Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Idadi ya vifo kutokana na Ebola yafikia 506 DR Congo

Kufikia tarehe 4 Julai 2026, katika ripoti iliyochapishwa asubuhi ya leo, jumla ya visa 1,561 vilivyothibitishwa vimerekodiwa tangu mlipuko huo utangazwe tarehe 15 Mei.

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Idadi ya vifo kutokana na Ebola yafikia 506 DR Congo

    Mamlaka za afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) zimetangaza kwamba idadi ya vifo kutokana na Ebola aina ya Bundibugyo imefikia 506.

    Kufikia tarehe 4 Julai 2026, katika ripoti iliyochapishwa asubuhi ya leo, jumla ya visa 1,561 vilivyothibitishwa vimerekodiwa tangu mlipuko huo utangazwe tarehe 15 Mei. Hivi sasa, wagonjwa 628 wametengwa au wamelazwa hospitalini katika majimbo matatu ya mashariki.

    Mkoa wa Ituri unabaki kuwa kitovu cha mlipuko huo, ukichangia zaidi ya 90% ya visa vyote vilivyothibitishwa. Unafuatiwa na Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

    Idadi ya jumla ya watu katika majimbo matatu yaliyoathiriwa inakadiriwa kuwa karibu milioni 15. Maafisa wa afya wana wasiwasi hasa kuhusu maeneo 36 ya afya yenye hatari kubwa, ambayo yanashuhudia uhamaji mkubwa wa watu.

    Uhamaji huu mkubwa unasababishwa hasa na watu waliokimbia makazi yao ndani ya nchi wakikimbia mapigano kati ya makundi ya waasi na vikosi vya serikali, pamoja na uhamaji mkubwa unaohusishwa na shughuli zisizo rasmi za uchimbaji dhahabu katika eneo hilo.

    Wiki saba baada ya mlipuko, juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa vya Kuzuia na Kudhibiti Maambukizi (IPC), ikiwa ni pamoja na Vifaa vya Kinga Binafsi (PPE) na klorini.

    Kuna visa 96 vilivyothibitishwa miongoni mwa wafanyakazi wa afya, 19 kati yao wamefariki.

    Ufuatiliaji wa watu waliogusana na wagonjwa unaongezeka kwa kasi, huku watu 10,079 wakiorodheshwa.

    Kati ya hawa, 8,221 wanafuatiliwa kikamilifu, ikiwakilisha kiwango cha ufuatiliaji cha asilimia 81.6 huku lengo likiwa 95.

    Katika ishara nyingine nzuri kwa timu ya mwitikio, idadi ya waliopona sasa imeongezeka hadi 254.

  2. Watu wasiopungua 14 wameuawa katika mashambulizi ya Urusi dhidi ya Kyiv ndani ya wiki moja

    Watu wasiopungua 11 wameuawa mjini Kyiv kufuatia usiku wa pili wa mashambulizi ya Urusi dhidi ya mji mkuu wa Ukraine ndani ya wiki moja, kwa mujibu wa mkuu wa utawala wa kijeshi wa jiji hilo.

    Takribani watu 46 wamejeruhiwa, wakiwemo watoto watano, amesema Timur Tkachenko. Maafisa wa huduma za dharura pia walisema watu wengine watatu wameuawa katika eneo kubwa la Kyiv.

    Juhudi za uokoaji zinaendelea katika zaidi ya maeneo 20, Tkachenko aliandika kwenye Telegram, akiongeza kuwa majengo marefu ya makazi yalilengwa katika wilaya mbili za jiji.

    Mashambulizi hayo yametokea siku moja kabla ya mkutano wa kilele wa NATO utakaofanyika nchini Uturuki, ambapo Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, anatarajiwa kukutana kwa mazungumzo na Rais wa Marekani, Donald Trump.

    Saa chache kabla ya mashambulizi hayo ya karibuni, Zelensky alikuwa ameonya kuwa Moscow ilikuwa ikijiandaa kufanya shambulio jingine "kubwa" dhidi ya Kyiv, kufuatia mashambulizi ya Alhamisi yaliyosababisha vifo vya watu 30.

    Ulikuwa ni usiku mwingine wa kutisha kwa wakazi wa mji mkuu, huku milipuko mikubwa na sauti za mifumo ya ulinzi wa anga ya Ukraine zikisikika. Kwa mara nyingine, wakazi wengi walikimbilia kujificha kwenye makazi ya chini ya ardhi.

    Meya wa Kyiv, Vitaly Klitschko, alisema makombora ya balestiki ya Urusi yaligonga majengo kadhaa katika maeneo mbalimbali ya jiji, na kusababisha moto kuzuka katika baadhi ya majengo ya makazi.

    Kwa mujibu wa meya huyo, maghala pamoja na karakana ya kutengeneza magari pia viliharibiwa katika mashambulizi hayo.

  3. Jinsi vita vilivyosababisha kuahirishwa kwa mazishi ya Khamenei

    Kutokana na vita kuendelea kupamba moto, maafisa wa Iran waliokuwa wakipanga mazishi ya mwezi Machi waliamua kuyaahirisha kabisa.

    Wakati huo, afisa mmoja alisema kulikuwa na maombi mengi kutoka kwa watu waliotaka kuhudhuria hafla hiyo ya siku tatu katika ukumbi wa sala ulioko Tehran, na kwamba maandalizi ya miundombinu yalihitajika ili kupokea umati huo.

    Khamenei aliuawa katika makazi yake mjini Tehran katika wimbi la kwanza la mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Marekani na Israel, pamoja na mkwe wake wa kike, mjukuu wake wa mwaka mmoja aitwaye Zahra Mohammadi Golpayegani, na maafisa kadhaa waandamizi.

    Mke wake pia iliripotiwa kuwa aliuawa katika shambulio hilo, ingawa baadaye chombo kimoja cha habari nchini Iran kilidai kuwa bado yuko hai.

    Shughuli ya mazishi ya kiongozi huyo wa kidini mwenye umri wa miaka 86 ilikuwa imepangwa kufanyika tarehe 4 Machi, ambapo waombolezaji walitarajiwa kutoa heshima zao huku mwili wake ukiwa umehifadhiwa katika Msikiti Mkuu wa Grand Mosalla ulioko mji mkuu, Tehran.

    Seyyed Mohsen Mahmoudi, mkuu wa Baraza la Uratibu wa Uenezi wa Kiislamu la Tehran, alisema kuahirishwa kwa mazishi hayo kulitokana na "idadi kubwa ya maombi ya kuhudhuria hafla hii na haja ya kuhakikisha maandalizi yanayofaa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi."

    Unaweza kusoma;

  4. Msafara wa mazishi ya Kiongozi Mkuu wa zamani wa Iran waanza mjini Tehran

    Msafara wa mazishi ya Kiongozi Mkuu wa zamani wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, umeanza safari yake kupitia mji mkuu, Tehran.

    Khamenei aliiiongoza Iran kwa zaidi ya miaka 35 kabla ya kuuawa katika mashambulizi ya anga yaliyotekelezwa na Marekani na Israel mwezi Februari.

    Mazishi yake yalianza Ijumaa na yatafanyika kwa kipindi cha siku saba, yakihusisha shughuli mbalimbali katika maeneo ya Iran na Iraq. Mamlaka za Iran zimesema kuwa kati ya watu milioni 12 na 20 wanatarajiwa kushiriki katika hafla hizo za mazishi.

    Mrithi wa Khamenei, mwanawe Mojtaba Khamenei, hadi sasa hajaonekana hadharani katika mazishi ya baba yake, licha ya kuhudhuriwa na viongozi kadhaa waandamizi wa utawala wa Iran.

    Uvumi kuhusu hali ya Mojtaba umeendelea kuenea, ukichochewa na taarifa zisizothibitishwa kuwa alijeruhiwa katika mashambulizi hayo hayo ya Marekani na Israel yaliyomuua baba yake.

    Hajajitokeza hadharani tangu ateuliwe mapema mwezi Machi.

  5. England yaichapa Mexico katika mechi ya kusisimua na kutinga robo fainali

    Uingereza ilionesha mchezo wao bora zaidi katika Kombe la Dunia huku kukiwa na shauku na hisia katika Uwanja wa Azteca na kupata ushindi mkubwa dhidi ya Mexico uliowasaidia kutinga robo fainali dhidi ya Norway.

    Huku mechi ikicheleweshwa kwa saa moja kutokana na dhoruba kali, kikosi cha Thomas Tuchel kilinusurika kadi nyekundu ya Jarell Quansah mapema kipindi cha pili na kurekodi moja ya ushindi wao bora zaidi katika miaka ya hivi karibuni.

    Mexico ilikuwa imepoteza michezo miwili tu kati ya 89 ya ushindani katika ngome yao ya Azteca, lakini mbinu ya Uingereza ya mapema iliwaruhusu kuongoza wakati Jude Bellingham alipofunga mabao mawili katika sekunde 98 kabla ya mapumziko.

    Mlinda lango wa Uingereza Jordan Pickford alikuwa katika hali nzuri sana, akiokoa mara mbili kwa ustadi mpira kutoka kwa Raul Jimenez, lakini hakuwa na nguvu ya kumzuia Julian Quinones akifunga bao la kurudisha kwa Mexico.

    Sauti za mara kwa mara za kelele, ziliongezeka wakati Quansah alipotolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Jesus Gallardo, lakini Uingereza ilirejesha uongozi wao wa mabao mawili wakati Harry Kane alipofunga kwa penalti baada ya Anthony Gordon kuangushwa na mlinda lango Raul Rangel.

    Wakati tu Uingereza ilipofikiri wamerejesha utulivu, Kane alimchezea visivyo Brian Gutierrez katika eneo la hatari, Jimenez akifunga penalti. Wakiwa na shinikizo na katika hali ya wasiwasi, Tuchel aliwaingiza Dan Burn na Djed Spence, wakirejea kwenye ulinzi wa wachezaji watano na kupata ushindi wa dakika 11 za mwisho.

    Unaweza kusoma;

  6. Shambulio la Israel liliua watu wawili huko Gaza, wahudumu wa afya wasema

    Shambulio la anga la Israel liliwaua takribani Wapalestina wawili katika Jiji la Gaza siku ya Jumapili, kwa mujibu wa maafisa wa afya.

    Wahudumu wa afya walisema watu hao wawili waliuawa baada ya shambulio la anga kulenga kundi la watu katika Barabara ya Omar Al-Mokhtar katikati ya jiji hilo, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza. Watu wengine kadhaa walijeruhiwa, waliongeza.

    Jeshi la Israel halikuzungumza kuhusu tukio hilo.

    Israel imeendelea kutekeleza mashambulizi katika Gaza tangu kusitishwa kwa mapigano kwa upatanishi wa Marekani kati yake na Hamas kufikiwa mwezi Oktoba mwaka uliopita.

    Israel imesema inalenga wanamgambo wanaotishia wanajeshi wake walioko Gaza au wale walioshiriki katika shambulio la mwaka 2023.

    Hamas imeishutumu Israel kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Wakati huo huo, Nikolay Mladenov, mjumbe wa Bodi ya Amani ya Gaza aliyeteuliwa na Rais wa Marekani Donald Trump, amesema kuwa pande zote mbili zimekiuka makubaliano hayo.

    Israel na Hamas bado zimekwama katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu utekelezaji wa awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yaanze kutekelezwa miezi minane iliyopita, zaidi ya Wapalestina 1,060, wengi wao wakiwa raia, pamoja na wanajeshi wanne wa Israel, wameuawa mjini Gaza, kulingana na takwimu zilizotolewa na kila upande. Hamas haijatangaza idadi ya wanamgambo wake waliouawa.

    Unaweza kusoma;

  7. Vietnam, kitovu cha kimataifa cha bidhaa bandia za kifahari, yaanzisha msako mkali dhidi ya soko la biashara haramu

    Mapema mwaka huu, polisi wa Vietnam walipovamia maghala mawili yaliyoko nje kidogo ya mji wa Ho Chi Minh, walikuta zaidi ya jozi 23,000 za ndala zilizokuwa na nembo za Nike, Adidas, Crocs na Gucci.

    Hata hivyo, kampuni hizo hazikuwa na uhusiano wowote na maghala hayo. Ndala zote zilizokutwa zilikuwa bidhaa bandia.

    Operesheni hiyo, iliyosababisha kukamatwa kwa bidhaa zenye thamani ya zaidi ya dola za Vietnam bilioni 2 sawa na dola za Marekani 76,053, ilikuwa sehemu ya kampeni dhidi ya biashara haramu ambayo imeendelea kushamiri waziwazi kwa miongo kadhaa.

    Takriban kilomita 30 kutoka eneo hilo, katika soko la bidhaa za mitumba lililopo katika kitovu cha utalii cha Ho Chi Minh, aina hizo hizo za ndala bandia, zinazoiga bidhaa ambazo huuzwa kwa hadi dola 900 katika masoko ya kimataifa, zinauzwa kwa dola 57 kwa jozi.

    Kando yake kuna bidhaa nyingine nyingi bandia, zikiwemo mikoba yenye chapa ya "Chanel", fulana za "Prada" na saa za "Rolex" zilizopangwa kwenye vibanda vya soko.

    Vietnam inatambulika duniani kama mojawapo ya vituo vikuu vya bidhaa bandia za bei nafuu, hasa bidhaa za kifahari za wabunifu maarufu, na ina baadhi ya masoko makubwa zaidi ya bidhaa hizo duniani.

    Sasa, huku ikikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, serikali ya Vietnam imeanzisha kampeni ya kuondoa sifa hiyo.

    Mnamo tarehe 7 Mei, serikali ilianzisha operesheni ya kitaifa dhidi ya bidhaa na shughuli zinazokiuka haki za umiliki wa ubunifu, ikiwemo utengenezaji na uuzaji wa bidhaa bandia, uharamia wa maudhui mtandaoni na ukiukaji wa alama za biashara.

  8. Nigeria yasema raia wake wawili wameuawa Afrika Kusini huku mashambulizi dhidi ya wahamiaji yakiongezeka

    Nigeria imesema kuwa raia wake wawili wameuawa nchini Afrika Kusini "wakati ambapo raia wa kigeni wanaendelea kulengwa isivyo haki" nchini humo.

    Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria ilisema kuwa Emeka Charles Iroegbu aliuawa tarehe 28 Juni, akidaiwa kufariki mikononi mwa maafisa wa polisi waliotumia "mbinu za kikatili za mahojiano". Pia ilisema kuwa mmiliki wa duka, Musa Yunana Joe, aliuawa siku hiyo hiyo na watu wasiojulikana.

    Hadi sasa, mamlaka za mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria, hazijatoa tamko kuhusu matukio hayo.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria ilisema kuwa matukio haya yanatokea wakati ambapo hisia za kupinga wahamiaji zinaongezeka nchini Afrika Kusini.

    Hali hiyo imesababisha takribani raia 25,000 kutoka mataifa mengine ya Afrika kurejeshwa katika nchi zao, wakiwemo takribani Wanigeria 700.

    Waandamanaji nchini Afrika Kusini wamekuwa wakiiomba serikali kuchukua hatua zaidi kudhibiti uhamiaji haramu. Wanasema kuwa raia wa kigeni wanachukua nafasi za ajira na kunufaika isivyo haki na huduma za umma.

    Nigeria pia imesema itadai fidia kutoka kwa Afrika Kusini kwa raia wake walioondoka nchini humo, ikiongeza kuwa serikali ya Abuja imeanza kuorodhesha biashara na mali zilizotelekezwa na Wanigeria.

    Hata hivyo, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ijumaa, Waziri wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Kusini, Khumbudzo Ntshavheni, alisema serikali yake haitalipa fidia na kwamba Wanigeria wanaweza kuuza mali zao zilizosajiliwa walizoacha nchini humo katika soko la Afrika Kusini.

    Unaweza kusoma;

  9. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu leo