Serikali ya Tanzania yapinga mijadala ya mapema kuhusu uchaguzi wa 2030
Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, kuwafuatilia na kuwabaini watu wanaoendeleza mijadala kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2030 badala ya kujikita katika shughuli za maendeleo.
''Mkuu wa mkoa fuatilia wale wote ambao wanaendelea kuzungumzia uchaguzi uliopita tunataka tuwajue'', Waziri Mkuu wa Tanzania amuagiza Kanali Mtambi.
Vile vile amesema: ''Tuna wananchi kiu yao ni kuona barabara.Sisi viongozi tunapata wapi muda?, Kila wakati kwa makundi ya whatsapp ni kujadili uchaguzi wa 2030,'' anasema Mwigulu.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Bunda, mkoani Mara, Dkt. Nchemba amesema serikali haitaki kuona au kusikia mijadala ya kisiasa kuhusu uchaguzi wa mwaka 2030 kwa wakati huu, akisisitiza kuwa mjadala huo hauchangii juhudi za kuwahudumia wananchi na kuharakisha maendeleo.
''Kama sio ubinafsi ninini?Tuachane na mambo ya ubinafsi, tuelekeze huku kwenye mambo ya maendeleo'',anaendelea kusisitiza agizo hilo.
Kauli hiyo inakuja wakati Tanzania ikiendelea kutekeleza ajenda yake ya maendeleo na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, uchaguzi mkuu hufanyika kila baada ya miaka mitano, huku mjadala kuhusu uchaguzi wa mwaka 2030 ukiibuka mapema katika baadhi ya mijadala ya kisiasa na kwenye mitandao ya kijamii.
Taasisi za kimataifa, zikiwemo Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, zimekuwa zikisisitiza umuhimu wa mazingira ya kisiasa yanayoruhusu ushiriki wa wananchi katika mijadala ya umma sambamba na kuendeleza juhudi za maendeleo na utawala bora.
Haya yanajiri baada ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema kuwa litachukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu watakaojihusisha na vitendo vinavyohamasisha vurugu na uvunjifu wa amani kwa maandamano yanayodaiwa kufanyika siku ya saba ya mwezi wa saba wiki ijayo.
Pia unaweza kusoma: