Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Vikosi vya Marekani vyashambulia meli za mafuta za Iran; IRGC yatangaza mashambulio ya kulipiza kisasi

Masaa kadhaa baada ya meli tatu za mafuta za Iran kushambuliwa, Jeshi la Wanamaji la IRGC lilithibitisha kuwa lilifyatua makombora matatu kutoka Sirik kuelekea mlango Bahari wa Hormuz yakilenga meli kubwa ya kubeba ndege na meli ya kivita ya Marekani.

Moja kwa moja

Na Sarafina Robi & Seif Abdalla

  1. Mlipuko wa volkano wasababisha kusitishwa kwa safari za ndege Indonesia

    Mlipuko wa volkano ya Anak Krakatau umesababisha kusitishwa kwa safari za ndege katika uwanja mkuu wa kimataifa wa Indonesia, huku makumi ya maelfu ya abiria wakikwama.

    Mamlaka zimesema safari 209 zilisitishwa baada ya majivu ya volkano hiyo kugunduliwa angani karibu na uwanja wa ndege wa Soekarno-Hatta, Jakarta, Jumapili asubuhi.

    Volkano hiyo ilianza kulipuka Ijumaa usiku, na milipuko mingine miwili ilitokea mapema Jumapili.

    Zaidi ya watu 22,000 wameathiriwa na kusitishwa kwa safari hizo, ambazo zimehusisha zaidi safari za kwenda na kutoka Singapore, pamoja na Doha, Sydney na Kuala Lumpur.

    Mamlaka zimesema hakuna tahadhari ya tsunami iliyotolewa kutokana na shughuli za volkano hiyo, iliyopo katika Mlango wa Sunda kati ya visiwa vya Java na Sumatra.

    Waziri wa Afya amewataka wakazi wa maeneo yaliyoathirika kubaki ndani na kuvaa barakoa ili kujikinga na athari za majivu kwenye mfumo wa upumuaji, macho na ngozi.

    Shughuli za volkano hiyo pia zimesababisha baadhi ya shule kusitisha shughuli na wavuvi kughairi safari za baharini baada ya watu kuripoti kuwashwa kwa macho kutokana na majivu.

    Anak Krakatau, maana yake "Mtoto wa Krakatoa", iliporomoka mwaka 2018 na kusababisha tsunami iliyoua zaidi ya watu 400 katika maeneo ya pwani ya Sumatra na Java.

  2. Watu 22 wafariki baada ya moto kuzuka kwenye harusi Kinshasa

    Takriban watu 22 wamefariki katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kinshasa, baada ya moto kuzuka kwenye sherehe ya harusi.

    Kwa mujibu wa mamlaka nchini humo, moto huo ulitokea jana usiku na kuendelea kwa saa kadhaa. Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.

    Meya wa Lingwala, Norbert Mushinga, amesema idadi ya waliofariki inaweza kuongezeka kwa kuwa watu wengi walikuwa wakishiriki katika sherehe hiyo.

    Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani wa DRC, Jacquemin Shabani, alitembelea eneo la tukio na kulielezea kuwa ni "janga".

    Tukio hilo ni la hivi karibuni katika mfululizo wa moto iliyosababisha vifo Kinshasa, hasa katika maeneo yenye watu wengi ambako huduma za kuzima moto na miundombinu ya mijini ni hafifu.

  3. Togo yaongoza kampeni ya kubadili ramani inayoonyesha ukubwa halisi wa Afrika

    Mamlaka nchini Togo zimekaribisha kura ya Umoja wa Mataifa kuunga mkono uwakilishi sahihi zaidi wa ukubwa wa Afrika kwenye ramani za dunia.

    Azimio hilo, lililopewa uzito na Umoja wa Afrika na kuongozwa na Togo, liliidhinishwa kwa kura 164 siku ya Ijumaa, Septemba 4, 2026. Marekani ndiyo nchi pekee iliyopiga kura ya kupinga, ikisema mpango huo ni wa "itikadi na unapelekea masuala muhimu zaidi kutojadiliwa.”

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Togo, Robert Dussey, aliiambia BBC kuwa kampeni hiyo "haikulenga nchi yoyote maalum, bali ilikuwa kuhusu kuwa na ramani yenye usawa".

    Alisema makadirio ya Mercator yamechangia "kutoa taswira potofu ya Afrika".

    Kwa mujibu wa Waziri huyo, Togo "itakuwa nchi ya kwanza kurekebisha masomo yake ya jiografia ili kuwa mfano kwa nchi nyingine".

    Azimio hilo linapendekeza matumizi ya ramani ya Equal Earth, ambayo huonyesha kwa usahihi zaidi ukubwa wa mabara. Kwa mfano, Afrika ni kubwa mara 14 kuliko Greenland, lakini kwenye ramani ya Mercator maeneo hayo mawili yanaonekana kuwa na ukubwa unaokaribiana.

    Azimio hilo si la lazima, hivyo ramani ya Mercator haitatoweka katika miezi ijayo. Togo imesema inapanga kushirikiana na nchi za Afrika, shule, mashirika ya kimataifa na kampuni za teknolojia za ramani na GPS kuhamasisha matumizi ya ramani hiyo mpya

  4. Iran yadai kuishambulia nyambizi ya Marekani

    Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi lasema limeshambulia manowari ya kijeshi ya Marekani (inayoendeshwa kwa mbali).

    Kulingana na mashirika ya habari ya Iran, Walinzi wa Mapinduzi walisema katika taarifa kwamba manowari hiyo ilikusudia kuingia katika "eneo lililolindwa" la Mlango-Bahari wa Hormuz.

    Mapema, Jumamosi jioni, Jeshi la Wanamaji la IRGC lilisema katika taarifa kwamba lilikuwa limelenga meli tatu za mafuta ambazo zilikuwa zikipitia "njia zisizoruhusiwa" katika Mlango-Bahari wa Hormuz, pamoja na meli zingine tatu za Marekani katika maeneo mengine, kujibu mashambulizi ya vikosi vya Marekani dhidi ya meli tatu za mafuta za Iran. Marekani bado haijatoa maoni kuhusu mashambulizi hayo.

    CENTCOM, Kamandi Kuu ya Marekani, ilitangaza Jumamosi asubuhi kwamba vikosi vya Marekani vilishambulia meli tatu za mafuta za Iran, ikiwa ni pamoja na moja nje ya pwani ya Kisiwa cha Kharg, kitovu kikubwa cha usafirishaji wa mafuta ya Iran.

  5. Mtangazaji miongoni mwa watu 12 waliohukumiwa kifo nchini Misri katika kesi ya dawa za kulevya

    Mtangazaji wa televisheni wa Misri, Sarah Khalifa, na watu wengine 11 wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.

    Kwa mujibu wa gazeti la serikali la al-Ahram, walikuwa sehemu ya genge la uhalifu lililoingiza nchini humo malighafi zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya kwa nia ya kuziuza.

    Pia walipatikana na silaha haramu na risasi. Khalifa, mwenye umri wa miaka 39, anajulikana zaidi kwa kipindi chake cha televisheni kiitwacho Mission Impossible, ambacho kiliangazia masuala ya uhalifu.

    Amekanusha mashtaka hayo. Washitakiwa wengine tisa wamehukumiwa kifungo cha maisha jela, huku saba wakiondolewa mashtaka na kuachiwa huru.

    Wakili wa Khalifa alisema atakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo ya kifo. Hukumu hiyo ilitangazwa kwa mara ya kwanza mwezi uliopita.

    Hata hivyo, ilithibitishwa mwezi mmoja baadaye baada ya mahakama kupata maoni ya kidini kutoka kwa Mufti Mkuu wa Misri,hatua ambayo ni sharti la kisheria katika kesi zinazohusisha hukumu ya kifo.

    Wakati wa kesi hiyo, mahakama ilielezwa kuwa mamlaka zilikuwa zimekamata zaidi ya kilo 750 za dawa za kulevya pamoja na malighafi zilizokuwa zimeingizwa nchini kwa ajili ya kuzitengeneza.

    Mashahidi ishirini walitoa maelezo kwa waendesha mashtaka, gazeti la *al-Ahram* liliripoti, sambamba na ushahidi wa kielektroniki uliotia ndani mazungumzo na video.

    Kwa mujibu wa gazeti la serikali la *Akhbar al-Youm*, alipoulizwa na jaji kuhusu madai ya kuhusika kwake wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo mwezi Septemba mwaka jana, Khalifa alisema hakuwahi kuona dawa zozote za kulevya hadi pale alipopigwa picha akiwa nazo ndani ya ofisi za mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya.

    Kwa mujibu wa ripoti ya Amnesty International ya mwaka 2025, kulikuwa na hukumu 492 za kifo katika mwaka huo, ambapo 23 kati yake zilitekelezwa.

    Washitakiwa walipatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya na ubakaji, makosa ambayo "hayakufikia kiwango cha 'mauaji ya makusudi', ambayo ndiyo kigezo pekee kinachoruhusu matumizi ya adhabu ya kifo kwa mujibu wa sheria na viwango vya kimataifa," ripoti hiyo ilisema.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Balozi wa Marekani nchini Israel akemea makazi "haramu" ya Israel katika Ukingo wa Magharibi

    Mike Huckabee, balozi wa Marekani nchini Israel, alisema kuwa raia wa Marekani wanaoishi katika eneo la makazi la Termeziya walielezea katika mkutano wa baraza la eneo hilo kuhusu nyumba zilizoharibiwa, vitisho dhidi ya watoto, pamoja na vitendo vya vurugu na vitisho vingine.

    Eneo hili liko Ramallah, katika Ukingo wa Magharibi, na ni makazi ya idadi kubwa ya Wamarekani.

    "Ninaamini kuwa Waisraeli wanaoishi Judea/Samaria (jina linalotumiwa na Israel kwa ajili ya eneo la Ukingo wa Magharibi linalodhibitiwa kimabavu) wana haki ya kuishi huko, na ninaunga mkono hilo, hata hivyo, si kila anayeamini katika Biblia anaunga mkono vitendo visivyo halali,"

    Huckabee aliandika katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X. Makazi ya Waisraeli katika eneo la Ukingo wa Magharibi linalodhibitiwa kimabavu yanachukuliwa kuwa haramu kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Israel yashambulia kusini mwa Lebanon kulipiza mashambulizi dhidi ya askari wake

    Israel yasema imelenga maeneo kusini mwa Lebanon kufuatia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya askari wake, Jeshi la Israel lilitangaza kuwa lililenga maeneo kadhaa kusini mwa Lebanon Jumapili asubuhi, ikiwa ni jibu kwa hatua ya Hezbollah kurusha ndege mbili zisizo na rubani dhidi ya askari wa Israel.

    Awali, jeshi la Israel liliwataka wakazi wa maeneo yanayozunguka jengo moja katika mji wa Arab Salem, kusini mwa Lebanon, kuhama, likisema jengo hilo lingelengwa kwa sababu lilikuwa likitumiwa na Hezbollah.

    Hezbollah bado haijatoa tamko lolote kuhusu suala hili. Israel inalitaja eneo la kusini mwa Lebanon kama ukanda wa usalama na kusema haitaondoka katika maeneo hayo hadi pale Hezbollah itakapoweka chini silaha zake.

    Tangu tarehe 2 Machi, mashambulizi ya Israel nchini Lebanon yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 4,300.

  8. Ukraine na Urusi: Mazungumzo kati ya ujumbe wa Putin na Trump yakamilika

    Mazungumzo kati ya Rais wa Urusi Vladimir Putin na wajumbe wa Rais wa Marekani Donald Trump, Steve Witkoff na Jared Kushner, yalihitimishwa katika ikulu ya Kremlin baada ya mkutano wa saa tatu na dakika 10 uliolenga juhudi za kumaliza vita nchini Ukraine.

    Mshauri wa Rais wa Urusi, Yuri Ushakov, alielezea mazungumzo hayo kuwa "yenye tija, ya kujenga, mazuri kabisa na yaliyojikita katika msingi wa kuaminiana," akisema kuwa hali ya mambo nchini Ukraine pamoja na masuala mengine kati ya Moscow na Washington yalijadiliwa.

    Mwanzoni mwa mkutano huo, Putin alisema kuwa mawasiliano na mazungumzo na Marekani "huwa na tija kila mara," na kusifu juhudi za Trump za kutafuta suluhu ya kumaliza vita.

    Wakati huo huo, Witkoff alifikisha salamu kutoka kwa Rais wa Marekani na kumshukuru Putin kwa hatua alizochukua kuhakikisha usalama wa ujumbe huo.

    Putin pia aliamuru vikosi vya Urusi kutoshambulia Kyiv kwa muda wa siku tatu, kuanzia saa sita usiku wa Jumamosi, huku wajumbe hao wawili wa Marekani wakijiandaa kusafiri kwenda mji mkuu wa Ukraine.

    Wakati huohuo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alitangaza kuwa nchi yake iko tayari kujiepusha na mashambulizi dhidi ya Moscow hadi mwisho wa siku ya Jumatatu, akitoa wito kwa Urusi kuchukua hatua kama hiyo dhidi ya Kyiv.

    Alisema: "Kuanzia sasa hadi mwisho wa Jumamosi, pamoja na Jumapili na Jumatatu, Ukraine iko tayari kujiepusha na kushambulia Moscow kwa makombora, na tunatarajia Urusi ifanye vivyo hivyo kwa Kyiv."

    Moscow haijatangaza kukubaliana na usitishaji wa mapigano wa siku tatu ambao ni mpana zaidi kuliko ule wa awali.

    Zelensky aliongeza kuwa alizungumza na wajumbe hao wawili wa Marekani, ambao alisema "tayari wameanza ushirikiano na upande wa Urusi," akithibitisha kuwa Kyiv iko tayari kwa "mazungumzo mazito" pindi ujumbe wa Marekani utakapowasili katika mji mkuu wa Ukraine siku ya Jumapili.

  9. Vikosi vya Marekani vyashambulia meli za mafuta za Iran; IRGC yatangaza mashambulio ya kulipiza kisasi

    Masaa kadhaa baada ya meli tatu za mafuta za Iran kushambuliwa, Jeshi la Wanamaji la IRGC lilithibitisha kuwa lilifyatua makombora matatu kutoka Sirik kuelekea mlango Bahari wa Hormuz yakilenga meli kubwa ya kubeba ndege na meli ya kivita ya Marekani.

    IRGC pia ilisema kuwa, ikiwa ni jibu kwa shambulio la Marekani dhidi ya meli za mafuta za Iran, ililenga meli tatu za mafuta zilizokuwa zikipita katika "njia zisizoruhusiwa kupitia mlango Bahari wa Hormuz" na pia ilishambulia meli ya kivita ya Marekani iliyokuwa ikijaribu kuingia katika mlango huo.

    Marekani bado haijatoa tamko lolote kuhusu mashambulio hayo.

    Mapema Jumamosi, CENTCOM ilitangaza kuwa vikosi vya Marekani vilishambulia meli tatu za mafuta za Iran.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ililaani mashambulio hayo na kusema kuwa Marekani ndiyo inayowajibika kwa matokeo ya vitendo hivyo. CENTCOM ilisema kuwa shambulio hilo lilifanyika baada ya IRGC kufyatua makombora ya balistiki dhidi ya meli mbili za kivita za Marekani.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja.