ikigeuzwa kuwa eneo la kudhibiti ugonjwa hatari ambao hatukuusababisha,” aliongeza.

    Atellah alisema kuwa katika milipuko iliyopita, Marekani ilikuwa ikipeleka raia wake nyumbani kwa matibabu badala ya kuwahamishia nchi nyingine.

    KMPDU pia imetaka makubaliano yoyote ya ushirikiano kati ya Kenya na Marekani kuhusu mpango huo kuwekwa wazi mara moja.

    Kauli zake zimekuja wakati mjadala mkubwa ukiendelea nchini Kenya kufuatia taarifa kuwa Marekani huenda ikawapeleka watu waliokumbana na Ebola nchini Kenya kwa uchunguzi au matibabu.

    Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Huduma za Matibabu, Ouma Oluga, amesema ushiriki wa Kenya katika kukabiliana na majanga ya afya duniani si suala la kuhatarisha taifa bali ni wajibu wa kitaalamu unaotokana na uzoefu wa nchi hiyo.

    “Huu ni wakati wa Kenya kujitokeza,” alisema, akiongeza kuwa mchango wa Kenya katika kudhibiti milipuko ya magonjwa katika ukanda na duniani unaonyesha uzoefu mkubwa wa muda mrefu katika usimamizi wa dharura za afya ya umma.

    Wizara ya Afya imesisitiza kuwa hatua za Kenya zitaendelea kuongozwa na sayansi, mifumo ya kisheria na masharti madhubuti ya afya ya umma huku ikijaribu kusawazisha ushirikiano wa kimataifa na usalama wa wananchi wa ndani.

    Soma zaidi:

  16. JD Vance: Marekani na Iran 'zakaribia' kufikia makubaliano, lakini mazungumzo bado hayajakamilika

    Makamu wa Rais wa Marekani, J.D. Vance, amesema kuwa Marekani na Iran bado zinapaswa kutatua masuala kadhaa yaliyosalia kabla ya kufikiwa kwa makubaliano kuhusu vita.

    Akijibu swali la BBC kuhusu iwapo Rais wa Marekani, Donald Trump, yuko karibu kutia saini makubaliano hayo, Vance amesema bado ni mapema kueleza “lini au kama” pande hizo mbili zitafikia makubaliano ya mwisho.

    Makubaliano hayo yanadaiwa kujumuisha kuongezwa kwa muda wa kusitisha mapigano kwa siku 60 pamoja na kuanza kwa mazungumzo kuhusu mustakabali wa mpango wa nyuklia wa Iran.

    Mapema Alhamisi, maafisa wa Marekani waliiambia BBC kwamba mataifa hayo mawili yalikuwa yamefikia mwafaka kuhusu mfumo wa makubaliano hayo, lakini yakahitaji kwanza kuidhinishwa na Donald Trump pamoja na viongozi wa Iran.

    Hata hivyo, shirika la habari la Tasnim ambalo lina uhusiano wa karibu na serikali ya Iran, liliripoti kuwa makubaliano hayo bado hayajakamilishwa wala kuthibitishwa rasmi.

    Vance alisema Alhamisi jioni kuwa wapatanishi kutoka pande zote mbili walikuwa bado “wakijadiliana kwa kina kuhusu masuala kadhaa yanayohusu maandishi ya makubaliano,” likiwemo “suala la urutubishaji.”

    “Bado hatujafikia hitimisho la mwisho, lakini tuko karibu sana na tutaendelea kulifanyia kazi,” aliwaambia waandishi wa habari.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja yenye taarifa tendeti na zinazochipuka.